Wednesday, July 26

Chai Huongeza Uwezekano wa Kupata Ujauzito?

Chai Huongeza Uwezekano wa Kupata Ujauzito?
  •  Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Marekani cha Boston umesema  unywaji wa chai vikombe viwili kwa siku huongeza uwezekano wa mwanamke kupata ujauzito. Katika utafiti uliohusisha wanawake 3,600 umeonyesha ya kwamba wanawake wanaokunywa vikombe viwili vya chai kwa siku wana asilimia 27 ya kupata ujauzito ikilinganishwa na wanawake ambao hawanywi  chai. Pia utafiti huo umeonyesha ya kwamba wanawake wanotumia  vinywaji baridi  viwili kwa  siku kama coca cola, hupunguza uwezekano wao wa kushika mimba kwa asilimia 20 na haijalishi kama vinywaji hivyo  vina sukari au la. 
Mtafiti  mkuu Profesa Elizabeth Hatch amesema alifanya utafiti huu ili kutaka kujua kama kuna uhusiano wowote wa kemikali aina ya caffeine inayopatikana kwenye chai, kahawa  na uwezo wa kushika mimba kwa wanawake.Utafiti huu ulifanywa kwa kuwahusisha wanawake wa kutoka  nchi ya Denmark   kutokana na nchi hiyo kuwa na mfumo wa kuwapa raia wao namba za uraia wa kudumu wakati wa kuzaliwa na hivyo kuwa rahisi kwa Profesa Hatch kuwafuatilia kwa njia ya intaneti kwa muda wa mwaka mmoja. 
Profesa Hatch amesema “Hatujui wanawake hawa walikuwa wakinywa chai ya aina gani, hatujui kama walikunywa chai bila kuongeza kitu chengine kwenye chai, kama waliongeza maziwa au limao kwenye chai, bali inaonekana kuna uhusiano wa caffeine na uwezo wa kushika mimba au uwezo huo umetokana na mfumo wa maisha wa wanawake hao au ni kutokana na  virutubisho vya chai hiyo”. 
Pia katika utaifiti huu wanawake waliambiwa waaandike kiwango cha chai ya kijani (green tea) au chai ya  tiba (herbal tea) wanayokunywa kwa siku na hakuna uhusiano wowote ulionekana kati ya chai ya kijani au chai ya tiba na kuongeza  uwezo wa kushika mimba kwa mwanamke. 
Tafiti zaidi zinahitajika ili kuweza kujua kama chai ya kijani husaidia wanawake kupata ujauzito au la. 
Ufuatiliaji zaidi utaweza kujua afya na saizi ya watoto wataokaozaliwa  na kina mama hawa wanaokunywa chai  vikombe viwili kwa siku na kama hawa wanawake waliweza kubeba mimba hizo kwa muda mrefu/mfupi au kama mimba hizo ziliharibika. 
Maha Ragunath, bingwa wa tiba ya uzazi katika kituo cha care fertility center cha Nottingham amesema “Kuna virutubisho maalum kwenye chai vinavyosaidia katika utungaji mimba. Chai huwa na kemikali nyingi aina ya anti-oxidants ambazo ni nzuri kwa uzazi kwa wanaume na wanawake lakini nadhani kwa wanawake wanaohitaji mtoto ni vizuri kunywa chai kwa kiwango cha wastani”. 
Laurence Shaw mkurugenzi katika kituo cha uzazi cha Bridge Fertility Centre jijini London amesema “Wanawake walio na umri zaidi ya miaka 35 wanaojaribu kushika mimba ni bora watafute ushauri kutoka kwa madaktari na si kunywa vikombe 10 vya chai eti kwa sababu wanataka mtoto”.  
Ni bora tusubiri matokeo zaidi ya wanawake ambao wamepata ujauzito wakati wa utafiti huu ili tupate majibu ya uhakika kuhusu maendeleo yao baada ya kushika ujauzito huo.

No comments:

Post a Comment