Dar es Salaam. Wakati Siku ya Mtoto wa Afrika ikiadhimishwa, ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni vimetajwa kuwa ni mizigo mikubwa anayoibeba mtoto wa Kitanzania.
Takwimu zinaonyesha kuwapo kwa ongezeko kubwa la matukio hayo na hivyo kumuweka mtoto njiapanda katika kupata haki zake za msingi.
Mbali na matukio hayo, bado watoto wengi wanakabiliwa na ukatili mwingine kama vipigo na kutumikishwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii na hivyo kukosa fursa ya kupata elimu.
Kwa mujibu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), mmoja kati ya watoto watatu wa kike, na mmoja wa kiume kati ya watoto saba hapa nchini wameshafanyiwa ukatili kama kunajisiwa, kulawiti na kuchezewa maungo yao.
Takwimu za Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi zilizotolewa mwaka jana zinaonyesha kuwa watoto 2,571 wa kike na kiume walibakwa na kulawitiwa hapa nchini, idadi inayoweza kuwa kubwa zaidi, kutokana na matukio mengi kutoripotiwa.
Utafiti wa Kidemokrafia wa Afya Tanzania (2015-2016) unaonyesha kuwapo kwa ongezeko la mimba za utotoni kutoka asilimia 23 mwaka 2010 hadi 27 mwaka jana.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau, wakiwamo wanaharakati wa masuala ya jinsia na haki za binadamu, walisema hali ya watoto wengi si shwari na kwamba ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni ni janga linalohitaji nguvu kubwa kupambana nalo.
Meneja wa Idara ya Ujenzi wa Nguvu ya Pamoja wa TGNP, Grace Kisetu alisema ukatili wa kingono kwa watoto ni mkubwa na kwamba, unaathiri makuzi ya mtoto na kumfanya ashindwe kutimiza ndoto zake kimaisha.
“Tatizo hili linapaswa kuchukuliwa kwa uzito mkubwa kwa sababu watoto ni nusu ya Watanzania wote na hawa ndio Taifa la kesho, hivyo lazima walindwe na kuandaliwa vizuri,” alisema.
Kisetu alisema licha ya ukatili huo, utafiti wa TGNP walioufanya hivi karibuni ulibaini kuwa asilimia 72 ya watoto wa kike na asilimia 71 ya watoto wa kiume wanapigwa.
Pamoja na ukatili huo wa kingono, watoto pia wanakabiliwa na tatizo la mimba za utotoni. Mwenyekiti wa Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania unaojumuisha zaidi ya mashirika 30 nchini, Valery Msoka alisema kuna ongezeko kubwa la mimba za utotoni hasa maeneo ya vijijini ikilinganishwa na mijini.
Msoka alisema katika utafiti uliofanywa na shirika hilo, asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 19, wamepata ujauzito (2015-2016).
“Kiwango hiki ni kikubwa ikilinganishwa na ripoti ya mwaka 2010 na takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 23 ya watoto walipata mimba,” alisema.
Ukatili unaofanywa na ndugu
Zipo simulizi nyingi za watoto waliofanyiwa ukatili, na tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa watoto wengi wanafanyiwa ukatili huo na watu wa karibu.
Mzazi (jina linahifadhiwa) alisimulia kuwa familia yao imeingia kwenye mtikisiko mkubwa baada ya mtoto wake kulawitiwa na mjomba wake aliyekuwa akimlea, katika eneo la Kimara jijini Dar es Salaam.
“Mwanangu yupo darasa la tatu na alikuwa anaishi na mjomba wake. Likizo hii ya mwezi wa sita amerudi cha ajabu amebadilika tabia na akawa anataka kufanya ngono na mdogo wake wa kiume,” alisema.
Alisema walipomuuliza kwa kina, akasema huwa kila siku anafanywa hivyo na mjomba wake.
“Tulipompeleka hospitali (walisema) mtoto alishaharibiwa siku nyingi. Tulimpeleka kwa mjomba wake kwa sababu ya urahisi wa elimu,” alisema.
“Tupo kwenye wakati mgumu na tunaendelea na taratibu za kumshtaki, japo ni kaka yangu.”
Pia hivi karibuni gazeti hili liliripoti habari ya mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 12, aliyejifungua mtoto wa kiume baada ya kubakwa na binamu yake.
Mtaalamu wa masuala ya saikolojia wa taasisi wa Mlee ya jijini Dar es Salaam, Dk Frank John alisema watoto wanapofanyika ukatili kila siku wanaharibiwa akili, na upo uwezekano mkubwa kwao kuwafanyia wengine.
“Mtoto aliyebakwa asiposaidiwa kisaikolojia, atabaki na maumivu makali ndani ya moyo wake, na akikua anaweza kuwa na kisasi,” alisema.
Alisema mtoto anapobakwa huwa anahisi upweke na kuanza kujitenga na wenzake.
“Mtoto huyu ataanza kuwa anazubaa, muoga na wakati mwingine kushuka kielimu. Kwa ujumla watoto wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia lazima wapewe matibabu kwa umakini zaidi,” alisema.
Imeandikwa na Tumaini Msowoya, Bakari Kiango, Colnely Joseph na Henerietha Katula.