Tuesday, June 13

IPTL, kaa la moto lililoteketeza vigogo kwa miaka 20


Sakata la mkataba wa kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) limezuka tena hivi karibuni baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati (Ewura) kutoa tangazo la kuongeza muda wa leseni ya kampuni hiyo hivi karibuni.
Kashfa ya mkataba wa IPTL uliosainiwa mwaka 1995 imekuwa ikigharimu madaraka ya baadhi ya viongozi kila inapoibuka na hivi karibuni imesababisha Mkurugenzi wa Ewura, Felix Ngamlagosi kusimamiswa kazi na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kashfa hii iliyozalisha kashfa nyingine ya Akaunti ya Tegeta Escrow pia ilisababisha kuvuliwa madaraka kwa mawaziri wa awamu ya nne ambao ni aliyekuwa Waziri Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo, huku baadhi ya watendaji wa Serikali na wanasiasa wakiitwa kwenye Tume ya Kijaji kuhojiwa kwa mgawo walioupata.
Chimbuko la IPTL
Mwaka 1994 kulitokea tatizo kubwa la umeme, hivyo Serikali ilitafuta suluhisho la dharura na la kudumu. Mwaka huo, aliyekuwa Waziri wa Mipango marehemu Horace Kolimba alitembelea nchini Malaysia na kuzungumza na wawekezaji katika sekta ya umeme nchini humo na kuwaomba waje nchini kuangalia uwezekano wa kuwekeza ili kupunguza tatizo la umeme.
Agosti 19, 2014, Mkurugenzi wa Kampuni ya Mechmar, inayomiliki asilimia 70 ya hisa za IPTL, Datuk Baharuden Majid, aliongoza ujumbe mzito kutoka Malaysia kuja kuzungumza na Serikali ya Tanzania.
Walioshiriki katika mazungumzo hayo kwa upande wa Tanzania walikuwa ni pamoja na Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa wakati huo Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Simon Mhaville, Kamishna wa Nishati Msaidizi, Ester Masunzu na Dk Juma Ngasongwa ambaye alikuwa msaidizi wa Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi wa mambo ya uchumi.
Septemba 1994, Mkataba wa Maelewano (MOU) ulifikiwa, licha ya tahadhari kutoka kwa washauri wa Tanesco ambao ni kampuni za Acres (Canada) na Hunton and Williams (Uingereza), kwamba uwekezaji huo ulikuwa ni janga kwa sekta ya umeme na kwa uchumi wa Taifa.
Kampuni hiyo ambayo wamiliki wake ni Mechmar ya Malaysia mwenye asilimia 70 na VIP ya Tanzania yenye asilimia 30 ilisaini mkataba wa miaka 20 (1995-2015) na Serikali ya Tanzania (Tanesco) ambapo kwa mujibu wa mkataba huo endapo kutatokea shauri lolote, uamuzi wa mwisho utatolewa na baraza la usuluhishi la migogoro ya kiuwekezaji (International Centre for Settlement of Investment Disputes-ICSID).
Chini ya mkataba huo, Tanesco ilitakiwa kuilipa IPTL Dola 3.6 milioni sawa na Sh7.92 bilioni kwa mwezi kama ada ya huduma za mtambo.
Juu ya malipo hayo, Tanesco pia inalipa senti 13 (dola) kwa kila uniti ya umeme (sawa na kilowati moja) kwa kuendesha mtambo kwa nusu ya uwezo wake kwa mwezi.
Mikosi yaanza
Kosa la kwanza la IPTL lilikuwa ni kutokamilisha mradi wake mwaka 1995 kwenye kipindi cha dharura na badala yake ikakamilisha mwaka 1998.
Hivyo mwaka 1998 Tanesco ilifungua shauri ICSID ikiilalamikia IPTL kwa kukuza gharama za uwekezaji na hivyo kukuza gharama za umeme.
Mwaka 2001 uamuzi wa ICSID ukatoka ikabainika ni kweli IPTL ilikuza gharama kwa kiasi cha Dola 27milioni.
Mwaka 2002 IPTL ikaanza kuiuzia umeme Tanesco lakini ilipofika mwaka 2004 ikabainika kuwa mwaka 2004 IPTL ilidanganya kuhusu mtaji.
Awali IPTL ilisema asilimia 30 ya mtaji ilikuwa nao kama ‘equity’ sawa na Dola 36 milioni na kwamba asilimia 70 ilikopa. Lakini baada ya ukaguzi ikabainika kuwa IPTL haikuweka dola 36 milioni kama equity bali iliweka dola 50 ambazo kwa wakati zilikuwa sawa na Sh50,000.
Kutokana na kasoro hiyo, Tanesco ikataka gharama ya umeme ishuke kwasababu bei ilizingatia ‘equity’ ya dola 36 milioni.
Mabishano yakaendelea mpaka mwaka 2006 ambapo Serikali ilishinikiza ifunguliwe akaunti maalumu (Tegeta Escrow) ili malipo yawekwe huko mpaka mgogoro utapokwisha kuhusu bei sahihi ndipo pesa hiyo igawanywe kwa kuzingatia bei sahihi kwa pande mbili.
Ilipofika mwaka 2008, IPTL ilishindwa kujiendesha hivyo ikawekwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA).
Hukumu ya Mahakama Kuu iliyotoka Septemba 2013 chini ya Jaji Utamwa iliamua IPTL iondolewe chini ya usimamizi wa Rita na mali zote za IPTL ipewe Kampuni ya Pan Africa Power Solutions Ltd (PAP) ya Harbinder Singh Sethi.
Sethi aliyetajwa katika rekodi za ufisadi tangu Kenya kwenye kashfa ya Goldenberg mwaka 2002 na hakuwahi kuwa mwekezaji katika sekta ya umeme, akapewa haki na mahakama kuzalisha ikisema atazalisha 500MW na kwamba ataiuzia umeme Tanesco kwa bei nafuu ya dola senti 6 mpaka 8 kwa uniti.
Hukumu hiyo ilitoka huku mmiliki wa asilimia 70 ya IPTL (Mechmar) akiwa mufilisi nchini Malaysia na zaidi ICSID kukiwa na kesi inayohusu mgogoro wa IPTL na Serikali uliofunguliwa na Standard Chartered Bank ambayo ilinunua deni la IPTL mwaka 2005 na ikaruhusiwa kuishtaki Serikali ya Tanzania kwenye baraza hilo lenye mamlaka ya mwisho.
Februari 2014, ICSID ilifanya uamuzi wa awali kwamba ni kweli IPTL inaitoza zaidi Tanesco na kuelekeza pande mbili zikafanye hesabu upya ndani ya siku 90 zilizoisha Mei 2014 kwa lengo la kujua ni kwa kiasi gani IPTL imeipunja Tanesco tangu 2002 mpaka 2013 katika bei.
Hata hivyo, Tanesco na Serikali hawakutoa ushirikiano ndani ya siku hizo 90 kutekeleza uamuzi huo. Inaelezwa kuwa wakati huo aliyekuwa Waziri wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa alikuwa mgonjwa.
Hadi Novemba 2013 wakati mchakato wa kukokotoa malipo hayo, hali ya Dk Mgimwa ilikuwa mbaya hospitalini nchini Afrika Kusini.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa Kampuni ya IPTL iliyowasilishwa bungeni Novemba 2014 ilionyesha kuwa fedha zilizokuwa kwenye akaunti hiyo ni Sh306 bilioni na zilitakiwa kurudishwa Tanesco.
Kutokuwepo kwa umakini kwa Serikali kulisababisha Kampuni ya PAP kujimilikisha fedha za IPTL kwa asilimia 70 bila kuwa na ushahidi wowote kwamba iliinunua IPTL ikiwemo malipo ya kodi kama ilivyofanya kwa VIP yenye asilimia 30 za hisa.
Mechmar yenyewe ilikanusha kuuza hisa zake za IPTL kwa kuwa ilikuwa chini ya ufilisi na kuitaka PAP kuonyesha cheti cha hisa.
Pamoja na maelezo hayo, Novemba 26, 2014 aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alilieleza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa fedha za Tegeta Escrow si za umma na kwamba bado Serikali ina mzigo wa madeni katika sakata hilo.
Msimamo huo pia ulitolewa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye aliwahi kunukuliwa akisema kwamba sakata la Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), ni upuuzi.
Kwa upande mwingine, mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira aligawa jumla ya Sh31 bilioni kwa watu binafsi wakiwemo wanasiasa na watendaji wa Serikali na makampuni.
Miongoni mwa waliokiri kupokea fedha hizo ni aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Profesa Anna Tibaijuka aliyepewa Sh1.6 bilioni akisema fedha hizo zilikuwa ni za mchango wa kulipa mkopo wa shule anayoisimamia.
Wengine waliopata fedha hizo ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge na wengineo.
Katika vikao vya Bunge wakati wa sakata la Escrow, aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wakati huo, Mwigulu Nchemba aliwataka wote waliopokea fedha hizo kuthibitisha mapato yao ili wakatwe kodi kutokana na fedha hizo ambazo pia zinapaswa kuhakikiwa na vyombo vya usalama kwamba ni mapato halali.
Hivi karibuni, Ewura imetoa tangazo la kutaka maoni ya wadau kwa ajili ya kuongeza muda wa leseni ya IPTL.
Tangazo hili limezua mjadala mzito miongoni mwa Watanzania wakiwemo wanasiasa na wanaharakati, wakihoji sababu ya IPTL kuongezewa muda.
Wakati mjadala ukiendelea, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kumsimamisa kazi Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, hatua iliyosababisha mamlaka hiyo kutoa tangazo lingine la kusitisha mchakato wa kuongeza leseni ya IPTL.

No comments:

Post a Comment