Thursday, July 2

Lukuvi: Marufuku kuchukua ardhi bila fidia.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.



Serikali imepiga marufuku halmashauri za wilaya na manispaa nchini, kuchukua ardhi ya wananchi bila kuwalipa fidia.
Amri hiyo imetolewa mjini hapa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani),   wakati akijibu malalako ya wananchi kuhusu upatikanaji na umiliki wa ardhi.
 
Lukuvi, alisema halmashauri na manispaa nchini, zimekuwa zikichukua ardhi ya wananchi bila makubaliano na kuwalipa fidia kwa kisingizo cha upimaji viwanja au kutoa maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji.
 
Alisema kitendo hicho ni dhuluma kwa wananchi na kwamba kamwe hakikubaliki.
 
Awali baadhi ya wakazi hao, walimlalamikia Waziri Lukuvi wakidai kuwa wamekuwa wakiporwa ardhi na maofisa wa halmashauri na manispaa bila maelezo.
 
Walidai wanapofuatilia kwenye ofisi zao, wamekuwa wakijibiwa vibaya na wakati mwingine kulipwa fidia kidogo ambayo haitoshi kununua kiwanja na kuwa  kero kubwa kwao na kukatisha tamaa.
 
Akizungumza huku akibubujikwa na machozi mbele ya Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani,  Zuhura Chavala, Mkazi wa Kijiji cha Migori, alidai maofisa ardhi wamekuwa wakiwadhulumu baada ya kuwaponya ardhi yao.
 
Zuhura alidai wanapofuatilia kwa lengo la kulipwa fidia, wamekuwa wakizungushwa hivyo kushindwa kujua hatma yao.
 
Wakati huo huo: Waziri huyo amewataka wakuu wa wilaya nchini kushiriki mikutano ya vijiji na  kutoa ardhi kwa wawekezaji ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
 
Alisema wakuu hao wanatakiwa kuwadhibiti baadhi ya viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakighushi mikutano hiyo na kuuza ardhi ya vijiji kwa wageni bila kupita kwenye mkutano mkuu wa kijiji.
 

Kilio bei mpya ya petroli kila kona.


Zikiwa ni siku mbili zimepita tangu Mamlaka ya Usimamizi wa Nishati na Maji (Ewura), itangaze kuongezeka kwa bei elekezi ya mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, wananachi wengi wameingiwa hofu kwa kuamini kuwa uamuzi huo utawaongezea makali ya maisha maradufu.
 
Juzi mamlaka hiyo ilitangaza ongezeko la bei elekezi ya mafuta na kuonyesha kuwa bei ya petroli imeongezeka kwa Sh. 232 kwa lita, dizeli Sh. 261 na mafuta ya taa Sh. 369. Katika soko la dunia, bei ya mafuta imekuwa ikishuka. Hata hivyo, taarifa ya Ewura ilitaja sababu za kupanda kwa bei ya nishati hiyo nchini kaunzia jana kuwa ni kuporomoka kwa thamani ya Shilingi na pia kuanza kutumika kwa tozo mpya za mafuta zilizopitishwa na bunge la bajeti kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
 
Kufuatia mabadiliko hayo, bei ya petroli kwa sasa jijini Dar es Salaam ni Sh. 2,198, dizeli Sh. 2,043 na mafuta ya taa ni Sh.1, 993; Arusha petroli Sh. 2, 282, dizeli Sh. 2, 127, mafuta ya taa Sh. 2, 077 huku maeneo mengine kama Bukoba bei ikiwa juu zaidi kwa petroli kuuzwa Sh. 2,413, dizeli Sh. 2, 258 na mafuta ya taa Sh. 2, 208.
 
TUCTA: BEI HII INAUMIZA WAFANYAKAZI 
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana,  Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gratian Mukoba, alisema, wafanyakazi wataumia zaidi kutokana na ongezeko hilo la bei ya mafuta kwani wanahitaji kutumia usafiri kwenda kazini huku wakiwa hawana marupurupu ya usafiri.
 
Mukoba aliongeza kuwa, ongezeko hilo pia litamuathiri mkulima kwa bei ya mazao kupanda kutokana na gharama za usafiri.
 
“Maoni yetu ni kwamba ukiongeza bei ya mafuta, unaongeza matumizi kwa mafanyakazi katika usafiri na chakula. Ni mzigo kwa mfanyakazi ukizingatia hawana ‘allowance ya commuter’ bajeti  ya usafiri,” alisema rais huyo. 
Alisema, serikali ilitakiwa kuangalia kitu kingine ambacho wangeongeza bei kisingeweza kuathiri  moja kwa moja.
 
CHAMATA: ONGEZEKO LIMETUATHIRI MNO
Kwa upande wake, Chama cha Madereva Tanzania, kimesema kuwa ongezeko hilo la bei ni kubwa na hivyo litaahiri madereva na kuwaneemesha wamiliki wa magari yao.
 
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid Salehe, alisema, bei hiyo ni kubwa kwani inawaumiza Watanzania wote kwani ndiyo wanaotumia usafiri wa pamoja.
 
“Athari ni kubwa… juzi tu ilikuwa Sh. 1, 900, sasa Sh. 2, 200. Tunaoathirika ni sisi tunaotumia usafiri wa pamoja,” alisema Salehe na kuongeza.
 
Hamad Mohamed, dereva wa daladala inayofanya safari zake kati ya Makumbusho na Posta, jijini Dar es Salaam, alisema, kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli kumewaathiri katika biashara hiyo ya usafiri kwani mabosi wao hawaguswi na hilo.
 
DARCOBOA: TUPENI MWEZI MMOJA
Umoja wa Wamiliki wa Mabasi ya Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), umesema kwa sasa unasubiri hali itakuwaje baada ya mwezi mmoja kabla ya kutoa maoni yao rasmi kuhusiana na  ongezeko hilo la bei ya mafuta.
 
Mwenyekiti wa umoja huo, Sabri Mabrouk, alisema, athari ni kubwa kwani bei imepanda kwa kishindo tofauti na kipindi cha nyuma ambacho ilikuwa ikipanda kati ya Sh. 50 na Sh. 60.
 
“Tumeshauriana na viongozi wenzangu, tuvumilie mwezi mmoja maana Ewura wana utaratibu wa kutangaza bei elekezi kila mwezi ili baada ya hapo tutoe madai yetu,” alisema mwenyekiti huyo.
 
TRAWU: HALI YA MFANYAKAZI KUWA MBAYA ZAIDI
Kaimu  Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu) Kanda ya Dar es Salaam, Yasin Mleke, alisema kupanda kwa bei ya mafuta nchini kutaendelea kusababisha maisha ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kuwa magumu kwa kuwa gharama ya usafiri itaongezeka na  bei ya bidhaa kuwa juu.
 
Aliishauri serikali kudhibiti mfumuko wa bei ili kuboresha maisha ya wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.

Lowassa: Nimechoka kuitwa fisadi

Wafuasi wa mbunge wa Monduli, Edward Lowassa 
wakimsindikiza nje ya ofisi za CCM Makao Dodoma jana
wakati wa kurejesha  fomu za kugombea urais.


Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa jana aliwataka wanaomhusisha na ufisadi kuacha mara moja kwa sababu hakuna hata chembe ya ukweli katika tuhuma hizo.
Lowassa, aliyeonekana kuzungumza kwa hisia, alisema hayo jana mara baada ya kurejesha fomu ya kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
Mbunge huyo wa Monduli alikuwa mmoja kati ya makada tisa waliorudisha fomu jana, ikiwa ni siku moja kabla ya kuisha kwa muda uliowekwa na chama hicho. Wengine waliorejesha fomu jana ni Elidephonce Bilohe, Mwigulu Nchemba, Luhaga Mpina, Dk Hamisi Kigwangalla, Hassy Kitine, Mariki Marupu, Dk Asha Rose Migiro na Lazaro Nyalandu.
Hadi sasa, tayari wanachama 32 kati ya 42 wa CCM walioomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wamerudisha fomu na kazi hiyo itahitimishwa leo.
Hakuna mtu ambaye amejitokeza hadharani kumtuhumu Lowassa kwa ufisadi, lakini tuhuma hizo zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na mbunge huyo wa Monduli kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu mwaka 2008 baada ya kuibuka sakata la mkataba wa ufuaji umeme wa dharura baina ya Serikali na Kampuni ya Richmond RDC ya Marekani ambayo ilionekana haina uwezo.
Wakati huo, Lowassa alisema kwenye hotuba yake ya kujiuzulu kuwa amefanya uamuzi huo “ili kuonyesha dhana ya uwajibikaji, lakini kutokubaliana na utaratibu uliotumika wa kusema uongo ndani ya Bunge kwa kumsingizia mtu.”
Akizungumza jana kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, Lowassa alirudia wito wake wa kutaka wenye ushahidi wa tuhuma hizo wajitokeze hadharani.
“Nataka nitumie fursa hii kuwataka wale wote ambao wamekuwa wakinituhumu kwa miaka kadhaa sasa na kunihusisha na suala zima la rushwa, nawaambia waache mara moja, kwani hakuna chembe hata ya ukweli wa maneno hayo,” alisema.
“Natoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi, autoe na aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani?”
Alisema yeye ni mwadilifu na anaposema atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu na bila kumuonea haya yeyote.
“Ndugu wanachama wenzangu na wananchi kwa jumla, ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema.
Ukumbi wa Whitehouse, jana ulijaa wana-CCM ambao walifika kushuhudia Lowassa akirudisha fomu tofauti na idadi iliyowahi kutokea kwa wagombea wengine kadhaa waliomtangulia. Hali hiyo ilisababisha foleni kwenye Barabara ya Mtaa wa Kuu unaopita mbele ya ofisi za CCM, na kusababisha usumbufu kwa wapita njia.
Lowassa alifika akiwa ameongozana na mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale Mwiru na wenyeviti wa chama hicho wa mikoa kadhaa pamoja na wabunge.
Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi Magharibi), Peter Serukamba (Kigoma Mjini), Diana Chilolo (Viti Maalumu), Profesa Juma Kapuya (Urambo Magharibi), Mary Chitanda (Viti Maalumu), Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk Makongoro Mahanga na Mary Mwanjelwa (Viti Maalumu).
Baadhi ya wenyeviti wa CCM wa mikoa waliomsindikiza ni Jesca Sambatavangu kutoka Iringa, Ramadhan Madabida (Dar es Salaam), Khamis Mgeja (Shinyanga), Mgana Msindai (Singida) na Joseph Msukuma (Geita).
Wa darasa la saba atia fora
Jana, Bilohe ambaye ni mgombea pekee mwenye elimu ya darasa saba, alitia fora kwa kushangiliwa na kupigiwa vigelegele na wananchi alipofika ofisi za CCM.
Bilohe, ambaye ni mkulima kutoka mkoani Kigoma, alipokewa kwa shangwe alipofika makao makuu ya chama hicho saa nane mchana, lakini hakuwamo kwenye orodha ya makada waliokuwa wanarudisha fomu, hivyo kulazimika kusubiri wanachama wengine wawili waliokuwa kwenye orodha.
Tofauti na makada wengine ambao si maarufu katika chama hicho, Bilohe alikumbatiwa na kupepewa na watu waliokuwa eneo hilo. Akitumia staili ya kupungia mkono watu, Bilohe aliyekuwa pekee yake, alishangiliwa hata baada ya kurejesha fomu yake ya kuomba kuwania kuteuliwa na CCM kuwania urais.
Akizungumzia safari yake ya kusaka wadhamini, alisema alipokewa vizuri na wana-CCM wenzake mikoani na hakuna aliyeonekana kujali kama yeye ni mkulima.
“Hatua hii inaonyesha ukomavu wa demokrasia ndani ya CCM. Watanzania mnapaswa kujivunia kwa kuwa Mungu kawaleta duniani na kuwachagulia Taifa mtakalozaliwa na kuishi,” alisema.
Alipoulizwa changamoto alizokutana nazo wakati wa kazi hiyo ya kusaka wadhamini, Bilohe alisema kuna baadhi ya sehemu alizokwenda ambako watu walitaka wapewe fedha ili wamdhamini.
“Umejiandaaje ilikuwa ni swali gumu sana? Wengine waliomba wapewe chochote na maji ya kunywa. Nikawaambia kwenye mkoba huu sijabeba fedha. Mimi ni mkulima wa kawaida. Nyie mna jukumu la kunidhamini kama chama. Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna pesa niliyowazawadia watu na nilipata udhamini kama chama kilivyoniagiza. Sina cha kuwalipa wote ambao waliacha kazi zao na kuja kunidhamini.”
Mwigulu aonya vurugu
Awali, Nchemba ambaye ni Naibu Waziri wa Fedha, aliwataka wanaoipinga Katiba Inayopendekezwa kufuata utaratibu wa kisheria badala ya kufanya fujo kwa sababu hata kile wanachokitaka watashindwa kukitumia.
“Tufuate utaratibu tusije tukagawanyika na kupigana, tusije kudhani kuwa nchi zilizopigana vita hazikuwa na Katiba nzuri, la hasha. Tufuate utaratibu wa kisheria ili kubadilisha kwa sababu hii si Biblia wala Quran Tukufu,” alisema.
Mwigulu alisema, katika safari yake ya kukusanya wadhamini, alikutana na utayari mkubwa na kuungwa mkono na wanachama wenzake, ambao alisema wengine walijitokeza wakati mwingine kuanzia saa mbili usiku hadi hata saa sita usiku ili mradi wamdhamini.
Mpina ataka mdahalo
Mbunge wa Kisesa, Mpina alikiomba chama chake kuandaa mdahalo kwa watu 42 waliomba nafasi hiyo ili waweze kuelewa vizuri watalifanyia nini Taifa.
“Nilikuwa nakiomba chama changu kiruhusu mdahalo kwa wagombea ili kila mmoja aweze kueleza atalifanyia nini Taifa kabla ya vikao vya uamuzi (kuchuja wagombea),” alisema.
Alisema katika safari yake ya kusaka wadhamini alikwenda na watu watatu kwa kutumia gari aina ya Toyota Noah na kuwashangaa wagombea wenzake ambao walitumia mabasi na mafuso kusomba wanachama kutoka maeneo mbalimbali.
“Hakuna mgombea hata mmoja anayenitia presha na  namuomba Mungu nipite na kuingia tatu bora,” alisema Mpina, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Biashara na Masoko.
Kigwangalla alia na ufisadi
kwa upande wake, Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega alisema Tanzania inahitaji mabadiliko na imechoshwa na ufisadi na kwamba akifanikiwa kuwa rais ataiongezea nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ili iweze kufanya kazi.
Alisema yuko tayari kushirikiana na mgombea yeyote atakayepitishwa na chama katika vikao vyote iwapo yeye hatateuliwa.
Kitine akomalia rushwa
Akizungumza jana, Dk Kitine ambaye ni mkurugenzi wa zamani wa Usalama wa Taifa alisema endapo atapitishwa, atakomesha rushwa ndani ya kipindi cha miaka miwili ya uongozi wake.
“Ninajua namna ya kushughulikia rushwa ambayo ni chanzo kikuu cha maovu nchini. Nitatumia miaka miwili kukomesha rushwa nchini,” alisema Kitine na kuongeza kuwa sheria ya kupambana na rushwa haitaacha mwanya kwa hakimu kutoa hukumu anayoiona yeye badala yake sheria itaainisha adhabu anayotakiwa kupata mtu atakayepatikana na hatia ya rushwa.
Marupu aonya wapambe
Baada ya kurejesha fomu, Marupu (34) ambaye ni mwanafunzi huyo wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aliwataka wagombea wenzake kuwa makini na wapambe wanaowaunga mkono wasije wakakipasua chama.
“Tunapata shida sisi wagombea, tunashindwa hata kusalimiana tukionana kwa kuogopa kupigwa na wapambe. Wagombea wenyewe hawana shida, shida ipo kwa wapambe. Mtatuua jamani,” alisema.
“Kama kuna mtu anamuabudu mgombea atuachie chama chetu. CCM haitapasuka nyie ndiyo mtapasuka nyote. Kama majina yatapita kama ilivyo nitawachakaza vizuri sana.”
Alisema amechukua wadhamini pia kutoka mkoa maalumu wa vyuo vikuu wa CCM.
Nyalandu ataka umoja
Waziri huyo wa Maliasili na Utalii, aliwataka wafuasi wa CCM kuimarisha kwa vitendo umoja ndani ya chama hicho.
Alisema katika ziara yake ya kutafuta wadhamini, aligundua kuwa vitu vinavyowaunganisha kama Taifa ni vingi kuliko vinavyowatenganisha.
Aliwataka pia wagombea wenzake na Watanzania kushiriki katika kupiga vita ubaguzi wa aina zote.

Chadema yaibwaga CCM mahakamani

Kiteto. Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imezidi kupata pigo baada ya Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji 16 vya mji mdogo wa Mirerani, kwa maelezo kuwa ulikiuka sheria na utaratibu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwezi mmoja kwa Mahakama kutengua matokeo ya uchaguzi huo ambao uliwaweka madarakani makada wa CCM.
Awali, Mei 30 Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kiteto ilitengua matokeo ya uchaguzi wa mwenyekiti wa Kijiji cha Lobosireti kwa kukiuka sheria na utaratibu.
Chadema ilifungua kesi kadhaa mahakamani hapo kupinga kitendo cha wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kufanya uchaguzi Desemba 14, mwaka jana.
Hukumu hiyo ya jana, inatokana na kesi zilizofunguliwa na Chadema wilayani Simanjiro kwenye kata za Endiamtu na Mirerani, wakipinga wagombea wa CCM kupewa ushindi bila kupigiwa kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana.
Hakimu Mkazi Mfawidhi mahakama hiyo, Elimo Massawe aliagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa viongozi wa vitongoji vya Zaire, Kisimani, Tenki la Maji, Endiamtu, Kairo na Kazamoyo vilivyoko Kata ya Ediamtu.
Hakimu Massawe alitaja vitongoji vingine kuwa ni Sekondari, Kilimahewa, Tanesco, Kazamoyo Juu, Mji mpya, Tupendane na vitongoji vya Kata ya Mirerani ambavyo ni Kangaroo, Songambele A, Getini na Songambele B.
Katika kesi hiyo, Chadema iliwakilishwa na mawakili James Millya, Shadrack Kimomogoro na Daudi Haraka na Mahakama iliamuru walipwe Sh160 milioni za gharama za kesi hiyo ambayo ilichukua takribani miezi sita hadi kutolewa hukumu.
Katibu Mwenezi wa Chadema mkoani Manyara, Ambrose Ndege alisema Mahakama imetenda haki kwa kutoa hukumu sahihi na wanajipanga ipasavyo kuhakikisha watashinda vitongoji vyote pindi uchaguzi huo utakaporudiwa.
“Tuliwaeleza tangu awali kuwa uchaguzi ukifanyika tutawashinda saa nne asubuhi hivyo tunawasubiri uwanjani na tutaongoza Mamlaka ya Mji wa Mirerani kwani wananchi wanatukubali,” alisema Ndege.
Hata hivyo, Katibu Mwenezi wa CCM wa Kata ya Endiamtu, Mashaka Jeroro alisema wanatarajia kukata rufaa kupinga hukumu hiyo akisema wagombea wa Chadema walikosea kujaza fomu ndiyo sababu wakawekewa pingamizi.

Maranda apangua kesi ya fedha za Epa

Dar es Salaam. Baada ya kupatikana na hatia katika kesi tatu za wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na hivyo kutumikia adhabu ya kifungo jela, hatimaye jana Kada wa CCM, Rajabu Maranda alipangua kesi mojawapo iliyokuwa ikimkabili.
Maranda alikuwa anakabiliwa na jumla ya kesi tano za Epa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, pamoja na wenzake akiwamo binamu yake na baadhi ya maofisa wa BoT.
Jana, Mahakama ya Kisutu ilitoa hukumu ya kesi ya nne kati ya tano zinazomuhusisha Maranda na kwa mara ya kwanza alishinda kesi hiyo na hivyo kuachiwa huru.
Maranda, ambaye hata hivyo alikuwa nje baada ya kumaliza vifungo katika kesi tatu alizokuwa ametiwa hatiani, aliachiwa huru jana baada ya Mahakama ya Kisutu kumuona hana hatia katika kesi hiyo.
Hukumu hiyo ilisomwa jana mchana na Hakimu John Utamwa kwa niaba ya jopo la mahakimu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo. Mbali na Utamwa ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama Kuu, mahakimu wengine katika jopo hilo ni Ignas Kitusi (sasa Msajili Mkuu wa Mahakama Kuu) na Eva Nkya.
 Katika kesi iliyotolewa hukumu jana, mbali na  Maranda washtakiwa wengine ambao pia waliachiwa huru ni pamoja na binamu yake Farijala Hussein, mfanyabiashara Ajay Somani na maofisa watatu wa BoT,  Iman Mwakosya, Ester Komu na Bosco Kimela.
Washtakiwa hao walikuwa wakidaiwa kuiba Sh207.3 milioni kutoka katika akaunti hiyo kwa kutumia nyaraka za kughushi, kuonyesha kuwa kampuni yao ya  Rashaz imepewa jukumu la kukusanya madeni kwa niaba ya Kampuni ya General Marketing ya India.
Walikuwa wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Septemba 8, 2003 na Agosti 18, 2008.
Hata hivyo, katika hukumu yake jana, Mahakama ya Kisutu iliwaachia huru washtakiwa wote baada ya kujiridhisha kuwa hawana hatia kwa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili.  Akisoma hukumu hiyo, Utamwa alisema, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili bila kuacha mashaka yoyote.