Monday, April 15

Mbowe, Slaa: Hatukubali Chadema kuhujumiwa

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe akizungumza kwenye kongamano la chama hicho lililofanyika jana jijini Dar es Salaam. Picha na Fidelis Felix.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa wamesema “hawatakubali wala kuvumilia” hujuma dhidi ya chama chao.
Dar es Salaam. Viongozi hao kwa nyakati tofauti jana walisema hujuma hizo zimekuwa zikifanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Serikali ambayo imekuwa ikitumia vyombo vya dola na kwamba sasa wanapanga ugaidi wa kuwateka maofisa wa ngazi ya juu wa Chadema.
Suala la ugaidi liliibuka kwa nguvu katika wiki ya kwanza ya Bunge la Bajeti na sasa limehamia nje ya chombo hicho cha kutunga sheria kutokana na Chadema kuwatuhumu CCM na Serikali yake kwamba wanapanga njama za kuwateka maofisa wakuu wa chama hicho.
Jana Dk Slaa alipokuwa akimkaribisha Mbowe kufungua Mkutano wa Mafunzo na Mipango ya Vuguvugu la Mabadiliko ‘M4C’ na Kongamano la Katiba Mpya kwa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, alisema taarifa walizonazo zinaonyesha kuwa CCM ndiyo wanaofanya vitendo vya kigaidi wakishirikiana na Serikali.
“Tuna taarifa zote zinazoonyesha kwamba CCM ndiyo magaidi wakishirikiana na Serikali yake, lakini sisi tuko makini kuliko hata Serikali ya CCM na tuko makini kuliko hata Usalama wa Taifa na umakini huu ndiyo utakaotupeleka Ikulu mwaka 2015,”alisema Dk Slaa.
Hata hivyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alipotafutwa kujibu tuhuma hizo alisema hakuna jipya ambalo Chadema wamelisema.
“Kuna jipya katika hilo, ni yale yale ya kawaida na jana (juzi) Mwingulu alizungumza vizuri sana bungeni. Hiyo ni sawa na mchawi anapomwangia mtu na kufa anakuwa wa kwanza kwenda kulia msibani, nchi siku yoyotete haijengwi kwa ngonjera za maneno bali inajengwa kwa mipango,”alisema Nape.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima alipotakiwa kutoa msimamo wa Serikali juu ya tuhuma hizo alisema, “Mimi siwezi kuzungumza ila mtafute Waziri (Dk Emmanuel Nchimbi),”alisema Silima.
Alipotafutwa Dk Nchimbi kupitia simu yake ya mkononi, ilikuwa ikiita bila kupokewa.
Kauli ya Mbowe
Kwa upande wake Mbowe alisema, CCM imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali kuhakikisha inakisambaratisha chama hicho bila mafanikio.
“Watu wa Usalama wa Taifa wakishirikiana na CCM wamekuwa wakifanya mipango ya kutaka kuwateka maofisa wetu. Hawa watu ni wepesi sana na msiwaogope hata kidogo,”alisema Mbowe huku akishangiliwa na wanachama na makada waliofurika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl.
Mbowe alisema: “Ukiona chama chochote tawala kinatumia jeshi la polisi kutengeneza ushahidi wowote wa kihalifu hiyo ni dalili ya hatari kwa mustakabali wa usalama wa nchi.”
Mbowe alisema mbinu za sasa za CCM zinatokana na kushindwa kukivuruga chama hicho kwa propaganda kuwa ni chama cha familia, ukabila, ukanda na baadaye udini.
Katiba na Elimu
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Mbowe alisema ikiwa itafika Aprili 30 mwaka huu bila hatua zozote kuchukuliwa, watamwamuru mjumbe wa tume hiyo kutoka Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kujiondoa.
Chadema kinataka Serikali iwasilishe bungeni, muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba ili yafanywe marekebisho mbalimbali kuhusu uwakilishi katika Bunge Maalumu la Katiba.
“Serikali inaona hili kama mchezo, sasa acha wakae kimya na baada ya Aprili 30 mwaka huu watachagua kusuka au kunyoa,”alisema Mbowe.
Kuhusu elimu, Mbowe alieleza kushangazwa na kile alichosema kuwa ni Serikali kutofahamu sababu za wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao.
“Serikali eti haijui na kama haijui basi Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) hatakiwi kuwa hapo alipo, kwani haiwezekani watoto wanafeli halafu anaunda tume,”alisema Mbowe na kuongeza:
“Mwaka 2011 waliunda tume ambayo ilitoa mapendekezo 27 lakini ripoti hiyo ilifichwa hadi mimi juzi (Jumatano) nilipoisoma bungeni wabunge wa CCM wakabaki vichwa chini.”
Alisema kuundwa kwa tume nyingine ambayo itatumia fedha za walipakodi ni kuwaumiza Watanzania ilhali tatizo na chanzo kinajulikana.
Ugaidi bungeni
Juzi wakati wa mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wabunge wa CCM na Chadema kwa nyakati tofauti walituhumiana kwa ugaidi kiasi cha kusababisha vurugu na kutoelewana miongoni mwao.
Alhamisi akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani, Mbowe alisema ugaidi ni ubunifu wa polisi na Serikali kwa ajili ya kuwabambikia kesi zisizo na dhamana kwenye mahakama maofisa wa vyama vya upinzani.
Kutokana na hotuba hiyo, Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba aliishambulia hotuba ya Mbowe akieleza kuwa wanahusika kupanga kumdhuru mwandishi wa habari.

ADHANA YARUHUSIWA SWEDEN KWA MARA YA KWANZA

Msikiti mmoja katika kitongoji cha mji mkuu wa Sweden, Stockholm umeruhusiwa kuadhini kwa kutumia kipaza sauti kilicho kwenye mnara kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Hii ni mara kwa kwanza kwa nchi hiyo ya Scandinavia kuruhusu adhana kwa sauti inayosikika nje ya msikiti.

Idara ya polisi mjini Stockholm imesema msikiti huo utaruhusiwa kuadhini kwa muda wa kati ya dakika tatu na tano katika kipindi cha baina ya saa sita na saa saba mchana kila Ijumaa.

Mkuu wa Jumuiya ya Utamaduni wa Kiislamu katika eneo la Botkyrka kusini mwa Stockholm Bw. Ismail Okur ameupongeza uamuzi huo. Ombi la kuadhini kwa sauti inayotoka nje ya msikiti liliwasilishwa miaka mitano iliyopita.

Kuna karibu Waislamu 7,000 katika eneo hilo na aghalabu wana asili ya Uturuki.

Chama chenye chuki dhidi ya Uislamu cha Sweden Democrats kimepinga uamuzi huo.

Katika miaka ya hivi karibuni, idadi ya Waislamu barani Ulaya imeongezeka kwa kasi na sambamba na hilo hitajio la misikiti pia limeongezeka. Waislamu raia wa nchi za Ulaya wamekuwa wakibaguliwa kwa muda mrefu na sasa wanapigania haki sawa na raia wengine wa Ulaya.