Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius
Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo
chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili
wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa
ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.
FAMILIA ya msanii Hussein Ramadhani Mkiety (Sharo
Milionea) aliyekufa katika ajali wilayani Muheza wiki iliyopita imedai kuwa
haiamini kwamba kifo cha mtoto huyo kilitokana na ajali, hivyo kulitaka Jeshi
la Polisi kufanya uchunguzi wa kina kubaini ukweli.
Mjomba wa marehemu , Mohamed Msenga alisema jana kwamba
familia imekuwa na shaka juu ya mazingira ya kifo hicho baada ya kurejeshewa
nguo za msanii huyo zilizokuwa zimeibwa baada ya ajali lakini hazikuwa na damu.
Msenga alisema muda mfupi baada ya mama mzazi wa Marehemu
Zaina Mwaimu Mkiety (54), kuitwa polisi na kukabidhiwa vitu mbalimbali zikiwamo nguo ambazo marehemu
alikuwa amevaa siku ya ajali hawakuona hata alama ya damu jambo ambalo
liliwashangaza.
Alisema shaka hiyo ilianzia katika eneo ambalo ajali hiyo
ilitokea akisema walipofika na kuonyeshwa mahala alipokuwa ameangukia,
hawakuona damu jambo ambalo liliwatia shaka.
Alisema begi la nguo za msanii huyo lilikuwa na udongo
mwingi likionyesha kwamba walioiba walikuwa wamelifukia kabla ya kusalimisha
lakini hakuna damu zilizoonekana.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Teule Muheza, Dk Julius
Mjema aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Sharo Milionea alisema sababu ya kifo
chake ni kichwa kupondeka.
“Mimi ndiye niliyefanyia ‘postmoterm’ (uchunguzi), mwili
wa Sharo Milionea, ni kwamba kichwa kilikuwa kimepondeka huku mifupa ya kichwa
ikiwa imepondeka pia,” alisema Dk Mjema.
Kuhusu madai ya nguo kutokuwa na damu, alisema marehemu
alipata mpasuko wa ndani kwa ndani na siyo wa
nje, ndiyo maana alipofikishwa chumba cha maiti damu zilionekana zikiwa
zimeganda masikioni.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga,
Constantine Massawe alipoulizwa kuhusu madai hayo ya familia alisema: “Hiyo ni taarifa ambayo jeshi la
polisi litaifanyia kazi kwa kuingia kwa kina katika kuchunguza ili kuridhisha
pande zote.”
Mama yake alia kukosa mjukuu
Katika hatua nyingine, mama mzazi wa msanii huyo amesema
kutoachiwa mjukuu na tarehe za mwisho wa mwezi ni alama ambazo zitasababisha
awe akimkumbuka mwanaye huyo milele. Akizungumza nyumbani kwake, katika
Kitongoji cha Jibandeni Kijiji cha Lusanga wilayani hapa alisema kila ulipokuwa
ukifikia mwisho wa mwezi ulikuwa ni muda wake wa neema kwani Sharo Milionea
alimtumia fedha za matumizi yake binafsi pamoja na familia nzima nyumbani hapo.
“Pamoja na kwamba kila mara alikuwa akinitumia fedha za
kutatua shida zangu mbalimbali nilizokuwa nikimweleza lakini kila mwisho wa
mwezi alikuwa akihakikisha anatuma fungu la matumizi yangu na ndugu zake hapa
nyumbani,” alisema mama huyo. Alisema mwisho wa mwezi itakuwa ni alama ya
kudumu ya kumbukumbu ya mwanawe kwa sababu ni wakati ambao alikuwa akimtumia
fedha za matumizi yake pamoja na familia nzima.
Kuhusu mjukuu alisema: “Sharo ni mwanangu wa pekee wa
kiume, amekufa bila kuniachia mjukuu.. hii inaniuma sana lakini namshukuru
Mungu kwani amechukua kiumbe chake na ndiye ajuaye siri iliyofichika mbele
yangu,” alisema.
Alisema hadi alipofariki hakuwahi kumdokeza juu ya kuwa
na mtoto wala kumpa mimba msichana yeyote... “Unajua Sharo Milionea alizaliwa
pacha na mwenzake Hassan lakini mwenzake alifariki dunia siku tano baada ya
kuzaliwa kwa hiyo katika kizazi changu mwanangu pekee wa kiume alikuwa Sharo
Milionea ambaye nilitumaini kwamba angeniletea wajukuu,” alisema Zaina.
Alisema Sharo Milionea amekufa kabla hajatekeleza ndoto
yake ya kumjengea nyumba ya kisasa pamoja na kuweka miradi ya kuboresha maisha
yake azma ambayo aliiweka mwezi mmoja kabla ya kupata ajali iliyotoa uhai wake.
Atoa ya moyoni kwa walioshiriki msiba
Zaina alitoa shukrani za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete na
mkewe, Salma kwa kutuma ujumbe maalumu pamoja na rambirambi kutokana na msiba
wa mwanaye huyo. Pia alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu, wasanii,
waandishi wa habari na kampuni mbalimbali zilizoshiriki pamoja na kutuma salamu
za rambirambi.