Wednesday, November 29

CNARED inamtaka Mkapa kuahirisha mazungumzo ya Arusha kuhusu Burundi

Mkutano wa viongozi wa CNARED mjini Brussels
Muungano wa vyama 25 vya upinzani vya Burundi CNARED, unamtaka mpatanishi wa mzozo wa Burundi, rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa kuahirisha duru ya nne ya mazungumzo ya Arusha ili kuruhusu pande zote kushiriki.
Pancrace Cimpye msemaji wa CNARED Burundi.
Pancrace Cimpye msemaji wa CNARED Burundi.
Akizungumza na Sauti ya Amerika kutoka Brussels siku ya Jumanne baada ya muungano huo kuwachagua viongozi wake wapya msemaji wake Pancrace Cimpaye, anasema hadhani duru hii ya mazungumzo itaweza kuleta suluhisho la kweli.
Anasema tatizo kubwa ni kwamba "baada ya matayarisho ya muda mrefu muungano mkubwa wa upinzani CNARED haujaalikwa na kwamba serikali pia haijapeleka wajumbe basi ni makubaliano gani yatafikiwa hapo Disemba 8 kama ilivyopangwa?"
Kiongozi mpya wa muungano huo unaojulikana kama Baraza la Kitaifa kwa ajili ya Kuheshimu Makubaliano ya Arusha ni Dk. Jean Minani aliyekua spika wa bunge la Burundi mara mbili, mara ya mwisho ikiwa kati ya 2002 hadi 2005.

Wabunge Uingereza wakerwa na 'tweets' za Trump

Waziri Mkuu Teresa May
Wabunge wa Uingereza wameonyesha kukerwa Jumatano na kitendo cha Rais Donald Trump alivyorudia kutuma ujumbe mfupi wa tweet uliokuwa na video isiyo na ukweli ndani yake dhidi ya Waislam.
Video hiyo ambayo Trump aliirudia katika twitter yake ilipostiwa kwanza na kiongozi wa kundi la Uingereza mwenye mrengo wa kulia ambaye aliwahi kuhukumiwa kwa kosa la kutumia kauli za chuki.
Wabunge kadhaa wamemtaka Waziri Mkuu Theresa May kufutilia mbali ratiba ya ziara ya kikazi ya rais Trump iliyopangwa kufanyika mwaka 2018.
“Huyu siyo mshirika au rafiki yetu,” amesema mbunge David Lammy, akiongeza kuwa rais wa Marekani hafai kutembelea Uingereza.

Msemaji wa Waziri Mkuu May amesema Trump amefanya makosa kutuma tena video hiyo ambaye haikuwa tukio la kweli katika ujumbe wake wa tweet.
“Wananchi wa Uingereza kwa pamoja wanapinga shutuma za kisiasa za kibaguzi za mrengo wa kulia, ambazo zinakiuka maadili ambayo yanawakilishwa na nchi hii—upole, kuvumiliana na heshima. Ni kosa kwa rais kufanya jambo kama hili,” amesema.
Kadhalika hata wale wanasiasa ambao kawaida ni washabiki wa Trump wamemkosoa Trump kwa kutuma tena ujumbe wa aina tatu wa twitter uliotolewa na Jayda Eransen, Naibu kiongozi wa kikundi cha mrengo wa kulia chenye sera ya Uingereza kwanza (Britain First) na msimamo dhidi ya wahamiaji, kinachotaka kurejeshwa “kwa maadili ya utamaduni wa Kiingereza” na kutaka kumaliza “kuenea kwa Uislam.”
Tweet alizozituma tena Trump Jumatano asubuhi kufuatia video ya kwanza iliyokuwa haijathibitishwa inayodai kuwa wahamiaji Waislam wakiwa wanampiga kijana wa kiholanzi aliyekuwa anatembelea magongo.
Muda mchache baadae rais alituma tena video ya pili ambayo ilipostiwa na Fransen, iliyodai kuwa “Muislam alikuwa analiharibu sanamu la Bikra Maria.

Tweet ya tatu ilikuwa na ujumbe : “Kundi la Waislam wakimsukuma kijana kutoka katika paa la nyumba na huku wakimpiga hadi kumuua!”
Fransen amekuwa akihojiwa na polisi mara kadhaa kwa sababu ya kutumia kauli zenye chuki kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa kikundi kinachojiita Uingereza Kwanza (Britain First) ambao wametuhumiwa kwa vurugu za kidini na uchochezi.
Mapema mwezi wa Novemba, Fransen alipatikana na hatia ya vurugu za kidini wakati alipomtukana mwanamke wa Kiislam kwa sababu amevaa hijabu.

Manyanyaso yanayowakuta watoto, kinamama Kenya

Watoto wa mitaani Kenya
Shirika binafasi la Shofco ambalo linafanyia shughuli zake mjini Mombasa nchini Kenya katika eneo la mabanda maarufu kama Bangladesh, limekuwa mstari wa mbele katika kushughulikia masuala ya kina mama na hasa watoto.
Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA anaripoti kuwa shirika hili hasa linawasaidia watoto ambao hukumbwa na manyanyaso ya mara kwa mara.
Kundi hilo linadai kuwa manyanyaso mengi yanawakumba wale ambao wanaishi katika maeno duni katika mitaa hiyo ya Bangladesh na mara nyingine hukosa hata msaada unaohusika kuwaondolea madhila waliyo nayo.
Shofco ina wafanyakazi wa kujitolea ambao lengo lao kuu ni kuisaidia jamii pale kunapotokea dhulma yoyote katika jamii hizo husika. Mwandishi wetu alipata fursa ya kuzuru mtaa wa mabanda wa Bangladesh mjini Mombasa na kukutana na baadhi ya kina mama ambao wanazungumzia yale ambayo huwasibu katika maisha yao ya kila siku.

MAONESHO YA UTALII WA TANZANIA SAUDI ARABIA YALIVYOFANA


Maonyesho ya Utalii wa Tanzania yalivyofanyika mjini Riyadh nchini Saudi Arabia kwa watu mbalimbali kutembelea kwenye maonyesho hayo yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia. Aidha Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza yupo nchini Tanzania kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
Maonyesho yakiendelea kwa wageni mbalimbali kuelezewa namna ya vivutio vya utalii wa Tanzania.Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza kushoto akiwa na mke wake, Maimuna Mgaza, wakiwa kwenye maonyesho hayo ya Utalii.
Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, H.E Hemed Mgaza mwenye suti nyeusi mkono wa kushoto akijadiliana jambo na wageni wake waliotembelea katika maonyesho ya utalii yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini hapa. 

Hapa maonyesho ya chakula yakiendelea mjini Riyadh, nchini Saudi Arabia.


Wizara ya fedha yashambuliwa Yemen

Bomu kubwa lililotegwa kwenye gari limelipuka katika mji ulioko kusini mwa mji wa Aden na kusababisha vifo vya takriban watu wanne, taarifa hii ikiwa ni kulingana na duru za usalama za eneo hilo

Selbstmordanschlag auf Gebäude der Sicherheitskräfte im jemenitischen Aden (Imago/Xinhua)
Bomu hilo lililipuka nje ya jengo la wizara ya fedha, mjini Aden, ambako ni makao makuu ya muda ya serikali ya Yemen, inayoungwa mkono na Saudi Arabia na inayotambulika na jumuiya ya kimataifa. 
Taarifa zilizoripotiwa na shirika la habari la AP zinasema baadhi ya maafisa na watu walioshuhudia zinasema bomu hilo kubwa lililotegwa kwenye gari limeliharibu jengo hilo la serikali na kusababisha vifo vya watu watano na wengine 12 kujeruhiwa.
Hata hivyo, duru za kiusalama zimearifu kwamba, kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu, IS limedai kufanya shambulizi hilo kwenye jengo hilo, na kusababisha vifo vya walinzi wawili na wengine wanne kujeruhiwa.
Kwenye taarifa kupitia tawi lake la propaganda la Amaq, wanamgambo wa IS wamedai kulipua bomu hilo lililotegwa kwenye gari lililokuwa limeegeshwa nje ya jengo la wizara ya fedha.
Taarifa zilizotolewa na taasisi moja binafsi ya habari ya Aden al-Ghad majengo sita ya ghorofa yaliharibiwa vibaya na mlipuko wa bomu hilo, likiangazia shuhuda zilizotolewa na wakazi wa eneo hilo. Mlipuko huo ulivunja vioo vya madirisha na makazi jirani, taarifa hiyo iliongeza.
Shambulizi hilo linalodaiwa kufanya na kundi la wanamgambo wa IS, ni la pili kufanywa na kundi hilo la itikadi kali katika mji wa Aden mwezi huu.
USA Sicherheitsrat der Vereinten Nationen Friedensverhandlungen in Kolumbien (picture-alliance/dpa/M. Rajmil)
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetaka kuongezwa ushirikiano wa kukabiliana na mitandao ya kigaidi
Hapo jana kwenye mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unaozungumzia ugaidi, unaofanyika makao makuu ya Umoja huo, Afisa mwandamizi kwenye ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa inayoshughulikia vita dhidi ya ugaidi Vladimir Voronkov, ametoa mwito wa kuongezwa kwa ushirikiano baina ya mataifa na kubadilishana taarifa ili kukabiliana na mitandao ya kigaidi.
Novemba 5, wanamgambo hao walisema walihusika na mashambulizi mawili yaliyofanyika wakati mmoja katika idara ya usalama ya mjini Aden, yaliyosababisha vifo vya takriban wanajeshi saba.
Mji huo wa Aden umeshuhudia wimbi la mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni, na hususan yakilenga vikosi vya usalama, maafisa wa serikali na wanasiasa, na kusababisha vifo vya mamia. Baadhi ya mashambulizi hayo yalidaiwa kufanywa na IS na mengine na Al-Qaeda.
Tangu mwaka 2014, Yemen, ambayo ni moja kati ya mataifa maskini zaidi za Kiarabu, imekabiliwa na machafuko makubwa kati ya serikali inayoungwa mkono na Saudi Arabi na waasi wa Houthi ambao ni washirika wa Iran. Waasi wa Houthi bado wanaudhibiti mji mkuu wa Yemen, Sanaa na maeneo mengine ya nchi hiyo, pamoja na mashambulizi yaliyoanzishwa na jeshi chini ya uongozi wa Saudi Arabia Machi 25, 2015, dhidi yao.
Pengo la kimamlaka limesababisha wapiganaji wa jihadi wa Al-Qaeda na wapinzani wao IS kuimarisha uwepo wao nchini Yemen, na hususan katika eneo la kusini linalodhibitiwa na serikali.
Huku wakiungwa mkono na Marekani, vikosi vinavyoongozwa na Saudi Arabia vimeongeza kampeni yake nchini Yemen, ya kukabilina na wapiganaji wa jihadi katika eneo hilo la Kusini, lakini bado wanadhibiti baadhi ya maeneo ya milimani na kwenye jangwa.

DAWA ZA SARATANI ZAPATIKANA KWA ASILIMIA 80 % KUTOKA ASILIMIA 4%

TAASISI ya Saratani ya Ocean Road wameipongeza Bohari ya Dawa (MSD), kwa usambazaji wa dawa katika taasisi hiyo na maeneo mengine nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage wakati akizungumza na watendaji wa MSD ambao walifanya ziara ya kikazi ya kujua changamoto mbalimbali za usambazaji dawa katika taasisi hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu.
Katika hatua nyingine  upatikanaji wa dawa za saratani,vifaa tiba na vitendanishi  vya maabara katika taasisi hiyo ni asilimia 80  kutoka asilimia nne mwaka 2015.
Kutokana na hatua hiyo taasisi hiyo imesema ipo haja jamii kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Bohari ya Dawa MSD katika kupunguza changamoto za huduma za saratani ambapo ilikuwa kero miaka miwili iliyopita.
 Mwaiselage alisema hapo awali  upatikanaji wa dawa vifaa tiba na vitendanishi ilikuwa ni changamoto kubwa katika utendaji.
"2015 taasisi hiyo ilikuwa ikipata dawa,vifaa tiba na vitendanishi asilimia nne sasa ni asilimia 80 haya ni matokeo mazuri ya utendaji wa kazi wa MSD," alisema.
Alisema bajeti ya taasisi hiyo mwaka 2015 ilikuwa ni sh.milioni 790 na sasa ni sh.bilioni saba jambo ambalo linatia faraja.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu alisema taasisi hiyo inatambua kuwa dawa za kansa ni gharama lakini atahakikisha zinaendelea kupatikana kwa wakati ili kuokoa maisha ya watanzania.Alisema suala la vifaa vya maabara ni tatizo linalohitaji mpango wa kitaifa wa manunuzi.
"Nawahakikishia Ocean Road ni mteja muhimu hivyo nipo tayari muda wote kuwahudumia leteni orodha ya mahitaji ya dharura hata leo," alisema.
Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Anna Kajiru alisema katika Hospitali hiyo upatikanaji wa dawa kutoka MSD ni asilimia 80 na kuwa hali hiyo imetokana na ushirikiano mzuri baina yao.
"Hivi sasa hali ya upatikanaji wa dawa ambazo zinahitajika sana na wananchi ni mkubwa mkubwa tofauti na zamani na hii inatokana na kazi nzuri inayofanywa na ninyi MSD" alisema Kajiru.
Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu na maofisa wake yupo katika ziara ya kikazi ya kutembelea Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam ambapo leo alitembelea Hospitali ya Rufaa ya Amana na Saratani ya Ocean Road na kesho atazitembelea Hospitali ya Taifa ya  Muhimbili, Vijibweni na Temeke.
  Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (kulia), akizungumza na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja Dar es Salaam leo ya kujua changamoto za upatikanaji wa dawa katika hospitali hiyo na kuzitafutia ufumbuzi. Kushoto ni Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Meshack Shimwela.
 Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Meshack Shimwela, akisisitiza jambo katika mkutano huo.
 Maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana wakimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa MSD,Laurean Bwanakunu.
 Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam , Celestine Haule akichangia jambo wakaz8i akizungumza na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana.
 Mfamasia wa Hospitali ya Rufaa ya Amana, Anna Kajiru (kulia), akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (wa sita kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Hospitali ya Rufaa ya Amana. 
 Mkutano ukiendelea.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage akizungumza katika mkutano huo.
 Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu akisisitiza jambo wakati akizungumza na maofisa wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road katika ziara hiyo ya siku moja.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dk. Julius Mwaiselage ( kulia), akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu wakati wa ziara hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD,  Laurean Bwanakunu (wa tano kulia), akiwa katika picha ya pamoja na maofisa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road. 

Kampuni ya Chai Bora yainunua kampuni ya Dabaga

Katika kutekeleza sera ya uwekezaji nchini ili kuendana na kasi ya serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda ifikapo mwaka 2025, kampuni ya Chai Bora imeinunua kampuni ya Dabaga iliyokuwa ikitamba na bidhaa za kuongeza ladha za vyakula kama vile Dabaga tomato sauce , Pilipili Mbuzi, Mango pickle na bidha nyinginezo.

Kampuni ya Chai Bora imekuwa ikifanya shughuli zake hapa nchini tangia mwaka 1990, Chai Bora inaogoza kama chata ya kuzalisha majani ya chai, Ikijikita zaidi katika uzalishaji wa bidhaa kama vile majani kama vile Black Tea, Green Tea pia Kahawa aina ya Café Bora. Kwa kuwa imeanza kazi tangia mwaka 1990 hadi sasa ni takribani miaka 27 inaashiria ukuaji katika sekta husika ya bidhaa za Chai . Katika hiyo miaka 27 Chai Bora imeinunua kampuni ya Dabaga, imeongeza uzalishaji wa bidhaa tofauti na imeboresha kiwanda cha Dabaga Iringa na teknolojia za kisasa.
Uwekezaji huo ambao umehusisha teknolojia za kisasa na mitambo ya kisasa zaidi ni wazi kuwa itaongeza ufanisi kwenye uzalishaji wa bidhaa husika na kusukuma ongezeko la ajira nchini. Kupitia uzalishaji huo kwa sasa kiwanda hicho kimetoa ajira ya moja kwa moja na ajira isiyokuwa ya moja kwa moja kwa wakazi wa kijiji cha Ikokoto cha wilayani Ilula, Iringa. Wakulima ambao wanaojihusisha na shughuli za malighafi za viwanda kama hicho hasa wakulima, wasambazaji wa bidhaa za kilimo pamoja na watoa huduma wengine kama vile kampuni za ulinzi, usafi na hata watoa huduma za vyakula nao watanufaika na uwekezaji huo.

Mkurugenzi wa Chaibora, Mr.Kapila Mr.Kapila Ariyatilakakaalisema wakulima watanufaika kwa kuuza mazao yao hasa nyanya kwa kuwa kwa sasa kiwanda hicho kinahitaji nyanya tani 300 hadi 400 kwa mwezi. "Hii inaashiria kuwa wakulima wa nyanya wa ndani na nje ya Iringa watanufaika na uwepo wa kiwanda hicho hasa kwa kuuza bidhaa zao humo" anasema Mr.Kapila Ariyatilaka. Anasema wasambazaji wanaojihusisha na bidhaa za kilimo nao wamepata mwanya wa kuuza bidhaa zao na hasa wanaweza kununua kwa wakulima na kisha kuuza kwenye kampuni hiyo na hivyo kuongeza wigo wa ajira.

Anaongeza kuwa watoa huduma za ulinzi kwa maana ya kampuni za ulinzi nao hawapo nyuma katika kunufaika na kiwanda cha Dabaga. Vijana wengi wamepata ajira kiwandani hapo huku wengine wakifanya kazi za uuzaji wa vyakula kwenye migahawa ya kiwandani hapo na wengine hufanya vibarua vya hapa na pale kiwandani. Sasa kwa kuwa wafanyakazi ambao wameajiriwa moja kwa moja kiwandani hapo ni 35 huku wale waliopo kwa ajira za muda ni 45 ni wazi kuwa wanaongeza mzunguko wa fedha kwenye maeneo ya jirani.

Lakini kwa ajira hii na nyinginezo zitokanazo kwa uwekezaji huo wa Chai Bora ni wazi kuwa familia za watanzania zitanufaika na uwekezaji huo kwa kuwa wafanyakazi hao ndio watakaopeleka huduma nyumbani. Pia imeongeza hali ya maisha kwa wakazi wa eneo kilichopo kiwanda kwa kuwa wameanza kupangisha nyumba zao za kuishi kwa wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Mzunguko wa fedha umeanza kuonekana kwenye jamii zao kwa kuwa kwa sasa wafanyakazi wa kiwanda hicho wananunua bidhaa kutoka kwa wafanya biashara hapo Ikokoto. Hiyo imesaidia kupunguza hali ya vijana kukaa vijiweni bila ya kuwa na kazi muhimu na kwa sasa wanakuwa wakipata angalau kipato kwa kufanya kazi kwenye kiwanda hicho au kujihusisisha na fursa nyingine kama kuuza bidhaa maeneo ya jirani na kiwanda.

Lakini pia kuna asilimia kubwa ya mafunzo yanatolewa na wataalamu wa kiufundi kutokea nje ya nchi hasa kutokea nchini China ambapo wachina ndio wamehusika na ujenzi wa mitambo hiyo ya kisasa ya kuzalishia bidhaa. Akizungumzia kuhusiana na changamoto kwenye uwekezaji wa Chai bora kwenye kiwanda cha Dabaga , alisema serikali ingetakiwa kuwa na sera ya kusaidia uwekezaji kwenye kilimo ambao unafanywa na wawekezaji nchini.

Alisema,"Ingetakiwa kuwepo kwa msamaha wa kodi hata kwa miaka mitano kwa uwekezaji wa asili ya bidhaa za kilimo ili kuongeza hamasa kwenye fani hiyo na kusaidia kukuza kilimo hapa nchini". Alisema, kwa sasa kampuni hiyo inalenga kuwakilisha vema kwenye soko la Afrika Mashariki na Kati na kwa hiyo ni vema ikasaidiwa kuimarisha mazingira bora zaidi ya kibiashara. Alisema, washindani wakubwa wa soko lake ni Red gold, American Garden, Pep Tang na Canadian. Lakini alibainisha kuwa changamoto nyingine kubwa inayowakabili kwa sasa ni kukosekana kwa umeme wa uhakika katika eneo la uwekezaji.

KILIMANJARO STARS YAONGEZA WATATU, KULIFUATA KOMBE LA CHALENJI KESHO

Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje, ameongeza nyota watatu katika kikosi chake mara baada ya Baraza la Soka la Afrika Mashariki (CECAFA), kuridhia kuongezwa wachezaji watatu kwa kila timu.
Awali, CECAFA ilihitaji wachezaji 20 tu, lakini sasa wameongeza watatu na kufanya idadi mpya ya wachezaji watakaoshiriki michuano hiyo ya Chalenji kwa mwaka huu kuwa 23.
Wachezaji walioongezwa na Kipa Ramadhani Kabwili kutoka Young Africans ya Dar es Salaam, Amani Kiata  wa Nakuru All Stars ya Kenya na Yahya Zayd kutoka Azam FC ya Dar es Salaam.
Kikosi cha wachezaji 20 wa awali wa Ninje - Kocha wa Daraja ‘A’ la Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), ni makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
Walinzi ni Gadiel Michael (Young Africans), Boniphace Maganga (Mbao FC), Kelvin Yondani (Young Africans), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni (Simba SC) na Mohammed Hussein (Simba SC).
Viungo wa kati ni Himid Mao ambaye ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Hamis Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Mzamiru Yassin (Simba SC), Raphael Daud (Young Africans), Shizza Kichuya (Simba SC), Abdul Hilal (Tusker/Kenya) na Ibrahim Ajib (Young Africans).
Washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes). 
Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa). 
Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Chalenji tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.

Mashindano ya mwaka huu CECAFA ilifikia makubaliano na kanda mbili za Kusini mwa Afrika - COSAFA na ile ya Kaskazini UNAF kualika timu mbili za kutoka kanda hizo na mataifa ya Libya na Zimbabwe.
Jumla ya timu shiriki kwenye CECAFA Senior Challenge Cup mwaka huu itakuwa 10 ambazo ni pamoja na wenyeji Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, South Sudan, Ethiopia, Zanzibar, Somalia, Zimbabwe na Libya. 
Sudan wenyewe wamejiondoa katika mashindano ya mwaka huu wakati mataifa mawili ya Eritrea na Djibouti nayo hayatashiriki.
Michuano hiyo itatumia viwanja vya Moi kilichopo Kisumu (Moi Stadium), Bukungu kilichopo Kakamega na Afraha kilichopo Nakuru wakati Uwanja wa Kasarani Nairobi na ule wa Kenyatta uliopo Machakos vitatumika kama viwanja vya ziada.

Makundi 2017 Cecafa Challenge Cup
Kundi A: Kenya, Libya, Rwanda, Tanzania, Zanzibar.
Kundi B: Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia, South Sudan.

Ratiba ya michuano hiyo mwaka huu ni kama ifuatavyo:
Desemba 3, 2017
Kundi A
Libya vs Tanzania
Kenya vs Rwanda

Desemba 4, 2017
Kundi B
Burundi vs Ethiopia
Uganda vs Zimbabwe
Desemba 5, 2017
Kundi A
Zanzibar vs Rwanda
Kenya vs Libya
Desemba 6, 2017
Kundi B
Sudan Kusini vs Zimbabwe
Uganda vs Burundi

Desemba 7, 2017
Tanzania vs Zanzibar
Rwanda vs Libya

Desemba 8, 2017
Kundi B
Sudan Kusini vs Ethiopia
Zimbabwe vs Burundi

Desemba 9, 2017
Kundi A
Rwanda vs Tanzania
Kenya vs Zanzibar
Desemba 10, 2017
Kundi B

Sudan Kusini vs Burundi
Ethiopia vs Uganda

Desemba 11, 2017
Kundi A
Libya vs Zanzibar
Kenya vs Tanzania

Desemba 12, 2017
Kundi B
Uganda vs Sudan Kusini
Zimbabwe vs Ethiopia

Desemba 13, 2017
Mapumziko
Desemba 14, 2017
Nusu fainali 1 (Mshindi Kundi A vs Mshindi wa pili Kundi B)
Desemba 15, 2017

Nusu fainali 2 (Mshindi Kundi B vs Mshindi wa pili kundi A)
Desemba 16, 2017

Mapumziko
Desemba 17, 2017
Mshindi wa Tatu & Fainali

……………………………………………………………………..……………..……
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

WAZIRI MKUU ABAINI SEMI TRELA 44 ZIKITAKA KUTOLEWA BANDARINI BILA YA KUFUATA UTARATIBU



Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa (mwenye Tai nyekundu) amefanya ziara ya kushitukiza katika Bandari ya Dar es salaam leo November 29, 2017 na kubaini Kampuni ya NAS ikitaka kutoa Semi Trela 44 bila ya kufuata utaratibu.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kuwakamata, Bw. Bahman wa kampuni ya NAS na Wakala wa Kampuni ya Wallmark Bw. Samwel kwa kutaka kutoa bandarini magari makubwa aina ya semi tela 44 bila ya kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha wa kodi kutoka kwa viongozi wa juu Serikalini.

“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais Dkt. John Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.”

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 29, 2017) alipofanya ziara ya ghafla bandarini baada ya kupata taarifa za mfanyabiashara huyo aliyetaka kuutapeli uongozi wa TPA kutaka kutoa magari hayo yaliyoingizwa nchini mwaka 2015 kutoka nchini Uturuki.

Hatua hiyo imekuja baada ya Bw. Bahman wa kampuni ya NAS kutaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.

Amesema Serikali inasisitiza watu kufuata sheria na taratibu za nchi ikiwa ni pamoja na kulipakodi ipasavyo na inataka watendaji wake wafanye kazi bila ya kubugudhiwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kufuata sharia za nchi na kwamba Serikali haina ugomvi nao. Waziri Mkuu amefafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa magari hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kwenye kampuni Serin ya nchini Uturuki.

“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakin huyu bwana hajafanya hivyo”

Waziri Mkuu amesema kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo ni kinyume cha sheria na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.

Amesema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhohofisha mahusiano mazuri iliyopo kati ya Tanzania na Uturuki kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko hayo katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini Tanzania.

“Uturuki wanawaamini sana wafanyabiashara wa Tanzania sasa huu ujanjaunja uliotumika katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuyasajili magari haya bila ya kuwa na bill of lading halisi unajenga sura mbaya kwa wafanyabiashara wengine waaminifu na watiifu wa sheria nawaagiza TRA kuchukua hatua kwa wahusika, hatuwezi kupoteza mahusiano na nchi kwa sababu ya utapeli wa mfanyabiashara mmoja.”

Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa Mawakala wa Forodha kuhakikisha wanakuwa makini katika kazi zao na Serikali haitawavumilia wababaishaji kwani inasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Awali, Mkurugenzi wa Mkuu wa TPA, Mhandisi Deusdedit Kakoko alimueleza Waziri Mkuu kuwa pamoja na vitisho vya mfanyabiashara huyo kuwa wasipotekeleza matakwa yake watapata matatizo, lakini waliendelea kusimamia sheria na taratibu.

TPDC laendesha zoezi la Upimaji Afya kwa Wananchi wa Songo Songo

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuanzia tarehe 24/11/2017 hadi 25/11/2017 limeendesha zaoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali kwa wananchi wa Songo Songo ambao wamekuwa wakilazimika kusafiri zaidi ya masaa mawili kufuata huduma ya vipimo hivyo katika Hospitali ya Kilwa kivinje.

Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni Tanzu ya TPDC inayosimamia uendesheshaji na utunzaji wa Miundombinu ya Uchakataji na Usafirishaji wa Gesi Asilia inayoitwa GAS COMPANY (GASCO) Mhandisi Baltazari Mrosso wakati wa ufungaji wa zoezi hilo ameeleza kuwa ni wajibu wao kama Shirika kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za kijamii zenye lengo la kuboresha maisha ya Wananchi wa Songo Songo ambao pia ni tegemeo kubwa katika shughuli zinazofanywa na Shirika kuanzia kwenye uzalishaji wa gesi visimani, uchakataji kiwandani na usafirishaji.
Diwani wa Kata ya Songo Songo Mh. Said Mwinyi akifungua rasmi zoezi la upimaji kwa kukipatiwa huduma ya upimaji wa Shinikizo la Damu kutoka kwa Daktari Octavian Modest.

“Sisi kama Shirika la Umma ambalo limewekeza katika Kisiwa hiki katika shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia tunao wajibu wa kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa Songo Songo ili kuboresha maeneo mbalimbali ya huduma za kijamii kwa lengo la kuboresha maisha ya wananchi, kuboresha uhusiano na kuendelea vyema na shughuli za uzalishaji na uchakataji wa gesi asilia na hivyo leo hii tunahitimisha zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi wa Songo Songo pamoja na kukabidhi vifaa tiba vya upimaji wa ugonjwa wa Kisukari ambavyo hapo awali havikuwepo.” Alieleza Kaimu Meneja Mkuu GASCO.
Daktari wa TPDC, Octavian Modest akimtibu moja ya Wazee wa Kijiji cha Songo Songo waliojitokeza katika zoezi la upimaji wa Afya liloratibiwa na kufadhiliwa na TPDC.

Mhandisi Mrosso aliongezea kuwa utaratibu huu wa upimaji wa Afya ni endelevu na utakuwa unafanyika mara kwa mara pamoja na kuchangia kwenye ununuzi wa vifaa tiba mbavyo vinasabisha usufumbufu kwa wananchi wa Songo Songo kusafiri baharini kwa mwendo wa zaidi wa masaa mawili kufuata huduma za vipimo na tiba mbalimbali katika Hospitali ya Kilwa Kivinje pamoja na hayo alimuomba Mh. Diwani wa Kata ya Songo Songo kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhamasisha Wananchi kuondoa woga wa kupima afya zao.
Wahudumu wa Afya wakimsaidia Mmoja wa Wazee waliojitokeza kupima afya zao katika Zahanati ya Songo Songo.

Aidha Mh. Diwani ndugu Mh. Said Mwinyi wa Kata ya Songo Songo ameonyesha kufurahishwa na kitendo cha TPDC kutekeleza zoezi hilo kwa wananchi wa Songo Songo ambalo limeonyesha utayari wa TPDC katika kuhakikisha Kijiji cha Songo Songo kinaimarika katika Sekta ya Afya.

“Kwakweli TPDC mmetupenda wana Songo Songo kwa kutupatia huduma hii muhimu kwa ajili ya kujua afya zetu kitendo ambacho kinamuwezesha kila mmoja kujitambua hali yake, kujikinga na kujitunza na maradhi mbalimbali pamoja na kupata tiba sahihi kulingana na tatizo lililogundulika kama hali halisi ilivyo bado tuna upungufu wa vifaa tiba na leo tunshukuru TPDC kutupatia vifaa vya kupima ugonjwa wa Kisukari ambavyo hatujawahi kuwa navyo na tunaamini vingine hapo mbeleni mtatuletea ili kuhakikisha nasi ndugu zenu tunapata huduma bora ya afya” alieleza Mh. Diwani.
Baadhi ya Wananchi wa Songo Songo wakiwa kwenye foleni ya kusubiri kufanyiwa vipimo vya magonjwa mbalimbali katika Zahanati ya Kijiji cha Songo Songo Mkoani Lindi.

Aidha wakati wa ufunguzi wa huduma hiyo, akieleza nia ya zoezi hilo muhimu kwa wananchi, Meneja Mawaasiliano wa TPDC, Marie Msellemu amesema upo umihimu mkubwa wa kila Mtanzania kujua afya yake ili aweze kujikinga na maradhi mbalimbali, kudhibiti madhara ya maradhi aliyonayo, kuimairisha afya zetu na kuweza kulitumikia taifa kikamilifu.

“Sisi kama TPDC tunaona ni wajibu wetu kuhakikisha ndugu zetu wa Songo Songo ambao eneo lao ndilo gesi iligundulika kwa mara ya kwanza wanapata fursa ya kupima na kutambua afya zao ili waweze kuwa na nguvu na afya bora na hivyo kuwawezesha kutekeleza shughuli zao za kila siku na ndio maana TPDC tumeamua kuendesha zoezi hili muhimu kwa wananchi wa Songo Songo” Alieleza Bi. Msellemu.

Zoezi la upimaji wa Afya liliambatana na mashindano ya mpira wa miguu, mpira wa pete na utoaji wa hundi ya Shilingi 4,613,100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la Mwalimu wa Shule ya sekondari ya Songo Songo.

Mhariri wa zamani Mwananchi afariki dunia


Dar es Salaam. Mhariri wa zamani wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Abdallah Yakuti amefariki dunia.
Alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Hindu Mandal jijini Dar es Salaam tangu Jumatatu Novemba 27,2017.
Rashid, mtoto wa kwanza wa Yakuti akizungumza kwa niaba ya familia amesema mazishi yatafanyika kesho Alhamisi Novemba 30,2017 saa kumi jioni katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.
“Baba yetu alikuwa anasumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu lakini hali yake ilibadilika ghafla Jumatatu; tulimpeleka hospitali kwa matibabu lakini akafariki dunia. Msiba upo nyumbani kwa marehemu Mabibo na mipango ya mazishi inaendelea,” amesema.
Mbali na MCL, Yakuti alifanya kazi Idara ya Habari (Maelezo), Shirika la Habari Tanzania (Shihata), Daily News na New Habari Corporation.
Yakuti ameacha wajane wawili, watoto wanne na wajukuu wanne.