JUMA Nature amevunja ukimya na kurejea kwa kishindo kwenye muziki ambapo amesisitiza kuwa mwaka huu amepania kuachia kazi za nguvu pamoja na shoo zisizokwisha za Afrika Mashariki kufufua soko lake.
Msanii huyo mahiri wa Bongo ambaye ni kiongozi wa Wanaume Halisi amesema kundi hilo limekamilisha albamu yao ambayo wataitaja miezi michache ijayo, lakini baadhi ya nyimbo tayari zipo redioni zikifanya vizuri.
Muda mwingi nilitulia na wenzangu tulikuwa tunaangalia upepo unavyokwenda na jinsi ya kuibuka tena na kufanya mambo ya uhakika zaidi, kukubalika na mashabiki hasa wa Afrika Mashariki, hatuangalii Tanzania peke yake. Albam za awali za Nature ni 'Nini chanzo' (2001), 'Ugali' (2003), 'Ubinadamu kazi' (2005), 'Zote story' (2006) na 'Tugawane Umaskini' (2009).
Staa huyo alisema kwa ushirikiano wa Dollo, Richie One, JB aliyekuwa Mabaga Fresh, Bob Q, D. Chief, Malipo, Kaka Man, Mzimu na Eddo wanakuja na kazi za mseto ambao mashabiki watajionea tofauti na kuamua.
Nyimbo ambazo tayari zimekamilika ni 'TMK', 'Able' na 'Mguu nje Mguu ndani remix' ambapo kazi kubwa imefanywa na Dolo, KR Mullah na JB.
Nature anasema Halisi Studio ni mali yake na itatumika kutengeneza kazi nyingi zake binafsi na kundi.
Amekiri kuwa studio yake ni ya kawaida kwa mtazamo wa haraka lakini ina vifaa vichache vyenye uwezo mkubwa na baadhi ya wasanii wameanza kufanyia kazi na wanataka kujiondoa katika mfumo wa kutegemea studio za watu.
Studio ipo wazi kwa wasanii wote na siyo Mwanaume Halisi pekee,anasema Nature na kuongeza kuwa licha ya yeye kuwa ndiye prodyuza, lakini wenzake katika kundi pia wanafanya kazi hiyo na wana mpango wa kumpata mtaalam zaidi.
Msanii huyo ambaye kesho jumapili atakuwa na shoo ya pamoja na msanii wa Kenya, Nameless kwenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala jijini Dar es Salaam, alisema; Hii shoo imekuja wakati muafaka kwani hata sisi tunataka kujipima baada ya kujifua kwa muda mrefu.