Moto wa Uchaguzi Mkuu wa 2015 ulishazimika lakini kuna kila dalili kwamba majivu yake bado hayajapoa na moja ya dalili za kuwapo kwa hali ya uvuguvugu ni kauli ya hivi karibuni ya Anna Mghwira dhidi ya Edward Lowassa kwamba njia aliyotumia kugombea urais ilikuwa ni aina nyingine ya ufisadi.
Katika uchaguzi huo, Mghwira ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alikuwa mwanamke pekee aliyegombea urais na kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alishika nafasi ya tatu nyuma ya Lowassa akipata kura 98,763 sawa na asilimia 0.65 ya kura zote.
Lowassa, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika Serikali ya Awamu ya Nne, katika uchaguzi huo aliwania kiti hicho kupitia Chadema akiungwa mkono na vyama vilivyoungana chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)na alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote. Dk John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.
Juni 3, Mghwira aliteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro wakati huo akiwa mwenyekiti wa ACT –Wazalendo na muda mfupi baadaye chama hicho kikamuondoa katika nafasi hiyo kutokana na uteuzi huo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili wiki hii, Mghwira alisema njia aliyoitumia Lowassa kugombea urais ilikuwa ni aina nyingine ya ufisadi wa kisiasa kwa kuwa hakupitishwa na chombo chochote ndani ya chama chake.
Alidai kuwa hata katika kampeni, Ukawa haukuzungumzia ajenda ya ufisadi baada ya waziri mkuu huyo wa zamani kujiunga Chadema.
“Kwenye kampeni 2015 chama kikuu cha upinzani (Chadema) hakikuwa kinazungumzia tena ufisadi labda kwa hofu kwamba mshutumiwa mmojawapo wa ufisadi ndio alikuwa mgombea wao. Kwa bahati mbaya ni wao walioibua tuhuma hizo za ufisadi. Lakini kuondoka Dk Slaa (Wilbroad aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema) nako kulileta tatizo ambalo watu hawakutaka kulifuatilia.
“Ni tatizo watu walitakiwa kuuliza alikuwa (Dk Slaa) na sababu ya msingi ya kuondoka? Ameondoka kwa nini? Anaenda wapi na anaenda kufanya nini. Ilikuwa ni ajabu kwamba kiongozi ambaye unataka uje kuwa mfano wa demokrasia, unaingia kugombea nafasi kubwa kama hiyo ya urais bila kuchaguliwa na chombo chochote cha chama,” alisema.
Mghwira aliendelea kujiuliza maswali kuhusu hatua hiyo ya Lowassa, “Umeingiaje? Inatokeaje?” Kisha alihitimisha, “Hiyo ni aina nyingine tena ya ufisadi wa kisiasa. Lowassa kama anataka kujisafisha vizuri kisiasa aangalie sana angeweza kufika mbali kama angetumia njia sahihi.”
Mghwira ambaye ni kiongozi wa kwanza wa upinzani kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, alisema, “Njia iliyotumiwa na Chadema si tu kwamba inarudisha nyuma siasa zetu lakini haikutoa picha nzuri ya uwepo wa demokrasia ndani ya upinzani. Hili lilikuwa doa kubwa kwa Mzee Lowassa.”
Uteuzi wa Lowassa kugombea urais kupitia Ukawa ulishuhudia Dk Slaa aliyetajwa sana wakati huo kuwa mgombea wa nafasi hiyo , akijiuzulu siasa na kwenda kuishi nje ya nchi.
Mbali na Dk Slaa, aliyekuwa mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba naye aliamua kuikimbia CUF aliyokuwa mwenyekiti wake kabla ya kurejea baadaye na kutambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa jambo lililozua mgogoro mkubwa ndani ya chama hicho hadi sasa.
Alikerwa kuvuliwa uenyekiti
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Shanty Town mjini Moshi, Mghwira alikumbuka karaha aliyoipata baada ya furaha ya kuaminiwa na Rais na kupewa wadhifa huo.
Alisema kama si ubabaishaji wa kisiasa Tanzania, asingeondolewa kwenye uenyekiti wa ACT-Wazalendo.
“Changamoto niliyokutana nayo ACT-Wazalendo kama mwenyekiti ni kukosa wigo sahihi wa kisiasa kwa sababu kama tungekuwa tunafanya siasa sahihi, nisingeondolewa uenyekiti,” alisema.
Mghwira alisema, “Naapishwa tu kuwa RC (mkuu wa mkoa) kesho yake naondolewa tena tukiwa tumepanga kukutana kwenye kikao na mpaka leo hatujawahi kukutana.
“Nimesoma kwenye magazeti kuwa mrithi wa Mghwira kutembelea mikoa saba, yaani na mrithi ameshapatikana. Hizo si siasa, huo ni ubabaishaji. Ubabaishaji wa kisiasa Tanzania ni tatizo,” alisema.
Aliongeza, “Sisi kina mama tukisimama imara tunaweza kuondoa dhana hii ya siasa za ubabaishaji. Ni siasa za kipuuzi kabisa. Mmekubaliana mkutane muongee, hamuongei wenzako wanakaa pembeni. Umechaguliwa na mkutano mkuu unaondolewa na kamati ndogo. Watu 370 karibu 400 hivi walikuchagua, siku ya kuondolewa unaondolewa na watu watatu au wawili au mmoja. Hiyo si siasa ni dalili tosha kuwa hakuna siasa.”
Alisema mbaya zaidi ni kuwa watu wanaokuondoa hawakutumwa na mkutano mkuu, wala hawakukaimishwa na kamati kuu.
Hakuna upinzani nchini
Baada ya kujumuisha yote hayo na hasa alivyotimuliwa kwenye uongozi, mkuu huyo wa mkoa akawa na jibu moja kuhusu siasa za upinzani, “Hakuna siasa za upinzani, bali zilizopo ni za kurudishana nyuma maendeleo.
“Siasa ni kitu kizuri kwa maana ya ile mijadala, kubadilishana mawazo na kuzungumzia masuala ya itikadi, mipango ya kijamii... hakuna hiki kitu Tanzania.”
Badala yake alisema, “Tumeweka siasa kama ni uhasama kati ya chama tawala kilichoshinda kihalali na vyama hivi vingine. Kila siku watu wanatafuta makosa ya wenzao (Serikali) hata kama inafanya vizuri. Hiyo sio siasa.
“Vyama vya upinzani hapa hatuendeshi siasa. Awali, chama chochote kitakachoibuka na siasa inayoeleweka kinaweza kutawala nchi hii kwa miaka 100 ilimradi tu kitoke na siasa inayoeleweka.”
Mghwira alisema, “Vikitokea vyama vitatu vinaendesha siasa inayoeleweka tunakuwa mahali pazuri zaidi. Kwa maana kwamba wale wakiongea jambo lao, hata kama hawatawali, mtawala asikie na kuthamini.
“Sisi hapa Tanzania kuna aina ya siasa za kudidimizana. Kwa sisi wanawake wanaharakati tunaziita PhD (pool her down). Unavutwa tu chini hutakiwi kukua. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.”
Alisisitiza, “Kuna watu wanafikiri kwamba ili kitu kiwe sahihi ni lazima wao wakifanye (upinzani) lakini kikifanywa na watu wengine hakiko sahihi. Hiyo ni kutokuwa mwanasiasa. Kuwa mwanasiasa si kugombana ni kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kuitetea na kuisimamia. Mwenzako akija na hoja kubwa zaidi kubali.”
Changamoto za ugombea urais
Mghwira alisema wakati akigombea urais alikumbana na changamoto mbili, moja ikiwa ni ya nchi na nyingine ni ya yeye kutojiandaa kugombea.
“Changamoto zangu binafsi sizijali sana kwa sababu sikuwa nimejiandaa kugombea urais. Ingawa sikushinda urais, lakini nilishinda hatua ya kushiriki kwenye kampeni. Nilishinda ndiyo maana hata Rais Magufuli ameona na akaniteua kuwa RC. Kushinda kwenye kampeni ni kushiriki na kutoka ukiwa umewaachia watu kitu.
“Nafikiri nimeacha hicho kitu. Kila mtu ana ushindi wa viwango vyake. Yeye (Rais Magufuli) alishinda ushindi halisi wa kura na nafasi lakini hajanyima nafasi, amegawa,” alisema na kuongeza kuwa kinachobaki ni kushirikiana ili kuijenga nchi.
“Kuna watu wanasema nilishindwa, sikushindwa kwa sababu sikuenda kushinda, bali nilienda kushiriki. Uchaguzi unashiriki kwanza, ukishashiriki wananchi ndio wanaamua nani ni mshindi.
“Kura zikishahesabiwa na akapatikana mshindi, mnarudi kuijenga nchi. Kuna wapinzani wa Magufuli ndani ya chama chake, nao wamo kwenye Serikali na tuko nao pamoja. Hao ni wabaya zaidi kuliko mimi kwa sababu mimi namkubali kwa asilimia 100 wao wanamkubali sehemu kwa sababu wanatoka chama kimoja. Wanajua mambo yao ndani ya chama yalikuwaje,” alisema.
Alisema wanaotoka upinzani wanaweza kuwa na ufanisi mzuri na uhusiano mzuri zaidi wa kikazi na Rais kwa sababu hawana masilahi ya kisiasa.
“Sina masilahi ya kisiasa CCM ila ACT-Wazalendo. Kama nina masilahi ya kisiasa kwenye chama changu hicho hakimdhuru yeye wala hakiharibu kazi yangu huku kwa sababu mimi na yeye tunahusiana kikazi tu,” alisisitiza.
ACT-Wazalendo ni CCM B?
Alipoulizwa kuhusu dhana iliyoanza kujengeka kuwa huenda ACT-Wazalendo ni tawi la CCM na ndiyo maana Rais ameteua wanachama wake wawili kushika nyadhifa kubwa serikalini alisema hilo si kweli.
Alisema katika kuunda Serikali ya mseto, ukitaka kwenda vizuri huchukui sana wale watu mnaopingana mno kwa kuwa mtapingana tu kila siku.
“Lazima uchukue watu ambao mnaendana katika utendaji kazi. Hata ACT-Wazalendo sidhani ana maanisha atachukua kila mtu...”
Mbali na Mghwira, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa mshauri wa chama hicho, Profesa Kitilla Mkumbo kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Uteuzi ambao uliibua mijadala katika mitandao ya kijamii baadhi wakipongeza na wengine wakishutumu, huku baadhi ya wana-CCM wakinuna.