Friday, April 27

‘Kuleni vyakula vya asili kujikinga na maradhi’


Mtaalamu asema wakazi wengi wa Zanzibar wameweka utaratibu wa kula nyama kila siku
Zanzibar. Wakazi wa visiwani Zanzibar wameshauriwa kupunguza matumizi ya ulaji wa nyama badala yake watumie vyakula vya asili ili kujikinga na maradhi ya saratani.
Ushauri huo umetolewa jana na mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini Unguja, Dk Msafiri Marijani wakati akizungumza na gazeti hili.
Alisema maradhi ya saratani kwa namna moja au nyingine yanasababishwa na ulaji wa nyama uliokithiri jambo ambalo alitaja siyo zuri kiafya.
“Kwa sasa walio wengi hapa Zanzibar wameweka utaratibu kula nyama kila siku nyumbani kwao na kibaya zaidi watu wameacha vyakula vya asili ambavyo ni bora kwa afya,” alisema Dk Marijani.
Daktari huyo alitaja sababu nyingine za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe pamoja na kuacha kufanya mazoezi.
Kutokana na hali hiyo pia alishauri jamii kuacha tabia ya matumizi ya sigara na unywaji wa pombe lakini pia kujiwekea utaratibu mzuri wa kufanya mazoezi kila siku angalau kwa dakika 30.
Katika hatua nyingine; alisema Hospitali ya Mnazi Mmoja ina vifaa vya kisasa vya kugundua ugonjwa huo wa saratani katika hatua za awali kabisa.
“Kila kitu tunafanya wenyewe hapa kuhusu saratani mgonjwa anayepewa uhamisho (transfer)ni yule anayehitaji kupigwa mionzi tu ambao ndio tunawapeleka Tanzania bara,” alisema Dk Marijani.
Katibu wa jumuiya ya watu wanaoishi na ugonjwa huo, Ali Zubeir Juma alisema maradhi hayo yanaongezeka siku hadi siku kutokana na jamii kukataa kubadili utaratibu wa maisha yao.

Ukarabati MV Mapinduzi wagharimu Sh300 mil


Zanzibar. Zaidi ya Sh300 milioni, zimetumika hadi sasa katika ukarabati wa meli ya MV Mapinduzi (11) kutokana na hitilafu zilizosababisha meli hiyo kutofanya kazi kwa zaidi ya miezi mitatu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Miundo Mbinu, Mustafa Aboud Jumbe alitaka kiwango hicho cha fedha juzi wakati alipotembelea meli hiyo katika Bandari ya Malindi mjini Unguja.
“Tumetumia kiwango hicho kutokana na kununua vifaa vipya kutoka Uholanzi, fedha zinaweza kuongezeka kwani kuna ukarabati zaidi,” alisema Jumbe.
Alifafanua kuwa kwa sasa tayari baadhi ya vifaa hivyo vimeanza kufungwa na mafundi wataalamu kutoka Uholanzi wakishirikiana na mafundi wazawa waliopo Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu sababu za kuharibika kwa mashine hiyo, alisema wanaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha kuharibika kwa kwake. “Nataka niweke wazi, hakuna mtu aliyehusika kuharibu mashine hii isipokuwa ni hitilafu, tunafanya uchunguzi kujua hitilafu hizo zilisababishwa na nini,” alisema Jumbe.
Kapteni mkuu wa meli hiyo, Aboubakar Mzee Ali alisema harakati za ufungaji wa vifaa kwenye mashine ya meli hiyo unaendelea vizuri na kuahidi ndani ya siku 10 zijazo watakuwa wamekamilisha.

TPDC yawataka wananchi kujiunga makundi kuomba kuunganishwa bomba la gesi asilia


Dar es Salaam. takriban nyumba 70 na viwanda viwili vinatarajiwa kunufaika na awamu ya kwanza ya usambazaji gesi asilia, huku watu wengine wakishauriwa kutuma maombi baada ya kujiunga kwa pamoja ili kupata huduma hiyo kwa gharama nafuu zaidi.
Hayo yalibainishwa juzi na kaimu mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba, wakati wa uzinduzi wa kituo cha kupunguza mgandamizo wa gesi na maungano ya bomba linalokwenda katika makazi ya watu.
Musomba alisema awamu ya kwanza viwanda viwili vya Mikocheni vitaunganishwa (CocaCola na Bidco), lakini itawanufaisha zaidi wakazi wa maeneo ambayo bomba hilo linapita ya Ubungo Kibo, Shekilango, Sinza Sarvey na Mikocheni na maeneo mengine ya karibu na hapo.
“Changamoto ya usambazaji wa huduma ya gesi ni gharama kuanzia vifaa vyake, awamu hii tumetumia kuanzia Sh4 bilioni hadi Sh5 bilioni... ni rahisi zaidi watu wengi wanaokaa sehemu moja wakiungana wakaomba kwa pamoja,” alisema.
Alisema gharama hiyo itazingatia zaidi umbali wa nyumba na mazingira yaliyopo kulifikia bomba kuu na kwamba, mabomba yanayotumika kuunganisha katika nyumba yanazalishwa nchini ila tatizo ni vifaa hivyo vingine ambavyo lazima viagizwe nje ya nchi.
Naye naibu meneja wa Kampuni ya Sinoma East Africa, Lu Xiaoqiang ambao ndiyo wanatekeleza awamu hiyo, alisema wanatarajia kukamilisha kazi hiyo kwa ubora na muda uliopangwa lakini zaidi watajikita kuwajengea uwezo wazawa ambao ndiyo watashirikiana.

Dk Slaa azungumzia maandamano nchini Sweden, polisi waonya

Wakati polisi wakitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu maandamano yaliyoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii na kupangwa kufanyika leo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amesema ofisi yake ilipokea barua kutoka polisi wa nchi hiyo kuhusu taarifa za Watanzania waliotaka kuandamana jana.
Hata hivyo, hapa nchini polisi imeonya ikisema maandamano hayo ni batili na atakayeshiriki atashughulikiwa.
Akizungumza na gazeti hili kutoka nchini Sweden, Dk Slaa alisema jana kuwa, polisi walisema wameshawapa kibali waandamanaji na watawapa ulinzi unaostahili.
“Ilipofika saa tatu asubuhi, walifika watu kumi, polisi hawakuwa na kazi kubwa waliwapangia wapi wasimame, walikuja na mabango yao. Lakini hakukuwa na muziki kwa sababu huku hawatakiwi kupiga muziki,” alisema.
Alisema baada ya kuwaona waandamanaji hao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, walikubaliana na polisi kuwa waingie ndani ili kujua nini wanachohitaji.
“Walikataa kuingia ndani na wakasema hawana sababu ya kujadiliana. Tukawaambia tunawaomba watupe viongozi wawili ili wawe wawakilishi na viongozi hao waseme nini wanachotaka. Lakini pia walikataa,” alisema.
Dk Slaa alisema Sweden ni moja ya nchi zenye vyama vya Watanzania vilivyosajiliwa kuanzia ngazi ya mkoa na kuendelea na viongozi wa vyama hivyo walipiga simu ubalozini wakimsifu Rais Magufuli.
“Nimepokea simu kutoka sehemu mbalimbali, kwamba wanamuunga mkono Rais John Magufuli. Wanataka Rais asilegeze kamba katika vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu vita hivyo vinatengeneza maadui ndiyo maana mambo kama haya yanatokea,” alisema.
Kuhusu ujumbe aliosema ni wa upotoshaji ulioandikwa kwenye mabango ya waandamanaji hao, Balozi Slaa alisema unamhukumu Rais kwa mambo ambayo mahakama haijathibitisha.
Polisi nchini yaonya
Akizungumza na waendesha bodaboda jana, kaimu kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Sweetbert Njolike alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kila mtu anafanya shughuli zake kama kawaida bila uvunjifu wowote wa amani.
“Niwahakikishie Jeshi la Polisi tumejipanga na mkoa wetu utaendelea kubaki salama hakuna maandamano yatakayofanyika, hivyo kila mtu aendelee na shughuli zake kama kawaida,” alisema.
Wakati hayo yakijiri Dar es Salaam, polisi mkoani Mwanza walifanya onyesho la utayari wa kiutendaji na vifaa vyao kwa kuzunguka mitaa kadhaa jijini humo.
Msafara wa magari zaidi ya 15 yaliyokuwa yamewasha taa na kupiga ving’ora ulihusisha askari wenye sare za kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), waliobeba silaha na kujihami kwa zana na vifaa vya kudhibiti na kukabiliana na ghasia. Miongoni mwa magari yaliyozungushwa mitaani ni ya doria ya kila siku, gari la maji ya kuwasha na malori, yote yakiwa na askari.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema wamejiandaa kikamilifu kukabiliana na kuwadhibiti wote watakaothubutu kujitokeza mitaani leo kushiriki maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Kutakuwa na doria ya askari wenye sare na wasio na sare mitaani na maeneo yote ya Mkoa wa Mwanza, watakaothubutu kuandamana watasimulia wengine kitakachowapata,” alisema.
Mkuu wa mkoa huo, John Mongella aliunga mkono kauli hiyo akisema maandamano hayo ni haramu kisheria kwa sababu hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa polisi kwa mujibu wa sheria.
Kutoka Dodoma polisi walipita mitaani baadhi wakiwa kwenye magari na wengine wakikimbia.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto alisema watakaothubutu kuandamana watakabiliwa na jeshi hilo ipasavyo.
Mkoani Mtwara, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya alisema watu wachache wanaohamasisha maandamano wasithubutu kuandamana kwa kuwa watapambana na nguvu ya dola na madhara yatakayotokea jeshi hilo lisilaumiwe.
Alisema katika kufuatilia wanaochochea, kuyahamasisha na kumkashifu Rais, wanafunzi tisa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine tawi la Mtwara wanashikiliwa.
“Wawili kati yao upelelezi tumekamilisha na kuwafikisha mahakamani, waliobakia tunaendelea kukamilisha upelelezi,” alisema.
Kwa upande wa Morogoro, mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana kudhibiti maandamano yasiyo halali yaliyopangwa kufanyika leo.
“Kama kuna watu wanataka kuandamana basi wajifungie chumbani waandamane lakini wakijaribu kuingia barabarani polisi hakikisheni mnawashughulikia,” aliagiza Dk Kebwe.
Kamanda wa polisi mkoani humo, Ulrich Matei alisema kwamba wapo askari na vifaa vya kutosha kukabiliana na maandamano hayo.
Marekani waandamana
Wakati huohuo, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani waliandamana hadi katika ofisi za ubalozi wa Tanzania mjini Washington kuwasilisha madai yao.
Baadhi ya picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha waandamanaji hao wakiwa na mabango wakiwa nje ya ubalozi huo huku wengine wakisikika wakizungumza mambo mbalimbali.
Baadaye watu hao waliokuwa wakizungumza Kiswahili walijipanga kando ya barabara wakiimba na kuendelea kuonyesha mabango yao.

Siri ya Diamond kupata mchongo wa Kombe la Dunia hii hapa


Huenda unajiuliza ni utaratibu gani ulitumika kumpa Diamond Platinumz kazi ya kushiriki wimbo maalumu wa Kombe la Dunia, jibu ni kwamba umahiri wake ulitumika kama kigezo.
Raia wa Afrika Kusini na mdau mkubwa wa burudani barani Afrika, Tim Horwood alipewa kazi ya kutafuta wanamuziki watano kuifanya kazi hiyo.
Alipofika ukanda wa Afrika Mashariki anasema hakuna jina jingine lililomjia katika orodha yake fupi zaidi ya Diamond. 
Horwood anasema ni msanii aliyeimarisha himaya yake ukanda wa Afrika Mashariki hivyo haikuwa rahisi kumchagua mwingine.
Wasanii wengine waliopata shavu hilo ni Sami Dan wa  Ethiopia; Lizha James wa  Mozambique; Ykee Benda wa  Uganda; na Casper Nyovest wa Afrika Kusini.

Mwili wa mtoto aliyeuawa kwa kuchomwa visu waagwa

 Mwili wa mtoto Joshua Michael Nzalila (2) aliyeuawa kwa kuchomwa kisu tumboni umewasili nyumbani kwao Kigamboni jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kuagwa.
Akizungumza na MCL Digital, baba mkubwa wa Joshua, Deus Lulyehu amesema mwili wa mtoto huyo utasafirishwa kwenda Sengerema, mkoani Mwanza kwa ajili ya maziko.
"Tunaendelea kuomboleza na tunausubiri mwili wa mtoto wetu mpendwa, kilichochelewesha ni upatikanaji wa dawa ya kuutibu," amesema.