Thursday, December 12

Mandela Kuzikwa Kimila,ng'ombe dume kumsindikiza kaburini


Johannesburg.
Ng’ombe dume (fahali) atachinjwa kisha kuwekwa katika kaburi atakamozikwa Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela, Kijiji cha Qunu, Mthatha Jimbo la Eastern Cape Jumapili hii.
Viongozi wa kimila wa Kabila la AbaThembu wametoa mwito kwa Serikali ya Afrika Kusini isiingilie taratibu za mazishi ya kiongozi huyo na kuonya kwamba ikifanya hivyo, ‘Mandela hatapokewa na miungu’ na kwamba roho yake inaweza kurejea na kuathiri familia.
“Jumapili baada ya mwili wake kuwekwa katika kaburi lake, taratibu zote za kimila zitafanywa na Himaya ya Kifalme,” alisema Kiongozi wa Jamii ya Xhosa, Nokuzola Mndende baada ya kutembelea familia ya Mandela, nyumbani kwao Houghton, Johannesburg na kuongeza:
“Zitakuwa ni mila na desturi za jadi, Serikali inapaswa kutupa nafasi na isituingilie. Fahali (ng’ombe dume) atachinjwa kwa ajili ya kumsindikiza, ni familia ya Mandela pekee watakaohusika na taratibu hizi za kumwandalia safari njema.”
Mandela anazaliwa katika Kabila la AbaThembu ambalo linazungumza Ki- Xhosa na kwa mujibu wa taratibu za kabila hilo, hata mwili wake utashushwa kaburini na viongozi wa kimila.
Hata hivyo, habari zaidi kutoka Qunu zinasema licha ya taratibu za kimila, pia kutakuwapo taratibu za Dini ya Kikristo, ambayo Mandela alikuwa muumini wake.
Kusafirishwa Jumamosi
Jumamosi Decemba 14, mwili wa Mandela utasafrishwa kutoka Uwanja wa Ndege wa Jeshi wa Waterkloof, Pretoria hadi Mthatha, Eastern Cape kwa ajili ya mazishi Jumapili.
Viongozi wa juu wa Chama Tawala cha ANC, watatoa heshima za mwisho muda mfupi kabla ya mwili huo kusafirishwa.
Taarifa ya Idara ya Habari na Mawasiliano ya Afrika Kusini (GICS), ilisema Jeshi la Afrika Kusini (SANDF), ndilo litakaloongoza shughuli zote za kuagwa kwa mwili wa Mandela.
Gwaride la heshima la askari wa SANDF litausindikiza mwili wa Mandela uwanjani hapo na baadaye gwaride kama hilo litatoa heshima, wakati mwili huo utakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Mthatha, huku askari wake wakihusika na kuuchukua kutoka kwenye ndege.
Jeneza lililobeba mwili wa Mandela litawekwa katika gari jingine maalumu. Wimbo wa Taifa utapigwa ukiongozwa na SANDF, wakati heshima za kijeshi zikitolewa.
Taarifa hiyo ya Serikali inasema baada ya taratibu hizo, mwili huo wa Mandela utasafirishwa hadi Kijijini Qunu ambako Kabila la AbaThembu watafanya taratibu za kimila.
Hitimisho la siku 10 za maombolezo ya msiba wa Mandela itakuwa Jumapili, Desemba 15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa katika makaburi ya familia.

Wakati wa mazishi SANDF pia wamepewa jukumu la kusimamia upelekaji jeneza makaburini na heshima za kitaifa zitatolea pamoja na wimbo wa Taifa kupigwa kabla ya maziko.

Graca, Winnie Mandela ni mtu na ‘dada yake’


Winnie Madikizela-Mandela, (77) aliinama kumbusu Graca Machel (68), kabla ya kukaa katika kiti cha tatu kutoka kile alichokalia mwanamke huyo. Graca Machel alimwambia maneno machache ‘dada yake’ Winnie wakati akimbusu.
Wanawake hao wote wakiwa wamevalia majaketi meusi na vilemba, walikumbatiana kwa sekunde kadhaa huku Winnie akitabasamu na Graca akitazama mbele.
Wote wawili wanaheshimika nchini Afrika Kusini kutokana na sababu mbalimbali. Winnie anaheshimika kwa mchango wake mkubwa wa kupigania ubaguzi wa rangi; Graca kwa moyo wake wa kujitolea kumtunza kiongozi wao mpaka anafariki dunia.
Hata hivyo Winnie amekuwa akikosolewa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ile ya kuruhusu wapinzani wake wauawe kwa kuchomwa moto wakitumia mafuta ya petroli na matairi ya magari.
Mwaka 1988 alipatikana na hati ya kumuua kijana wa miaka 14 ambaye ilidaiwa alimtuhumu kuwa kibaraka, hata hivyo hukumu yake ilipunguzwa kutoka kuwa kifungo cha miaka sita jela na kuwa faini.
Winnie pia anatuhumiwa kwa kutokuwa mwaminifu katika ndoa yake iliyodumu kwa miaka 38 ingawa 27 kati ya hiyo hakuwa na mumewe ambaye alikuwa akitumikia kifungo katika gereza la Robben.
Graca Machel alifunga ndoa na Mandela wakati wa sherehe yake ya kutimiza miaka 80. Pamoja na kuwa Winnie na Mandela walitengana, katika kipindi cha ugonjwa wake kilichodumu kwa siku 181, alikuwa akimtembelea mara kwa mara.
Mjane wa Mandela, Graca,ambaye pia ni mjane wa Rais wa zamani wa Msumbiji, Hayati Samora Machel, alitumia muda wote kuwa pembeni mwa kitanda cha Mandela mpaka alipokata roho.
Ndugu wa karibu wanasema, daktari aliposema hakuna kitu kinachoweza kufanyika kuokoa uhai wa Mandela, Winnie alifika nyumbani hapo na alikuwepo muda wote mpaka kiongozi huyo alipokata roho.
Tangu Mandela afariki, Winnie amekuwa akionekana sana tofauti na Graca. Jumapili ya wiki iliyopita, ikiwa ni siku tatu tangu Mandela afariki, Winnie alikwenda kusali katika kanisa ambalo lilikuwa likifanya misa kuu ya kitaifa kumuombea Mandela .
Winnie alikaa pembeni ya Rais Jacob Zuma. Hata hivyo siku yake iliharibia na Mchungaji, Mosa Sono aliyekuwa akiongoza ibada hiyo baada ya kumtambulisha kwa jina la Graca. Kwa upande wake Graca alisali katika kanisa dogo lililopo karibu na nyumba ya Mandela.
Graca ni mdogo wangu
Kwa muda mrefu sasa Winnie amekuwa akisisitiza kuwa hakuna uhasama baina yake na Graca na anamuona kama mdogo wake kwa kuwa kiumri pia amemzidi.
Winnie aliwahi kunukuliwa akisema: “Namuita mdogo wangu, na yeye huwa ananiita dada, hata tunapozungumza huwa maongezi yanamuhusu mume wetu,” anasema Winnie.
Dunia yamuaga Mandela kwa heshima ya kipekee
Dunia imeamua kumpa heshima ya kipekee Nelson Mandela kwa mkusanyiko wa aina yake wa kumuaga kwenye kitongoji cha Soweto, ambapo zaidi ya viongozi 100 wa dunia wanahudhuria ibada hiyo.
Tangu viongozi walioko madarakani mpaka waliostaafu, halijawahi kushuhudiwa kuwa na watu wengi kiasi hiki; zaidi ya watu 95, 000 wamefurika uwanjani tangu usiku wa manane kuhakikisha wanapata nafasi.
Kitongoji hicho cha Jonnesburg ndiko alikokuwa akiishi Mandela kabla ya kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa miaka 27, kwa hivyo ni mahala pa kihistoria kutoa heshima za mwisho kwa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi.
Kiasi cha viongozi 100 wanahudhuria, wakiwamo wa mataifa na Serikali, wafalme au warithi wao, achilia mbali watu wengineo mashuhuri duniani ikiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon.
Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma, na wajumbe wa Baraza la Wazee la Kimataifa aliloliunda mwenyewe Nelson Mandela, akiwamo Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter.
Marekani inawakilishwa na Rais Barack Obama na mkewe pamoja na marais wa zamani, George W. Bush na Bill Clinton na mkewe, waziri wa zamani wa mambo ya nchi za nje, Hillary Clinton.
Viongozi wengine ni pamoja na Rais Raul Castro wa Cuba, Hamid Karzai wa Afghanistan, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, na Mwana wa mfalme Charles, Rais Pranab Mukhrejee wa India, Rais Dilma Russels wa Brazil na watangulizi wake wanne ikiwa ni pamoja na Lula da Silva,
Waziri mkuu wa Italia Enrico Letta, Kiongozi wa Mamlaka ya Utawala wa Ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas na mawaziri wakuu wa Norway, Sweden na Canada, kwa kuwataja wachache tu.
China inawakilishwa na Makamu wa Rais, Li Yuanchao huku Japan ikiwakilishwa na mrithi wa kiti cha mfalme, Mwanamfalme Naruhito. Ujerumani inawakilishwa na Rais Joachim Gauck. Takriban viongozi wote wa bara la Afrika wanahudhuria pia ibada hiyo.
Ibada kuendelea
Ibada kadhaa nyingine zinafanyika hadi siku ya mazishi ya Mandela katika kijiji walichotokea wazee wake, Qunu, Desemba 15.
Mbali na ibada rasmi ya mazishi, maiti ya Nelson Mandela imewekwa katika Ikulu kuanzia Jumatano hadi ijumaa itakaposafirishwa kwa ndege hadi Mashariki ya Cape Town kwa mazishi.
Hatua za ulinzi zimeimarishwa. Afrika Kusini inauzoefu kutokana na maandalizi ya Kombe la Dunia la mwaka 2010.
Waziri wa Ulinzi, Nosiviwe Mapisa-Nqakula, amesema,”Kila kitu kiko tayari, tumejiandaa tangu miaka mitatu au minne iliyopita.”
Makala hii imeandikwa na Julieth Kulangwa kwa msaada wa vyombo vya habari.

Azimio la kuwataka Ghasia, Mwanri na Majaliwa kujipima lapitishwa


Dodoma.Bunge limepitisha azimio la kuwataka mawaziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kujipima iwapo wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo nyeti.
Azimio hilo lilipitishwa jana na wabunge kwa kura ya ndiyo bila kupingwa, baada ya kuhojiwa na Spika wa Bunge Anne Makinda iwapo wanaipokea taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Laac) iliyowasilishwa na Mwenyekiti wake Rajabu Mbaruku.
Moja ya mapendekezo yake ni Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia na manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa kujipima kama wanatosha kuendelea kuongoza wizara hiyo kutokana na kugubikwa na vitendo vya ufisadi.
Kwa mujibu wa taratibu za Bunge, taarifa ya kamati inapowasilishwa na kupitishwa pamoja na mapendekezo yake, huwa ni azimio kamili ambapo Serikali hutakiwa kutoa maelezo ya utekelezaji wake.
Kabla ya azimio hilo kupitishwa, Mwenyekiti wa Laac, Rajabu Mbaruku alijibu michango ya wabunge waliochangia katika taarifa ya kamati yake iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita, akiwemo Waziri Ghasia.
Akizungumza baadaye, Mbaruku alisema hayo ndiyo mapendekezo na Serikali itatakiwa kuyatolea maelezo ya jinsi yatakavyotekelezwa. “Hata waziri mkuu nimemtaja kwa jina, na nimesisitiza kama ananisikia kuhusu ofisi yake,” alisema.
Katika mchango wake, Waziri Ghasia alijaribu kupangua tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa katika wizara yake ikiwamo kuwapo ufisadi, ubadhirifu na mtandao wa wizi unaohusisha Hazina, Wizara na Halmashauri.
Ghasia alikiri Halmashauri ya Mbarali ilitumiwa fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na Bunge na kwamba
suala la halmashauri mbili za Tanga kupewa zaidi ya Sh2 bilioni haikuwa sahihi bali yalikuwa ni makosa ya Mkaguzi Mkuu wa Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kuhusu ufisadi wa zaidi ya Sh600 milioni zilizotolewa na wafadhili kwa ajili ya mpango wa maboresho ya Serikali za Mitaa, alisema haamini kama maneno yaliyonukuliwa na vyombo vya habari kuhusu fedha hizo yalisemwa na wafadhili.
Wafadhili wa mradi huo walinukuliwa wakilalamikia ufisadi huo na kudai kwa sasa hawana la kufanya na wanamwachia Rais, huku wakieleza kushangazwa na Rais kuteua watu dhaifu kuendesha wizara nyeti kama Tamisemi.
Kuhusu hilo, Ghasia alisema hadhani maneno hayo ni ya wafadhili akisema ni majungu, ni maneno ya waandishi kwa sababu huwa wanatafuta mambo yanayogusa jambo fulani ili kuuza magazeti.
Hata hivyo, Ghasia alikiri kwamba ulifanyika ukaguzi na yalibainika matumizi ambayo hayakufuata taratibu na kusisitiza kuwa fedha zilizotumika bila kufuata taratibu zilikuwa Sh444.8 milioni na siyo Sh600 milioni.
Alisema kuwa tuhuma kwamba anawalinda watuhumiwa wa ufisadi na kuwahamisha wale wanaotuhumiwa si za kweli kwani wizara imekuwa ikichukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hao na hata kuwafikisha kortini.
Alitolea mfano wa Halmashauri ya Kishapu ambayo watumishi 14 wamesimamishwa kazi na masuala yao hivi sasa yanashughulikiwa na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na Ofisi ya Takukuru.
Pamoja na maelezo ya Waziri Ghasia, bado Mwenyekiti wa Kamati alisisitiza kuwapo matatizo makubwa
Tamisemi na ndipo alipowataka Ghasia na Manaibu wake kujipima wenyewe kama bado wanafaa kuongoza wizara hiyo nyeti.
Mwenyekiti huyo alisema si kweli kama alivyosema Waziri Ghasia kuwa hakuna mtandao wa ufisadi na
kusisitiza kuwa fedha zilizopelekwa jijini Tanga hazikurudishwa Hazina na badala yake zilitumiwa na Halmashauri hiyo.
Alisema kinachoonekana ni kwamba ulikuwapo mpango wa kuzipeleka fedha kwenye baadhi ya Halmashauri nje ya fedha zilizoidhinishwa lakini baadaye fedha hurudishwa kwa wanamtandao huo baada ya kutakatishwa.
Mwenyekiti huyo alisema Halmashauri zinazopelekewa fedha hizo zilizo nje ya bajeti, hupelekewa fedha hizo kwa malengo ya kuzitakatisha kisha kuzirejesha Hazina ambapo wahusika hunufaika nazo.
Ijumaa wakati akiwasilisha taarifa ya kamati, kamati hiyo iliilipua Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ikiituhumu kuwa sehemu ya mtandao wa ufisadi serikalini.
Alisema bado kuna ubadhirifu, ufisadi na utovu wa nidhamu wa hali ya juu wa matumizi ya fedha za umma kutokana na Tamisemi kutosimamia au yenyewe kuhusika moja kwa moja na ufisadi huo.
Mfano wa mwaka 2011/2012 ambapo Sh1.6 bilioni zilitumika nje ya bajeti iliyoidhinishwa katika halmashauri 38 na Sh2.6 bilioni zilihamishwa kutoka akaunti moja kwenda nyingine bila kurudishwa.
Kamati hiyo imebaini kwamba upo mtindo wa Serikali kutuma kwa Halmashauri kiasi kikubwa cha fedha kuliko kiasi cha fedha kilichoidhinishwa na Bunge katika fungu husika wakati wa upitishaji wa bajeti.
Kamati hiyo imetolea mfano wa Sh2 bilioni zilizotumwa Halmashauri ya Jiji la Tanga na Sh500 milioni zilizotumwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe zikiwa zaidi ya kiasi kilichokuwa kimeidhinishwa na Bunge.
“Kitendo hiki ambacho kinafanyika kwa ushirikiano wa hali ya juu wa Hazina,Tamisemi na Halmashauri kinaashiria kuwapo mtandao wa kutisha wa kifisadi baina ya mamlaka hizo,” alisema.
Kamati hiyo imeituhumu pia Tamisemi inayoongozwa na Waziri Hawa Ghasia, kuwahamisha haraka watumishi wanaotuhumiwa kufanya ubadhirifu kutoka halmashauri moja kwenda nyingine.
“Kamati imebaini kwamba Tamisemi imekuwa ikitumia mtindo huu kuwalinda watumishi mafisadi ndani ya halmashauri na kuifanya kamati iamini Tamisemi ni sehemu ya mtandao huu,” imesema.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alisema kwa makusudi mazima, Tamisemi imekuwa ikieneza saratani hiyo ya ufisadi kwenye halmashauri nyingi iwezekanavyo na kuitaka Serikali kuachana na mtindo huo.
Ubadhirifu Wakurugenzi 70
Itakumbukwa Agosti 19 mwaka huu, Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ilitoa taarifa yake baada ya kubaini kuwepo kwa mtandao wa ufisadi unaoshirikisha Wakurugenzi 70 wa Halmashauri mbalimbali hapa nchini ambao wanashirikiana na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Kitengo cha Hazina.
Baadhi ya halmashauri hizo ni pamoja na Wilaya ya Monduli, Arusha, Mwanza, Mbeya na Ilala.
Ilielezwa kuwa Tanzania Bara ina halmashauri 134, kwa hiyo ina maana zaidi ya nusu ya wakurugenzi wanajihusisha na mambo hayo.
“Baadhi ya wakurugenzi hao walihamishwa kwenye vituo vyao vya kazi kutokana na kashfa ya matumizi mabaya
ya fedha za Serikali, lakini bado wanajihusisha na mambo haya,” alisema Mbarouk alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa waandishi wa habari.
“Kuna zaidi ya Wakurugenzi 70 wako kwenye mtandao wa ufisadi kwa kushirikiana na watendaji wa Hazina na Tamisemi, jambo ambalo limesababisha halmashauri zao kupata hati chafu kwa miaka mitano mfululizo,” alisema Mbarouk.
Aliongeza wakurugenzi hao wamekuwa wakishirikiana na wahasibu wao katika kutumia vibaya fedha za Serikali zinazotolewa kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri zao.
Akitolea mfano wa Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Wilson Kabwe ambaye halmashauri yake ilifanya vibaya katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), lakini hajachukuliwa hatua na badala yake amehamishwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam.