Thursday, December 8

Kardinali Pengo akerwa na matanuzi


Pwani. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amewataka waumini wa madhehebu hayo kutotumia muda na mali zao kufanya sherehe kubwa, badala yake wajikite katika ujenzi wa makanisa.
Alitoa rai hiyo juzi alipokuwa mgeni rasmi kwenye harambee ya kuchangia Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Katoliki Tumbi, Kibaha mkoani hapa.
Kanisa hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia waumini 1,232 kwa wakati mmoja.
Kardinali Pengo alisema ili wanadamu waishi kwa furaha, upendo na amani wanapaswa kupewa ujumbe wa neno la Mungu wakiwa kwenye mazingira bora, hivyo ni vyema jitihada za dhati zikafanyika kujenga makanisa zaidi.
“Nakushukuru Padri Beno (Kikudo) wa kanisa hili ambaye uliona ni vyema utumie siku ya maadhimisho ya miaka yako 50 ya kuzaliwa kufanya harambee hii kukusanya fedha za kukamilisha ujenzi wa kanisa, kuliko wengine ambao wamekuwa wakitumia sherehe hizo maeneo ya fukwe za bahari,” alisema. Alisema makusudi ya Mungu siyo kufuja mali ambazo anawajalia wanadamu, bali kutumia mapato yao kwenye mambo ya maendeleo.
Padri Kikudo aliwashukuru waumini kwa kuonyesha juhudi na moyo wa michango ya hali na mali tangu ujenzi wa kanisa hilo ulipoanza.
Alisema ujenzi wa kanisa hilo umefanyika kwa njia tofauti, ikiwa ni pamoja na waumini kuuza kuku na kujitolea kwa nguvukazi kulingana na vipawa na ujuzi walionao ili kufanikisha ujenzi huo.

Serikali yaombwa kuisadia Dangote

Mtwara. Serikali imetakiwa kukaa na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Aliko Dangote kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokikabili kiwanda hicho kwa kuwa anaweza kuwa balozi wa wawekezaji nchini.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe  ametoa ombi hilo jana akisema Dangote ana jina kubwa, iwapo kungekuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji angesaidia kuwavutia wengine.
 “Siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kadhaa katika vyombo mbalimbali vya habari zinazohusiana na kiwanda cha Dangote, kutozalisha kwa kile kinachoelezwa ni kutokana na hitilafu za ufundi.  Kwa kuwa tatizo la ufundi limejitokeza kipindi ambacho tayari kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wamiliki juu ya gharama za uzalishaji, inasababisha kuwapo mkanganyiko kujua kiini cha tatizo,” amesema Akwilombe.