Friday, April 27

Ukarabati MV Mapinduzi wagharimu Sh300 mil


Zanzibar. Zaidi ya Sh300 milioni, zimetumika hadi sasa katika ukarabati wa meli ya MV Mapinduzi (11) kutokana na hitilafu zilizosababisha meli hiyo kutofanya kazi kwa zaidi ya miezi mitatu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Miundo Mbinu, Mustafa Aboud Jumbe alitaka kiwango hicho cha fedha juzi wakati alipotembelea meli hiyo katika Bandari ya Malindi mjini Unguja.
“Tumetumia kiwango hicho kutokana na kununua vifaa vipya kutoka Uholanzi, fedha zinaweza kuongezeka kwani kuna ukarabati zaidi,” alisema Jumbe.
Alifafanua kuwa kwa sasa tayari baadhi ya vifaa hivyo vimeanza kufungwa na mafundi wataalamu kutoka Uholanzi wakishirikiana na mafundi wazawa waliopo Zanzibar.
Akizungumzia kuhusu sababu za kuharibika kwa mashine hiyo, alisema wanaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha kuharibika kwa kwake. “Nataka niweke wazi, hakuna mtu aliyehusika kuharibu mashine hii isipokuwa ni hitilafu, tunafanya uchunguzi kujua hitilafu hizo zilisababishwa na nini,” alisema Jumbe.
Kapteni mkuu wa meli hiyo, Aboubakar Mzee Ali alisema harakati za ufungaji wa vifaa kwenye mashine ya meli hiyo unaendelea vizuri na kuahidi ndani ya siku 10 zijazo watakuwa wamekamilisha.

No comments:

Post a Comment