CHADEMA YAFANYA VIZURI KATA 11KATI YA 17, YASHINDA PIA UDIWANI MWANZA. SONGEA,MBEYA,CUF YAPETA TANGA
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeongoza kwenye kura za awali kwa mgombea wake, Joshua Nassari kupata kura nyingi katika kata 11 kati ya Kata 17 za Jimbo la Arumeru Mashariki.
Dakika chache kabla ya kutangaza matokeo hayo, baadhi ya wafuasi wa CCM waliokuwa wamefurika katika Ofisi za Mji Mdogo wa Usa River na baadhi ya polisi, walikuwa wameondoka eneo hilo, wakiwaacha wapambe wachache wa mgombea wao, Sioi akiwamo, Beno Malisa.
Huu ni uchaguzi wa kwanza mdogo kwa Chadema kushinda katika jimbo lililokuwa likishikiliwa na CCM na uchaguzi wa pili kwa chama hicho cha upinzani, kushinda katika uchaguzi mdogo baada ya ule uliofanyika katika Jimbo la Tarime, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Chacha Wangwe.
Katika matokeo hayo yanayokusanywa na kujumlishwa katika ofisi za mji mdogo wa USA River, CCM, imefanya vema katika kata tatu ambako mgombea wake, Sioi Sumari amepata kura nyingi ikilinganishwa na Nassari.
Takwimu zinaonyesha kuwa Chadema wanaongoza katika kata za Akheri ambako ni nyumbani Kwa Sioi, Poli, USA-River, Mbuguni, Seela, Sing'isi, Nkoarua, Maji ya Chai, Kikwe, Maroroni, Nkoaranga, King'ori na Songoro ambako ni nyumbani Kwa Nassari. Jimbo la Arumeru Mashariki lina kata 17.
Mgombea wa CCM Sioi ameongoza katika kata za Makiba, Leguruki na Mkoandrua hadi saa 7:15 usiku jana ambapo msimamizi wa uchaguzi, Trasias Kagenzi alikuwa akisubiri masanduku ya kura kutoka kata mbili.
Kata ambazo masanduku na matokeo yake yalichelewa kutokana na umbali wa maeneo hayo ni Kikatiti na Ngarenanyuki.
Mbali na Chadema kuongoza Arumeru chama hicho pia kimeibuka kidedea katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Mwanza.
CUF imeambulia kiti kimoja cha udiwani Tanga na CCM Dar es Salaam.
Katika tukio lingine, wakala wa Chadema katika chumba Cha kujumlisha kura, Godbless Lema, jana alilazimika kutumia nguvu dhidi ya msimamizi msaidizi wa kata ya Maroroni ambaye jina lake halikupatikana mara moja baada ya kumtuhumu kutaka kubadili tarakimu za matokeo kwenye fomu rasmi zilizowasilishwa.
"Yule msimamizi alikuwa akitaka kuchezea tarakimu katika fomu za matokeo kutoka kwenye kata yake bila kujua kama nilikuwa namfuatilia," alisema Lema.