BAADA ya serikali kupitisha miswada mitatu bungeni inayohusu ulinzi wa rasilimali za Taifa wiki iliyopita, Rais John Magufuli ametakiwa kujiandaa kwa mapambano makali zaidi katika siku zijazo.
Katika mapitio ya nyaraka mbalimbali na mahojiano na watafiti na sekta ya uziduaji yaliyofanywa na gazeti hili baada ya kupitishwa kwa miswada hiyo mitatu muhimu; imefahamika kwamba bado kuna kazi kubwa ya kufanywa katika kuhakikisha dhamira ya serikali kuwa Taifa linafaidika na utajiri wake inafikiwa.
Miswada ambayo ilipitishwa wiki iliyopita ni ile ya Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za Nchi wa Mwaka 2017; Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa Mwaka 2017 na ule wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2017.
Mmoja wa wanasheria na watafiti maarufu katika fani ya uziduaji, Dk. Rugemeleza Nshalla, ameliambia gazeti hili kwamba sheria hizo mpya haziwezi kuleta mabadiliko makubwa kama serikali haijaangalia pia mikataba ya pande mbili na pande tatu iliyoingia na nchi na jumuiya mbalimbali duniani.
Anapozungumzia pande mbili, Dk. Nshalla anazungumzia mikataba ile ambayo Tanzania imeingia na nchi moja moja (bilateral) na pande tatu ni ile ambayo imeingia na nchi zaidi ya moja (multilateral).
Alisema wakati sheria mbili mpya zilizopitishwa bungeni zinazungumzia migogoro ya kisheria kuamuliwa na mahakama za ndani, ipo mikataba ya pande mbili na pande tatu ambayo inasema wazi kwamba migogoro itaamuliwa na Mahakama za Kimataifa.
“ Ndiyo maana nasema sheria hizi zilizopitishwa zinanyimwa nguvu na mikataba ya pande mbili na pande tatu ambayo Tanzania iliingia huko nyuma na baadhi ya nchi na jumuiya za kibiashara.
“ Katika hilo hakuna la kufanya zaidi ya kuingia kwenye majadiliano upya na nchi hizo tulizoingia nazo mikataba ili tufanye marekebisho na huko pia. Bila hivyo, kazi yote hii iliyofanywa na serikali haitakuwa na maana inayotarajiwa,” alisema Nshalla ambaye amesomea shahada yake ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu maarufu cha MIT nchini Marekani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika baadhi ya mikataba ya pande mbili umeona vipengele mahususi vilivyowekwa vinavyosema wazi kwamba migogoro yote itapelekwa kwenye Mahakama za Kimataifa.
Kwa mfano, kwenye mkataba wa pande mbili kati ya Tanzania na Canada, kifungu cha 24 kinatamka bayana kwamba migogoro itapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID).
“ Pande hizi mbili zimekubaliana kwamba kama kutatokea mgogoro wowote unaohitaji usuluhishi, basi mgogoro utatatuliwa kwa kupitia sura ya pili ya mkataba wa ICSID au ibara ya pili ya mkataba wa New York, inasema ibara hiyo ya mkataba wa pande mbili kati ya Tanzania na Canada.
Canada ndiko makao makuu ya kampuni ya Barrick inayomiliki kampuni ya Acacia; ambayo imeingia katika sintofahamu na serikali ya Rais Magufuli katika mgogoro wa usafirishaji wa makinikia ya madini.
Kwa mujibu wa tovuti inayoeleza kuhusu mkataba huo kati ya Tanzania na Canadahttp://international.gc.ca/trade-commerce/trade-agreements-accords-commerciaux, mkataba wa pande mbili baina ya Tanzania na Canada, yaani A bilateral Foreign Investment Promotion and Protection Agreement (FIPA) uliingiwa rasmi Desemba, 2013.
Katika mazungumzo yake na Raia Mwema, Dk. Nshalla alisisitiza kwamba mikataba mingi ya pande mbili au tatu huingiwa kwa dhana potofu kwamba pande mbili zinazokubaliana zina uwezo sawa kiuchumi – jambo lisilo la kweli.
“ Utakuta Tanzania inaingia mkataba na Uingereza kuambiana kwamba yenyewe itapata fursa za kuwekeza kule na iachie huku fursa hizo kwa Waingereza. Lakini hata Mwalimu Nyerere aliwahi kuhoji huko nyuma, hivi Stamico au NDC zetu zinaweza kushindana na Waingereza kwenye mitaji huko kwao?”, alisema Nshalla.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema sheria hizo mpya zinapaswa kupongezwa kwa uzalendo wake lakini akasema kuna mambo yanatakiwa kusemwa lakini serikali haiyasemi.
Alisema dalili zimeanza kujionyesha kwamba mgogoro wa sasa unaweza kupunguza mitaji ya uwekezaji kutoka nje (FDI) kwa sababu wawekezaji hawana uhakika na mwelekeo mpya wa Tanzania.
Alisema kwa sasa dhahabu imekuwa ya pili kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni kwa Tanzania; ikizidiwa na sekta ya utalii pekee, na kwamba uwekezaji ukipungua, nchi itaanza kuumia kiuchumi.
“ Hatua zilizochukuliwa na serikali ni nzuri lakini inatakiwa iwaambie watu wajiandae na machungu yanayokuja. Makampuni ya nje yatataka kuonyesha umwamba wao kwetu kwa kupunguza uwekezaji.
“ Namna pekee ya kufanya ni kwa serikali kuongeza uuzaji nje wa mazao kama vile korosho, pamba, mawese, katani na pia kupunguza idadi ya bidhaa inazoagiza kutoka nje ili kupunguza matumizi ya fedha za kigeni.
“ Kwa maoni yangu, huu ndio wimbo ambao serikali ilitakiwa ianze kuuimba sasa kwa maana ya kuwaandaa watu na kile kinachoweza kutokea. Jambo ambalo silielewi ni kwamba serikali haiwaambii watu ukweli huu ili wajiandae na kinachokuja,” alisema Zitto ambaye alikuwa ni mmoja wa wabunge wa mwanzoni kabisa kuzungumzia suala la serikali kunyonywa mapato katika eneo la madini.
Mmoja wa wanaharakati maarufu nchini aliiyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yake, alifananisha kilichofanywa na serikali sawa na kitendo cha kumtishia uhai mtu ili muingie makubaliano na mtu huyo kwa kuwa katika hali hiyo anaweza kukubali chochote kuhofia maisha yake.
“Hapa inaonekana mkakati wa serikali ulikuwa ni sawa na kutishia kuua mtu kwa kumwekea bastola kichwani. Chochote kitachotokea kumnusuru maisha yake ataona ni ushindi.
“Yaani ifanye hali ionekane ngumu kwa mpinzani wako. Akipata chochote cha afadhali atashukuru. Baada ya kibano walichopewa hawa wawekezaji, serikali inaweza kupata faida ambayo isingeipata kama isingeingia na mkwara ilioingia nao,” alisema mwanaharakati huyo aliyedai kwamba mawazo ya taasisi yaliwasilishwa kwenye semina ya wabunge na asingependa mawazo yake binafsi nayo yawe hadharani.
Hata hivyo, mwanaharakati huyo alisema upo uwezekano wa baadhi ya kampuni ambazo tayari zimefanya uwekezaji kuamua kuondoka kwa kutoridhishwa na mazingira na huenda zikaenda kudai fidia kwenye Mahakama za Kimataifa.
“ Nitakupa mfano wa Statoil ya Norway. Wao wanadai kwamba hadi sasa tayari wamewekeza kiasi cha dola bilioni mbili (shilingi trilioni nne) katika utafutaji wa gesi na mafuta hapa nchini.
“ Sasa watu kama hawa wakiamua kwenda kudai fidia na kusema wanataka kuondoka huko walikoweka bima, si ajabu ukasikia tunatakiwa kulipa fidia ya shilingi trilioni nne. Sasa hapo kama Wachina hawajaja kutuokoa unadhani tutazitoa wapi hizo,” alihoji.
Kwa mujibu wa taratibu za biashara za kimataifa, kampuni kubwa huwa na utaratibu wa kuweka bima zao kupitia taasisi iliyo chini ya Benki ya Dunia (WB) iitwayo MIGA kwa lengo la kujilinda wakati wakiwekeza katika nchi za kigeni.
Kama ikitokea kwamba nchi walikowekeza imevunja mkataba isivyo halali, MIGA huwalipa wawekezaji hao hasara waliyoipata lakini taasisi hiyo huanza kudai fedha hizo katika nchi husika; ambazo zenyewe (kama ilivyokuwa kwa Tanzania), zilikubali utaratibu wa MIGA.
Kwa maana hiyo, kama nchi itakataa kulipa, kuna uwezekano wa WB na nchi nyingine tajiri maarufu zikazuia misaada yote inayopitia nchi zao hadi pale nchi inayodaiwa itakapolipa fedha hizo. MIGA pia inaruhusiwa kukamata mali za nchi inayodaiwa na taasisi hiyo.