Tuesday, December 20

Trump aadhinishwa rasmi Rais wa Marekani


Washington, Marekani. Wajumbe wa Jopo la Kuamua Mshindi wa Urais nchini Marekani wamemuidhinisha Donald Trump kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Novemba. Wajumbe hao walikutana katika majimbo yao kupiga kura.
Awali, kulikuwa na juhudi za kutaka kumzuia bilionea huyo kuingia ikulu kwa madai amekuwa akiendesha siasa za kibaguzi.
Hata hivyo, Trump amesema atakuwa rais wa Marekani wote na atafanya kila liwezekanalo kuwaunganisha wananchi.
Wajumbe walikuwa wametumiwa ujumbe kupitia baruapepe na pia kupigiwa simu wakihimizwa kutomuunga mkono bilionea huyo kabla yao kukutana kupiga kura.
Shughuli yao ya kupiga kura kwa kawaida huwa kama shughuli ya kutimiza wajibu kwani mara zote  huwa wanamuidhinisha mshindi.
Kumekuwa na lawama kuwa uchaguzi wa mwaka huu ulitawaliwa na hila ikiwamo vitendo vya udukuzi kutoka Urusi. Madai hayo yamepuuzwa na Urusi iliyosema hayana msingi wowote.
Jimbo la Texas hatimaye lilimuwezesha kufikisha idadi ya kura 270 za wajumbe alizohitaji,, licha ya wajumbe wawili wake kugeuka na kupiga kura kumpinga.
Matokeo ya kura hiyo yatatangazwa rasmi 6 Januari 6 kwenye kikao maalum cha pamoja cha Bunge la Congress.
"Nawashukuru Wamarekani kwa kunipigia kura kwa wingi kuwa rais wa Marekani," alisema Trump kupitia taarifa baada ya matokeo kutangazwa.
"Kwa hatua hii ya kihistoria tunaweza sasa kutazama mbele na kutarajia maisha ya kufana siku za usoni. Nitafanya kazi kwa bidii kuunganisha nchi yetu na kuwa rais wa Wamarekani wote," alisema.

Baba wa msaidizi wa Mbowe kukagua maiti iliyowekwa kwenye kiroba


Moshi. Wakati polisi wakisema kuwa wanaufanyia mchakato wa vipimo vya vinasaba (DNA), mwili wa mtu anayedaiwa kuuawa nje kidogo ya mji wa Moshi na kuwekwa kwenye kiroba na kuchomwa moto, familia ya Ben Saanane, msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye hajulikani aliko imesema inaenda kuuangalia mwili huyo.
Hatua hiyo ya polisi kupima DNA ilielezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa baada ya hadi jana, mwili huo kutotambuliwa.
Mauaji hayo yaligunduliwa Ijumaa iliyopita, baada ya watu waliokuwa na gari ndogo ambao hawajafahamika, kumchoma moto mtu huyo katika Kijiji cha Ongoma na kisha kutoweka kusikojulikana.
Kamanda Mutafungwa aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mtu huyo hajafahamika na wala hakuna mtu aliyejitokeza kuutambua mwili huo hivyo kulilazimu jeshi kufanya uchunguzi huo wa kisayansi.

Wahifadhi wamwambia Majaliwa, hakuna kaburi la Faru John


Arusha. Sakata na kifo cha Faru John (38), limechukua sura mpya baada ya wahifadhi wa eneo la Sasakwa Singita Grumet kueleza kuwa hakuna kaburi lake kwa kuwa hakuzikwa.
Wamesema hayo siku moja baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza kuunda timu mpya kuchunguza mazingira ya kifo cha faru huyo huku akihoji mambo manne yaliyozua utata.
Mambo aliyohoji wakati akifanya majumuisho ya ziara yake mkoani Arusha ni juzi, Faru John aliumwa lini, aliumwa nini, daktari gani aliyemtibu na zilipo taarifa za matibabu yake.
Pia aliagiza mwili wa faru huyo kufukuliwa na kutazama kama vinasaba vyake vinaendana na watoto wake 26 ambao bado wapo katika Creta ya Ngorongoro.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, mmoja wawahifadhi wa Sasakwa Grumet aliyeomba kutotajwa jina ili kutoathiri uchunguzi wa tukio hilo, alisema kitaalamu wanyama ambao wanakufa bila kuwa na magonjwa ya mlipuko katika maeneo ya hifadhi hawazikwi.
“Faru John baada ya kufa aliondolewa pembe zake na kutupwa ili kiwe chakula cha wanyama wengine wanaotegemea mizoga, lakini kuna mifupa yake,” alisema.
Alisema faru huyo aliombwa na Grumet kwenda kupanda faru waliopo katika eneo hilo, hasa baada ya dume aliyekuwapo huko kuuliwa na tembo.
“Baada ya kuonekana kuna haja ya kutafuta dume, ndipo tuliomba kupata faru dume na tukaletewa na baadaye alikufa,” alisema.
Eneo hilo la Sasakwa Singita Grumet ni mali ya mfanyabiashara mkubwa raia ya Marekani, bilionea Tudor Jones ambaye amewekeza katika maeneo kadhaa ya uhifadhi.
Akifafanua hatua zinazochukuliwa baada ya mnyama kufa katika hifadhi, mhifadhi Peter Isango alisema kwa kawaida huzikwa au kuchomwa moto pale tu wanapobainika kuwa na magonjwa kama kimeta.
“Kama mnyama ana magonjwa ambayo yanaweza kuambukiza, basi anachomwa moto au kufukiwa lakini kama anakufa kawaida na magonjwa ya kawaida huwa anatupwa ili fisi, bweha na wanyama wengine wanaokula mizoga wale na hii ndiyo ikolojia,” alisema.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mkurugenzi mkazi wa shirika la uhifadhi la kimataifa la Frankfurt Zoological Society, Gerald Bigurube ambaye alisema kwa kawaida wanyama wanaokufa hifadhini huwa hawazikwi.
Bigurube ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) alisema kwenye kanuni za uhifadhi kitu chochote, kinachokufa ndani ya hifadhi huachwa kwa ajili ya kulinda ikolojia na bionuwai.
“Mnyama ambaye anakufa kwa kifo cha kawaida mzoga wake unapaswa kuachwa kuoza na kutumiwa na wanyama wengine,” alisema.
Alisema hata wanyama wa kawaida kama swala na wengine wanapoumwa huwa hawatibiwi tofauti na wanyama kama tembo, faru na wengine wakubwa ambao hutibiwa.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu Faru John, Bigurube alisema taasisi yake haikuwahi kushiriki katika suala hilo.
Wapata dhamana
Katika hatua nyingine, Polisi imewaachia kwa dhamana maofisa watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Tanapa waliokuwa wanashikiliwa kwa tuhuma za kumhamisha Faru John kutoka Creta ya Ngorongoro na kumpeleka Sasakwa Grumet.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa licha ya dhamana hiyo, uchunguzi unaendelea.
Watuhumiwa hao ni Israel Naman ambaye alikuwa kaimu mkuu wa idara ya hifadhi wakati faru huyo akiondolewa, Cuthbert Lemanya aliyekuwa mkuu kanda ya Creta, Dk Athanas Nyaki ambaye ni daktari wa mifugo wa mamlaka hiyo.
Wengine ni aliyekuwa kaimu mkuu idara ya maendeleo ya jamii, Kuya Sayaleli na kaimu mkuu idara ya ikolojia, Patrice Mattey.
Kabla ya kukamatwa, maofisa hawa walikiri kushiriki kumhamisha Faru John kutoka Creta ya Ngorongoro hadi Sasakwa kwa maelezo kuwa ilikuwa ni kuendeleza uhifadhi wa faru na pia kutokana na ukorofi wa Faru John kuhodhi majike yote ndani ya Creta kuua madume wengine waliozaliwa.
Akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha, Waziri Mkuu alitoa taarifa za kifo cha faru John huku akiwatuhumu baadhi ya watendaji wa NCAA kuhusika na njama za kumuuza kwa Sh200 milioni ambazo alisema walishapokea malipo ya awali ya Sh100 milioni.
Baada ya maelezo hayo, Waziri Mkuu alitaka kupewa taarifa kamili za tukio hilo, pamoja na pembe za faru huyo, ambazo alikabidhiwa Desemba 8 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na kaimu mkurugenzi wa msaidizi kitengo cha kupambana na ujangili, Robert Mande ambaye alimweleza kuwa taratibu zilifuatwa katika kumhamisha.

Aliyebadili dini afariki baada ya kubatizwa


Moshi. Mkazi wa Mailisita wilayani Hai, Paulo (35) amekufa maji baada ya kuzama katika mto Kikafu, dakika chache baada ya kubadili dini na kubatizwa na maji ya mto huo kwa imani ya dini ya Kikristo.
Paulo ambaye jina lake la awali lilikuwa Issa Juma kabla hajabadili dini, alifariki Jumapili iliyopita katika mto huo, wakati shamrashamra za kubatizwa kwake zikiendelea pembeni ya mto.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi lililazimika kuwakamata wachungaji wawili wa kanisa la Efatha waliombatiza lakini waliachiliwa baada ya Polisi kujiridhisha kuwa Paulo alikufa maji baada ya kubatizwa.
Habari zilizothibitishwa na Polisi, zimeeleza baada ya kubatizwa saa 8:30 mchana na wakati waumini wakiimba kwa ajili ya kurudi kanisani, ndipo Paulo na mwenzake waliamua kurudi kuogelea.