Utafiti uliofanywa na Umoja na Mataifa kupitia Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) miaka 12 iliyopita ulionyesha utalii wa utamaduni unaohusisha vivutio vya asili ulikuwa umeanza kushika kasi duniani.
Katika utafiti huo, Unesco ilieleza utalii wa aina hiyo unaotokana na vivutio vya asili kuwa ndio unaoelekea kuteka soko la sekta hiyo duniani.
Shirika hilo katika utafiti wake liliainisha sababu mbili kubwa za watu kuanza kupenda utalii wa aina hiyo.
Mosi, lilitaja sababu ya watu wengi duniani kuanza kumiliki wanyama katika makazi yao - sababu ambayo imewafanya wengi wao kutopenda kusafiri kwenda kuangalia wanyama, ilhali wanapatikana mahali walipo.
Kutokana na sababu hiyo, watu wanaopenda kusafiri kwa shughuli za utalii kufuata vivutio vya wanyama duniani walikuwa wameanza kupungua, lakini wengi wanaokwenda kutalii hufuata zaidi vivutio vya asili.
Unaweza kushangaa mbona unawaona watalii wengi wanakuja nchini na kutembelea maeneo ya hifadhi za Taifa. Jibu ni jepesi, nalo ni ukweli kwamba hifadhi nyingi zinatofautiana katika mambo mbalimbali ambayo pia ni vivutio kwa upande wake. Mathalan, Hifadhi ya Ruaha ndiyo kubwa kuliko zote, lakini ina wanyama wengi aina ya tembo, jamii ya miti na maua ambavyo havipatikani katika sehemu nyingine nchini na duniani kwa ujumla.
Vivyo hivyo ndivyo ilivyo Rubondo, uwapo wake kama kisiwa ndani ya ziwa unaifanya iwe na upekee ikiwa na ndege na pia huwavutia watalii kuitembelea kwa upekee wa utalii wa uvuvi.
Kuna Ngorongoro yenye eneo la kreta inayovutia kwa umbile lake la mfano wa sahani na uwapo wa idadi kubwa ya wanyama wanaoishi ndani ya ‘sahani’ hiyo, lakini pia namna wanavyoishi kwa kukwepana kati ya walao nyama na wanaoliwa ni aina ya kivutio cha pekee.
Ndivyo pia ilivyo kwa Serengeti ambako ni makazi ya nyumbu wanaohama nyakati fulani za mwaka na kuhamia Maasai Mara nchini Kenya wakifuatana katika mtitiriko unavyovutia macho kuwaangalia. Hivyo ndivyo ilivyo katika vivutio vya wanyama.
Sababu ya pili ni ukweli kwamba, utalii wa wanyama umezoweleka na umekuwapo duniani kwa miaka nenda rudi, hiyo ikiwa na maana kuwa karne nyingi zilizopita vivutio vya wanyama vilitumika kuwafanya watu kusafiri kwenda kuwaangalia mahali walikokuwa.
Licha ya hilo, katika dunia ya sasa watu wanafuga wanyama mbalimbali katika makazi yao wakiwa na hifadhi ndogo walizojianzishia na hilo linawafanya wawatumie kama vivutio vya utalii kwao na hata watu wanaohitaji kwenda kuwaangalia.
Utalii wa malikale, utamaduni
Utalii wa malikale na utamaduni unaingia katika kundi moja, lile ambalo uasili wa vitu unawekwa pamoja katika misingi ya utalii. Ndani ya malikale kuna vitu vilivyotumiwa zamani kama mikuki, mishale na mawe; mabaki ya viumbe vya kale kama wanyama, binadamu, ndege na mimea.
Ndani ya utamaduni kuna ngoma, majengo, minara (inayoonyesha utamaduni wa maeneo husika), mavazi, mapishi, chakula, lugha, heshima na mazungumzo. Pia kuna mambo ya utamaduni yanayoingia katika kundi hilo kama malezi, misiba, harusi, jando na unyago.
Katika mataifa yaliyoendelea, utalii wa utamaduni na malikale unapigiwa chapuo kuliko ule wa wanyama. Wanafanya hivyo pengine kutokana na kutokuwa na hifadhi nyingi kubwa zenye vivutio vingine ndani yake vinavyovutia watalii.
Ndiyo maana miji mikubwa katika Brussels (Ubelgiji), Paris (Ufaransa), London (Uingereza), Dublin (Ireland), Washington na New York (Marekani) imekuwa ikitengeneza vivutio binafsi ili kuwavutia watalii, lakini pia ina malikale nyingi ambazo zimehifadhiwa kwa miaka mingi.
Hizo ni pamoja na minara ya kumbukumbu, majengo ya zamani, maeneo ya kumbukumbu za vita, viwanja vya michezo na mazoezi, kumbi za burudani, maktaba kubwa zenye vitabu na machapisho ya karne, maumbile ya kuchora, nyumba walizoishi watu walioacha rekodi mbalimbali, picha, michoro na nyaraka za zamani.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2017, Ubelgiji yenye wakazi 11,303,528 ikiwa na pato la Dola 508.598 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh1117.6 trilioni) kwa mwaka huku pato la mwananchi wa kawaida likiwa ni Dola 44,881 (zaidi ya Sh98.7 milioni, inategemea nusu ya pato lake litokane na utalii wa vivutio vya asili.
Nchi hiyo ina vituo vingi vya asili kuanzia maktaba kubwa, makumbusho na majengo ya zamani yanayovutia mamilioni ya watu kutoka mabara yote duniani kuitembelea. Ubelgiji haina hifadhi kubwa, mbali na ile maarufu ya Public Aquarium iliyopo katikati ya Jiji la Brussels.
Licha ya hifadhi hiyo ambayo haizidi kilomita 1.5 za mraba nyingine ni T’struisvogelnest (Lier), Bouillon Wildlife Park (Bouillon), Le Parc a Gibier (La Roche-en-Ardenne), La grange aux papillons (Chimay), Olmense Zoo (Olmen), Sea life (Blankenberge), De Zonnegloed Sanctuary (Vleteren), Serpentarium (Blankenberge), Bellewaerde (Ieper (Ypres) na Aquarium et Musee de Zoologie iliyopo Liege.
Kwa pamoja, maeneo hayo madogo ya kuhifadhi wanyama na mimea yaliyotengenezwa yanaiingizia nchi hiyo pato lisilozidi Dola 17 milioni za Marekani (zaidi ya Sh37.4 bilioni) kwa mwaka.
Nchi nyingi zilizoendelea zimefanikiwa kuutuza utalii wa malikale kuliko ule wa utamaduni. Utamaduni katika mataifa mengi hasa yaliyoendelea umekufa na nyingi ya nchi hizo zinaigana katika mambo mengi kama vile mavazi na chakula.
Ndiyo maana katika utalii wa vivutio vya asili bado nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania zinaweza kutumia fursa hiyo kuingiza mapato makubwa kuliko kutegemea hifadhi pekee.
Kwa Tanzania, utalii wa utamaduni uko zaidi katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi wanaishi kiasili. Huko ndiko bado kuna ngoma za asili, vyakula na hata mavazi mfano mzuri ni Umasaini.
Pia, Tanzania ina malikale nyingi zilizotapakaa kila kona. Mifano ya malikale hizo ni magofu ya Bagamoyo; mabaki ya majengo ya biashara ya watumwa yaliyopo Kilwa Kisiwani, Kilwa Kivinje na Kilwa Masoko; eneo la historia ya binadamu wa kale la Oldupai; mahala yalipogunduliwa mabaki ya mjusi aliyeishi miaka 150 milioni Tendaguru mkoani Lindi; michoro ya mapangoni ya Amboni na Kondoa; makaburi ya Waarabu ya Bagamoyo na Kunduchi yaliyojengwa kati ya karne ya tisa hadi 11.
Maeneo mengine yanayoweza kuchangia katika uchumi wa nchi kupitia utalii iwapo yatatangazwa ipasavyo ni yale ya matambiko ya makabila mbalimbali yakiwamo mapango, mawe makubwa, miti na maporomoko ya maji.
Si hayo tu, kuna minara, makumbusho mbalimbali na maeneo ya kihistoria mathalan yaliyotumiwa na wapigania uhuru kufanyia harakati zao, makaburi na majengo waliyolala au kuishi wapigania uhuru wa nchi zao za kusini mwa Afrika.
Kwa ujumla yapo maeneo mengi ya kale yaliyobeba historia inayoweza kuchangia pato la Taifa kupitia utalii, lakini tatizo mengi hayafahamiki kwa wananchi na hayajaendelezwa kuwezesha utalii kufanyika.
Fursa kwa Tanzania inawezekana iwapo Serikali itayaendeleza maeneo hayo kwa kuyapa ‘uhai’ wa miundombinu yaweze kufikiwa, mkakati wa kuyatangaza na pia kuzijengea uwezo jamii zinazoishi jirani au maeneo husika namna zinavyoweza kutumia fursa kujikwamua kiuchumi.
Ofisa utalii wa kampuni ya All Safaris, Fidelis Olakamtwa anasema watalii wengi wanaowahudumia wanapenda kuangalia na kujifunza juu ya malikale na vivutio vya asili, lakini mara nyingi hupendelea vilivyopo Ngorongoro (NCAA) kwa kuwa tayari vimeendelezwa.
Anavitaja vivutio hivyo kuwa ninyayo za binadamu wa kale, eneo la mabaki ya binadamu wa kale na wanyama pamoja na mchanga unaohama kutoka sehemu moja hadi nyingine. “Huu ndio utalii unaowavutia, hata tunapojitangaza tunazingatia sana kutumia vivutio vya aina hiyo. Vingine ni kama Makumbusho ya Kalenga (Iringa), nyayo zile za zamadamu, pale Bagamoyo kuna vivutio vingi sana vya kihistoria na vya asili,” anasema.
Mhitimu wa stashahada ya malikale na utalii wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ole Naikoli anaishauri Serikal kutangaza utalii kwa kuangalia zaidi vivutio vya asili na malikale zilizotapaa nchini.
“Tunaweza kuona havina maana kwetu, lakini vina mchango mkubwa sana katika pato endelevu kwenye uchumi wa nchi ikizingatiwa kwamba baada ya miaka michache ijayo ni watu wachache watakaokimbilia kushangaa wanyama hifadhini,” anasema.
Hivi karibuni naibu waziri wa Maliasi na Utalii, Japhet Hasunga akiwa mkoani Rukwa alisema Serikali imepanga kuendeleza utalii katika maeneo ya Kusini, lakini itajikita pia kuangalia namna ya kuviendeleza vivutio vya asili. Hasunga aliyasema hayo alipotembelea maporomoko ya Kalambo ambayo ni ya pili kwa kina kirefu barani Afrika ambayo yamekuwa hayatembelewi na watalii wengi kutokana na kutotangazwa ipasavyo.
Akizungumza hivi karibuni juu ya uendelezwaji wa eneo la Tendaguru lililopo mkoani Lindi mahala ambapo watafiti wa Ujerumani walifukua na kuondoka na mabaki ya mjusi wa kale maarufu dinosaria zaidi ya miaka 100 iliyopita, mkurugenzi wa utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Deogratius Mdami alisema Serikali inafanyia kazi maeneo yote ambayo yanahitaji uendelezwaji kwa ajili ya kuja kuwa vivutio vya utalii.