Wednesday, August 2

MHANDISI MAKANI ASISITIZA UTALII WA MISITU YA ASILI NCHINI KAMA CHANZO MUHIMU CHA KUONGEZA PATO LA TAIFA NA JAMII KWA UJUMLA

NA HAMZA TEMBA - WMU
.........................................................................................
Katika kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha utalii wa Misitu ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.

Hayo yamesemwa jana wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali ya uhifadhi.

Alisema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.

“Tumezoea zaidi utalii wa wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa fursa pana ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia mafanikio, Makani alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema pamoja na faida hizo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu ya asili ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.

“Ni lazima tutafute njia endelevu ya ulinzi wa misitu, hatuwezi kuwa na askari wa kutosha, walinzi na mitutu, njia sahihi ni ulinzi shirikishi, tuwaelimishe wananchi umuhimu wa misitu na tuwaeleze watanufaikaje, tofauti na zile faida za ujumla za upatikanaji wa mvua na hali nzuri ya hewa, hii itasaidia sana kuwaleta karibu kwenye uhifadhi wa pamoja”, alisema Makani.

Akizungumza na wananchi wa kijiji Nywelo wilayani humo kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya kijiji hicho na shamba la miti Shume, Makani alisema tatizo lililopo ni uelewa tofauti kuhusu mpaka huo baina ya pande hizo mbili,  hivyo akuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutuma wataalamu wa upimaji waliopima eneo hilo awali waje wafanye uhakiki wa mpaka huo kwa kushirikisha uongozi wa wilaya, halmashauri na kijiji hicho ili kuondoa tofauti hizo na kumaliza mgogoro huo ndani ya wiki mbili zijazo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ya asili, uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto misitu na uhaba wa watumishi.

Katika ziara yake hiyo wilayani Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na Shamba la Miti la Shume, alifanya pia vikao vinne vya ndani na mkutano mmoja wa hadhara ambapo alijibu kero mbalimbali za wananchi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akijibu kero mbalimbali za uhifadhi kwa wananchi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana. 
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akisikiliza moja ya kero kuhusu uhifadhi kutoka kwa Abunio Abraham Shangali (wa pili kulia) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kikundi cha uhifadhi na utalii cha Friends of Usambara kilichopo Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti Lugangika katika kijiji cha Shume Nywelo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mwalimu Elias Mkwilima akijibu baadhi ya hoja katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Nywelo jana wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.

RC Rukwa Amezionya Halmashauri Dhidi ya Matumizi Mabovu ya Mashine za EFD



RC Rukwa  Mh. Zelote Stephen akiwaonesha waheshimiwa madiwani   (hawapo pichani)risiti ambazo tayari zimeshakatwa kabla ya kutumiwa. 


P_20170731_160828_vHDR_Auto
RC Rukwa akiwaonesha waheshimiwa madiwani   (hawapo pichani) kitabu cha hoja za mthibiti na mkaguzi wa serikali kwa  Manispaa ya Sumbawanga.
P_20170731_162142_vHDR_Auto

RC Rukwa akitoa ufafanuzi. 


…………………………….
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amezionya halmashauri zote mkoani Rukwa kuhakikisha wanazitumia vizuri manshine za EFD kwa kuongeza mapato katika halmashauri zao.

Ametoa onyo hilo kwenye kikao maalum cha kujibu hoja za ukaguzi wa hesabu za serikali kwa madiwani wa  Manispaa ya Sumbawanga katika kumalizia ziara yake maalum kwa halmashauri zote mkoani humo kujua namna Halmashauri zilivyojipanga ili hoja hizo zisijirudie miaka inayofuata.  
Akiongea huku akionesha risiti alizozikamata katika maeneo mbalimbali ya mauzo alisema kuwa serikali inafanya kila liwezalo katika kuhakikisha inakusanya maopato lakini bado kuna watumishi wanatafuta namna ya kuiskosesha serikali mapato hayo.

“katika kila sehemu za mauzo lazima mashine hizi ziwepo na kuwepo sio mtindo huu (akionesha msururu wa risiti zilizokatwa tayari kwa matumizi) hizi nimezikamata maeneo anajua Mkurugenzi, asubuhi watu wanagawana, ndio mchezo uliopo, pamoja na jitihada tunazofanya bado watu wanatafuta mbinu za kuiba, hii sio kwamba nimeleta iwe mfano, hapana, nimezikamata na mfahamu kuwa mimi ni mtaalamu wa kukamata,”Alisema

Katika Kusisitiza suala la uwazi wa matumizi ya fedha za halmashauri kwa waheshimiwa madiwani Mh. Zelote alitaja majukumu kadhaa ya Mkurugenzi wa Halmashauri na kusema kuwa moja ya kazi za Mkurugenzi ni kuhakikisha kuwa madiwani wanapata taarifa za fedha za halmashauri.
“Hapa mmezungumza na mmenionyesha kwa kiasi kikubwa kwamba hamnazo taarifa na nikiangalia kazi moja wapo ya waheshimkwa madiwani ni kiusimamia matumizi ya fedha za halmashauri zao sasa mtasimamiaje ikiwa hamna taarifa,” Alisema.

Na kukumbusha kuwa Mkurugenzi ndio katibu wa kamati ya fedha ya halmashauri lakini na kuonya kuwa kamati hiyo ibebe sura ya halmashauri na sio sura ya kamati na kuwasisitiza kufuata taratibu nyingine za ikiwa kurudisha mrejesho kwa wengine juu ya mipango na maazimio yaliyofikiwa.
Katika kikao hicho Mh. Zelote alimtambulisha mtaalamu wa TEHAMA ili awaelezee waheshimiwa madiwani namna mifumo ya fedha inavyofanya kazi ili nao wawe na uelewa mpana katika kufuatilia mapato na matumizi ya halmashauri.

“Suala la kukusanya mapato limekuwa likiimbwa asubuhi, mchana na usiku, kuwa tuhakikishe tunajipanga vyema kukusanya mapato ya halmashauri kwa kupitia utaratibu uliopo, suala la kutumia hizi mashine sio la kuhoji tena mwisho ulikuwa mwezi wa tatu ndio agizo lililopo kwa wakurugenzi kuwa mashine hizi ziwepo na zinafanya kazi,” Alisema.

Na katika kuhakikisha kuwa vitabu hivyo havipati nafasi Mh. Zelote alitoa siku saba vitabu hivyo kurudishwa maghalani na kuongeza kuwa watumishi wanaokiuka miiko ya kazi zao kuwajibishwa kulingana na madhara waliyosababisha na kuwaasa kujenga uaminifu katika utumishi ndani ya halmashauri.

“Sitaki kusikia tena kuwa kwenye mkoa wangu kuna halmashauri inanyooshewa kidole, mmeshanyooshewa kidole mara moja sitaki kuona tena hicho kidole,” alimalizia.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya nSumbawanga Mh. Julieth Binyura alishanngazwa na wataalamu hao kushindwa kudhiti hoja na hatimae wao kuwa chanzo kikuu cha kuzalisha hoja.

“Mtu kama unaitwa mtaalamu na serikali imekuamini kwanini tena unaizalishia serikali hoja, na suala la fedha ni suala nyeti sana hivyo linahitaji umakini wa haloi ya juu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili na si vinguinevyo,” Alisema.

Akifunga kikao hicho Mstahiki meya wa Manispaa ya Sumbwanga Mh. Justin Malisawa alimuahidi Mkuu wa Mkoa kusimamia yale yote aliyoyaelekeza na kuomba msaada wake pindi pale watakapokwama. 

VITO VYA THAMANI VYAPITISHWA KIMAGENDO RUKWA


NAIBU WAZIRI WA MALISILI NA UTALII,MHANDISI RAMO MAKANI AZUNGUMZA NA WAKAZI WA KIJIJI CHA MSHIRI WILAYANI MOSHI KUHUSU ENEO LA NUSU MAILI


Mkuu wa Wilaya ya Moshi Kippi Warioba akiongozana na Naibu Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani walipotembelea kijiji cha Mshiri katika wilaya ya Moshi kusikiliza Changamoto zinazo wakabili wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro .
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani akiwa na Mbunge wa Jimbo la Vunjo,James Mbatia katika mkutano wa wananchi katka kijiji cha Mshiri wilayani Moshi uliohusu Zaidi changamoto iliyopo katika eneo la Nusu Maili katka Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro .
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mshiri wilayani Moshi waishio kando ya Hifadhi ya taifa ya Mlima Kilimanjaro waliofika kwa ajili ya kumueleza Naibu Waziri wa Malisli na Utalii,Mhandisi Ramo Makani changamoto zinazowakabili hususani eneo la Nusu Maili.
Niabu Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mshiri wilayani Moshi ,alipotembelea kijiji hicho kusikiliza Changamoto zinazo wakabili hususani katika eneo la Nusu Maili lililopo chini ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Baadhi ya Wakazi wa Kijiji cha Mshiri wilayani Moshi wakimsikiiza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani (Haupo pichani ) alipozungumza nao.
Mbunge wa jimbo la Vunjo ilipo kijiji cha Mshiri ,James Mbatia akizungumza katika mkutano huo kuhusu Changaoto mbalimbali zinazowakabili wananchi kaika kijiji hicho.
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Mshiri wilani Moshi.
Mku wa wilaya ya Moshi ,Kippi Warioba akizungumza katika mkutano huo.
Baadhi ya viongozi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) walioongozana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani kutembelea kijiji cha Mshiri,kutoka kulia ni Meneja Mawasiliano wa TANAPA,Pascal Shelutete,Meneja Utalii wa Tanapa.Bw Manase na Mhifadhi Ujirani Mwema KINAPA,Bi Hobokela Mwamjengwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifdhi za Taifa (TANAPA) Mtango Mtahiko akiwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) Betrita Loibook katika mkutano wa Naibu Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani na wananchi katika kijiji cha Mshiri.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Kaimu Mkurugenzi wa Uhifadhi wa TANAPA,Mtango Mtahiko akitoa salamu katika mkutano huo.
Baadhi ya Wananchi katika kijiji cha Mshiri.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (KINAPA) Betrita Loibook akizungumza jambo katika mkutano huo.

Bomoabomoa yaikumba nyumba ya Sh1 bil


Fundi akiondoa mabati katika paa la moja ya

Fundi akiondoa mabati katika paa la moja ya nyumba ya mkazi wa  Mbezi Kibanda cha Mkaa, jijini Dar es Salaam,  Margaret Kawa ili kupisha upanuzi wa Barabara ya  Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya.  Picha na Emmanuel Herman 
Dar es Salaam. Kuna vilio vingi vya kupoteza mali kutokana na bomoabomoa inayoendelea kupisha ujenzi wa barabara ya Morogoro, lakini sikia cha cha familia hii. Hivi sasa familia hiyo iliyowekeza kwenye ujenzi wa zaidi ya Sh1 bilioni katika eneo la Mbezi-Kibanda cha Mkaa, Dar es Salaam imeanza kuvunja nyumba zake kutii agizo la Wakala wa Barabara (Tanroards) la kutaka wabomoe wenyewe kabla hawajabomolewa.
Familia hiyo ya Magreth Kawa, iliwekeza nyumba kubwa nne za makazi kwenye eneo moja zikiwa zimezungukwa na fremu za maduka hiyo ikiwa ni mbali ya madarasa mawili ambayo mwalimu huyo mstaafu alikuwa akiyatumia kufundishia watoto wa chekechea.
Licha ya kuwapo kwa kesi mahakamani, baadhi ya wakazi hao wanaendelea kuvunja nyumba zao kwa hiari wakihofia kupoteza mali zaidi ikiwa bomoabomoa ya Serikali itaanza.
Waandishi wetu walishuhudia baadhi ya watu wakitokwa na machozi, wakati wakiendelea na shughuli ya kuvunja nyumba zao ama wenyewe au kwa kutumia mafundi.
Simulizi ya familia
Akizungumza kwa huzuni, Magreth alisema alijenga nyumba hizo tangu mwaka 1992, akishirikiana na watoto wake na kwamba amelazimika kubomoa ili kuokoa baadhi ya mali kabla hawajavunjiwa na kuambulia patupu.
Wakati mazungumzo na familia hiyo yakiendelea, baadhi ya mafundi walikuwa wakiendelea kuvunja nyumba hizo ili kuokoa bati na vifaa vingine kama milango, mbao na vile vya ndani yakiwamo masinki.
Ilikuwa ni kama tupo msibani kwa sababu waliokuwa wamekaa pembeni kusubiri nyumba hizo zivunjwe walikuwa wameshika tama huku wengine wakibubujikwa machozi.
Kilichowashtua hadi kuanza kubomoa nyumba hizo ni hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia umeme jambo lililowapa ishara kwamba suala la ubomoaji huo halikwepeki.
“Kabla ya kuanza ujenzi maeneo haya yalikuwa mashamba yetu, baadaye tukaanza kujenga kidogokidogo,” alisema mmoja wa watoto wa mama huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Alisema awali, wakati wameanza ujenzi sheria ilikuwa inawataka wajenge umbali wa mita 60 kutoka usawa wa barabara jambo ambalo, walilitekeleza.
“Wakati tunaanza ujenzi hatukuwa kwenye hifadhi ya barabara, tulikuwa nje kabisa lakini sasa wamekuja na sheria mpya kwamba ni mita 120, hivyo nyumba zetu zote zimejikuta zipo kwenye hifadhi,” alisema.
Alisema walikamilisha uwekezaji kwenye eneo hilo miaka mitano iliyopita na kwamba muda huu ulikuwa wa kuanza angalau kupata faida.
“Familia yetu tunaishi kwa pamoja hivyo uwekezaji huu tumeufanya pamoja tukimsaidia mama yetu, zipo nyumba ambazo tulikuwa tunaishi na nyingine tumepangisha,” alisema.
Magreth alisema kinachowaumiza zaidi ni kutoambulia fidia ya aina yoyote kutokana na uwekezaji mkubwa walioufanya.
Alisema kwa kuwa hawakuwa wamejipanga, wamelazimika kuweka baadhi ya vyombo vyao kwa ndugu wakati wakitafakari watakavyoanza maisha mapya.
Kama ulidhani hicho ndicho kilio kikubwa pekee sikia na hiki cha mkazi wa Kimara Stop Over, Santand Kayu. Huyu tayari ameshavunja nyumba yake aliyoijenga kwa mkopo miaka minne iliyopita ikigharimu zaidi ya Sh120 milioni, fedha ambazo bado anaendelea kulipa.
“Nimevunja ili walau niokoe bati na vitu vingine, tunaendelea kusubiri kesi iliyo mahakamani,” alisema.
Alisema tathmini ya awali iliyokuwa imefanywa, wale waliojenga kabla ya barabara hiyo walitakiwa kulipwa fidia lakini tathmini mpya haijaainisha malipo ya fidia yoyote.
Simulizi ya wajane wawili
Tukiendelea kutembelea makazi yaliyowekewa alama ya X nyekundu na maandishi ‘Bomoa’ , waandishi wetu walifika katika nyumba ya vyumba sita iliyojengwa na Joyce Elias (70) akishirikiana na marehemu mumewe tangu mwaka 1994.
Nyumba hiyo inadaiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh60 milioni lakini inatakiwa kuvunjwa.
Mwandishi wetu alifika katika nyumba hiyo juzi saa 10 jioni na kumkuta Joyce akiwa ameketi nje huku akitengeneza ufagio wa ‘chelewa’ kwa kutumia majani ya minazi iliyokauka.
Alionekana tofauti kabisa na wananchi wengine wa eneo hilo ambao wengi wao walikuwa ‘bize’ wakivunja nyumba zao. Alikaa tu kana kwamba hajui kinachoendelea huku pembeni yake wakiwapo watoto wawili ambao baadaye alisema ni wajukuu wake, hao walikuwa wakichambua mboga za majani, mara alimwagiza mmoja wao, “Rebecca mletee dada yako kiti.”
Baada ya kuketi, mwandishi wetu alimuuliza kuhusu bomoabomoa hiyo na mama huyo alijibu kwamba anajua kwamba nyumba yake inatakiwa kuvunjwa lakini haamini kama hilo litatokea hivyo anasubiri mpaka dakika ya mwisho maana hana pa kwenda huku akiwa na mgonjwa ndani na wajukuu watano ambao wote wanamtegemea.
“Leo wananiambia nihame hapa nitakwenda wapi? Ndani nina mgonjwa mdogo wangu.”
Alisema mdogo wake huyo, Rose Elias (68) ambaye pia ni mjane, baada ya kupata taarifa za kubomolewa kwa nyumba yao amepooza.
“Alikuwa anaumwa muda mrefu hili suala la kubomolewa ndiyo limemmaliza zaidi sasa hivi kapooza hawezi kutembea,” alisema.
Akieleza ilivyokuwa mpaka mdogo wake kupooza, Joyce alisema siku maofisa wa Tanroads walipoenda kuweka alama ya kuvunjiwa nyumba alikuwa amekaa nje na mdogo wake huyo, pamoja na mmoja wa wajukuu wake, Rebecca.
“Tukiwa hapa nje tukashuhudia wakiweka alama kwenye nyumba. Tuliamini wataishia nyumba za juu mara tukaona wamefika hadi kwenye nyumba yangu na kuweka alama, mdogo wangu alikuwa amekaa hapa (akionyesha kwa mikono) nikasikia akisema ‘Ha! Ha! Ha Rebeca tutakwenda wapi mjukuu wangu!’” alimnukuu.
Alisema baada ya kusema hivyo alianguka hivyo wakalazimika kumpepea, ingawa baadaye alipata nafuu, alisema ilipofika usiku hali ilibadilika tena akashindwa kuongea wala kutembea na alipopelekwa hospitali ikaonekana amepooza.
“Ndo hivyo ilivyokuwa mjukuu wangu kwa hiyo bibi yako yupo tu ndani kalala, nitakupeleka ukamuone, sasa hawa wote wananiangalia mimi, mgonjwa ana wajukuu zake hapa ambao ni watano baba yao aliwatelekeza na mama yao alishafariki kwa hiyo naishi nao,” alisema.
Joyce alisema nyumba yake ilikuwa na wapangaji watano wote wameondoka na wengine bila kulipa madeni aliyokuwa akiwadai na fedha alizokuwa nazo zimetumika kumtibu mdogo wake na kumzika mtoto wa mdogo wake ambaye alifariki wiki mbili zilizopita kwa maradhi mengine ambayo alisema hayahusiani na bomoabomoa hiyo.
Baadhi ya majirani wa Joyce walisema mjane huyo anaishi maisha magumu, “Ile familia kiukweli ina wakati mgumu mno, tunafahamu kuna mwingine alipooza ghafla tu baada ya kupata mshtuko” alisema Rehema Kihondo.     

Serikali yamjibu Mbowe




Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe 
Dar es Salaam. Serikali ‘imemjibu’ Freeman Mbowe kuhusu madai ya hali mbaya ya  uchumi nchini huku ikisema uchumi wa Taifa umeendelea kuimarika na si kama mwenyekiti huyo wa Chadema anavyodai.
Juzi, Mbowe akisoma maazimio ya kikao cha Kamati Kuu ya Chadema, alitoa tathmini ya hali ya uchumi ambayo pamoja na mambo mengine, alisema hali ya uchumi imekuwa tete katika awamu ya tano ya utawala ikilinganishwa na iliyopita.
Mbowe alitaja baadhi ya mambo ambayo yanaashiria kushuka kwa uchumi kuwa ni pamoja na hali ya ukata, kushuka kwa ununuzi wa bidhaa za ndani, kuongezeka kwa Deni la Taifa pamoja na kushuka kwa uwekezaji.
Lakini jana Serikali kupitia kwa msemaji wake, Dk Hassan Abbasi imesema uchumi uko imara na kuwataka wananchi waachane na ushabiki wa kisiasa.
Dk Abbasi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), aliwaambia waandishi wa habari kwamba uchumi wa dunia uliyumba mwaka uliopita na ndiyo maana hali ilionekana kuwa ngumu, lakini sasa imeimarika.
“Tanzania inapata heshima duniani. Jina Magufuli ni brand kwa sasa duniani kutokana na mambo anayoyafanya,” alisema. “Takwimu za BoT (Benki Kuu ya Tanzania) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) pamoja na changamoto za duniani, lakini uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara na kiujumla unakua kwa asilimia 7.”
Akitumia takwimu mbalimbali za kitaifa na kimataifa, Dk Abbasi alitaja mambo mbalimbali ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya ikiwamo kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, rushwa na utoaji wa elimu bure.
Alisema tangu Serikali ya Rais Magufuli imeingia madarakani, kiwango cha mapato ya kodi kwa mwezi kimeongezeka kutoka  Sh925 bilioni mwaka 2015 hadi  Sh1 trilioni mwaka uliopita.
Kuhusu mfumuko wa bei, alisema umeshuka kutoka asilimia sita hadi asilimia tano wakati mwaka 2015 ulikuwa ni zaidi ya asilimia nane, “Wakati sisi tuko tano, Ukanda wa Afrika Mashariki ukomo wa mfumuko wa bei ni asilimia nane,” alisema.
Uwekezaji
Tathmini ya Chadema, ilieleza kutokuwapo mazingira bora ya uwekezaji nchini kutokana na masuala mbalimbali likiwamo la usafirishaji wa mchanga wa madini (makinikia).
Dk Abbasi alisema taarifa za kuwa uwekezaji umeshuka si za kweli na kwamba Tanzania ipo katika nafasi ya nane kwa Bara la Afrika na ya kwanza Afrika Mashariki kwa kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji, “Biashara nyingi zimefunguliwa kuliko zilizofungwa.”
Afya
Katika sekta ya afya, Dk Abbasi alisema katika miaka iliyopita, bajeti ya dawa 2015 ilikuwa Sh30 bilioni, lakini imeongezwa hadi Sh261 bilioni mwaka huu wa fedha ili kuhakikisha hospitali na vituo vya afya zinapata dawa na vifaa tiba.
Alisema ongezeko hilo litaboresha huduma za afya kwa Watanzania wengi.
Elimu
Msemaji huyo wa Serikali pia aligusia hoja ya elimu bure na kusema hilo limesimamiwa vyema na Serikali ya Rais Magufuli na kuhakikisha vifaa vya kusomea ikiwamo madawati vinapatikana kwa kila mwanafunzi.
“Jumla ya Sh18 bilioni zinatolewa kila mwezi kwa ajili ya kutekeleza mpango wa elimu bure,” alisema.
Alisema mikopo ya elimu ya juu imepewa kipaumbele ikiwamo kuongeza bajeti kutoka Sh341 bilioni hadi Sh475 bilioni mwaka huu. “Nchi yetu ina furaha na amani pamoja na changamoto zetu kama Taifa ni wajibu wa kila mtu achape kazi kwa maendeleo na siyo kushabikia siasa,” alisema.

Uhuru wa habari
Dk Abbasi ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema pia kwamba Taifa linatambua umuhimu wa vyombo vya habari na kutekeleza mikataba ya kimataifa.
“Tanzania ni moja ya nchi chache duniani zilizotunga Sheria ya Huduma ya Habari ambayo inampa uhuru mwanahabari,” alisema.
Alisema hadi sasa kuna magazeti 430, redio 140 na televisheni 32 nchini.    

Mkemia: Mkojo wa Wema ulibainika kuwa na bangi



Mlimbwende wa Tanzania 2006, Wema Sepetu

Mlimbwende wa Tanzania 2006, Wema Sepetu 
Dar es Salaam. Elias Mulima, ambaye anatoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyoupima mkojo wa mlimbwende wa Tanzania 2006, Wema Sepetu na kubaini kuwa ulikuwa na bangi.
Shahidi huyo wa kwanza wa upande wa mashtaka akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula aliyaeleza hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alipokuwa akitoa ushahidi wa sampuli ya mkojo huo aliodai kuupokea Februari 8.
Alidai kuwa siku hiyo, Wema alipelekwa ofisini kwa Inspekta Wills na WP Mary na kwamba baada ya kufikishwa, alimfanyia usajili na kupewa lebo namba 321/2017.
Katika ushahidi huo ulioanza kutolewa saa 7:25 mchana hadi saa 8:54, Mulima alieleza kuwa walimpeleka kwa sababu walitaka apimwe mkojo na kwamba alitoa kontena maalumu na kumpatia WP Mary ambaye aliongozana na Wema kwenye vyoo ambako alitoa sampuli ya mkojo huo.
Shahidi huyo alidai baada ya Wema kutoa sampuli hiyo, ilipelekwa maabara ambako aliipokea na kuendelea na uchunguzi. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kupata chembechembe za dawa za kulevya ndani ya mkojo wa Wema na kwamba baada ya uchunguzi, iligundulika kuna dawa za kulevya aina ya bangi.
Shahidi huyo alibainisha kuwa kitaalamu, bangi inaweza kuonekana kwenye mkojo kwa muda wa siku 20. Baada ya kuthibitisha hilo, aliandaa taarifa ya mchunguzi ambayo aliisaini yeye mwenyewe na ikathibitishwa na kaimu mkemia mkuu wa Serikali na kwamba aliisaini Februari 8.
Shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa anaweza kutambua taarifa hiyo kwa sababu ina saini yake, muhuri wa moto na namba ya maabara na akaomba kuitoa mahakamani kama kielelezo cha ushahidi.
Wakili Peter Kibatala anayemtetea Wema, alipinga akitaka ripoti hiyo isipokewe kwa sababu haijakidhi Kifungu cha 63 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Sura ya 20 iliyofanyiwa marekebisho 2002.
Kibatala alidai kuwa kifungu hicho kinaeleza utaratibu wa kufanya uchunguzi wa kitabibu kwa mshtakiwa ambaye yupo chini ya ulinzi kuwa ni lazima polisi awasilishe maombi mahakamani.
“Kwa sababu hakukuwa na ombi wala amri kutoka mahakamani ni lazima ripoti hiyo ikataliwe,” alieleza Wakili Kibatala.
Pia alipinga ripoti hiyo isipokewe kwa sababu pia haijaambatanishwa na fomu namba DCEA 001.
Kutokana na hoja hizo za Kibatala, Kakula alidai fomu yenye namba 001 inatumiwa na Polisi wanapopeleka sampuli na fomu namba 009 ni taarifa ya mkemia na kwamba fomu moja haitegemei nyingine kwa kuwa zinaandaliwa na watu tofauti.
Kakula alidai kuwa sheria haijasema kama ni lazima muda wote maombi yapelekwe mahakamani na oda itoke ndipo mshtakiwa afanyiwe uchunguzi wa kitabibu, ila pale ambako mshtakiwa hataki, polisi wanaweza kufanya maombi mahakamani.
Kibatala alisisitiza kuwa kuchukua kipimo cha utabibu ni lazima Polisi aende mahakamani na kwamba ripoti haijakidhi vigezo.
Kutokana na ubishani huo wa kisheria, Hakimu Simba alitaka Mahakama ipewe nafasi ya kuzipitia nyaraka zinazobishaniwa na kesi imeahirishwa hadi Agosti 4, 2017.    

Taasisi za serikali kuacha kutumia mkaa na kuni


Serikali imeanzisha mkakati wa kuzitaka rtaasisi zake kuacha kutumia mkaa na kuni kama njia ya kupambana na kupoteza misitu kutokana na ongezeko la ukataji ovyo miti.
Waziri wa Nchi Ofisi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari Makamba, amesema jiji la Dar es Salaam pekee limekuwa likitumia wastani wa tani 500,000 ya mkaa kila mwaka huku kukiwa na uwezekano wa kiwango hicho kuongezeka kutokana na jiji hilo kuendelea kupanuka.
Waziri Makamba amesema iwapo hali hiyo itaachwa iendelea kama ilivyo taifa linaweza kutumbukia katika jangwa na hivyo kuvuruga pia shughuli nyingine za maendeleo.
“Kwa kutambua hilo Serikali inakusudia kuipa uhai kampeni yake ya kupiga marufuku matumizi ya mkaa na tunataka baadhi ya taasisi za umma kuanza kuachana na matumizi ya mkaa na kuhamia katika utumiaji wa gesi,” alisema.
Inakadiriwa kuwa kila mwaka Tanzania hupoteza ekari milioni moja kutokana na matumizi ya mkaa na kuni na kwamba kiwango hicho kinaweza kuongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo.
Kama sehemu ya kuzidisha ufahamu juu ya athari zitokanazo na ukataji wa miti, Serikali inakusudia kuandaa maonyesho maalumu yatayofanyika mwakani yakiwa na lengo la kuibua mbinu mbadala ya nishati ya mkaa.

WHC yajenga nyumba 500 Dodoma kuwawahi watumishi wapya


Kampuni ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Serikali (WHC), imeanza ujenzi wa nyumba 159 kati ya 500 huko mkoani Dodoma.
Ujenzi huo wa nyumba za watumishi unatekelezwa katika eneo la Njedegwa lenye ukubwa wa ekari 55.
Hayo yamesemwa leo jumanne na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Dk Fred Msemwa, wakati akizungumza na waandishi Wa Habari.
Dk Msemwa amesema nyumba hizo zimezingatia ubora wa kisasa. Amesema ujenzi wa nyumkba hizo umesukumwa na matakwa ya serikali kuhamishia shughuli zake Dodoma.
“Tunaamini mradi huu utasaidia kuwapatia makazi bora watumishi wanaohamia Dodoma,” amesema.
Amesema katika ujenzi wa nyumba hizo, WHC wamezingatia hali ya kipato cha watumishi ambapo ujenzi ukikamilika nyumba hizo zitauzwa kwa bei nafuu huku bei ya kuanzia ni Sh46 milioni.
"Nyumba ni za kisasa zenye vyumba vitatu ikiwa ni matakwa halisi ya mahitaji ya watumishi wengi… bei hiyo niliyoitaja imejumuisha na kodi ya ongezeko la thamani (VAT), " amesema Dk Msemwa.
Mkuu wa kitengo cha masoko na mauzo, Raphael Mwabuponde, amesema watumishi sasa wanaweza kununua nyumba hizo kwa njia ya mpangaji mnunuzi.
Chini ya mpango huo, mtumishi anaweza kulipa asilimia 5 ya bei huku akipangiwa kiasi kilichobaki kukilipa kama kodi ya kila mwezi kama anavyolipa katika nyumba ya kupanga hadi deni litakapomalizika.

Kitila Mkumbo awasha moto Dawasco


Katibu Mkuu wa wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema ameapa kuwashughuklikia watumishi wachache chini ya wizara yake ambao bado wanaendekeza maisha ya ujanja ujanja kazini.
Profesa Kitila ameitoa kauli hiyo leo Jumanne wakati akizungumza na watendaji na mameneja wa Shirika la Maji Safi na Taka Dar es Salaam (Dawasco) kwenye ofisi za makao makuu ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Amesema ingawa Dawasco imefanikiwa kuboresha huduma zake, lakini wapo watumishi wa chache ambao bado wanafanya kazi kwa ubabaishaji.
Amesisitiza kuwa zama za ujanjaujanja zimekwisha na wale wachache wanaoshiriki mbinu za kulihujumu shirika hilo hawatavumiliwa na watendaji wa shirika hilo kutoa taarifa kwa watakaobainika.
Wakati huo mhuo, Profesa Mkumbo amewashukuru watendaji na watumishi wa dawasco akibainisha kuwa siku hizi simu za malalamiko anazopigiwa na wateja kuhusu huduma za maji zinazotolewa na Shirika hilo zimepungua sana.
Amesema hali hiyo inatokana na Dawasco kuboresha huduma zake.
Amesema hivi sasa anatumiwa ujumbe mfupi wa kupongezwa kuhusu huduma za zinatolewa na Dawasco na kulitaka shirika hilo kuendelea kuchapa kazi ya kutoa ya kuwahudumia wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
“Hongereni kwa huduma nzuri mnazitoa kwa wakazi wa mikoa hii. Nyie ndiyo taswira ya Serikali katika utoaji wa huduma za maji. Bila nyie Ukatibu wa Mkuu hauna maana kwa mkoa wa Dar es Salaam hata waziri na wizara kwa ujumla,” amesema Profesa Mkumbo.
Profesa Mkumbo amesema wizara yake haina mipaka katika utendaji kazi na kwamba ipo wazi kuwasiliana mtendaji yeyote atakayetaka huduma kuto