Monday, August 3

Watu milioni 1.6 wamdhamini Lowassa


Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa akipungia wananchi 
wakati akiondoka kutoka makao makuu ya Chadema Kinondoni, 
 baada ya kurudisha fomu ya kugombea urais kupitia chama hicho. 
Dar es Salaam. Kada mpya wa Chadema, Edward Lowassa jana amerejesha fomu ya kuwania urais, huku akifanikiwa kupata wadhamini milioni 1.6, zaidi ya nusu ya kura za urais ambazo chama hicho kilipata kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
Naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu alisema idadi hiyo ya wadhamini inaashiria ushindi wa kishindo, kwa maelezo kuwa inakaribia idadi ya kura alizopigiwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alipogombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Katika Uchaguzi huo, Dk Slaa alishika nafasi ya pili baada ya kupata kura 2,271,941 sawa na asilimia 26.34, huku Rais Jakaya Kikwete akipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 61.17.
Lowassa alipochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, kabla ya kuhamia Chadema, alidhaminiwa na wanachama 870,000 nchi nzima.
Dk Slaa, ambaye hajaonekana hadharani tangu Lowassa ajiunge Chadema, jana hakuwapo kwenye ofisi za chama hicho wakati mbunge huyo wa Monduli alipokuwa akirejesha fomu.
Hakuna kiongozi aliyekuwa tayari kuzungumzia suala lake, lakini baadhi ya maofisa wa Chadema walisema wanaendelea kuchapa kazi.
Kama ilivyokuwa juzi katika hafla fupi wakati Lowassa akichukua fomu, umati mkubwa ulifurika na kusababisha Mtaa wa Ufipa uliopo Wilaya ya Kinondoni kufungwa, watu walijazana tena na safari hii umati huo ukiwa umebeba mabango ya kumsifu Waziri Mkuu huyo wa zamani.
Katika hafla ya jana, makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Profesa Abdallah Safari alieleza jinsi Chadema ilivyojipanga kuchukua nchi na siyo kushinda ubunge na udiwani pekee na kwamba Lowassa amebakiza hatua mbili tu kuingia Ikulu, jambo walilodai kuwa limeichanganya CCM.
Wakati Lowassa ambaye alitangaza rasmi kujiondoa CCM na kujiunga na Chadema Julai 28 mwaka huu akisubiri kupitishwa na Mkutano Mkuu wa chama hicho utakaofanyika Agosti 4, habari za ndani zinaeleza kuwa vigogo kadhaa wa CCM watatambulishwa katika mkutano huo.
Habari hizo zinaeleza watakaotambulishwa siku hiyo ni wenyeviti wa CCM wa mikoa, wilaya na waliokuwa wabunge wa chama hicho ambao wanamuunga mkono Lowassa.
Jana Lowassa, aliyekuwa amevaa shati jeupe na suruali nyeusi na aliyekuwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser VX, alifika makao makuu ya Chadema saa 9:35 alasiri akiwa pamoja na familia yake na alipokewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya ujumbe huo ni “Chini ya Lowassa umaskini haupo”, “Kwa Lowassa hata maskini atapata ajira” na “Kingunge Ngombare-Mwiru karibu Ukawa”. Kingunge ni kada mkongwe wa CCM na anamuunga mkono Lowassa.
Mbali na kubeba mabango, watu hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kumsifu Lowassa na kushangilia pale ilipokuwa ikitajwa mikakati ya chama hicho kushika dola.
Kura milioni 1.6
Akieleza taratibu na kanuni za kudhamini mgombea urais, mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema mgombea urais anatakiwa kudhaminiwa na wanachama wasiopungua 200.
“Naamini fomu za Lowassa zitakuwa na idadi hiyo ya wadhamini. Ila baada ya mgombea kuchukua fomu jioni yake wanachama wa Chadema, wapenzi na Watanzania walifurika katika ofisi za Kanda, mikoa na majimbo nchi nzima wakiomba kumdhamini,” alisema Kigaira.
Alisema wanachama hao walidhani fomu hizo zimepelekwa kila mkoa, kutokana na kuepuka kuwanyima fursa hiyo chama hicho kilipeleka fomu ili wanachama wamdhamini na kupewa masharti kuwa lazima wawe wamejiandikisha kupiga kura, wataje namba zao za simu.
Huku akionyesha fomu chache za wadhamini kutoka mikoa mbalimbali nchini, Kigaira alitaja idadi ya watu waliomdhamini Lowassa katika mikoa yote 32 kuwa ni 1,662,397.
Akizungumzia udhamini wa wanachama Mwalimu alisema: “Lowassa alitakiwa azunguke mikoani kusaka wadhamini ila siku zilikuwa zimebaki mbili. Tuliwataka wanachama wanaotaka kumdhamini (Lowassa) wafike makao makuu, siku uliyochukua fomu. Wanachama 700 walikuja kukudhamini.”
Alisema kitendo hicho kiliiibua malalamiko kutoka kwa wanachama wa mikoa mbalimbali nchini, hivyo kuagizwa fomu za udhamini zipelekwe mikoani.
Safari ya Lowassa haitavurugwa
Katika maelezo yake, Mwalimu alisema CCM inafanya vikao ili kuivuruga Chadema, lakini akasema kuwa hilo halitafanikiwa na hakuna wa kuivuruga safari ya Lowassa.
“Tunajua kuna mikakati na vikao vinavyoendelea kwa nia ya kumzuia Lowassa katika safari hii ya Chadema na Ukawa, lakini tunawaambia Lowassa kuja Chadema ni mpango wa Mungu. Hatujamuokota barabara, ni Mungu amemuongoza kuja chama chetu kwa sababu Mungu ameshakiandikia neema chama hiki kutokana na falsafa inazokisimamia tangu kuanzishwa kwake.”
“Njama zozote za kishetani, kihafidhina na kifedhuli zitalegea na kupotezwa. Lowassa amebakiza hatua mbili, ya kwanza ni kumaliza mchakato wa ndani ya chama kupitia Mkutano Mkuu na hatua ya pili ni kuapishwa.”
Mwalimu alisema Chadema inaunga mkono kauli ya Lowassa ya kuuchukia umaskini, kwamba nchi imeshindwa kupata maendeleo kutokana na kuongozwa na viongozi wa CCM wenye fikra za kimaskini, za kuamini ili uwe kiongozi lazima uwe maskini.
Alisema baada ya Lowassa kupitishwa na Mkutano Mkuu chama hicho, atazunguka mikoa mbalimbali nchini kuanzia Dar es Salaam Agosti 9.
Lengo ni kuchukua nchi
“Kuna watu walidhani Lowassa hawezi kurejesha fomu. Safari ya kuelekea uchaguzi mkuu imefikia hatua muhimu. Kinachofuata ni Kamati Kuu kupitisha fomu hizi. Naamini hakuna pingamizi lolote maana mpaka sasa hakuna aliyejitokeza kuchukua fomu za kugombea urais kupitia Chadema na Ukawa,” alisema Profesa Safari.
Alisema wapo wanaosema mwaka huu wapinzani wataambulia wabunge na madiwani tu siyo rais, jambo alilodai kuwa si kweli na kwamba lengo lao ni kushinda kiti cha urais.
“Wazanzibari wana msemo wao kwamba goli unafungwa, lakini chenga twawala. Sisi chenga tutapiga na magoli tutafunga,” alisema.
Vigogo CCM
Habari za ndani kutoka chama hicho zinaeleza kuwa vigogo wa CCM watatambulishwa kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, wakiwemo wabunge mashuhuri.
“Siku ya mkutano mkuu watatambulisha wabunge na viongozi wa CCM. Ni wengi na wengine watawashangaza watu kwa kweli kwa sababu si watu wanaotarajiwa kuihama CCM, “ alisema mpashaji habari wetu.
Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye ndiye anayeambatana na Lowassa na amehudhuria hafla zote za uchukuaji na urejeshaji fomu, mara zote akiulizwa amekuwa akijibu kuwa ni mshauri wa mbunge huyo wa Monduli wa masuala ya kupambana na rushwa.
Chizii agoma kuzungumza
Naye kada mkongwe wa CCM, Matson Chizii ambaye naye amekuwa bega kwa bega na Lowassa tangu ahamie Chadema, alipoulizwa kama amehamia katika chama hicho kikuu cha upinzani nchini alisema hana cha kujibu, kusisitiza kuwa atajibu suala hilo siku mbili zijazo.

Mbowe: Nitamzungumzia Dk Slaa muda ukifika

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (pichani) amezungumzia kukosekana kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa katika vikao vya chama hicho vinavyoendelea jijini, akisema: “Nitazungumzia suala hilo muda muafaka ukifika.”
Mbowe alisema hayo jana katika Hoteli ya Ledger Plaza Bahari Beach kilipokuwa kinafanyika kikao cha Kamati Kuu ya Chadema jana.
“Siwezi kusema zaidi ya hapo,” alisema Mbowe alipoulizwa sababu za kutokuwapo Dk Slaa katika vikao hivyo muhimu na kuongeza atatoa baadaye, mrejesho wa kikao hicho.
Kauli hiyo ya Mbowe haikuondoa wingu zito lililotanda Chadema baada ya kutoonekana hadharani kwa kiongozi huyo katika matukio manne muhimu ya chama hicho kikuu cha upinzani, tangu waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ajiunge nacho.
Tofauti na Dk Slaa, Naibu Katibu Mkuu (Bara), John Mnyika alionekana jana kwa mara ya kwanza katika kikao hicho na kufuta uvumi uliokuwa umesambaa kuwa alikuwa na mpango wa kuachana na Chadema kama inavyodaiwa kwa Dk Slaa.
Viongozi hao walianza kutoonekana katika shughuli za chama tangu Lowassa alipojiunga na Chadema Julai 28 na kukabidhiwa fomu ya kugombea urais Julai 30 na juzi Agosti Mosi alipozirejesha.
Hata hivyo, viongozi waandamizi wa Chadema wamesema suala la kutokuwapo kwa Dk Slaa halipaswi kukuzwa kwa kuwa ‘anafanya kazi nyingine za chama.’
Alipoulizwa jana, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema: “Suala la kutokuwapo Dk Slaa ni kitu cha kawaida, anafanya kazi nyingine huko, lakini pia kuna wasaidizi wake hapa ambao ni sisi manaibu. Mlikuwa mnazungumzia Mnyika naye haonekani, si huyo. Hatuwezi kuendelea kujibu ‘rumors’ (uzushi) wa kwenye mitandao… nyie subirini si tupo mtaona kama yupo au la.”
Mnyika atinga kikaoni
Jana, Mnyika alionekana katika viwanja vya hoteli hiyo lakini alikataa kuzungumzia kwa undani suala hizo.
“Siwezi kuzungumza chochote,” alisema Mnyika na hata alipoulizwa ni lini atawaeleza Watanzania juu ya kutoonekana kwake alisisitiza mara tatu kuwa “Siwezi kuzungumza chochote.”
Chama hicho kinaendelea na mfululizo wa vikao vya vyombo vya juu ambapo leo kinatarajia kutafanya kikao cha Baraza Kuu kabla ya Mkutano Mkuu kesho kumpitisha mgombea wa urais kesho.
Kura za maoni Kibamba zaahirishwa
Mchakato wa kura za maoni wa kumpata mgombea wa ubunge wa chama hicho katika Jimbo Kibamba utafanyika leo baada ya kuahirishwa juzi.
Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa kichama Kinondoni, Rose Mushi alisema kura hizo zitapigwa leo kuanzia saa nne asubuhi, Kimara Baruti. “Kila kitu kinakwenda vizuri, nadhani kesho (leo), tutafanya mchakato huu wa kura za maoni, kama kutakuwa mabadiliko nitakutaarifu,” alisema Mushi.
Awali, Mratibu wa Chadema Kanda Pwani, Casmir Mabina alisema: “Jana (juzi), tulishindwa kufanya kwa sababu mmoja wa watia nia alikuwa mgonjwa. Hakupata taarifa za mchakato huo, tukatumia demokrasia ya kuahirisha.”
Mwenyekiti wa Jimbo la Ubungo, Boniface Jacob alisema kura za maoni katika jimbo hilo (Kibamba) huenda zikafanyika leo baada ya kupokea taarifa kutoka kanda. “Sisi kazi yetu ni kuratibu mchakato wa kura za maoni ila maelekezo yote yanatoka juu, inawezekana ikiwa kesho (leo) jioni sina uhakika,“ alisema Jacob.
Juzi, hali ya sintofahamu iliwakumbuka wajumbe na watia nia wa jimbo hilo baada ya kufika kwenye ukumbi wa mikutano na kuambiwa kuwa mchakato wa kura za maoni umeahirishwa kwa madai kuwa mmoja ya watia nia hakupewa taarifa.
Hatua hiyo ilizua minong’ono miongoni wa wajumbe na watia nia ambao waliokuwa wamejiandaa kwa mchakato huo wakidai kuna hujuma zinataka kufanyika.

Mawaziri watano waanguka kura za maoni

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kiislamu Kondoa Dodoma, 
Hamisi Salum akikabidhi kadi ya CCM kwa ajili ya uhakiki wa 
taarifa zake kabla ya kupiga kura kumchagua mgombea udiwani na 
ubunge wa jimbo hilo katika Kituo cha Maji ya Shamba. Awali, 
kura za kituo hicho zilichomwa baada ya kubainika kuwa na udanganyifu. 

Dar/mikoani. Kishindo cha kura za maoni ndani ya CCM kimeendelea kuwakumba baadhi ya vigogo wa chama hicho baada ya jana mawaziri wengine watano kuanguka.
Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe aliyekuwa akiwania kupitishwa tena kugombea tena ubunge wa Nachingwea.
Chikawe ambaye pia alishindwa katika kinyang’anyiro cha urais kupitia chama hicho, alidondoshwa na Hassan Masala aliyepata kura 6,494 akifuatiwa naye akipata 5,128.
Wagombea wengine ni Steven Nyoni (1,438), Amandus Chinguile (1,274), Fadhili Liwaka (1,171), Benito Ng’itu (797), Greyson Francis (671), Albert Mnali (763), Issa Mkalinga (466), Mustafa Malibiche (427) na Ali Namnjundu (319).
Mbali ya Chikawe pia manaibu waziri wanne wameangushwa katika kura hizo. Hao ni Mahadhi Juma Maalim (Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa), Perera Ame Silima (Mambo ya Ndani), Amos Makala (Maji) na Saning’o ole Telele (Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi).
Mahadhi alianguka katika Jimbo la Paje, Zanzibar kwa kupata kura 1,785 huku Jaffar Sanya Jussa ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) Mkoa wa kusini akiibuka mshindi kwa kura 3,368.
Silima aliyepata kura 1,218 katika Jimbo la Chumbuni alibwagwa na mpinzani wake, Ussi Pondeza aliyepata kura 1,952.
Katika Jimbo la Mvomero, Suleiman Murad alishinda kwa kura 13,165 dhidi ya Makalla ambaye alikuwa anatetea jimbo hilo akipata 10,973.
Ole Telele alipata kura 5, 126 huku William ole Nasha akiibuka mshindi kwa kura 23, 563 akifuatiwa na Elias Ngolisa aliyepata 11, 442 na Dk Eliamani Lalkaita 7,135. Matokeo hayo hayakujumlisha kura za matawi matano ambayo Katibu wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Elihudi Shemauya alisema hayawezi kubadili matokeo.
Katika Jimbo la Uzini, Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Muhammed Seif Khatib ameshindwa baada ya kupata  kura 1,333 huku mpinzani wake Salum Mwinyi Rehani akiibuka kidedea kwa kura 1,521.
Kigogo mwingine wa CCM, Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi, ameshinda kura hizo Jimbo la Mtama kwa kura 9,344 dhidi ya mpinzani wake Selemani Methew aliyepata kura 4,766.
Jimbo la Chwaka mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 20,  Yahya Kassim Issa aliangushwa baada ya kupata kura 1,572 dhidi ya mpinzani wake, Baguwanji Mensuriya Baguwanji aliyepata kura 1,951.
Wakati mawaziri hao wakianguka, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alishinda katika jimbo jipya la Welezo huku Waziri wa Ulinzi, Hussein Mwinyi akishinda katika Jimbo la Kwahani.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM, Masauni Hamad Masauni ameshinda Jimbo la Kikwajuni kwa kura 2,222 dhidi ya mpinzani wake, Mussa Shaali Choum aliyepata kura 461.
Katika Jimbo la Jang’ombe, Ali Hassan Omar ameibuka mshindi kwa kupata kura 879 dhidi ya mpinzani wake Abdullah Hussein Kombo (639).
Aliyekuwa Waziri Kiongozi Zanzibar na waziri wa zamani wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha aliibuka mshindi katika Jimbo la Kijito Upele.
Jimbo la Malindi Abdullah Juma Abdulla alishinda kwa kura 558 dhidi ya mpinzani wake, Kombo Mshenga Zubeir aliyepata kura 241. Jimbo hilo nafasi ya uwakilishi, Mohammed Ahmada Salum alishinda kwa kura 336 na dhidi ya Abdulrahman Hassan (271).
Majimbo mengine
Liwale:  Faith Mitambo (7,238), Zainabu Kawawa (3,126).
Ruangwa: Naibu Waziri (Tamisemi), Kassim Majaliwa (11,988), Bakari Nampenya (2,678).
Kilwa Kaskazini: Murtaza Mangungu alishinda kwa kura 7,140.
Kilwa Kusini: Hasanain Dewji ameshinda kwa kura 3,859.
Lindi Mjini: Hassani Kunje (3,428) Mohamedi Ulthali (2,314).
Jimbo la Mchinga: Said Mtanda ameshinda kwa kura 3,101, Riziki Lulida (2,217).
Serengeti: Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Kebwe Steven Kebwe aliibuka mshindi kwa kura 29,268 akiwashinda, Dk James Wanyancha (5,980) na Mabenga Magonera (1,638).
Nyamagana: Aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Stanslaus Mabula ameibuka mshindi kwa kura 9,553, Joseph Kahungwa (3,947) na Raphael Shilatu (894) na kufuatiwa na wenzao 17.
Ukerewe: Christopher Nyandiga aliongoza kura 8,077, Gerald Robert (142), Laurent Munyu (197), Emmericiana Mkubulo (242), Bandoma Kabulule (414), Bigambo Mtamwega (477), Dk Elias Missana (648), Hezron Tungaraza (693), Dk Deogratias Makalius (727), John Mkungu (775), Osward Mwizalubi (1,098), Maliki Malupu (1,443), Deogratias Lyato (1,824), Sumbuko Chipanda (2,016) na Magesa Boniphace (2,552).
Morogoro Mjini: Abdulaziz Abood amepata kura 20,094 na Simon Berege (429).
Mikumi: Jonas Nkya alipata kura 947 ameshinda dhidi ya Abdulsalum Sas (544).
Kilombero: Mbunge wa jimbo hilo, Abdul Mteketa alianguka baada ya kushika nafasi ya tatu kwa kupata kura 2,646 nyuma ya Abubakar Assenga aliyepata kura 6,629 na Abdul Liana 3,999.
Mlimba: Godwin Kunamba ameshinda kwa kura 6,233 Dk Fredrick Sagamiko (2,203), Jane Mihanji (2,073).
Gairo: Mbunge wa sasa, Ahmed Shabiby alishinda kwa kura 15,920 akifuatiwa na Omari Awadhi 886.
Morogoro Kusini Mashariki: Omary Mgumba alishinda kwa kura 3,393 akifuatiwa na Jamila Taji (2,914) na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dk Lucy Nkya (1,710).
Msoma Vijijini: Profesa Sospeter Muhongo aliibuka mshindi kwa kura 30,431 waliofuatia ni Anthony Mtaka (3,457), Evarest Mganga (2,556), Profesa Edson Mjungu (898), Mafuru Mafuru (421), Wits Onyango (392) na Nelson Semba (186).
Butiama: Nimrodi Mkono ameshinda kwa kupata kura 19,366, Chirstopher Siagi (2,457), Samweli Ndengo (745), Jacob Thomas (502), Mwita Wariuba (1,346), Moringe Magige (317), Godfrey Wandiba (303), Joseph Nyamboha (262) na Samweli Gunza (73).
Musoma Mjini: Vedastus Mathayo alishinda kwa kura 6,691 akifuatiwa na Paul Kirigini (1,174), Dk Msuto Chirangi (1,082), Juma Mokili (681), Deus Mnasa (378), Nicodemus Nyamajeje (183), Emmanuel Mwita (155), Felix Mboje (131) na Zerulia Mneno (61).
Kyela: Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Harrison Mwakyembe ameshinda kwa kupata kura 15,516, George Mwakalinga (4,905) na Martin Kipija (2,301).
Njombe Kusini: Edward Mwalongo (3,870), Romanus Mayemba (2,153),  Daniel Msemwa (1,976), Arnold Mtewele (1,136), Alfred Luvanda (978), Hassan Mkwawa (152),  Vitalis Konga (76) na Mariano Nyigu (86).
Makambako: Deo Sanga (7,643) Alimwimike Sahwi (499).
Ludewa: Deo Filikunjombe kabla ya kata tatu alikuwa na kura18,290 akiwaacha Kapteni Jacob Mpangala (205) na Zephania Chaula (770).
Wanging’ombe; Gerson Lwenge kabla ya kata tatu alikuwa na kura 11,322, Thomas Nyimbo (1,871),  Yono Kevela (1,819), John Dugange (466),  Richard Magenge (417), Abraham Chaula (382), Kennedy Mpumilwa (332), Hoseana Lunogelo (322), Malumbo Mangula (304), Nobchard Msigwa (216), Abel Badi (106) na Eston Ngilangwa (47).
Kiteto: Mjumbe wa NEC, Emmanuel Papian ameshinda kwa kupata kura 40,636 mbunge aliyemaliza muda wake Benedict Ole Nangoro (21,461), Amina Said Mrisho (2,118),  Ally Lugendo (287) na Joseph Mwaseba (250).
Bunda Mjini: Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira ameshinda kwa kupata kura 6,429 dhidi ya kura 6,206 alizopata mshindani wake wa karibu, Robert Maboto. Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Christopher Sanya alipata kura1,140, Exavery Lugina (846), Simon Odunga (547), Magesa Mugeta (446), Peres Magiri (385) na Brian Bitta (263).
Handeni na Bumbuli
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba wameshinda katika mchakato wa kura za maoni katika majimbo ya Handeni na Bumbuli.

Binti wa Sokoine atwaa mikoba ya Lowassa

Arusha. Binti wa Waziri mkuu wa zamani, Edward Sokoine, Namelock Sokoine ameshinda kura za maoni kugombea ubunge Jimbo la Monduli kupitia CCM huku mkwe wa Lowassa, Siyoi Sumari akishindwa Jimbo la Arumeru Mashariki.
Namelock ambaye ni mbunge wa Viti Maalumu (CCM) alipata kura 29,582 akifuatiliwa na Loota Sanare aliyepata kura 8,809 na nafasi ya tatu, ilichukuliwa na Lolinyu Mkoosu aliyepata kura 235 na Payani Leyani akipata kura 226.
Arumeru Mashariki: Sumari aliyewania jimbo hilo kwa mara ya kwanza baada kifo cha baba yake Jeremia Sumari na kushindwa na Joshua Nassari wa Chadema alipata kura kura 3,664 dhidi ya 12,071 za John Pallangyo. Mshindi wa tatu alikuwa ni William Sarakikya ambaye alipata kura 3,552 na wagombea hao waliwaacha mbali wapinzani wao wengine wanne.
Arusha Mjini: Katika Jimbo la Arusha Mjini, mfanyabiashara Philemon Mollel ameshinda kwa kura 5,320, akifuatiliwa na mfanyabiashara mwingine Justine Nyari aliyepata kura 1,894 na nafasi ya tatu, ilichukuliwa na Moses Mwizarubi aliyepata kura 1,205.
Karatu: Dk Willibrod Lorry alishinda baada ya kupata kura 17,711, Rajabu Malewa (911), John Dado (745) na Joshua Mwambo (67).
Masele ambwaga Mlingwa
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira),  Steven Masele amembwaga waziri mwingine wa zamani, Dk Charles Mlingwa baada ya kupata 70,900 dhidi ya 669 za mpinzani wake. Wagombea wengine Abdallah Seni alipata kura 391, Erasto Kwilasa (232), Hassan Athuman (164), Mussa Ngangala (116), Hatibu Malimi (69), Wille Mzava (65) na Tara Omari (43).
Ushetu: Elias Kwandikwa (11,554) Isaya Sino (5,241) na Elfaidi Sikuli (2,007).
Kahama Mjini: Jumanne Kishimba (9,754), Kintoki Godwin (433), Nkuba Charles (389), Bundala Maiko (284), Sazia Robert (257), Kapela Robert (135), Ngalawa Adamu (126), Luhende Jerard (106), Malele Charles (91), Tunge John kura (78), Mpangama Deogratias (57), Machunda Eliakimu (56), Masanja Andrew (48) na Kambarage Masusu (28).
Msalala: Ezekiel Maige (11,575), Emmanuel Kipole (1,197), John Sukili (962), Nicholas Mabula (668), Maganza Mashala (597), John Lufunga (29) na Wankia Welema (14).
Solwa:  Mbali ya matokeo ya kata moja ambayo imerudia uchaguzi, Ahamed Salum alikuwa akiongoza kwa kura 17,485 akifuatiwa na Amos Mshandete (2,028), Cyprian Mhoja (1,586), Luhende Richard (1,273), Kasile Paul (637), Gabriel Shija (361), Renatus Chokala (357) na Hosea Somi (255).
Kishapu: Kabla ya matokeo ya kata tatu, Suleiman Nchambi alikuwa akiongoza kwa kura 13,443, William Bonda (6,143), Kishiwa Kapale (500), Limbe Moris (393), Heke Bulugu (356) na Timoth Ndanya (193).
Mawaziri watamba Kanda ya Ziwa
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Titus Kamani ameshinda kura za maoni Jimbo la Busega baada ya kupata kura 10,697 dhidi ya mbunge wa zamani wa jimbo hilo, Dk Rafael Chegeni aliyepata kura 9,661. Buchosa: Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ameibuka mshindi kwa kupata kura 26,368 dhidi ya Eston Majaliwa aliyepata 9,213.
Misungwi: Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Kitwanga ameibuka mshindi kwa kura 26,171, akimwangusha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Jacob Shibiliti aliyepata kura 7,009. Shomari Chalamila alipata kura 1,840, Dk Makene Doshi (1,339), Cleophace Jerome (1,051).
Ilemela: Mkuu wa Wilaya ya Iringa Angelina Mabula ameibuka mshindi katika Jimbo la Ilemela kwa kupata kura 6,324 mbele ya Barnabas Mathayo (3,562), John Buyamba (1,167) na wagombea wengine 16.
Tabora Kaskazini: Almasi Maige (9,466), Shaffin Sumari (6,392) na Joseph Kidawa (5,965).
Bariadi: Andrew Chenge (20,200), Masanja Kadogosa (2,986) na Cosmas Manula (270).
Meatu: Salum Mbuzi (13,180), Oscar Maduhu (2,988), Romano Thomas (358) na Donard Jinasa (350).
Itilima: Njallu Daudi (44,486), Simon Ngagani (2,759) na Danhi Makanga (814).

Manji, Fella washinda Mbagala

Dar es Salaam. Wadau wawili wa michezo na burudani nchini; Yusuf Manji na Said Fella wameibuka kidedea katika kinyang’anyiro cha udiwani katika jimbo jipya la Mbagala jijini hapa.
Manji ambaye ni Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Quality Group, alishinda katika udiwani katika Kata ya Mbagala Kuu wakati Fella ambaye ni msimamizi wa kazi za wasanii na muasisi wa Kundi la Mkubwa na Wanawe, alishinda katika Kata ya Kilungure.
Fella ni Meneja wa mwanamuziki maarufu nchini, Diamond Platnumz, TMK Family na Yamoto Band.
Kaimu Katibu CCM Wilaya ya Temeke, Rutami Masunu alisema uchaguzi huo ulikwenda vizuri katika maeneo mengi isipokuwa changamoto kidogo katika kata moja ambayo itafanya uchaguzi huo leo.
Alisema tayari matokeo ya kata 28 kati ya 32 za wilaya yake yamewasilishwa ofisini kwake na baada ya kuyapitia na kukusanya taarifa zinazowahusu madiwani na wabunge na muda wowote leo atatoa taarifa kamili.
Vurugu Jangwani, Buguruni
Uchaguzi wa kumteua mgombea wa udiwani Kata ya Jangwani wilayani Ilala, umeingia dosari baada ya kikundi cha vijana wanaosadikiwa kutokea Kinondoni kuvuruga upigaji kura na kuvunja hema jambo lililosababisha polisi kuingilia kati.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Ramadhan Manda alisema jana kuwa kundi hilo linadaiwa kutumwa na watoto wa mmoja wa wagombea kutokana na dalili za wazi za kushindwa uchaguzi huo.
Mkazi wa Mtaa wa Mtambani B, Suleiman Maarufu alisema: “Saa nne asubuhi nilisikia vurugu nje, nikatoka na kuona kikundi cha vijana kutoka Tawi la Mkombozi kikivutana na mmoja wa makada ninayemfahamu. Wale vijana wakapiga teke masanduku, wakavunja hema… sasa wakati naingia kuamulia, wakanipa misukosuko na kipigo na baada ya kuamka nikakuta nimeumia unyayoni na kwenye goti.”
Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni, Ernest Chale alisema ni makundi matatu ya wagombea yaliyochangia kuibuka kwa vurugu hizo na kusababisha uchaguzi kutomalizika.
“Kutokana na haya yaliyotokea tutakaa vikao vya siasa kujadili, kwa maana hiyo hii kata itaendeshwa kama eneo maalumu. Kinachoonekana hapa mtu anatafuta uongozi kwa nguvu lakini uongozi unatolewa na Mungu, mimi naona ni bora akatulia kama anaona haki haitatendeka ni bora angesubiri akate rufaa.”
Mmoja ya wagombea wa udiwani, Abdul Faraji alisema: “Uchaguzi ilibidi ufanyike jana (juzi) na maeneo mengine lakini uliahirishwa kutokana na matatizo ya kwenye matawi… sasa tena unaahirishwa lakini hapa inaonekana bayana ni vigumu haki kutendeka.”
Katika Kata ya Buguruni wilayani Ilala, baadhi ya wanaCCM ambao tangu juzi walikesha kwenye ofisi cha chama hicho kulinda kura za wagombea udiwani, wanadaiwa kumshambulia Mjumbe wa Kamati ya Siasa, Tawi la Madenge, Ramadhani Mfinanga.
Tangu juzi saa tano usiku, wanaCCM hao wanaofikia 40 waliweka kambi katika ofisi hizo wakipinga matokeo ya kura za maoni zilizopigwa katika Tawi la Kisiwani.
Mfinanga alifika jana katika ofisi hizo na kusema matokeo hayatabadilishwa kauli iliyowakera na kuanza kumshambulia hadi alipojinasua baada ya kujichanganya na wafanyabiashara walioko katika Soko la Buguruni.
Mmoja wa wagombea wa udiwani katika Kata ya Buguruni, Barua Mwakatanga alisema walibaini kwamba kura zilizopigwa katika Tawi la Kisiwani zilikuwa 411 wakati idadi ya wapigakura ilikuwa 337.
Alisema walimweleza Katibu wa CCM, Kata ya Buguruni ambaye ndiye msimamizi wa uchaguzi, Abdul Kinogozi aliyewata wapeleke masanduku kwenye Ofisi za Kata ya Buguruni kwa ajili ya uhakiki.
“Tulipeleka lakini ilipofika saa tano usiku alisema amechoka na uhakiki utafanyika kuanzia saa mbili asubuhi leo (jana),” alisema.
WanaCCM hao waliamua kukesha ili kulinda kura hizo zisibadilishwe wakidai kuna njama za ‘kumbeba’ mgombea mmoja.

Mauzauza kura za maoni CCM



Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa kura za Moniwa Kta ya Kisukulu 
B,Christopher Masinde akionyesha kadi ya mpigakura 
halali kwa wajumbe wa mkutano huo jana wakati wa kuhakiki majina 
kabla ya kupiga kura kuchagua wagombea udiwani na ubunge kwenye 
jimbo la Segerea ,Dar es Salaam .

Dar es Salaam. Mauzauza jana yalitawala mchakato wa kura za maoni kwa ajili ya kupata wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya CCM kutokana na kuwapo kwa vitendo vya rushwa, vurugu, kura kuchomwa moto, makada kukamatwa, wanachama kutoruhusiwa kupiga kura na kugundulika kwa karatsi zilizokwishapigwa kura.
Kwenye baadhi ya maeneo kazi hiyo iliahirishwa hadi leo kutokana na vifaa kuchelewa na pia tatizo la kugundulika kwa shahada ambazo zimeshapigwa kura zikiwa ndani ya maboksi.
Lakini matukio yaliyotawala kura za maoni ni makada kukamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kugawa fedha au kuchapisha karatasi bandia za kupigia kura.
Dar es Salaam
Wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, Takukuru inawashikilia wagombea sita kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wajumbe ili wachaguliwe kwenye kura za maoni.
Makamu mkuu wa Takukuru wilayani Kinondoni, Denis Manumbu aliwataja waliokamatwa kuwa ni katibu wa kata ya Kibamba, Denisi Kalela, katibu wa itikadi, Babu Kimanyo, diwani wa viti maalumu wa Goba, Rehema Luhanja,
Wengine ni mwenyekiti kata ya Goba, Pili Mustafa, mgombea udiwani, Msigani Mwasha na Eliasi Nawera ambaye anagombea ubunge Jimbo la Kawe.
Alisema kuwa Kalela, na Kimanyo walikamatwa juzi saa 4:00 usiku maeneo ya Kibamba CCM, huku Mustafa na Luhanja wakikamatwa maeneo ya Goba Kati na Kawe.
“Walikamatwa wakiwa wanatoa rushwa na wengine walikamatwa wakiwa na kiasi cha pesa ambazo bado walikuwa wanazigawa huku wengine wakiwashawishi wajumbe kupokea rushwa,” alieleza Manumbu.
Manumbu alisema katika kipindi hiki cha uchaguzi ofisi yao inafanya kazi saa 24 ikipokea taarifa zote zinazohusu rushwa.
Kondoa
Lakini hali ilikuwa mbaya wilayani Kondoa, Dodoma ambako CCM ililazimika kuchoma moto makasha sita ya kupigia kura baada ya kubainika kuwa baadhi ya wanachama walitumia kadi ya CCM pekee bila ya kitambulisho cha kupigia kura.
Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Shaaban Kissu, mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Othman Gora na kamanda wa polisi wa wilaya, Nyantora walikubaliana kuchomwa moto baada ya kubaini tatizo hilo.
Hatua hiyo, inatokana na wanachama kuanzisha zogo kuwa vitambulisho vya kura havikutumika kabla ya uamuzi huo kufikiwa. Tayari zaidi ya wanachama 200 walikuwa wamepiga kura hizo.
Maboksi hayo yalichomwa mbele ya kituo cha kupigia kura cha Ubembeni na kushuhudiwa na wananchi, wananchama wa CCM, polisi na uongozi wa CCM.
Baada ya kuyachoma, Kissu alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo baada ya dosari hiyo na kwamba utarudiwa leo.
Baadaye kamanda wa polisi wa wilaya aliamrisha watu wote kutawanyika eneo hilo hadi leo.
Awali kulitokea vurugu baada ya baadhi ya wanachama kunyakua sanduku lililokuwa na kura na kutaka kukimbia nalo kwa tuhuma kuwa mawakala hawakuwa wakitenda haki kwa wapiga kura
Mbeya
Kashfa ya matumizi ya rushwa pia ilijitokeza mkoani Mbeya ambako mgombea udiwani mmoja kulalamikiwa kwa madai ya kuwakodisha wanafunzi wampigie kura kwa malipo ya Sh2,000 kwa kila mmoja.
Mgombea huyo wa udiwani wa Kata ya Mbalizi Road analalamikiwa pia alikwenda kwenye kilabu za pombe kuwatafuta watu wanaotaka kumpigia kura ili awanunulie kinywaji.
Miongoni mwa walalamikaji ni Ally Salum na Aziza Mbika wa eneo la Sabasaba ambao walisema walimwona mgombea huyo akitoa fedha na pombe kwa vijana mbalimbali .
Msimamizi wa uchaguzi wa Kituo cha Meta, Ndoni Mwakalukwa alikiri kupokea malalamiko ingawa hakushuhudia utoaji wa fedha hizo na kwamba atayazungumza baada ya kumaliza kazi ya upigaji kura.
Vituo vingine, vikiwamo vya Kata za Ruanda na Sinde, vilikosa wanachama wa kupiga kura na badala yake walifika mmoja mmoja kila baada ya saa kupita.
Wasimamizi wa uchaguzi maeneo hayo walikuwa na kazi ngumu ya kuwaita watu waliokuwa wakipita wakiwaomba wakapige kura kama ni wanachama wa CCM.
“Tatizo ni kwamba vituo vya kupigia kura havijawekewa alama yoyote, hivyo wanachama wengi hawajui,’’ alisema msimamizi wa kituo cha Soweto, Ambakisye Kitunga.
Lindi
Rushwa pia ilijitokeza kwenye Jimbo la Mchinga (CCM) ambako mbunge wa viti maalumu, Fatuma Mikidadi alikamatwa na Takukuru kwa tuhuma za kutoa rushwa kwa wafanyakazi wa taasisi hiyo waliomkamata kwa tuhuma za hongo.
Habari zinasema kuwa mgombea huyo alikutwa na wafanyakazi wa Takukuru akitoa rushwa kwa wanachama wa Kata ya Mchinga.
Alipotakiwa kuzungumzia tuhuma hizo, Mikidadi alikasirika akisema: “Uongo, uongo, huu ni uzushi kabisa.”
Alipoulizwa kwa nini anafikiri wamemsingizia, alisema: “sijui hawa wanasingizia singizia tu, uongo.” Hata hivyo, kamanda wa Takukuru wa mkoa wa Lindi, Steven Chami alisema Fatuma alikamatwa saa 5:00 usiku Kata ya Mchinga akigawa fedha kwa wanachama.
Chami alisema akiwa ofisi za Takukuru baada ya mahojiano, mtuhumiwa huyo alitoa tena Sh780,000 kwa ajili ya kuwahonga maofisa hao ili wasiendelee na suala hilo.
Alisema kutokana na kitendo hicho, Takukuru itamfikisha mahakamani muda wowote baada ya mwanasheria kutafsiri na kubainisha tuhuma zake.
Wakati huohuo, kamanda huyo alisema mgombea ubunge wa Jimbo la Lindi Mjini, Mohamedi Utali alishikiliwa kwa muda wa saa kadha kwa mahojiano na Takukuru baada ya kukutwa na Sh4milioni saa 8:30 usiku akiwa Kata ya Mbanja.
Chami alisema kukamatwa kwa mgombea huyo kulitokana na ushirikiano baina ya wananchi na taasisi hiyo.
Shinyanga
Mjini Shinyanga, katibu wa Kata ya Mjini Shinyanga, Ramadhani Majani amenusurika kipigo baada ya kukamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa ofisini kwake na mmoja wa wagombea udiwani na ubunge katika Jimbo la Shinyanga Mjini.
Mashuhuda wa tukio hilo waliwaeleza waandishi wa habari jana kwamba Majani alikutwa na kadhia hiyo baada ya watu waliotilia shaka nyendo zake kwa kitendo chake cha kuongozana na mmoja wa wagombea nyakati za usiku kuingia ofisini na hivyo kuhisi kuna jambo lisilokuwa la kawaida walilopanga kufanya.
Walisema waliamua kuwapigia simu wagombea wengine waliokwenda ofisi hizo na kumkuta mgombea mmoja (jina limehifadhiwa) akiwa anaongea naye, hata hivyo walishituka ghafla baada ya kuona kundi la wana-CCM wakijongea ofisini hapo.
“Sisi tulipigiwa simu usiku saa 4:45 na baadhi ya watu wanaoishi jirani na ofisi yetu ya kata kwamba wamemuona katibu kata wetu akiwa na mgombea udiwani pamoja na wapambe wake. Walidai inavyoelekea walikuwa wakipanga mikakati mibovu ya kutaka kuiba kura,” alisema Rashidi Abdalah.
“Taarifa hizo zilitushangaza sana. tuliamua kuchukua gari na kwenda katika eneo la ofisi na kweli tulimkuta katibu kata akiwa na mgombea (anamtaja jina) wakiwa nje ya ofisi za CCM wakitaka kuingia ndani, ghafla walipotuona mgombea na wapambe wake walikimbia na katibu kata aliingia ofisini na kuufunga mlango,” alieleza aliongeza.
Abdalah alidai kitendo cha Majani kukimbilia ofisini kilisababisha baadhi ya watu kushikwa na hasira na kutishia kuvunja mlango ili kumtoa nje na kumshushia kipigo, lakini mgombea
mwingine alimsihi ajisalimishe na kufanikiwa kutuliza ghasia.
Majani alikiri kutaka kupigwa na kundi la wana-CCM na kwamba ni kweli muda huo wa usiku alikuwa ofisini akifanya kazi ya kugonga muhuri kwenye karatasi za kupigia kura japo hakuweza kufafanua kitendo cha mmoja wa wagombea kuwa katika maeneo hayo nyakati hizo za usiku.
“Nilikuwa naendelea na kazi zangu lakini baadaye nilishangaa watu wanakuja na fimbo wakidai niko na mgombea ilibidi nijifungie ofisini kwangu,” alisema Majani.
Handeni
Hali ya sintofahamu ilitanda kwenye tawi la Bomani, Kata ya Vibaoni wakati zaidi ya wanachama 60 walipogoma kupigia kura wagombea udiwani kwa maelezo kuwa hawawafahamu kwa kuwa hawakufika eneo hilo kujinadi na badala yake kuamua kupiga kura ya wagombea ubunge.
Wakizungumza jana wakati wa kuwasubiri wagombea, wanachama hao walisema kuwa walikutana kuanzia saa 9:00 alasiri kwa ajili ya kuwasubiri, lakini hawakutokea hadi saa 12:00 jioni, kitu ambacho walidai kuwa ni dharau.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bomani, John Mohamed alisema kuwa walikubaliana kukutana na madiwani hao kwa mara ya kwanza, lakini akidi ya wanachama haikutimia ikawabidi kuahirisha kikao hicho hadi jana lakini kitu cha ajabu wagombea hao hawakutokea hadi jioni.
Arusha
Sakata la karatasi bandia za kupigia kura pia liliibuka mkoani Arusha, ambako viongozi wawili wa CCM walikamatwa kwa tuhuma hizo. Waliokamatwa ni katibu wa Kata ya Mjini Kati, Ally Meku na mwenyekiti wa Mtaa wa Bondeni, Yakub Shaban.
Katibu wa Wilaya ya Arusha, Feruz Bano alisema: “Ni kweli wamekamatwa, lakini tunafuatilia kujua kosa lao kwa kuwa hawana ofisi, hivyo walikuwa wanapeleka karatasi hizo kwenye chumba cha kupigia kura kidogo kidogo,” alisema.
Dodoma
Rafu iligubika uchaguzi huo mkoani Dodoma ambako baadhi ya wanachama walikamatwa na shahada bandia, huku vurugu zikiripotiwa maeneo kadhaa.
Waliokamatwa na tuhuma kuwa walikuwa na shahada bandia ni katibu wa vijana Tawi la Chang’ombe, Nasra Salum akiwa na shahada 20 za kupigia kura, 20 za udiwani, Bakari Fundikira (za ubunge), na David Malolle.
Mwingine aliyekamatwa kwa tuhuma hizo ni Faisi Mussa ambaye CCM imeeleza alikutwa na shahada 15 bandia.
Aidha, baadhi ya kata zilishindwa kufanya uchaguzi kutokana sababu mbalimbali ikiwemo kuchelewa kwa vifaa na karatasi za kupigia kura kuwa na makosa. Miongoni mwa kata zilizoshindwa kufanya uchaguzi huo ni Tambukareli na Kilimani mjini Dodoma.
Katibu wa CCM wa mkoa, Albert Mgumba alisema kata ambazo hazijafanya uchaguzi, kazi hiyo itafanyika leo kabla ya saa 4:00 asubuhi. Kuhusu makada waliokamatwa, katibu huyo alisema jambo hilo waulizwe makatibu wa wilaya kwa kuwa ndiyo wasimamizi wa uchaguzi huo.
Katika hatua nyingine, vurugu zimetokea katika tawi la Mji Mpya lililoko Kata ya Uhuru kutokana na baadhi ya wanachama kudai kuna mamluki wameingia kupiga kura.
“Asubuhi walikuja watu kutoka Tawi la Uhuru wakidai kuwa kuna mamluki wanataka kupiga kura kwenye tawi letu, lakini baada ya viongozi kufika tulirekebisha na zoezi likaendelea kwa amani na utulivu,” alisema msimamizi wa kituo hicho, Mariam Jumbe.
Bukoba
Hali ilikuwa tofauti mkoa Kagera ambako uchaguzi huo majina ya wanachama waliofariki dunia yalikuwapo kwenye orodha ya wapiga kura Jimbo la Nkenge huku kukiwa na hofu ya kuanguka kwa vigogo.
Hali hiyo ilitokea katika vituo vya Mutemba na Igayaza. Hata hivyo, katibu wa CCM wa Wilaya ya Missenyi, Mwajuma Mboha alisema kujulikana kwa majina hayo, ni matunda ya uwepo wa mawakala katika uchaguzi huo.
Pia kumekuwa na tatizo la kukosekana kwa majina ya baadhi ya watu waliofika kupigakura. Katika kata hiyo ya Nsunga kulikuwa na watu saba waliolalamikia kutoorodheshwa.
Mtwara
Kukosekana kwa majina katika orodha ya wapigakura pia ilijitokeza kwenye Manispaa ya Mtwara Mindindani.
Wakiongea na Mwananchi, Shangani Aisha Ismail na Salima Nassoro wa Tawi la Vigaeni walisema wanashangazwa na kitendo cha uongozi wa CCM kuwapa kadi za chama bila kuweka majina yao katika daftari la wapigakura.
“Sisi tumepewa kadi tunazo mikononi hatujui kama nyingine zimesajiliwa au la. Nyingine tumezilipia na majina yetu hayapo. Kuna kadi nyingine za mwaka 2000 hadi mwaka 1950 zipo na majina yao yapo na sisi majina yetu hayapo kuna nini hapa?” alihoji Aisha
Katibu wa itikadi na uenezi wa wilaya, Mohamed Watanga alikiri kuwapo na tatizo hilo, akieleza kuwa wanalitafutia ufumbuzi.
Njombe
Pia mkoani Njombe, wanachama walishindwa kupigakura kutokana na kadi zao za uanachama kuonekana kuwa zilikatwa baada ya Julai 15, siku ambayo CCM ilifunga kazi ya kuandikisha wanachama wapya.
Msimamizi wa uchaguzi wa kituo cha Mpechi, Sarah Nyandoa alisema licha ya uchaguzi kufanyika kwa amani, alikiri kuwapo kwa wanachama waliokuwa na kazi walizopata baada ya Julai 15.
“Ni kweli kuna baadhi ya watu wanakuja na kadi zao zilizochukuliwa baada ya Julai 18, lakini tumewarudisha baada ya kuwaelimisha wameridhika,” alisema Nyadoa.
Pwani
Mchakato kura za maoni umeingia dosari katika vituo kadhaa baada ya baadhi ya wanachama kukatwa majina yao kwenye daftari la orodha ya wanachama wa chama hicho.
Mbali ya kuwepo majina yaliyokatwa, pia baadhi ya wanachama walikutwa wakipiga kura kwa kutumia stakabadhi ya malipo ya wanachama maarufu badala ya kutumia kadi ya uanachama wa CCM.
Kasoro hizo zilisababisha vurugu kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura mjini Kibaha na kumlazimu mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini, Maulid Bundala kusitisha uchaguzi huo kwenye vituo kadhaa vilivyokua na kasoro.
Bundala alisema jana mchana kuwa vituo vilivyofutiwa kufanya uchaguzi ni Morning Star na Machinjioni vilivyoko Kata ya Tangini mjini Kibaha. Uchaguzi huo utarudiwa leo.
Alipoulizwa sababu za kuwepo tofauti ya idadi ya majina yaliyomo kwenye daftari la uanachama na idadi ya wenye kadi za chama eneo hilo, alisema wamebaini kasoro hiyo imesababishwa na baadhi ya mabalozi kutowasajili kwenye daftari la chama la wapigakura.
Katika hatua nyingine, baadhi ya wanachama waliokuwa wakipiga kura Kibaha Mjini wamelalamikia kuwepo rafu katika mchakato wa upigaji kura wakisema baadhi ya matawi yaliweka orodha kubwa ya wanachama wanaoruhusiwa kupiga kura ikilinganishwa na idadi ya awali iliyobandikwa kwenye kuta za ofisi za matawi yao.
Tarime
Mjini Tarime mkoa wa Mara, uchaguzi ulilazimika kuahirishwa hadi leo baada ya kukamatwa kwa karatasi bandia za kupigia zilizokuwa zimeshawekewa alama ya ndiyo kwa wagombea wa ubunge Jimbo la Tarime, na Tarime Mjini.
habari kutoka ndani ya CCM zinasema kuwa karatasi hizo zinazoendelea kukusanywa, zilitengenezwa na mmoja wa viongozi wa wilaya, Bernard Nyerembe ambaye amekamatwa na kufikishwa Takukuru kwa mahojiano zaidi.
Habari hizo zinasema kuwa karatasi hizo zilikuwa zichanganywe na karatasi halali baada ya wanachama kupiga kura za maoni.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya, Rashid Bogomba alithibitisha kukamatwa kwa karatasi hizo jana asubuhi.
Alisema kwa Jimbo la Tarime, kura hizo zimekamatiwa katika vijiji vya Nyamwaga, Masanga na Nyamongo na kwa Jimbo la Tarime Mjini zimekamatwa Mtaa wa Bomani, Magena na Romori.
Bogomba alisema kutokana na kukamatwa kwa karatasi hizo, uchaguzi umeahirishwa.
Kamanda wa polisi wa Tarime/Rorya, Benadict Mambosasa pia alithibitisha kukamatwa kwa Nyerembe na kwamba amepelekwa Takukuru kuhojiwa. Alisema Nyerembe alikamatwa akiwa ofisi ya CCM ya wilaya baada ya wanachama kumtuhumu kuwa alikuwa na karatasi zilizokwishapigwa kura kwa ajili ya wagombea wawili wa majimbo hayo.
Mwananchi ilipomtafuta Nyambari Nyangwine anayetetea ubunge wa Tarime, na Waziri Gaudensia Kabaka (Tarime Mjini) wote wwalikanusha kuhusika na kudai hizo ni njama zilizopikwa dhidi yao.
Makada wengine wanaowania ubunge wa Tarime ni Christopher Kangoye ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Arusha, Nyambari Nyangwine (mbunge), Pius Marwa, John Gimunta, Maseke Muhono, Lucas Mwita, Paul Matongo na Charles Machage.
Kwa jimbo jipya la Tarime Mjini wanaogombea ni Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, Maico Kembaki, Philipo Nyirabu, Jonathani Machango, Ditu Manko na Brito Burure.