Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo katika jimbo la Arusha Mjini Estomih Mallah amefariki dunia usiku wa kuamkia leo huko KCMC, Moshi alikohamishiwa jana kwa matibabu zaidi.
Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Shaaban Mambo amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema alipigiwa simu alfajiri leo na mtoto wa kiume wa marehemu kumweleza kuwa baba yao alikuwa amefariki dunia.
Taarifa za awali zinasema kuwa marehemu alianza kuugua Jumanne baada ya mkutano uliohutubiwa na mgombea urais wa chama hicho, Anna Mghwira uliofanyika eneo la Ngaramtoni.
Mambo aliiambia Mwananchi Digital kuwa marehemu alipelekwa hospitali ya Mtakatifu Thomas iliyopo jijini Arusha alikolazwa hadi jana alipohamishiwa KCMC kwa matibabu zaidi ambako mauti yamemkuta.
Mambo alisema chama chake kimeshaanza vikao kujadili taratibu za mazishi na kwamba taarifa zaidi zitatolewa baada ya kujadiliana na familia.
Alisema Mallah aliyehudumu pia kama Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi ameacha pengo kubwa kutokana na nafasi yake iliyomfanya awe katika utendaji wa shughuli za kila siku za chama hicho.
Mwaka 2010 aligombea na kushinda nafasi ya udiwani katika kata ya Kimandolu kupitia Chadema na baadaye kuchaguliwa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha katika uchaguzi uliozua mgogoro baina ya CCM na Chadema.
Mwaka 2011 Mallah na madiwani wengine watatu (John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni) walivuliwa uanachama wa Chadema katika kile kilichoonekana kushamiri kwa mgogoro wa kisiasa ndani ya chama hususani katika kuwania nafasi ya umeya wa halmashauri ya jiji hilo.
Baadaye alitua ACT-Wazalendo ambako alipitishwa na chama hicho kuwania ubunge wa Arusha Mjini katika uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu akipambana na mbunge anayetetea kiti chake, Godbless Lema wa Chadema na Philemon Mollel wa CCM.