Wednesday, August 2

WHC yajenga nyumba 500 Dodoma kuwawahi watumishi wapya


Kampuni ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa Serikali (WHC), imeanza ujenzi wa nyumba 159 kati ya 500 huko mkoani Dodoma.
Ujenzi huo wa nyumba za watumishi unatekelezwa katika eneo la Njedegwa lenye ukubwa wa ekari 55.
Hayo yamesemwa leo jumanne na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Dk Fred Msemwa, wakati akizungumza na waandishi Wa Habari.
Dk Msemwa amesema nyumba hizo zimezingatia ubora wa kisasa. Amesema ujenzi wa nyumkba hizo umesukumwa na matakwa ya serikali kuhamishia shughuli zake Dodoma.
“Tunaamini mradi huu utasaidia kuwapatia makazi bora watumishi wanaohamia Dodoma,” amesema.
Amesema katika ujenzi wa nyumba hizo, WHC wamezingatia hali ya kipato cha watumishi ambapo ujenzi ukikamilika nyumba hizo zitauzwa kwa bei nafuu huku bei ya kuanzia ni Sh46 milioni.
"Nyumba ni za kisasa zenye vyumba vitatu ikiwa ni matakwa halisi ya mahitaji ya watumishi wengi… bei hiyo niliyoitaja imejumuisha na kodi ya ongezeko la thamani (VAT), " amesema Dk Msemwa.
Mkuu wa kitengo cha masoko na mauzo, Raphael Mwabuponde, amesema watumishi sasa wanaweza kununua nyumba hizo kwa njia ya mpangaji mnunuzi.
Chini ya mpango huo, mtumishi anaweza kulipa asilimia 5 ya bei huku akipangiwa kiasi kilichobaki kukilipa kama kodi ya kila mwezi kama anavyolipa katika nyumba ya kupanga hadi deni litakapomalizika.

No comments:

Post a Comment