Thursday, November 23

Raila arejea Kenya baada ya mapumziko Zanzibar


Zanzibar/Nairobi. Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Nasa nchini Kenya, Raila Odinga amerejea nyumbani baada ya kujichimbia kwa siku nne Zanzibar nchini Tanzania.
Mwanasiasa huyo ambaye amegoma kuutambua ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta alikuwa visiwani Zanzibar kwa mapumziko baada ya kumaliza ziara ya siku 10 nchini Marekani.
Taarifa za kurejea nyumbani kiongozi huyo zimethibitishwa na msemaji wake, Dennis Onyango ambaye aliliambia gazeti la Nation kuwa Odinga amerejea Kenya.
Pia, mkurugenzi wa mawasiliano wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), Philip Etale amezungumzia kuwasili kwa Odinga mjini Nairobi.
Ingawa baadhi ya picha zimekuwa zikimuonyesha mwanasiasa huyo akiwa mapumzikoni katika hoteli moja Zanzibar lakini ziara yake imehusishwa na hali ya kisiasa nchini mwake.
Mapokezi ya Odinga mwishoni mwa wiki aliporejea Kenya baada ya kuwa nje ya nchi kwa siku 10 yalikumbwa na taharuki baada ya kutokea ghasia zilizohusisha wafuasi wake na polisi.

No comments:

Post a Comment