Tuesday, June 13

UFAFANUZI MUHIMU KUHUSU USAJILI WA ACCACIA.



NA   BASHIR  YAKUB - 

Kwa kutumia kigezo cha usajili, Tanzania tunazo aina kuu mbili za  kampuni. Kampuni za ndani(Local companies) na kampuni za kigeni ( foreign companies).

Kampuni za ndani ni zile  zote zilizoanzishwa  hapa nchini na kusajiliwa hapa nchini. Hata kama wanahisa wake wote ni raia wa kigeni kwasababu tu ya kuanzishwa hapa na kusajiliwa hapa zinakuwa ni kampuni  za ndani.

Kampuni ya kigeni ni ile iliyoanzishwa na kusajiliwa nje ya Tanzania lakini ikaanzisha ofisi/biashara/tawi hapa Tanzania. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni kifungu cha 433 kinasema hivyo. Kampuni kama imeanzishwa nje hata kama wanahisa wake wote ni Watanzania, hapa kwetu hiyo bado ni kampuni ya kigeni.

Kampuni ya ndani inaposajiliwa hupatiwa cheti cha usajili kiitwacho "Certificate of Incorporation" kwa mujibu wa kifungu cha 15(2) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya ndani inapopata cheti hiki basi usajili wake huwa umekamilika na inatambulika rasmi kama kampuni ya ndani.

Kampuni ya kigeni inaposajiliwa hapa Tanzania hupatiwa cheti kiitwacho "Certificate of  Compliance" kwa mujibu wa kifungu cha 435(1) Sheria ya Makampuni. Kampuni ya kigeni inapopata cheti hiki basi  usajili wake huwa umekamilika na hutambulika rasmi kama kampuni ya kigeni.

Acacia ni kampuni ya kigeni. Kwa maana kuwa ilianzishwa nje ya Tanzania na kufungua shughuli zake hapa nchini. Kwa hiyo ili ihesabike imesajiliwa Tanzania ilitakiwa kuwa na cheti kiitwacho"Certificate of Compliance". Kutokuwa na cheti hiki maana yake ni kuwa haijasajiliwa Tanzania na haitambuliki.

Nimesikia mjadala BBC SWAHILI leo wanaojadili wakijiuliza inawezekanaje kampuni kubwa kama hii ikafanya biashara bila usajili. Watanzania wengi pia wanajiuliza swali hili.

Jibu lake ni hili. Acacia ni kampuni tanzu(Subsidiary  Company) ya Barrick. Kampuni inakuwa tanzu pale ambapo zaidi ya nusu ya hisa zake zinamilikiwa na kampuni nyingine. Ile inayomiliki huitwa "holding company" na inayomilikiwa huitwa "subsidiary company". Kwahiyo  Barick ni " holding" wakati Acacia ni "subsidiary".

Barrick inamiliki hisa za Acacia 63.9%. Kwa kusema hivi maana yake Barrick ndiye mwenye Acacia. Hata hivyo kwa mujibu wa sheria hizi zinahesabika kampuni mbili tofauti na kila moja inabeba wajibu na hatia zake yenyewe(its own responsibility& liability).

Basi kumbe kilichotokea ni kuwa Acacia walikuwa wakifanya biashara kwa jina la Acacia lakini wakibebwa na mgongo wa  Barrick. Walijificha hapa na wakaweza kuishi bila usajili wa kwao kama wao. Walijibeba kwenye usajili wa Barrick.

Barrick wao wanao usajili na wanayo " Certificate of Compliance" ya kwao ambayo tayari wameitoa hadharani. Kwakuwa haya ni makampuni mawili tofauti kila moja inatakiwa kuwa na cheti chake  kwa mujibu wa kifungu cha 487 Sheria ya Makampuni na kutokufanya hivyo ni kosa kabisa. Kwa hiyo hivi ndivyo ilivyowezekana kampuni hii kufanya biashara bila usajili miaka hii yote.

Adhabu ya kosa kama hilo ni kifungo jela. Sheria Na. 12 Sheria ya Makampuni iliyofanyiwa Marekebisho mwaka 2002, kifungu cha 472 kinasema hivyo.

MWANDISHI   WA   MAKALA  HAYA   NI   MWANASHERIA  NA  MSHAURI   WA  SHERIA  KUPITIA  GAZETI   LA  JAMHURI   KILA   JUMANNE.  0784482959,  0714047241 email bashiryakub@ymail.com

WILAYA ZA MUFINDI NA KILOLO MKOANI IRINGA ZATUMIA TEHAMA KUBORESHA UTOAJI WA HUDUMA KWA UMMA

Je unajua jinsi TEHAMA inavyoboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma katika Mkoa wa Iringa hasa Wilaya ya Kilolo na Mufindi. Usikose kuangalia kipindi hiki.

Nani alifanya nini mikataba ya madini

Wakazi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro wakiwa kwenye bar iliyopo katika eneo la Plaza wakitazama matangazo ya moja kwa moja kwenye luninga kuhusu tukio la Rais John Magufuli kupokea ripoti ya kamati ya pili ya uchunguzi wa madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi lililofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. 
Ripoti ya kamati ya pili ya makinikia iliyowasilishwa jana imeibuka na majina ya vigogo ikieleza jinsi walivyohusika kuingia mikataba mikubwa ya migodi ya madini na kulitia hasara Taifa.
Kamati hiyo iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na mchanga wenye madini unaosafirishwa nje ya nchi yakiwamo makontena 277 imependekeza vigogo hao wachukuliwe hatua za kisheria.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro akiwasilisha ripoti kwa Rais Magufuli mbele ya viongozi wengine wakuu wa Serikali, Ikulu jijini Dar es Salaam jana, aliwataja Dk Abdallah Kigoda (marehemu), Daniel Yona, Nazir Karamagi, William Ngeleja na Profesa Sospeter Muhongo kuhusika
Hao wote wamewahi kushika nafasi ya Waziri wa Nishati na Madini kwa vipindi tofauti.
Wengine ni wanasheria wakuu wa zamani na manaibu; Andrew Chenge, Johnson Mwanyika, Felix Mrema na Sazi Salula.
Mbali na hao pia wamo makamishina wa madini na wakuu wa idara ya mikataba wa zamani; Paulo Masanja, Ally Samaje Dk Dalaly Kafumu, Maria Ndossi na Julius Malaba.
Kamati ya Profesa Osoro imeitaka Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba, makamishna wa madini na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia imetaka hatua zichukuliwe kwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.
Ndani ya ripoti
Katika ripoti hiyo, Profesa Osoro ameeleza jinsi Dk Kigoda alipokuwa Waziri wa Nishati na Madini alivyoingia mkataba na mgodi wa Bulyanhulu Gold Mines Ltd (Kahama Mine Corporation Limited) ambapo kwa jitihada kubwa alifanikiwa kujadiliana na kampuni hiyo na kuiwezesha Serikali kupata asilimia 15 ya hisa katika kampuni za uchimbaji.
“Hata hivyo, mkataba huo ulifanyiwa marekebisho Juni, 1999 na kusainiwa na Waziri wa Nishati na Madini aliyefuata, Dk Abdallah Kigoda. Marekebisho hayo yaliondoa asilimia 10 ya hisa ambazo Serikali ilikuwa inamiliki na kubakiza asilimia tano tu,” alisema.
Alisema marekebisho mengine katika mkataba huohuo yalifanyika Oktoba, 1999 ikiwa ni miezi minne tangu yale ya awali yafanyike.
“Marekebisho haya ya pili pia yalitiwa saini na Dk Abdallah Kigoda, ambayo yaliondoa asilimia tano ya hisa za Serikali zilizokuwa zimebakia na hivyo Serikali kubaki bila hisa yoyote.”
Profesa Osoro alisema katika marekebisho hayo, Serikali ilikubali kulipwa Dola 5 milioni za Marekani ikiwa ni malipo ya mauzo ya hisa zake.
Vilvile, Serikali ilikubali kuendelea kulipwa kiasi cha Dola 200,000 za Marekani kila mwaka.
Hata hivyo, alisema kamati yake haikuweza kupata uthibitisho wa kufanyika kwa malipo ya jumla ya Dola 6,800,000 za Marekani.
“Kamati imeona kwamba marekebisho hayo ya mkataba yaliyofanywa na Mheshimiwa Dk Abdallah Kigoda hayakuwa na masilahi kwa Taifa kwani Serikali ilipoteza haki ya umiliki wa hisa na kuinyima mapato kutokana na gawio,” alisema Profesa Osoro.
Mlolongo wa hatua haukuishia kwa waziri huyo ambaye Rais Magufuli alisema marehemu tu ndio hawatachukuliwa hatua, pia ulienda kwa mawaziri wengine Yona na Karamagi katika kampuni ya Pangea Gold Mine.
Profesa Osoro alisema kampuni hyo ina mikataba miwili ya uchimbaji madini na wa kwanza ulisainiwa Desemba 2003 na Yona akiwa Waziri wa Nishati na Madini na wa pili ulisainiwa na Karamagi akiwa waziri wa wizara hiyo.
“Katika mikataba hii yote Serikali haina hisa yoyote katika kampuni na pia mkataba huu unatoa nafuu kubwa sana za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato,” alisema Profesa Osoro.
Yona aliingia tena kwenye mkataba wa kampuni ya North Mara Gold Mine ambao aliusaini Juni 1999 akiwa waziri wa wizara hiyo na baadaye marekebisho ya mkataba huo yalifanywa mwaka 2007 na Karamagi.
“Katika mkataba huo Serikali haina hisa yoyote katika kampuni. Aidha katika mkataba wa awali uliotiwa saini na Yona, Serikali ilitoa nafuu ya asilimia 15 ya nyongeza ya mtaji wa kampuni na kuifanya kampuni hiyo iwe inajilipa kwanza ili kurudisha mtaji wake na asilimia 15 iliyopewa na Serikali na hivyo kusababisha kampuni kutangaza hasara katika biashara kila mwaka. Jambo hilo limekuwa linaikosesha Serikali kodi ya mapato,” alisema.
Mwenyekiti huyo wa kamati aliongeza kuwa, wamebaini kwamba marekebisho yaliyofanyika mwaka 2007 kuondoa nafuu ya asilimia 15, bado malimbikizo ya hasara kutokana na nafuu ya kodi iliyokuwa imetolewa na Serikali iliendelea kudaiwa na kampuni hiyo. Haikuishia hapo katika mkataba wa kampuni ya Geita Gold Mine (AngloGold Ashanti) uliosainiwa na Dk Kigoda akiwa waziri, Serikali haikupata hisa yoyote na pia mkataba huo unatoa nafuu mbalimbali za kodi kwa kampuni, jambo ambalo linaikosesha Serikali kodi nyingi na mapato. “Mikataba ya uchimbaji madini inaeleza kuwa inaongeza na kurekebisha masharti yaliyomo katika leseni za uchimbaji madini,” alisema.
Alisema kuwa kamati inaona kuwa masharti ya aina hiyo ni batili kisheria kwa kuwa waziri hawezi kurekebisha masharti ya leseni yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria na kanuni kupitia vifungu vya mkataba wa uchimbaji wa madini.
Profesa Osoro alisema kamati imebaini kuwa kumekuwapo na uongezaji wa muda wa leseni wa maeneo ya uchimbaji madini kinyume cha sheria na bila kuzingatia masilahi ya Taifa.
“Kwa mfano, kuongeza muda wa leseni na maeneo ya uchimbaji uliofanywa na Ngeleja na Profesa Muhongo, kwa kampuni za North Mara Gold Mines Limited na Pangea Minerals Limited. Pia leseni mbalimbali zilizotolewa na Kamishna Paulo Masanja, Kamishna Dalaly P. Kafumu na Kaimu Kamishna Ally B. Samaje,” alisema mwenyekiti huyo.
Alisema katika kipindi hicho washauri wakuu wa Serikali kwa masuala ya kisheria walikuwa ni pamoja na Chenge, Mwanyika na manaibu wanasheria wakuu ambao ni Mrema na Salula na wakuu wa idara ya mikataba, Maria Ndossi na Julius Malaba.
Dk Kafumu Ngeleja wazungumza
Dk Kafumu ambaye ni mbunge wa Igunga akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema yuko tayari kuhojiwa na vyombo vitakavyomhitaji. “Nisingependa kuzungumza lolote kuhusu mapendekezo hayo, nitakuwa ninazungumza kabla ya kuhojiwa na Serikali, kwani ni mmoja kati ya waliotajwa, nitakuwa tayari kuhojiwa kwa sababu ni maagizo ya Rais,” alisema Dk Kafumu.
Kwa upande wake, Ngeleja alisema hawezi kuzungumzia agizo la Rais Magufuli la kuhojiwa na vyombo vya usalama kutokana na kuhusika kwake katika mikataba ya madini. Hata hivyo alitaja uzembe wa usimamizi wa sheria kuwa ndiyo uliolifikisha Taifa hapo kwa kuwa sheria zilizopo ni nzuri, lakini hazisimamiwi ipasavayo.
“Kuhusu kuhojiwa au kuwajibika sina neno la kusema lakini nampongeza sana kwa moyo wa dhati Mheshimiwa Rais maana amezungumza kwa hisia na uzalendo kabisa kuhusu tunachostahili kupata badala ya tunachopata,” alisema Ngeleja ambaye pia mbunge wa Sengerema.
Hata hivyo, alikiri kuwa mikataba mingi iliyopitishwa siyo mizuri kwa kuwa inawanyonya Watanzania ambao wameshindwa kupitia sheria mpya (ya madini ya mwaka 2010) kuifanyia kazi.
“Kifungu cha 11 pia kinachosema mikataba yote ipelekwe bungeni baada ya miaka mitano na kifungu cha 10 kinasema Serikali ishiriki kimkakati kwenye migodi, lakini usimamizi wake ndiyo shida,” alisema Ngeleja.
Kuhusu mchanga kusafirishwa nje ya nchi, alisema walishaliona jambo hilo mapema lakini wakabainisha kuwa mashine za kufanya kazi hiyo zina gharama kubwa zaidi hivyo kuhitaji ubia katika ujenzi baina ya Serikali na sekta binafsi.
Wakati Ngeleja akisema hayo, Chenge hakutaka kuzungumza na waandishi habari waliomfuata mara baada ya kuahirishwa kikao cha Bunge jana. “Siongei na watu,” ndiyo maneno pekee aliyoyasema mbunge huyo mkongwe wa Bariadi Magharibi.

IPTL, kaa la moto lililoteketeza vigogo kwa miaka 20


Sakata la mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) limezuka tena hivi karibuni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kutoa tangazo la kuongeza muda wa leseni ya kampuni hiyo hivi karibuni.
Kashfa ya mkataba wa IPTL uliosainiwa mwaka 1995 imekuwa ikigharimu madaraka ya baadhi ya viongozi kila inapoibuka na hivi karibuni imesababisha Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlagosi kusimamiswa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kashfa hii iliyozalisha kashfa nyingine ya Akaunti ya Tegeta Escrow pia ilisababisha kuvuliwa madaraka kwa mawaziri wa awamu ya nne ambao ni aliyekuwa Waziri Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, huku baadhi ya watendaji wa Serikali na wanasiasa wakiitwa kwenye Tume ya Kijaji kuhojiwa kwa mgawo walioupata.
Chimbuko la IPTL
Mwaka 1994 kulitokea tatizo kubwa la umeme, hivyo Serikali ilitafuta suluhisho la dharura na la kudumu. Mwaka huo, aliyekuwa Waziri wa Mipango marehemu Horace Kolimba alitembelea nchini Malaysia na kuzungumza na wawekezaji katika sekta ya umeme nchini humo na kuwaomba waje nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza ili kupunguza tatizo la umeme.
Agosti 19, 2014, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mechmar, inayomiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL, Datuk Baharuden Majid, aliongoza ujumbe mzito kutoka Malaysia kuja kuzungumza na Serikali ya Tanzania.
Walioshiriki katika mazungumzo hayo kwa upande wa Tanzania walikuwa ni pamoja na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa wakati huo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Simon Mhaville, Kamishna wa Nishati Msaidizi, Ester Masunzu na Dk Juma Ngasongwa ambaye alikuwa msaidizi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi wa mambo ya uchumi.
Septemba 1994, Mkataba wa Maelewano (MOU) ulifikiwa, licha ya tahadhari kutoka kwa washauri wa Tanesco ambao ni kampuni za Acres (Canada) na Hunton and Williams (Uingereza), kwamba uwekezaji huo ulikuwa ni janga kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa Taifa.
Kampuni hiyo ambayo wamiliki wake ni Mechmar ya Malaysia mwenye asilimia 70 na VIP ya Tanzania yenye asilimia 30 ilisaini mkataba wa miaka 20 (1995-2015) na Serikali ya Tanzania (Tanesco) ambapo kwa mujibu wa mkataba huo endapo kutatokea shauri lolote, uamuzi wa mwisho utatolewa na baraza la usuluhishi la migogoro ya kiuwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes-ICSID).
Chini ya mkataba huo, Tanesco ilitakiwa kuilipa IPTL Dola 3.6 milioni sawa na Sh7.92 bilioni kwa mwezi kama ada ya huduma za mtambo.
Juu ya malipo hayo, Tanesco pia inalipa senti 13 (dola) kwa kila uniti ya umeme (sawa na kilowati moja) kwa kuendesha mtambo kwa nusu ya uwezo wake kwa mwezi.
Mikosi yaanza
Kosa la kwanza la IPTL lilikuwa ni kutokamilisha mradi wake mwaka 1995 kwenye kipindi cha dharura na badala yake ikakamilisha mwaka 1998.
Hivyo mwaka 1998 Tanesco ilifungua shauri ICSID ikiilalamikia IPTL kwa kukuza gharama za uwekezaji na hivyo kukuza gharama za umeme.
Mwaka 2001 uamuzi wa ICSID ukatoka ikabainika ni kweli IPTL ilikuza gharama kwa kiasi cha Dola 27milioni.
Mwaka 2002 IPTL ikaanza kuiuzia umeme Tanesco lakini ilipofika mwaka 2004 ikabainika kuwa mwaka 2004 IPTL ilidanganya kuhusu mtaji.
Awali IPTL ilisema asilimia 30 ya mtaji ilikuwa nao kama ‘equity’ sawa na Dola 36 milioni na kwamba asilimia 70 ilikopa. Lakini baada ya ukaguzi ikabainika kuwa IPTL haikuweka dola 36 milioni kama equity bali iliweka dola 50 ambazo kwa wakati zilikuwa sawa na Sh50,000.
Kutokana na kasoro hiyo, Tanesco ikataka gharama ya umeme ishuke kwasababu bei ilizingatia ‘equity’ ya dola 36 milioni.
Mabishano yakaendelea mpaka mwaka 2006 ambapo Serikali ilishinikiza ifunguliwe akaunti maalumu (Tegeta Escrow) ili malipo yawekwe huko mpaka mgogoro utapokwisha kuhusu bei sahihi ndipo pesa hiyo igawanywe kwa kuzingatia bei sahihi kwa pande mbili.
Ilipofika mwaka 2008, IPTL ilishindwa kujiendesha hivyo ikawekwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoka Septemba 2013 chini ya Jaji Utamwa iliamua IPTL iondolewe chini ya usimamizi wa Rita na mali zote za IPTL ipewe Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP) ya Harbinder Singh Sethi.
Sethi aliyetajwa katika rekodi za ufisadi tangu Kenya kwenye kashfa ya Goldenberg mwaka 2002 na hakuwahi kuwa mwekezaji katika sekta ya umeme, akapewa haki na mahakama kuzalisha ikisema atazalisha 500MW na kwamba ataiuzia umeme Tanesco kwa bei nafuu ya dola senti 6 mpaka 8 kwa uniti.
Hukumu hiyo ilitoka huku mmiliki wa asilimia 70 ya IPTL (Mechmar) akiwa mufilisi nchini Malaysia na zaidi ICSID kukiwa na kesi inayohusu mgogoro wa IPTL na Serikali uliofunguliwa na Standard Chartered Bank ambayo ilinunua deni la IPTL mwaka 2005 na ikaruhusiwa kuishtaki Serikali ya Tanzania kwenye baraza hilo lenye mamlaka ya mwisho.
Februari 2014, ICSID ilifanya uamuzi wa awali kwamba ni kweli IPTL inaitoza zaidi Tanesco na kuelekeza pande mbili zikafanye hesabu upya ndani ya siku 90 zilizoisha Mei 2014 kwa lengo la kujua ni kwa kiasi gani IPTL imeipunja Tanesco tangu 2002 mpaka 2013 katika bei.
Hata hivyo, Tanesco na Serikali hawakutoa ushirikiano ndani ya siku hizo 90 kutekeleza uamuzi huo. Inaelezwa kuwa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa alikuwa mgonjwa.
Hadi Novemba 2013 wakati mchakato wa kukokotoa malipo hayo, hali ya Dk Mgimwa ilikuwa mbaya hospitalini nchini Afrika Kusini.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL iliyowasilishwa bungeni Novemba 2014 ilionyesha kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni na zilitakiwa kurudishwa Tanesco.
Kutokuwepo kwa umakini kwa Serikali kulisababisha Kampuni ya PAP kujimilikisha fedha za IPTL kwa asilimia 70 bila kuwa na ushahidi wowote kwamba iliinunua IPTL ikiwemo malipo ya kodi kama ilivyofanya kwa VIP yenye asilimia 30 za hisa.
Mechmar yenyewe ilikanusha kuuza hisa zake za IPTL kwa kuwa ilikuwa chini ya ufilisi na kuitaka PAP kuonyesha cheti cha hisa.
Pamoja na maelezo hayo, Novemba 26, 2014 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alilieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa fedha za Tegeta Escrow si za umma na kwamba bado Serikali ina mzigo wa madeni katika sakata hilo.
Msimamo huo pia ulitolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye aliwahi kunukuliwa akisema kwamba sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ni upuuzi.
Kwa upande mwingine, mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira aligawa jumla ya Sh31 bilioni kwa watu binafsi wakiwemo wanasiasa na watendaji wa Serikali na makampuni.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka aliyepewa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Wengine waliopata fedha hizo ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge na wengineo.
Katika vikao vya Bunge wakati wa sakata la Escrow, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wakati huo, Mwigulu Nchemba aliwataka wote waliopokea fedha hizo kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Hivi karibuni, Ewura imetoa tangazo la kutaka maoni ya wadau kwa ajili ya kuongeza muda wa leseni ya IPTL.
Tangazo hili limezua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania wakiwemo wanasiasa na wanaharakati, wakihoji sababu ya IPTL kuongezewa muda.
Wakati mjadala ukiendelea, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kumsimamisa kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, hatua iliyosababisha mamlaka hiyo kutoa tangazo lingine la kusitisha mchakato wa kuongeza leseni ya IPTL.

Acacia kikaangoni, yajibu mapigo


Dar es Salaam. Kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi katika mchanga wenye madini unaosafirishwa nje imetoa mapendekezo 21 kwa Serikali, ikiwamo kuichukulia hatua za kisheria kampuni ya Acacia ambayo imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kinyume na matakwa ya sheria.
Mapendekezo hayo yote yamekubaliwa na Rais Magufuli na ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuanza mara moja kuwachunguza wote waliohusika katika kulitia Taifa kwenye hasara kubwa kutokana na upotevu wa rasilimali ya madini na kuwachukulia hatua za kisheria.
Hata hivyo, Acacia imeeleza kusikitishwa na matokeo ya ripoti ya pili ya kuchunguza makinikia iliyowasilishwa kwa Rais Magufuli.
Katika maelezo yaliyotolewa jana na kampuni hiyo, ilieleza kusikitishwa na matokeo yaliyotolewa na kamati ya pili na kudai ilijikita katika yaliyobainika kwenye ripoti ya kwanza iliyowasilishwa Mei 24 ambayo waliyakanusha.
“Kamati ilijikita katika kuchunguza sampuli kutoka makontena 44. Katika miaka 20 na takwimu tulizonazo ni vigumu kubainisha uchunguzi huo na iko wazi wameongeza thamani ya makinikia kwa zaidi ya mara 10,” ilieleza taarifa ya Acacia.
Kamati ya pili imeonyesha jinsi Acacia imekuwa haiweki bayana malipo ya kodi na mapato kwa miaka kadhaa ambayo ni mabilioni ya dola za Marekani.
Hata hivyo, kampuni hiyo imekanusha kwa kile ilichoeleza ni tuhuma mpya zilizotolewa.
“Tumekuwa tukifanya biashara zetu kwa kiwango cha juu na kuendesha shughuli zetu kwa kufuata sheria za Tanzania,” ilieleza taarifa yao.
Kamati hiyo iliyoundwa Aprili 10 ilitoa mapendekezo hayo ikiwa ni wiki tatu tangu kamati ya kwanza ilipowasilisha taarifa yake kwa Rais Magufuli, naye akaamua kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo jana Ikulu jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wake, Profesa Nehemiah Osoro alibainisha mapendekezo mengine kuwa ni Serikali kudai kodi na mrabaha kutoka kwa kampuni zote za madini ambayo yamekwepwa kulipwa na mrabaha stahiki kwa mujibu wa sheria.
Profesa Osoro alisema kampuni nyingi za madini zimekuwa zikiliibia Taifa kutokana na mikataba mibovu wanayoingia na pia kuendesha shughuli zao kwa kukwepa kodi na kutofuata sheria na taratibu nyingine za madini.
“Kuna tatizo kubwa katika mikataba yetu, lakini pia watendaji wetu wamekuwa hawasimamii masilahi ya Taifa. Naweza kusema wanaangalia masilahi binafsi katika kusimamia madini yanayozalishwa nchini,” alifafanua Profesa Osoro.
Mwenyekiti huyo aliishauri Serikali kuendelea kuzuia usafirishaji wa mchanga wenye madini kwenda nje ya nchi mpaka pale kampuni zinazodaiwa zitakapolipa kodi, mrabaha na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati ni Serikali kuanzisha utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia (smelter) ili kuondoa upotevu wa mapato na kutengeneza ajira kwa Watanzania.
Kamati hiyo imependekeza Serikali ifanye uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa mawaziri, wanasheria wakuu wa Serikali na manaibu wao, wakurugenzi wa idara za mikataba na makamishna wa madini pamoja na wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini.
Pia, kamati imependekeza kuwa watumishi wengine wa Serikali na watu wote waliohusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini, utoaji wa leseni za uchimbaji wa madini na kuongeza muda wa leseni, watumishi na wamiliki wa kampuni za madini, kampuni zilizohusika kuandaa nyaraka za usafirishaji wa makinikia na kampuni za upimaji wa madini kwa kuvunja sheria za nchi na upotoshaji.
Profesa Osoro alitaja mapendekezo mengine ya kamati kuwa ni Serikali kufanya uchunguzi kuhusu mwenendo wa watumishi wa idara ya walipakodi wakubwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwenye kushughulikia madai ya kodi ambayo mabaraza ya rufani ya kodi na mahakama zimekwishayatolea uamuzi.
Mapendekezo mengine ni Serikali kufuta utaratibu wa kupokea malipo ya mrahaba ya asilimia 90 na kusubiri malipo ya asilimia 10 kulipwa baadaye wakati kampuni za madini zinauza madini na kupewa fedha taslimu kwa mkupuo.
Kamati hiyo imependekeza pia Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ifuatilie malipo ya fedha za kigeni yanayotokana na mrahaba kwa mauzo ya madini, jambo ambalo lilikuwa halifanyiki kwenye sekta ya madini kwa muda mrefu.
Profesa Osoro aliongeza kuwa Serikali ianzishe utaratibu wa kulinda maeneo ya migodi na viwanja ndege vilivyopo migodini ili kudhibiti vitendo vya hujuma vinavyoweza kufanywa na kampuni za migodi ikiwamo utoroshaji wa madini.
Kamati hiyo iliyotumia miezi miwili kukamilisha ripoti yake, imependekeza Serikali kupitia wataalamu wabobezi katika majadiliano na mikataba wapitie mikataba yote mikubwa ya uchimbaji madini na kufanya majadiliano na kampuni za madini ili kuondoa misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija kwa Taifa na badala yake kuweka masharti yenye tija kwa pande zote mbili kwa kuzingatia masilahi ya nchi.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati yalitaka mabadiliko ya sheria ya madini ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha adhabu kwa makosa ya ukiukwaji wa sheria ya madini na sheria ya kodi.
Mabadiliko mengine ni sheria kuweka kiwango cha asilimia za hisa ambazo zitamilikiwa na Serikali; kutamka bayana kuwa madini ni mali asili ya Watanzania na iwekwe chini ya udhamini wa Rais na mikataba yote ya uchimbaji wa madini isiwe ya siri na iridhiwe na Bunge.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema sheria pia iondoe mamlaka ya waziri wa Nishati na Madini, kamishna wa madini na maofisa wa madini na iweke masharti kwa waombaji leseni ya uchimbaji kuonyesha mchanganuo wa mafunzo kwa wazawa.
Mabadiliko mengine yaliyopendekezwa na kamati ni sheria ielekeze kampuni za madini kuweka fedha zinazotokana na mauzo ya madini katika benki zilizopo nchini.
“Serikali iunde chombo cha kusimamia biashara ya usafirishaji bidhaa nje ya nchi kupitia bandari kama lilivyokuwa shirika la Nasaco ili kudhibiti biashara haramu na kuondoa mianya ya ukwepaji kodi,” alibainisha Profesa Osoro.
Pia, kamati imependekeza kuwa Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa sheria ya madini na sheria za kodi ili kuondoa pamoja mambo mengine masharti yote yasikuwa na manufaa kwa Taifa ikiwa ni pamoja na yaliyomo kwenye kifungu thabiti.
Vilevile kamati hiyo imemtaka kamishna wa madini kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa kampuni za madini ili kuhakikisha uzingatiaji wa ukiukwaji wa sheria na kuchukua hatua.

Ripoti ya makinikia yaibua uozo wa mikataba ya madini


Kamati ya pili iliyoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza masuala ya kiuchumi na kisheria kwenye makinikia iliyotolewa jana imeibua uozo uliopo kwenye mikataba ya madini, huku ikifichua kutosajiliwa kwa kampuni ya Acacia Mining inayojinasibisha kuwa mmiliki wa kampuni za Bulyanhulu Gold Mines, North Mara Gold Mine na Pangea Minerals.
Ripoti hiyo ilitanguliwa na ripoti ya kwanza iliyokabidhiwa Mei 21 kwa Rais Magufuli ikieleza upungufu katika mapato ya madini.
Akiwasilisha ripoti hiyo jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Nehemiah Osoro alisema kampuni hiyo haikuwahi kuandikishwa Tanzania.
“Kamati imebaini na kuthibitisha kwa mujibu wa nyaraka na maelezo kutoka ofisi ya msajili wa makampuni (Brela) kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc haikusajiliwa nchini Tanzania na wala haina hati ya utambuzi kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni, Sura ya 212,” alisema Profesa Osoro.
Alisema kamati yake pia imebaini kampuni hiyo haikuwahi kuwasilisha nyaraka wala taarifa yoyote kuonyesha kuwa ni mmiliki wa kampuni zinazomiliki wala kuwa na hisa katika kampuni hizo.
“Kwa kuwa Acacia Mining Plc haina usajili wala utambuzi wa kisheria nchini Tanzania, haina sifa ya kupata leseni, kuchimba wala kufanya biashara ya madini nchini Tanzania. Hivyo basi, kamati imebaini kuwa Acacia Mining Plc, inafanya biashara ya madini hapa nchini kinyume cha sheria za nchi,” alisema.
Kuhusu biashara ya uuzaji na usafirisaji wa makinikia nje ya nchi, Profesa Osoro alisema uuzwaji wake umekuwa ukifanyika kwa udanyanyifu Bulyanhulu Gold Mines Ltd na Pangea Minerals Ltd.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 44,077 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha mwaka 1998 hadi 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani cha Sh132.56 trilioni au Sh229.9 trilioni kwa kiwango cha juu,” alisema Profesa Osoro.
Kuhusu thamani ya madini yaliyomo kwenye makinikia katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi cha kati ya 1998 na 2017 kwa kutumia kiwango cha wastani ni Sh183.597 trilioni.
“Jumla ya thamani ya madini katika makontena 61,320 yaliyosafirishwa nje ya nchi katika kipindi kati ya 1998 na 2017, kwa kutumia kiwango cha juu ni Sh380.499 trilioni,” alisema.
Aliongeza kuwa jumla ya mapato ya Serikali ambayo ilipoteza ni Sh68.59 trilioni ambazo ni sawa na bajeti ya miaka miwili ya Serikali kwa kigezo cha makadirio ya mwaka 2017/2018. “Robo ya fedha hizo zingetosha kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza,” alisema Profesa Osoro.
Kiasi cha mapato ambacho Tanzania imepoteza (kiwango cha juu) ni Sh108.46 trilioni ambazo ni sawa na bajeti inayokaribia miaka mitatu ya Serikali kwa kigezo cha makadirio ya matumizi ya mwaka 2017/2018 na gharama ya kujenga reli ya standard gauge kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza.
Kuhusu uchenjuaji wa makinikia nje ya nchi, Profesa Osoro alisema kamati hiyo ilisoma mikataba ya mauzo kati ya kampuni za uchimbaji na wachenjuaji na kugundua kuwa Serikali siyo sehemu ya mikataba hiyo, licha ya kuwapo na salio la kodi katika makinikia hayo. “Kwa msingi huo, taarifa ambazo zimekuwa zikiwasilishwa kwa TMAA (Wakala wa Ukaguzi wa Madini) baada ya kuomba taarifa hizo kutoka makampuni ya madini hazina ukweli na hazibebi takwimu sahihi kuhusu aina, kiasi na thamani ya madini yaliyochenjuliwa ambazo zingewezesha TRA kutoza kodi stahiki,” alisema Profesa Osoro.