Sunday, January 19

Serikali yawabeba waliofeli kidato cha pili


Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakisubiri matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013, imebaini kuwa Serikali imetoa agizo kwamba wanafunzi wote waliofeli mtihani huo kuendelea na masomo ya kidato cha tatu, huku wakisoma mafunzo ya kurudia mtihani wa kidato cha pili.
Licha ya matokeo hayo kutotangazwa hadi sasa, imebainika kuwa waliofaulu mtihani huo uliofanywa Oktoba 7 hadi 21 mwaka jana ni asilimia 62 tu, asilimia 31 wakitakiwa kukariri (kurudia) kidato cha pili mwaka huu, huku asilimia saba wakishindwa mtihani huo kwa mara ya pili.
Jumla ya wanafunzi 531,457 walitajwa na Wizara ya Elimu mwaka jana kuwa watafanya mtihani huo.
Uamuzi huo wa Serikali ni tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa Novemba 4, mwaka 2012, kwamba kuanzia wakati huo mtihani wa kidato cha pili utakuwa ni wa mchujo na kwamba atakayefeli atatimuliwa.
Dk Kawambwa alisema matokeo ya mtihani wa kidato cha pili yatatumika kama kigezo cha kuchuja na kukariri kidato cha pili kwa watahiniwa watakaoshindwa kufikia wastani wa ufaulu wa alama 30.
Alisema mtahiniwa ataruhusiwa kukariri kidato cha pili mara moja tu na endapo mtahiniwa atashindwa mtihani kwa mara ya pili kwa mwaka utakaofuatia, itabidi aendelee na elimu ya sekondari nje ya mfumo rasmi.
Gazeti hili limeiona barua iliyoandikwa Januari 16 mwaka huu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kusainiwa na Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kwenda kwa wadau wa elimu nchini, wakiwamo maofisa elimu wa mikoa na Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule Binafsi (Tamongsco).
Katika barua hiyo, wizara hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani huo, wanaendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Matokeo ya kidato cha pili yamepokewa na kufanyiwa uchambuzi ili kupata taswira ya taifa. Taarifa ya matokeo hayo imebaini kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kufaulu ni sawa na asilimia 62 tu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo na kuongeza;
“Hali hii inaonyesha kuwa asilimia 31 ya wanafunzi watatakiwa kukariri kidato cha pili, 2014. Wale walioshindwa kwa mara ya pili ambao ni asilimia saba wanatakiwa kuendelea na masomo nje ya mfumo rasmi.”
Barua hiyo inaeleza kuwa wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 na kuendelea waendelee na masomo ya kidato cha tatu mwaka 2014, wakati awali Serikali ilitoa tamko kuwa watakaoshindwa kufikisha alama 30 watatimuliwa.
“Wanafunzi waliofaulu kwa wastani wa alama 20 hadi 39 wapewe mafunzo rekebishi ‘Remedial class’ wakiwa kidato cha tatu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.
Inaeleza kuwa uamuzi huo unawahusu wote wakiwamo wale walioshindwa kwa mara ya pili, “Kwa maana hiyo hakuna mwanafunzi atakayerudishwa nyumbani.”
Mwisho barua hiyo imewataka wadau hao kuhakikisha kuwa inawapa taarifa mameneja na wamiliki wa shule na seminari ili kusimamia utekelezaji wa uamuzi kuhusu matokeo hayo.
Kauli ya wizara
Akitolea ufafanuzi suala hilo, Profesa Mchome alisema, “Suala la wizara kuagiza wanafunzi wote waliofeli kuendelea na masomo ya kidato cha tatu mimi sijalisikia, ninachojua ni kwamba wapo watakaorudia.”
Alisema kuwa tayari wizara imeshapeleka taarifa za matokeo hayo na uamuzi wa Serikali katika kila kanda nchini. “Kila shule ina taarifa hizo. Wapo wanafunzi watakaorudia.”
Akizungumza kuhusu matokeo ya kidato cha pili mwaka 2013 kutotoka mpaka sasa alisema, “Ninachofahamu ni kwamba matokeo ya kidato cha pili yameshawasilishwa katika kanda zote nchini.”
“Unajua matokeo ya kidato cha pili siyo kama matokeo ya darasa la saba, kidato cha nne na sita. Matokeo ya kidato cha pili ni kama mwendelezo wa tathmini ‘Continuous assessment’ kwa mwanafunzi, hutumika pia katika mtihani wa kidato cha nne.”
Alisema ndiyo maana matokeo hayo hupelekwa katika shule husika. “Baada ya kupelekwa katika shule husika, hapo ndipo inaweza kutolewa taarifa za matokeo hayo pamoja na ufafanuzi.”
Kwa nyakati tofauti gazeti hili lilimtafuta Dk Kawambwa na Naibu wake, Phillip Mulugo ili kutolea ufafanuzi suala hilo, lakini simu zao za mkononi zilikuwa zikiita bila majibu.
Msimamo wa Tamongsco
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Tamongsco, Benjamin Nkonya kueleza kama wanakubaliana na agizo hilo la Serikali alisema, “Inaonekana Serikali haiko tayari kutekeleza mkakati wake wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).”
“Kama wizara inalazimisha wanafunzi walio na ufaulu mdogo kuendelea na masomo katika mfumo wa vidato (formal education), lazima tutegemee kuona wanafunzi wakifanya vibaya katika mitihani ya kidato cha nne.”
Alisema kuwa asilimia 98 ya wanachama wa chama hicho ni Watanzania wazalendo kwamba hawapo tayari kutekeleza agizo la Serikali kwa sababu siyo la kizalendo na limetolewa kwa ajili ya kutimiza malengo ya kisiasa ya kujiongezea umaarufu wa muda mfupi, huku Watanzania wakiogelea kwenye dimbwi la umaskini unaotokana na ujinga.
“Wachache watakaosaliti msimamo huu watakuwa wamekubali kupoteza muda wa vijana wetu huku wakijua kwamba watafika kidato cha nne, kupata daraja sifuri na kuishia kuwa machangudoa, wauza dawa za kulevya, bangi, wizi na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema.
Alisema ili kuwasaidia wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo yao; “Mwanafunzi ambaye ufaulu wake utakuwa chini ya asilimia 45 aondolewe katika mfumo wa elimu ya vidato (formal education) na kuingizwa katika mfumo wa elimu ya ufundi mchundo (TVET - Technical education and vocational education).”
Alisema wanachama wa Tamongsco wanamiliki vyuo 586 kati ya vyuo 750 vya ufundi mchundo (VETA) na wanamiliki vyuo 1975 kati ya vyuo 1988 vya ufundi stadi (technical institutes) ambavyo vinasimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi Stadi (NACTE).
“Vyuo hivi vina uwezo wa kuchukua wanafunzi wote ambao wana ufaulu wa chini ya asilimia 45 kuwaendeleza hadi chuo kikuu. Kikwazo pekee kilichopo ni kwa Serikali kukubali kuchangia gharama za uendeshaji wake.”
“Kikwazo hiki kitaondoka endapo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi itakubali kutekeleza sera, sheria na kanuni za ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) partnership) kama ilivyopitishwa na Bunge mwaka 2010.
Kidato cha pili 2012
Katika mtihani huo mwaka 2012 wanafunzi 136,923 kati ya 386,271 waliofanya mtihani huo walifeli. Idadi ya waliofeli ilikuwa sawa na asilimia 35.5, wakiwamo wasichana 74,020 na wavulana 62,903, waliofaulu walikuwa wanafunzi 245.9,32.

Rais Kikwete ateua makatibu


Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa makatibu tawala wapya wa mikoa mitano na kuhamisha wengine, huku akiwateua makatibu wa wizara wawili kuwa makatibu tawala wa mikoa.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue iliyotolewa jana usiku, ilieleza kuwa uteuzi na uhamisho huo ulianza jana.
Mhandisi Omari Chambo ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Uchukuzi anahamishiwa Mkoa wa Manyara kuwa Katibu Tawala wa Mkoa huo na Dk John Ndunguru aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi anahamishiwa Mkoa wa Kigoma kuwa Katibu Tawala wa mkoa huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, makatibu tawala wapya na mikoa yao katika mabano ni Wamoja Dickolangwa (Iringa), Abdallah Chikota (Lindi) na Symthies Pangisa (Rukwa).
Wengine ni Alfred Luanda (Mtwara) na Jackson Saitabau (Njombe).
Taarifa hiyo iliwataja waliohamishwa kuwa ni Beatha Swai aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani na sasa anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Sipora Liana ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI; Benedict Ole Kuyan ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tanga anahamishiwa Mkoa wa Mara na Salum Chima ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa anahamishiwa Mkoa wa Tanga.
Wengine waliohamishwa ni Mgeni Baruani ambaye alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe anahamishiwa Mkoa wa Pwani; Juma Iddi ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya anahamishiwa Jiji la Arusha.

BARAZA LA MAWAZIRI LABADILIKA

MH. BALOZI OMBENI Y. SEFUE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, amewahamisha na kuwateua baadhi ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kama ifuatavyo:-

1.0 OFISI YA RAIS
Hakuna mabadiliko.

2.0 OFISI YA MAKAMU WA RAIS

2.1   Waziri wa Nchi (Muungano) - Hakuna mabadiliko

2.2    Mhe. Eng. Dr. Binilith Satano MAHENGE (Mb)
Waziri wa Nchi (Mazingira).

2.3   Mhe. Ummy Ali MWALIMU (Mb)
Naibu Waziri

3.0 OFISI YA WAZIRI MKUU

Hakuna mabadiliko

4.0 WIZARA
4.1 WIZARA YA FEDHA
4.1.1 Mhe. Saada Mkuya SALUM (Mb)
Waziri wa Fedha
Mhe. Mwigulu Lameck NCHEMBA (Mb)
Naibu Waziri wa Fedha
4.1.2 Mhe. Adam Kighoma Ali MALIMA (Mb)
Naibu Waziri wa Fedha

4.2 WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Hakuna mabadiliko

4.3 WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
4.3.1 Mhe. Dkt. Asha-Rose Mtengeti MIGIRO (Mb)
Waziri wa Katiba na Sheria

4.3.2 Naibu Waziri - Hakuna mabadiliko

4.4 WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
Hakuna mabadiliko

4.5 WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA

4.5.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

4.5.2 Mhe. Janet Zebedayo MBENE (Mb)
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara

4.6 WIZARA YA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA
Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi (Mb)
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

4.7 WIZARA YA UJENZI

Hakuna mabadiliko

4.8 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

4.8.1 Mhe. Mathias Meinrad CHIKAWE (Mb)
Waziri wa Mambo ya Ndani

4.8.2 Naibu Waziri - Hakuna Mabadiliko

4.9 WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
4.9.1 Mhe. Dkt. Seif Seleman RASHIDI (Mb)
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii

4.9.2 Mhe. Dkt. Kebwe Stephen KEBWE (Mb)
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii

4.10 WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
4.10.1 Waziri: Hakuna mabadiliko

4.10.2 Mhe. Jenista Joakim MHAGAMA (Mb)
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi

14.11 WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO

14.11.1 Waziri: Hakuna mabadiliko

14. 11.2 Mhe. Dkt. Pindi Hazara CHANA (Mb)
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto

14.12 WIZARA YA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI
14.12.1 Mhe. Dkt. Titus Mlengeya Dismas KAMANI (Mb)
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi

14.12.2 Mhe. Kaika Saning’o TELELE (Mb)
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi

14.13 WIZARA YA KAZI NA AJIRA

Hakuna mabadiliko

14.14 WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Hakuna mabadiliko
14.15 WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI
14.15.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

14.15.2 Mhe. George Boniface Taguluvala SIMBACHAWENE (Mb)
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

14.16 WIZARA YA MAJI
14.16.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

14.16.2 Mhe. Amos Gabriel MAKALLA (Mb)
Naibu Waziri wa Maji

14.17 WIZARA YA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA

14.17.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

14.17.2 Mhe. Godfrey Weston ZAMBI (Mb)
Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika

4.18 WIZARA YA UCHUKUZI
Hakuna mabadiliko

4.19 WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
4.19.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

4.19.2 Mhe. Juma Selemani NKAMIA (Mb)
Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo

4.20 WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
4.20.1 Mhe. Lazaro Samuel NYALANDU (Mb)
Waziri wa Maliasili na Utalii

4.20.2 Mhe. Mahmoud Hassan MGIMWA (Mb)
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii

4.21 WIZARA YA NISHATI NA MADINI

4.21.1 Waziri - Hakuna mabadiliko

4.21.2 Naibu Waziri (Madini) - Hakuna mabadiliko

4.21.3 Mhe. Charles Muhangwa KITWANGA (Mb)
Naibu Waziri (Nishati)

Balozi Ombeni Y. Sefue
KATIBU MKUU KIONGOZI
Ikulu
DAR ES SALAAM
19 Januari, 2014