Monday, June 5

Sipati picha Chadema bila Ndesamburo



Mengi yamekwishasemwa kuhusu kifo cha Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo. Sifa zake nyingi zimetajwa, zikihusisha ni mcgangio kiasi gani alikuwa nao kwa chama hicho na kwa taifa kwa ujumla.
Pamoja na hayo yote, jambo ambalo wengi wanajiuliza ni baada ya kifo hicho cha ghafla cha mfadhili mkuu wa chama na mwana mikakati ya ushindi, Chadema mkoa wa Kilimanjaro itakuwaje bila yeye?
Mipango mingi ya kimkakati na kifedha ilimtegemea Ndesamburo kwa kiwango kikubwa. Alikuwa akirusha helkopta yake katika majimbo mbalimbali ya mkoa Kilimanjaro ili kutafuta ushindi kwa chama.
Ndesamburo aliyekuwa na kadi namba 10 ya uanachama wa Chadema, akiwa Mbunge wa Jimbo la Moshi Mjini kwa vipindi vitatu (2000-2015), alifadhili sehemu kubwa ya kampeni ya madiwani waliounda halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kipidi chote hicho.
Kwa maneno mengine, mtu anaweza kusema kwa Kilimanjaro, Ndesamburo ndio alikuwa Chadema na Chadema ilikuwa Ndesamburo, bila yeye chama kisingeweza kufurukuta dhidi ya CCM.
Aliyekuwa katibu wake wa nafasi ya ubunge kwa vipindi vyote vitatu ambaye pia ni Katibu wa Chadema mkoa Kilimanjaro, Basil Lema anasema itachukua muda kumpata mtu wa aina ya Ndesamburo.
Sifa ndani ya chama
Lema anasema kuna sifa kuu tano za Ndesamburo, ambazo inawezekana ikachukua muda mrefu kupata mtu wa kuzifikia na hivyo pengo lake kuiathiri sana Chadema. “Kikubwa sana ambacho kitaonekana ni kwamba Ndesamburo alikuwa ni mtu mwenye ushawishi mkubwa. Alipewa hata jina la Koffi Annan alipofanikiwa kusuluhisha mgogoro wa uongozi huko Rombo,” anasema.
“Kweli tumempoteza mtu aliyekuwa na uwezo wa kuzileta pande zinazokinzana mezani zikasikilizana. Lakini tumempoteza mtu mwenye nguvu ambaye akikuita unakwenda ukiwa na hofu.”
“Hofu kwa maana ya busara zake nyingi, hofu kwa maana ya umri wake mkubwa na hofu kwa maana ya sifa aliyonayo kwa jinsi alivyoijenga ngome imara ya Chadema,” anasema Lema na kuongeza:
“Unaenda ukiwa na hofu kuwa aliyekuita ndiye mwenye chama na amekifikisha hapo kilipo yeye mwenyewe. Hiyo hofu lazima ikupate unavyomfuata pale ofisini kwake Keys au nyumbani.”
“Pia hofu kutokana na nguvu yake ya kifedha kwamba yeye ni mfadhili mkuu wa chama. Ni mfadhili wetu binafsi.”
“Sasa anapokuita, umeitwa na mamlaka ya fedha pia.”
“Lazima uangalie amekuita mwenye pesa na hiyo ni nature (asili). Tunawaheshimu watu wenye pesa. Anapendwa sana na anaheshimiwa sana kwa hiyo akikuita unajua umeitwa na kipenzi cha watu.”
“Kwa hiyo watu watakushangaa sana kama unapambana na mtu anayeheshimika sana na mtu unique (wa kipekee) na mtu mwema. Wewe ndio unaonekana wa ajabu.”
“Pia alikuwa ni mwana mikakati ya ushindi, mimi nimekuwa katibu wake. Ningekuwa na sababu nyingi za kufikia juu kabisa kwenye hatima yangu ya kisiasa lakini nilibaki naye.”
“Nilikuwa navutwa mno kufanya kazi na mtu mwenye mipango na mikakati yenye akili sana. Ndesamburo ni mjanja ni mtu wa mikakati mno. Anapanga mikakati ya miaka 10 mbele na inakua.”
“Anapanga kuanzia mbinu, gharama na wahusika. Sasa hayupo tuna kazi ngumu. Tunahitaji mwana mikakati, tunahitaji msuluhishi sasa hayupo ni hatari kwetu. Na inawezekana chama kikateketea kwa kukosa msuluhishi,” anasema Lema ambaye mwaka 2015 alijitosa kumrithi Ndesamburo lakini akalazimika kuondoa jina lake baada ya kuombwa na Ndesamburo.
Nini kitainusuru Chadema
Katibu huyo anasema hakuna mtu binafsi ambaye ni mbadala wa Ndesamburo, kinachotakiwa ni chama kuheshimu katiba, kanuni na maadili.
“Kwa kuwa chama kilidekezwa kuanzia makao makuu kikijua kuna mbeleko ya kubeba mizigo, uchafu, uvunjaji wa katiba kikijua yupo mbebaji,” anasema Lema na kuongeza:
“Basi itabidi chama kianze kuwa mtiifu sana kwa katiba, kanuni na maadili kushughulikia wakosaji mara moja. Kisiendelee kuamini yuko Ndesamburo kwamba atamaliza tatizo la Kilimanjaro.”
“Hayupo tena. Mbadala wa Ndesamburo ni katiba, maadili na kanuni za chama. Ugonjwa ulioingia kwenye chama unaopambana na mikakati ni tamaa ya madaraka.”
“Ndesamburo ameondoka, kama chama hakitarithi mila za kuenzi na kuheshimu wana mikakati lazima watu wenye tamaa ya madaraka wajenge ufalme wao kwa kuwa hakuna mtu wa kuwatisha tena.”
“Matokeo yake chama kitapasuka vipande vipande, migogoro itakuwa mikubwa na itaanzishwa na wenye fursa ya uongozi wakitengeneza ufalme wao.”
CCM waitabiria Chadema shida
Sio wana Chadema pekee wanaoona kivuli cha Ndesamburio, washindani wao CCM pia wanaona kuondoka kwa Ndesamburo kunaweza kukiteteresha chama hicho katika Mkoa Kilimanjaro kutokana na kumpoteza mtu mwenye ushawishi wa usuluhishi.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Moshi Mjini, Priscus Tarimo anasema inahitajika kazi ya ziada kuwarudisha wanachama na viongozi katika kundi moja, kama kweli wanataka Chadema ibaki imara.
“Kwa kweli itakuwa ni ngumu maana ushawishi wake haukuwa ndani ya chama tu, bali zaidi nje ya chama. Watu walikuwa wanamkubali, mzee mtu mzima (Ndesamburo) akisema kitu anamaanisha,” anasema Tarimo
Anaongeza, “Kwa hiyo heshima ya Chadema Moshi ilikuwa inamtegemea sana Ndesamburo kama mtu, si chama. Hapa ndipo utagundua umuhimu wa yule mzee licha ya hapa mwishoni kuanza kubeza kazi yake.”
“Ukiangalia katika vipindi vya nyuma Rais anashinda wa CCM na Baraza la Madiwani linakuwa la CCM lakini alipoingia kuwa mbunge ndio akabadili, baraza likawa la Chadema.”
“Heshima yake ilikuwa yeye kwanza kabla ya chama na hiyo ndiyo ilisababisha Chadema ikawa na nguvu hapa Moshi. Kwa kweli bila yeye Chadema itakuwa na kazi ya kufanya,” anasisitiza Tarimo.
Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Chadema Moshi mjini hawakurudi wamoja, kulikuwapo kundi linalomtii Ndesamburo na jingine linalomuunga mkono mbunge, Jaffar Michael.
Lakini kitendo cha baadhi ya wabunge akiwamo Anthony Komu wa Moshi Vijijini, kumpinga waziwazi Ndesamburo asigombea uenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini kwa sababu ya umri, nacho kilichochea zaidi mgogoro.
Nguvu ya Ndesamburo
Kada huyo maarufu kwa jina la ‘Ndesa Pesa’ kutokana na kumiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya nchi, ndiye anayetajwa kukijenga chama hicho mkoani Kilimanjaro na kuwa na nguvu kubwa.
Katika Uchaguzi Mkuu 2015 ambapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa alipeperusha bendera ya Ukawa katika nafasi ya urais, Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa iliyofanya vizuri.
Akiwa ni mwenyekiti wa mkoa, Ndesamburo pamoja na viongozi wenzake, walimwezesha Lowassa kupata kura 266,636 dhidi ya 167,691 alizopata Rais John Magufuli na kuzoa majimbo saba kati ya tisa.
Si hivyo tu, ni chini ya utawala wake, Ndesamburo aliiwezesha Chadema kupata wabunge tisa, madiwani 145, vitongoji 910, vijiji 472 na mitaa 38 katika uchaguzi wa mitaa 2014 na Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Lakini kubwa zaidi, katika uchaguzi huo, Chadema iliibuka mshindi katika majimbo ya Hai linaloongozwa na Freeman Mbowe na Rombo linaloongozwa na Joseph Selasini.
Mbali na majimbo hayo, Chadema ilishinda katika majimbo ya Same Mashariki kwa Naghenjwa Kaboyoka; Dk Godwin Mollel wa Siha na Anthony Komu (Moshi Vijijini).
Kubwa zaidi ambalo bado litabaki katika vichwa vya wengi, ni kitendo chake cha kumtangaza Jaffar Michael kama mrithi wake na akampigania hadi akashinda katika uchaguzi huo wa 2015.
CCM wakati huo ikimtegemea mfanyabiashara tajiri nchini, Davis Mosha iliamini kwa kutumia mwanya huo wa Ndesamburo kustaafu ubunge ingeweza kushinda lakini haikuwa hivyo.
Kwa hiyo, kuondoka kwa Ndesamburo hakika kutaifanya Chadema ifanye kazi ya ziada na kuja na mikakati mipya ya kuwaaaminisha wananchi kuwa bila Ndesamburo mambo yataenda kama uilivyokuwa.
Meya wa Manispaa ya Moshi (Chadema), Ray Mboya alisema Ndesamburo alikuwa ni baba wa Jimbo la Moshi mjini na kifo chake kimewashtua wengi kwa kuwa aliamka asubuhi akiwa mzima wa afya.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa alisema chama kimepoteza mtu aliyekuwa na mchango mkubwa.
“Alikuwa na mchango mkubwa ndani ya chama chetu. Kwa muda mrefu amekuwa akikisaidia chama. Wakati mwingine tumekuwa tukitumia chopa yake,” alisema.
“Pengo kubwa sana kwa sisi, busara zake, mawazo yake kwa kweli tuta-miss sana. Lakini kwa sababu wote tutapita njia hiyo hiyo, hatuna la kufanya.”
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Martha Mlata alisema Ndesamburo alikuwa mzalendo wa kweli na kama kuna jambo ambalo wapinzani wanatakiwa kujifunza ni yale mazuri ambayo amefanya wakati wa uhai wake.
“Nakumbuka wakati wote alipokuwa mbunge hajawahi kusikika akikashifu wala kusema maneno makali bungeni. Kama alikuwa anataka kushauri jambo, alitumia maneno ya hekima na busara. Wapinzani wakitaka kuheshimika wafuate mazuri aliyoyafanya mzee Ndesamburo. ‘Tulimmisi’ bungeni lakini tutaendelea kumkumbuka sana kwa hekima na busara zake,” alisema.
Mbali na wanasiasa, Ndesamburo alijenga jina hata nje ya chama kama anavyoeleza Askofu wa Kanisa la Victorious, Dk Sixbert Mkelemi kuwa kanisa limepokea kwa masikitiko kifo chake kwa kuwa alikuwa mmoja wa wadhamini wa Umoja wa Kongamano la Makanisa Afrika.

KWAHERI MZEE NDESAMBURO





Wafanyakazi wa Manji walipa faini kuikwepa jela



Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana iliwahukumu wafanyakazi 16 wa Kampuni ya Quality Group Ltd, inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu, Yusuph Manji kulipa faini ya Shilingi laki tano katika kila kosa linalowakabili ama kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela.
Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mfawidhi, Cyprian Mkeha alisema mshtakiwa wa kwanza hadi wa 14 wanakabiliwa na mashtaka matatu hivyo katika kila kosa, kila mmoja atatoa jumla ya faini ya Sh1.5 milioni.
Iwapo wangeshindwa, kila mshtakiwa angetumikia kifungo cha miaka mitatu jela katika kila kosa hivyo kufanya watumikie kifungo cha miaka tisa jela.
Kwa upande wa washtakiwa 15 na 16 ambao ni Meneja mradi Jose Kiran na Katibu wake, Prakash Bhatt walihukumiwa kulipa faini ya Shilingi laki tano au kwenda jela miaka mitatu.
Kiran na Bhatt, wao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma za kukiuka amri ya Ofisa Uhamiaji na kujaribu kutoroka. Hata hivyo, washtakiwa hao wamekwepa kifungo kwa kulipa faini hiyo.
Kiran na Bhatt wanadaiwa kuwa Februari 20, 2017, wakiwa ni waajiriwa wa Quality Group Ltd, walimzuia Ofisa wa Uhamiaji kufanya kazi zake na kwamba, walikataa kuripoti katika ofisi za Uhamiaji zilizopo jijini Dar es Salaam kwa kujaribu kutoroka nchini kwa kupitia mpaka wa Horohoro.
Washtakiwa 14 ambao ni washauri, Jagadish Mamidu (29), Niladri Maiti (41), Divakar Rajasekaran (37), Mhasibu, Mohammad Taher Shaikh (44), mshauri Bijenda Kumar (43) na mshauri Prasoon Kumar Mallik(46).
Wengine ni mshauri Nipun Dinbadhu Bhatt (32), Meneja Msaidizi, Pintu Kumar (28), mshauri Anuj Agarwal (46), mshauri Varun Boloor (34), mshauri Arun Kumar Kateel (46), mshauri Avinash Chandratiwari (33) na mshauri Vikram Sankhala (50), wamefanikiwa kulipa faini na kukwepa vifungo hivyo na waliambiwa ili waweze kuendelea kuishi Tanzania lazima wafuate sheria za nchi.
Wakili wa Serikali wa washtakiwa hao, Hudson Ndusyepo kabla ya hukumu kutolewa, aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza hadi wa 14 hawakuwa na nia mbaya ya kutenda makosa hayo.
Alidai kuwa walikutana na Ofisa wa Uhamiaji wakamwambia wanahitaji kuongeza muda wa viza za kufanya kazi na wakamkabidhi hati zao za kusafiria na baadae aliwarejeshea zikiwa na viza ndani.
Aliendelea kudai kuwa, wao waliamini viza hizo zilipatikana kwa halali na malipo yalifanyika na fedha kuingia serikalini kupitia mpaka wa Tunduma na risiti walipata.
Alidai baada ya kukamatwa iligundulika zilipatikana kinyume cha sheria.
Alikiri hilo ni kosa lao la kwanza na akaomba Mahakama iwasamehe, wapewe adhabu ndogo na nafasi nyingine ya kuwapo nchini.
Mwendesha Mashtaka wa Idara ya Uhamiaji, Method Kagoma alidai washtakiwa waliingia nchini mwishoni mwa 2016 na wakapewa viza za miezi mitatu za kufanya kazi. 


Mdee, Bulaya ‘out’ mpaka bunge lijalo la bajeti


Halima Mdee na Esther Bulaya wamehukumiwa kutohudhuria vikao vyote vya bunge linaloendelea mpaka mkutano ujao wa Bunge la Bajeti ya 2018/19.
Hukumu hiyo imeungwa mkono na wabunge wengi waliopitisha azimio hilo.
Mapema leo, Jumatatu Kamati ya Maadili  ilisema Bulaya na Mdee wamemaliza adhabu za kawaida zilizopo kwenye kanuni za bunge.
Hata hivyo, Bunge liliendelea  kujadili makosa ya wabunge hao wa Bunda na Kawe.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, George Mkuchika aliliomba Bunge kujadili adhabu inayostahili kulingana na makosa yao.
Kanuni inasema, mbunge anayefanya kosa la kwanza anaweza akazuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 10 na atayakosea kwa mara ya pili anaweza kuzuiwa kuhudhuria vikao visivyozidi 20.