Monday, January 13

Mbowe kumburuta Zitto kortini


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe anapanga kumchukulia hatua za kisheria Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kutokana na kile alichodai kuwa ni kuzusha tuhuma zenye lengo la kumchafua yeye binafsi na chama hicho.
Tuhuma hizo ni zile zilizowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuandikwa katika vyombo mbalimbali vya habari kuanzia Januari 6 mwaka huu, zikimnukuu Zitto akieleza kuwa Mbowe amewahi kuhongwa mamilioni ya fedha na Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono.
Tuhuma dhidi ya Mbowe ziliibuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu kumtuhumu Zitto kuwa amehongwa magari mawili na Mkono.
Hata hivyo, Mkono katika taarifa yake alikanusha madai ya Zitto kuhusu kuwapa fedha Chadema, pia alitoa ufafanuzi kwamba hakuwahi kumhonga mbunge huyo magari kama ilivyodaiwa na Lissu bali alimuuzia gari moja na kumkodisha gari la pili.
Taarifa ya kusudio la Mbowe kumburuza Zitto mahakamani ilitolewa jana na Ofisa Mwandamizi wa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, huku ikikanusha tuhuma zote zilizotolewa dhidi ya Mbowe.
“Mbowe ameshawasiliana na mawakili walifanyie kazi suala hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria. Mwenyekiti wa chama hajawahi kupokea msaada wa fedha hizo kutoka kwa waliotajwa kwa malengo yaliyosemwa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo ambayo hata hivyo haikumtaja Zitto moja kwa moja.
Jana gazeti hili lilimtafuta Zitto ili aweze kuzungumzia suala hilo lakini hakupatikana.
Msingi wa taarifa
Taarifa hiyo ilieleza kuwa tuhuma hizo zinasambazwa na watu wanaotaka kuhamisha mjadala wa makosa yanayowaandama ya utovu wa maadili na usaliti dhidi ya chama hicho.
Kauli hiyo ni dhahiri inamlenga Zitto, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo, kwani walivuliwa nyadhifa zao kutokana na kuandaa waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013, uliolenga kufanya mapinduzi ya uongozi ndani ya Chadema.
Taarifa hiyo imesema tuhuma zinazoshughulikiwa ni zile zinazodai kwamba Mbowe alichukua Sh40 milioni mwaka 2005  kutoka kwa Mkono ili asifanye kampeni katika Jimbo la Musoma Vijijini.
Tuhuma nyingine ni kuwa 2008 Mkono alimpatia Mbowe Sh20 milioni kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Tarime, kwamba Mbowe alizitoa fedha hizo kwenye chama kama mkopo na akalipwa.
“Wanasema mwaka 2010, wakati wa uchaguzi mkuu eti Mkono alimpatia Mbowe Sh200 milioni kwa ajili ya kampeni za mgombea urais. Mwaka huo huo eti Mbowe alipokea Sh100 milioni kutoka kwa Rostam Aziz kwa ajili ya kampeni,” inaeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa hakuna ukweli wowote katika tuhuma hizo, kwamba ni uzushi  uliopangiliwa kama moja ya mikakati ya watu wenye malengo ya kutaka kuilaghai jamii kwamba viongozi wa Chadema hawana tofauti na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Wanataka kuwafanya Watanzania waamini kuwa viongozi wa Chadema hawana tofauti na wale wa CCM, waamini kuwa chama hiki kikuu cha upinzani kinachobeba matumaini ya Watanzania kionekane hakina tofauti na chama kilichoko madarakani,” inaeleza.
Inaeleza kuwa lengo la watu hao ni kutaka kuisaidia CCM na kugeuza mjadala husika dhidi yao.
“Waliozusha tuhuma hizo, ni vyema wakatunza heshima kidogo waliyobakiza katika jamii kutokana na kuelemewa na mzigo wa tuhuma za utovu wa maadili na usaliti dhidi ya Chadema,” inaeleza na kuongeza;
“Wajibu masuala ya msingi yanayowaandama kuhusu mikakati yao ya kuhujumu Chadema na viongozi wake, ambayo iwapo chama kisingebaini na kuchukua hatua za kinidhamu, ingesababisha kuua ndoto na matumaini ya Watanzania kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiutawala, kwa kuiondoa CCM madarakani.”
Ufafanuzi wa Mkono
Januari 6 mwaka huu Mkono alitoa taarifa kuhusu tuhuma zilizorushwa dhidi yake na kufafanua kuwa magari mawili aina ya Toyota Land Cruiser na Nissan Patrol yanayodaiwa kuwa alimpa Zitto, moja alimuuzia na jingine  amemkodisha.
Kuhusu tuhuma kwamba anawahonga wapinzani wake wajitoe katika uchaguzi ili apite bila kupingwa alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, 2005 na 2010 alipita bila kupingwa kutokana na uchapakazi wake wa kiwango kikubwa.
Mkono pia alijibu tuhuma zilizotolewa na Zitto kwamba Mbowe alipewa mamilioni ya fedha na Mkono kwa nyakati tofauti na kusema hajawahi kutoa fedha zozote kusaidia Chadema.
Mvutano kati ya Zitto na Chadema ulishika kasi baada ya Mbunge huyo kufungua kesi Mahakama Kuu kuomba mahakama hiyo kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Zitto alishinda katika shauri hilo.