Hayo yameelezwa leo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi yake na wenzake watatu ilipotajwa.
Katuga aliiambia mahakama kuwa upelelezi bado haujakamilika na akaomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 4, 2017.
Katika kesi hiyo, Manji na wenzake wanakabiliwa na mashtaka saba chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa Taifa kwa kukutwa na vitambaa vinavyotengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania vyenye thamani ya zaidi ya Sh 200 milioni pamoja na mihuri.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda(28), Abdallah Sangey(46) na Thobias Fwere (43).
Awali, akiwasomea hati ya mashtaka inayowakabili washtakiwa hao, Wakili wa Serikali, Tulumanywa Majigo amedai kuwa Juni 30,2017 katika eneo la Chang’ombe ‘A’wilaya ya Temeke Dar es Salaam washtakiwa hao kwa pamoja wamekutwa na askari polisi wakiwa na mabunda 35 ya vitambaa vinavyotumika kushonea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania zenye thamani ya Sh 192.5milioni na kwamba mali hiyo ilipatikana kinyume cha sheria.
Katika shtaka la pili, Wakili Majigo alidai kuwa Julai Mosi, 2017 huko Chang’ombe ‘A’ washtakiwa hao walikutwa na polisi wakiwa na mabunda manane ya vitambaa vinavyotumika kushonea sare za Jeshi la Wananchi Tanzania zenye thamani ya Sh44 milioni mali ambayo ilipatikana isivyo halali.
Katika shtaka la tatu, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 Chang’ombe ‘A’ walikutwa na muhuri wa Jeshi la Wananchi Tanzania wenye maandishi ‘Mkuu 121 kikosi cha JWTZ’ bila ya kuwa na uhalali kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Wakili Majigo katika shitaka la nne, anadai kuwa Juni 30, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ Manji na wenzake hao watatu walikutwa wakiwa na muhuri wenye maandishi’ Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupola Dodoma bila ya kuwa na uhalali kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Shitaka la tano, Manji na wenzake hao wanadaiwa kuwa Juni 30, 2017 huko Chang’ombe ‘A’wamekutwa na muhuri wa Jeshi la Ulinzi la Tanzania wenye maandishi (Commanding Officer 835 KJ Mgambo P.0. Box 224 Korogwe) kitendo ambacho kingehatarisha usalama wa nchi.
Katika shtaka la sita, washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 katika eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ walikutwa na askari polisi wakiwa na namba za usajili SU 383 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Kwenye shtaka la saba washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Julai Mosi, 2017 kwenye eneo hilo la Chang’ombe ‘A’ washtakiwa hao walikutwa na skari polisi wakiwa na namba za usajili wa gari SM 8573 ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa hawakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.
Manji na wenzake wanatetewa na mawakili Hudson Ndusyepo, Malimi Seni na Emmanuel Safari.
No comments:
Post a Comment