Thursday, March 8

Polisi waanza uchunguzi kutekwa mwanafunzi UDSM


Mafinga. Jeshi la Polisi mkoani Iringa limefungua jalada la uchunguzi kwa lengo la kubaini ukweli juu ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Abdul Nondo anayedaiwa kutekwa na watu wasiojullikana na kutelekezwa wilayani Mufindi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 8 ofisini kwake mjini hapa, kamanda wa polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amesema Nondo aliripoti kituo cha polisi cha Mafinga wilayani Mufindi jana  saa moja jioni.
“Baada ya kumhoji Nondo alisema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana ambao walimtekeleza  Wilaya ni Mufindi,” amesema kamanda huyo.
Nondo (24) ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) na mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitoweka juzi katika mazingira ya kutatanisha. Mara ya mwisho alionekana jijini Dar es Salaam.
“Tunaendelea kufanya uchunguzi kama ametoa taarifa za uongo kwa nia ovu kwa lengo la kutaka kuhamasisha wanafunzi wenzake ili kuleta uvunjifu wa amani nchini tutamshughulikia kama wahalifu wengine," amesema Bwire.
Amesema kama kweli mwanafunzi huyo atakuwa ametekwa jeshi hilo litawasaka watuhumiwa na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
Kamanda Bwire amewaomba wananchi wenye taarifa mbalimbali kuhusiana na tukio hilo watoe ushirikiano  ili kukamilisha uchunguzi huo mapema.

RC Mtwara amtupa selo ofisa kiwanda cha Dangote



Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa 
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa, amemwagiza kamanda wa polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya  kumuweka ndani ofisa kazi wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Nadhiru Omary  kwa madai ya kushindwa kutatua malalamiko ya wafanyakazi ambayo yanaelekezwa katika ofisi yake.
Byakanwa ametoa maagizo hayo leo Jumatano,  Jana Machi 7, alipofika kiwandani hapo baada ya baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda hicho kugoma kuendelea na kazi kwa muda usiojulikana kwa madai mbalimbali.
Wafanyakazi hao wanadai kunyanyaswa, kutolipwa mishahara yao kwa wakati na kufukuzwa kazi bila kuzingatia sheria.
“Tangu nimefika hapa wewe bwana umelaumiwa na umetuhumiwa kwa mambo mengi,hata vikao vyote tulivyokaa hujabadilika, kwa sababu kama ungebadilika taarifa hizi tungezijua mapema,” alisema na kuongeza kuwa:
“Sisi kama Serikali tungekaa na watumishi hawa kabla hawajaanza kuandamana, RPC huyu akapumzike kwanza, kamata huyu mtu tuondoke naye hatuwezi kuendelea na watu ambao badala ya kusikiliza malalamiko ya watu.”
“Kama unakaa sehemu ya kazi halafu chama cha wafanyakazi hakipo na ofisa kazi hauchukui hatua zozote unapoteza sifa zote, inaonekana ni tatizo la kudumu na ni tatizo sana.”
Mhasibu idara ya usafirishaji kiwandani hapo, Justie Fumbuka ameiomba Serikali kuchunguza utaratibu wa utoaji vibali vya kufanya kazi na kuishi nchini kwa kuwa umegubikwa na rushwa inayotolewa kwa watendaji wa idara ya kazi na Uhamiaji wasiokuwa waadilifu.
“Mchakato uchunguzwe kwani vibali vimekuwa vikitolewa kwa wasio na sifa na ni wanyanyasaji wa wafanyakazi na tunaiomba Serikali iwaondoe nchini mara moja,” ameeleza Fumba mbele ya mkuu wa mkoa.
Machi 3 mwaka huu, waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage alitembelea kiwandani hapo na kuzungumza na uongozi wa kiwanda hicho na baadaye alikutana na baadhi ya wafanyakazi wakiwamo madereva.
Wafanyakazi hao walimpa malalamiko yao ambapo aliahidi yatafanyiwa kazi baada ya kiwanda hicho kuanza uzalishaji Machi 15.

UWT watoa msaada wa Sh7 milioni Mwananyamala


Dar es Salaam. Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi wameadhimisha siku ya mwanamke kwa kutoa msaada kwa akina mama katika Hopitali ya Mwananyamala wilayani Kinondoni yenye thamani ya Sh7 milioni.
Wametoa msaada huo leo Machi 8 ikiwa ni siku ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Msaada huo ni pamoja na sabuni, taulo za watoto (pampasi), mabeseni, mafagio, dawa za meno ambavyo wamevikabidhi katika wodi za akinamama
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, katibu wa UWT Kinondoni, Nuru Mwaibako amesema mwanamke ni nguzo muhimu katika familia hivyo wanahitaji kuthaminiwa.
Amesema lengo la msaada huo ni kuwafariji akina mama hao kama sehemu ya kujumuika nao kuadhimisha siku hiyo.
“Siku ya leo ni maalumu kwetu sisi wanawake, hivyo tumeamua kuja kwa wenzetu hapa hospitali kama sehemu ya kuwatembelea wajione nao ni miongoni mwa wanawake duniani katika kuadhimisha siku hii muhimu,” amesema.
Mbali na sehemu hiyo ya msaada, Mwaibako amesema mwanamke ni mlezi katika familia, hivyo ameshauri wanawake wapewe heshima na kwa wale wanaowanyanyasa wachukuliwe hatua.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mkazi wa Kinondoni Khairath Hamisi ameshukuru umoja huo kwa msaada waliowapatia na ameomba misaada hiyo iwe endelevu.
“Tunashukuru sana tumeletewa sabuni, pampasi na vingine vingi msaada huu utatusaidia kwa sababu pengine kuna watu hawakuwa na uwezo wa kuvinunua,”amesema.
Mwenyekiti wa umoja huo, Renalda Kageuka amesema lengo la msaada huo ni kuwafariji wanawake waliolazwa hospitalini hapo kwa matatizo mbalimbali.
“Tumependelea siku hii iwe maalumu kwa ajili ya kutembelea wenzetu waliopo hapa ili wafurahi na ndio maana msaada huu umelenga wanawake wenzetu,”amesema.
Kwa upande wake, daktari bingwa wa magojwa ya akina mama, Luzango Maembe amesema, “tunashukuru kupokea misaada hii kusaidia akina mama ambao wamekuja hapa kupata huduma.”
 

Serikali yawachimba mkwara wanaume wanaokopea mali za familia

Mkuu Wa wilaya ya Arusha  Fabian Daqarro
Mkuu Wa wilaya ya Arusha  Fabian Daqarro (kushoto) akipokea sehemu ya mashuka 50 kutoka kwa Mwenyekiti Wa wananchama Wa  Chuo cha maendeleo ya jamii tengeru Rose Mtei  kwa ajili ya kukabidhi katika hospitali mbali mbali za Jiji  la Arusha  kama sehemu ya kumfunika mwanamke. Tukio lililofanyika katika kuadhimisha Siku ya mwanamke duniani katika viwanja vya Sheik Amri Abeid 
Arusha. Serikali imewapiga marufuku wanaume wanaotumia mali za familia kama dhamana za mikopo bila kuwashirikisha wake zao kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria, kanuni na taratibu za ndoa nchini.
Hayo yamesemwa leo Machi 8 na mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fabian Daqarro kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Daqarro amesema kuwa wapo wanaume wanaotumia mali za familia kama nyumba kukopa bila kuwashirikisha wake zao na wakishindwa kulipa mikopo, mali ya familia hupigwa mnada.
 “Niwakaribishe kwangu mje mtoe taarifa endapo ukigundua mume wako amechukua mkopo na kuweka dhamana mali ya familia kati ya nyumba, gari, shamba au chochote nawaahidi nitasema nao kwa mujibu wa sheria maana ndio wanaotujengea wingi wa watu tegemezi baadae,” amesema.
 Mbali na hilo amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kupinga ukatili wa kijinsia na mila potofu hasa za umiliki wa ardhi na mali za familia lakini pia kuungana kwa pamoja.
“Nguvu ya kutokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia iko mikononi mwenu wanawake kwa kupendana na kuacha husuda na chuki za waziwazi baina yenu, badala yake muwezeshane maana mafanikio ni kumiliki uchumi lakini pia kupendana kwani wengine wanaotekeleza ukatili huu kwa mwanamke ni wanamke wenyewe,” amesema Daqarro na kuongeza:
“Ukomavu wa kumiliki uchumi ndio nguvu  ya mwanamke na silaha pekee ya kupinga ukatili  hivyo wajengeeni watoto wenu wa kike hili tangu wadogo huku mkiwapa elimu maana ndio nguzo kuu ya familia na jamii, mkitimiza haya yote basi ukatili na unyanyasaji mtakuwa mmeutokomeza maana hamtakuwa mnategemea kuwezeshwa bali kuwezesha.”
Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, Athumani Kihamia amesema kuwa zaidi ya vikundi 110 vya wanawake vimewezeshwa mikopo ya zaidi ya Sh2 bilioni kwa lengo la kuwapa fursa ya kutekeleza nchi ya viwanda katika vikundi vya ujasiriamali.

Profesa Ndalichako: JPM ana imani na wanawake

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako 
Dar es Salaam. Serikali imechukua hatua kadhaa kuhakikisha kwamba wanawake wanapata nafasi kwenye vyombo vya maamuzi, baadhi yake ikiwa ni kuwapa nafasi za uongozi katika ngazi za juu serikalini.
Hayo yamesemwa leo Machi 8, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akifungua kongamano la kimataifa la wanawake likijadili nafasi yao katika Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG).
Profesa Ndalichako amesema Rais John Magufuli ana imani na utendaji wa wanawake ndio maana amewateua kwenye wizara nyeti kama vile elimu, afya na madini akiamini kwamba watafanya kazi kikamilifu kuleta maendeleo ya nchi.
Amesema Serikali imejidhatiti kutekeleza malengo yote 17 ya maendeleo endelevu ikiwamo kuleta usawa wa kijinsia na kuleta kutoa fursa ya elimu hasa kwa mtoto wa kike.
"Serikali tunajitahidi kutekeleza malengo ya maendeleo hasa lengo la nne la elimu. Tumeshuhudia ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa kupitia sera ya elimu bure. Pia, tumeboresha mafunzo ya walimu na kuweka uwiano wa mwalimu na mwanafunzi darasani," amesema.
Amesema Serikali inasisitiza elimu kwa watoto wa kike kwa sababu wananyimwa fursa ya kwenda shule ili kujikomboa kifikra, pia kupata fursa ya ajira kuwawezesha kumudu maisha yao.
"Tunafanya jitihada kuboresha elimu hapa nchini. Tunaangalia pia elimu ya juu, tunashirikiana na wadau mbalimbali katika kuboresha mfumo wa elimu hapa nchini," amesema Profesa Ndalichako.
Awali, akizungumzia nafasi ya mwanamke kwenye elimu, Balozi wa Ufaransa nchini, Frederic Clavier amesema nchi yake inashirikiana na Serikali kuhakikisha kwamba wanaboresha masomo ya sayansi kwa shule za sekondari na vyuo vikuu hapa nchini.
Amesema siku chache zijazo, timu ya wanafunzi wa elimu ya juu kutoka Ufaransa watafika hapa nchini kujifunza na kubadilishana uzoefu na wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya hapa nchini.
"Tutaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika elimu. Lakini pia Tanzania inatakiwa kuhamasisha umahiri wa lugha zaidi ya moja, nchi mbili za jirani (Rwanda na Burundi) zinatumia kifaransa, itapendeza Tanzania ikiweka mkazo kwenye lugha hiyo," amesema Clavier.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Taaluma za Sayansi Tanzania (Taas), Profesa Esther Mwaikambo amesema idadi finyu ya wanawake wanashiriki katika maeneo ya utafiti na maendeleo, uchapaji, uongozi serikalini na sekta binafsi.
Ameongeza kuwa sababu za wanawake kukosa fursa katika nyanja za  sayansi, teknolojia na uvumbuzi zinaanzia katika ukosefu wa fursa ya elimu na uwiano katika uwekezaji, mazingira ya kazi yasiyo rafiki, imani za kitamaduni na mila potofu.
"Kila mahali duniani lazima kushirikisha wanawake katika maamuzi ili maendeleo yawe fanisi na endelevu. Hili litakamilika kwa kubadilisha mtazamo wa jamii, kuleta uhuru na usawa wa kijinsia, kuamua ukubwa wa familia," amesema Profesa Mwaikambo.

RC aagiza polisi kukamatwa aliyeshinda zabuni


Bukoba. Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu amemuagiza kamanda wa polisi mkoani humo kumsaka na kumkamata mkandarasi wa kampuni ya Mecco aliyeshinda zabuni ya Sh6 bilioni za ujenzi wa barabara za lami katika Manispaa ya Bukoba na baadaye kugoma kujitokeza kusaini mkataba.
Agizo hilo amelitoa leo Machi 8  baada ya meya wa manispaa hiyo, Chifu Karumuna kulalamika kwenye kikao cha bodi ya barabara kuwa mkandarasi huyo amewaingiza hasara kwa kuwa aliingia kwenye ushindani wa zabuni, akashinda  na baadaye akakataa kusaini mkataba hali iliyosababisha mchakato uanze upya.
Amekieleza kikao hicho kuwa kampuni ya Mecco ilishinda tenda kwa kuwa na sifa ya ziada ya kujenga kiwanja cha ndege cha Bukoba, ambapo aliomba msaada wa Serikali kwa kuwa fedha hizo zimetolewa na Benki ya Dunia na kuwa wananchi wanacheleweshwa kupata barabara imara.
Akifunga kikao hicho, mkuu wa mkoa ameagiza mkandarasi huyo asakwe, akamatwe na kupelekwa ofisini kwake akiwa na pingu akisisitiza kuwa hawezi kuruhusu ubabaishaji unaokwamisha maendeleo ya wananchi.

Mama Magufuli aongoza sherehe Siku ya Wanawake



Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli 
Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli  
Dar es Salaam. Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli leo  Machi 8, ameongoza maelfu ya wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake Duniani, huku akiziomba asasi za kiraia  na watu binafsi kushirikiana na Serikali kuwapa akina mama mbinu mbalimbali za mafunzo, mitaji na kuwatafutia masoko ya bidhaa zao.
Mama Magufuli pia ameupongeza mkoa huo kwa kuanzisha vikundi zaidi ya 400 vya wanawake vinavyojishughulisha na usindikaji mazao, ushonaji na uchoraji.
Pia ameupongeza kwa kuwa na vikundi vya kukopeshana (Vicoba) vipatavyo 2,748 ambavyo kwa pamoja vina mtaji wa jumla ya  Sh10.4 bilioni
"Ni imani yangu kuwa kama mikoa yote na taasisi nyingine za kiserikali na kiraia zitaiga mfano wa Dar es Salaam katika kuwawezesha wanawake kiuchumi pamoja na kuwashirikisha kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda, basi tutawawezesha wanawake kiuchumi ikiwemo kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa viwanda", amesema.
Mama Magufuli ameyasema hayo katika sherehe hizo zilizofanyika ukumbi wa Mlimani City.
Amesema japokuwa Serikali inajitahidi kuweka usawa wa jinsia na kuwawezesha wanawake kisiasa, kiuchumi, elimu na afya, peke yake haiwezi kuzimaliza changamoto zote, hivyo ni lazima wananchi wenyewe washiriki katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Mama Magufuli amewapongeza viongozi wa awamu zote za nchi, ikiwa ni pamoja na akina mama shupavu wa Tanu na ASP na baadaye CCM ambao kwa namna moja ama nyingine wameshiriki katika harakati za kumkomboa mwanamke nchini.
"Kutokana na umuhimu wa siku ya leo naomba nitambue mchango wa Mama Maria Nyerere, Mama Fatma Karume, Bibi Titi Mohamed, Mama Sophia Kawawa,  Hadija Jabir,  Johari Yusuf Akida, Mwajuma Koja,  Mtumwa Fikirini na wengineo wengi.
Hatuna budi kuwapongeza  akinamama hawa kwa kupigania haki za wanawake nchini," amesema.

Ajali ya gari yajeruhi polisi watatu Arusha


Arusha. Askari watatu wa Jeshi la Polisi mkoani Arusha wamejeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha gari la polisi na lori.
Kaimu kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha, Yusuph Ilembo amesema kuwa, ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia leo Machi 8 katika barabara ya Tengeru- Arusha saa 9 alfajiri wakati gari la polisi lililokuwa likisindikiza gari la Benki Kuu kupeleka fedha mkoani Tanga lilipogongwa na lori aina ya tipa.
Ajali hiyo iliwajeruhi askari waliokuwa katika gari hilo na dereva kuvunjika miguu yote na kuumia vibaya kichwani. 
Kamanda Ilembo amesema kuwa, ajali hiyo ilisababisha majeraha kwa askari wengine wawili waliokuwa kwenye gari hilo.
Jeshi la polisi linamsaka dereva wa lori ambaye alikimbia baada ya ajali hiyo.

Bashe: Kupeleka hoja binafsi ni wajibu wangu kikatiba -VIDEO


Mbunge wa Nzega Mjini (CCM),Hussein Bashe 
Dar es Salaam. Mbunge wa Nzega Mjini (CCM),Hussein Bashe amesema amechukua hatua ya kuwasilisha hoja binafsi kwa Katibu wa Bunge kwa kuwa ni wajibu wake kikatiba.
Bashe amesema amechukua hatua hiyo kwa sababu amefanya uchunguzi kwa miezi mitano juu ya matukio ya utekaji, mauaji na watu kupotea yaliyotokea tangu mwaka 2010.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 8, 2018 huku akinukuu vifungu vya Katiba,  Bashe amesema hoja yake hiyo inawakilisha mawazo ya wananchi kuhusu matukio ya uhalifu, utekaji na watu kupokea. 
Amesema katika hoja hiyo, ataambatanisha matukio ya tangu mwaka 2010 yakiwamo yaliyotokea katika uchaguzi mbalimbali kwa maelezo kuwa amefanya uchunguzi wa kutosha. 
"Watanzania wanalalamika na haya ninayoyafanya yapo katika Katiba ya chama changu. Msingi wangu wa kubeba hii hoja ni katiba ya chama changu na katiba ya nchi.  
"Ili CCM iendelee kuimarika lazima isimamie misingi yake. Nakwenda bungeni na hoja hii kama mbunge wa CCM. Nimechukua hatua hii sababu ni kiapo changu kwa Chama Cha Mapinduzi. Siwezi kulalamika mitaani nitatumia nafasi yangu kuwasilisha jambo hili," amesema.
Amesema mpaka sasa viongozi wa CCM waliouawa Kibiti wanafika 14, huku viongozi wengine wa upinzani nao wakipoteza maisha akiwamo aliyekuwa kiongozi wa Chadema, Alphonce Mawazo. 
"Nani anafanya haya matukio mbona hakuna haki? Rais amezungumzia mambo haya likiwamo la Akwilina. Ila kauli ya Rais haizuii sisi wengine kufanya haya nifanyayo. Azory Gwanda mpaka leo hajulikani alipo," amesema. 
Amesema kuwasilisha hoja hiyo ni kutimiza wajibu wake kama mbunge wa CCM,
"Nitaheshimu mawazo ya wengine kuhusu hoja yangu ili mwisho wa siku tufikie uamuzi kwa maslahi ya nchi na chama change,” amsema.
Amesema amefanya utafiti kwa zaidi ya miezi mitano na kwamba ataukabidhi utafiti huo ili kila Mtanzania ajue mambo hayo aliyoainisha katika hoja yake. 
 

Mbunge wa CCM ataka mauaji yachunguzwe

Mbunge huyo wa Nzega Mjini Hussein Bashe amefikisha hoja binafsi kwa katibu wa Bunge la Tanzania ili baadae iingizwe bungeni na bunge liunde tume itakayochunguza kwa uhuru na haki kukithiri ukiukaji wa haki za binadamu.

 
Sikiliza sauti03:11

Mahojiano na mbunge Hussein Bashe

Miongoni mwa vitendo hivyo vya ukiukaji wa haki za binadamu ni vile vya utekwaji, upoteaji na mauaji yanayotokea humo. DW imezungumza na mbunge Bashe na kwanza ilimuuliza amefikia hatua gani katika azma yake hiyo?

TRILIONI 1.2 HUTUMIKA KUDHIBITI UKIMWI KWA MWAKA

Tanzania hutumia Sh trilioni 1.2 kwa ajili ya shughuli za kudhibiti Ukimwi kwa mwaka.

Aidha, asilimia 93 ya fedha za kudhibiti Virusi vya Ukimwi (VVU) hutolewa na wahisani ambapo kati ya hizo asilimia 86 hutoka Marekani.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Yasin Abbas, amesema hayo leo Alhamisi Machi 8, wilayani Bagamoyo wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu uandaaji wa programu bora za VVU na Ukimwi.
Amesema asilimia kubwa ya fedha hizo hutumika katika kununua dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs).
“Asilimia 93 ya fedha hufadhiliwa na wadau wa maendeleo kutoka nje ya nchi, kati ya hizo asilimia 86 zinatoka Marekani kupitia programu yake ya PEPFAR na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund ATM).
“Tanzania hutoa asilimia saba tu ya fedha zote. Hivyo, kupitia Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi (ATF), tunatarajia kuongeza rasilimali za ndani kutoka asilimia saba mwaka 2015 hadi asilimia 30 mwaka huu,” amesema Abbas.
Hata hivyo, amesema iwapo watafanikiwa kufikia lengo, Tanzania itaondokana na utegemezi kwa asilimia kubwa.

Wanawake 500 wamesafirishwa kiharamu kutoka Burundi

Shirika hilo limewaorodhesha wanawake zaidi ya 500 nchini Burundi waliohusishwa na biashara ya watu.Haki miliki ya pichaBBC/TWITTER
Image captionShirika hilo limewaorodhesha wanawake zaidi ya 500 nchini Burundi waliohusishwa na biashara ya watu.
Katika mkesha wa siku ya wanawake duniani, shirika moja la kutetea haki za binaadamu nchini Burundi limewaorodhesha wanawake zaidi ya 500 nchini humo waliohusishwa na biashara ya watu.
Shirika hilo limeitaka serikali ya Burundi kupambana na maovu hayo ya kuuzwa kinamama na wasichana kwa kusafirishwa katika nchi za kiarabu.
Kwenye Ripoti yake ya mwaka, Shirika la ONLCT la kutetea haki za binadamu na kupiga vita biashara ya watu, limesema wanawake zaidi ya 500 wameuzwa katika nchi za kiarabu ikiwa ni pamoja na Oman, Saudi Arabia, Kuwait na Lebanon.
Uchugunzi uliofanywa na shirika hilo unaonyesha kuwa wasimamizi wa mtandao huo wanapokea mapato yasiyopungua dola elfu moja kwa kila mwanamke au kwa kila msichana.
Wakili Prime Mbarubukeye ambaye ni mkuu wa shirika hilo la ONLCT, wanawake na wasichana 527 ndio wameuzwa katika biashara hiyo mwaka jana.
Amesema kuwa serikali ni lazima iunde Tume ya kitaifa ya kupiga vita biashara ya watu hususan wanawake.
Anasema changamoto nyingine ni rushwa wanayopokea baadhi ya maafisa wa Serikali ambao wanahusika katika biashara hiyo.
"Watu wa mitandao hiyo wana pesa nyingi kiasi kwamba kutoa hongo ni jambo la kawaida mno katika biashara ya watu."

'Kwa kweli sitaki usikilize muziki huu'' DJ anayetengeneza muziki wa kulala

Tom MiddletonHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMwanamuziki Tom Middleton
"Kiukweli sitaki usikilize muziki huu''. Inawezakana Tom Middleton akawa mwanamuziki wa kwanza kutumia maneno hayo wakati anatangaza albamu yake mpya.
Akiwa ni Dj wa kimataifa,Tom ameweza kuwaburudisha zaidi ya watu milioni katika mataifa 49 na kuwafanya wanamuziki kama Kanye West, Lady Gaga na Snoop Dogg kuanza kupendwa.
Lakini sasa Tom amekuja kivingine baada ya kufanya uchunguzi wa muda mrefu wa tafiti za kisayansi, na kuamua kutengeneza wimbo ambao hauwashirikishi wasikilizaji wake kuusikiliza bali unawataka walale.
Tom alianza kufanya shughuli za kimuziki mnamo miaka ya 90, akiwa anashirikishwa na Aphex Twin pamoja na Mark Pritchard.
Amekuwa akitengeneza muziki kwa kutumia majina mbalimbali katika majukwaa ikiwa ni pamoja na "Reload,Cosmos na Modwheel.
Tom anasema kitu ambacho kimemshawishi kuja na ubunifu huu wa kuandaa muziki wa kumfanya mtu apate usingizi ni kwa sababu amekuwa anafanya kazi karibu na wanasayansi na watafiti.
kkHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMuziki wa kukufanya ulale
Hivyo alidhani kwamba anaweza kutumia ujuzi wake wa kielektroniki na kuandaa mradi huo.
"nilifikiria mara mbili kuwa ni kitu gani ambacho kilishawahi kufanywa hivyo nikaamua kutumia utaalamu wa sayansi kutengeneza midundo ambayo itamfanya mtu apumzike".
Nyimbo hizi zimebuniwa ili kumtuliza msikilizaji na kumfanya apumue kwa kasi pamoja na kushusha mapigo ya moyo ambayo yatamsaidia mtu apumzike.
Hata hivyo mwanamuziki huyo amesema kwamba nyimbo hizo ambazo kwa sasa ziko sokoni hazijawahi kufanyiwa jaribio la kisayansi.
Na anadhani kwamba itavutia zaidi kama wataangalia utafiti ambao ulifanywa ,ni sauti zipi ziliweza kufanya kazi vizuri na kelele zipi ambazo ziliwahi kufanyiwa jaribio
sayansiHaki miliki ya pichaCARSTEN WINDHORST
Image captionTom sasa ni mtaalamu wa kisayansi wa kumfanya apate usingizi
Mwanamuziki huyo anataka kuongeza eleo kwa watu kwa kuandaa tamasha kuhusiana na hiki alichokiandaa .
"Mtu hawapaswi kusikiliza muziki huu wakati anaendesha gari,anaongoza mtambo wowote katika maji".
Mpaka sasa anasema ameona mafanikio makubwa wakati alipofanya jaribio la kuwasikilizisha watu na kweli uliwafanya wapate usingizi.
Tom anasema kutengeneza albamu hii ni moja ya kazi ambayo imekuwa na changamoto kubwa katika maisha yake na katika taaluma yake kwa ujumla ingawa kwake hayo ni mafanikio makubwa.

Wakimbizi kutoka Burundi waliokuepo DRC wahamishiwa Rwanda

Wakimbizi wa Burundi waliohama ni wanawake na watoto
Image captionWakimbizi wa Burundi waliohama ni wanawake na watoto
Wakimbizi zaidi ya 2000 walioingia nchini DRC tangu mwaka 2015, wamefika katika mpaka wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda bila taarifa wakiwa wamesindikizwa na wanajeshi wa umoja wa umoja wa mataifa wa Monusoco .
Kwa mujibu wa taarifa kutoka idara ya sekta ya uhamiaji nchini DRC, wanasema kiongozi mmoja wa shirika la Monusoco ambaye hakukata jina lake litajwe alisema hata wao walishanga kuona kundi kubwa la watu hao wakiwa wamefika kwenye mpaka na hawakuwa na taarifa yeyote kutoka serikali ya Rwanda wala ya Kongo kuwa wakimbizi hao watafika katika eneo hilo.
watotoHaki miliki ya pichaREUTERS
Image captionWakimbizi wa Burundi
Kwa upande wa shirika lisilokuwa la kiserikali la kijiji cha kamanyola ambako wakimbizi hao walikuwa wakiishi wanasema hawakubaliani kabisa na kitendo cha wakimbizi hao kuhamishwa ghafla.
Beatrice Tuptunzie ni kiongozi wa shirika la raia kijiji cha kamyola anathibitisha kuwa umoja wa mataifa uliwasindikiza, lakini namna walivyowahalisha ndio haikutufurahisha hata kidogo. Kwa sababu waliona wanawake wengi na watoto lakini wanaume hawakuonekana na haijulikani walienda wapi ?
Huku wakazi wa eneo hilo kuna walishtushwa na tukio hilo wakati wengine wakifurahia kuhamishwa kwa wakimbizi hao ingawa wapo waliokuwa na wasiwasi kuwa kwamba wanaweza kurudi kulipa kisasi kwa kuwa kuna wakimbizi waliouwawa mwaka jana.
Inaelezwa kuwa wakimbizi hawa hawakukubaliwa kukaa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo licha ya kuwa waliomba nafasi kwa muda mrefu na kuweza kufanikiwa kukaa nchini humo kwa takribani miaka mitatu.

Ilikuwaje leo Machi 8 ikawa Siku ya Wanawake Duniani?

Siku ya kimataifa ya Wanawake mjini Diyarbakir, Uturuki mwaka 2016Haki miliki ya pichaAFP
Image captionSiku ya kimataifa ya Wanawake mjini Diyarbakir, Uturuki mwaka 2016
Huenda umeshuhudia siku ya Wanawake Duniani ikitajwa kwenye Vyombo vya Habari au kusikia kwa marafiki .
Lakini kwa nini? Lini? Je ni sherehe au maandamano? na Je kuna siku kama hiyo ya kimataifa kwa Wanaume?
Kwa zaidi ya karne sasa, watu duniani wamekuwa wakisherehekea siku hii.

1. Ilianzaje?

Siku ya wanawake duniani ilianza kutokana na jitihada za wanawake 15,000 mwaka 1908 walipoandamana mjini New York Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura.Kilikuwa chama cha kisoshalisti cha Amerika kilichotangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake, mwaka mmoja baadae.
Wazo la kuwa siku ya kimataifa lilianzishwa na mwanamke kwa jina Clara Zetkin.
Alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake huko Copenhagen Denmark.
Kulikuwa na wanawake 100 hapo kutoka nchi 17 na wakakubaliana kwa pamoja.
Kwa mara ya kwanza ilisheherekewa mwaka 1911, Austria, Denmark,Ujerumani na Switzerland.
Sherehe ya 100 ilifanyika mwaka 2011, hivyo mwaka huu ni sherehe ya 107 ya wanawake duniani.
Clara Zetkin alianzisha siku hii mwaka 1910Haki miliki ya pichaTOPICAL PRESS AGENCY
Image captionClara Zetkin alianzisha siku hii mwaka 1910
Suala hilo likawa rasmi mwaka 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuanza kusherehekea siku hiyo na baadae kubuni kauli mbiu.Ya kwanza mwaka 1996 ilikuwa ''furahia yaliyopita, panga kwa ajili ya baadae''.
Siku ya kimataifa ya wanawake duniani imekuwa siku ya kutathimini maendeleo ya wanawake katika jamii katika nyanja za siasa na uchumi, kulikuwa pia na migomo na maandamano yaliyoratibiwa kwa ajili ya kusisitiza masuala ya usawa.
2.Ilikuwalini?
Tarehe 8 mwezi Machi. Wazo la Clara Zetkin la Siku ya kimataifa ya wanawake duniani halikuwa na tarehe maalum na haikuwa rasmi mpaka kipindi cha vita ya mwaka 1917 wakati wanawake wa kirusi walipodai Amani na kufanyia kazi tatizo la upungufu wa chakula (Waliimba Amani na Mkate).
Siku nne za mgomo, zilifanya watawala wa Urusi kuwapa wanawake haki ya kupiga kura.Tarehe ambayo mgomo ulianza ulikuwa kwenye kalenda ya Julian, ambayo ilikuwa ikitumika Urusi wakati huo, ilikuwa siku ya Jumapili tarehe 23 Mwezi Februari.
Siku hii katika kalenda ya Gregoria ilikuwa tarehe 8 mwezi Machi.
Na ndio hii inayosherehekewa leo.
3.Je kuna siku ya wanaume?
Ndio ipo, tarehe 19 Novemba. Lakini iliadhimishwa tangu miaka ya 90 na haitambuliwi na Umoja wa Mataifa.Watu huiadhimisha katika nchi zaidi ya 60. Lengo la siku hii ni kutazama afya za wanaume na wavulana, kuimarisha mahusiano ya jinsia,usawa wa jinsia na kutathimini jinsia ya kiume kama watu wa mfano wa kuigwa.Kauli mbiu ya mwaka 2017 ilikuwa 'kuwaadhimisha wanaume na wavulana'
4.Siku ya wanawake duniani inaadhimishwaje duniani?
Mwanamke akiwa amebeba maua mjini Roma, siku ya Wanawake duniani mwaka 2012Haki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionMwanamke akiwa amebeba maua mjini Roma, siku ya Wanawake duniani mwaka 2012
Siku ya kimataifa ya wanawake ni siku ya mapumziko katika nchi nyingi ikiwemo Urusi, ambapo mauzo ya maua huwa mara mbili zaidi wakati wa siku tatu au nne kabla ya siku yenyewe, ambapo wanaume na wanawake huwapa maua wapendwa wao wa kike na wafanyakazi wenzao.
Nchini China, wanawake wengi hufanya kazi nusu siku tarehe 8 Machi, kama ilivyoshauriwa na Baraza la nchi hiyo ingawa waajiri si mara zote wanatekeleza utamaduni huo.
Nchini Italia, siku ya kimataifa ya wanawake au La Fiesta della Donna inasheherekewa kwa kupeana maua chanzo cha utamaduni huu hakifahamiki lakini inaaminika ilianzia Roma baada ya vita ya pili ya dunia.
Nchini Marekani, Mwezi Machi ni mwezi wa historia kwa wanawake. Rais hutambua kila mwaka na kuthamini mafanikio ya wanawake wa Marekani.

5. Mwaka huu kinafanyika nini?

Kampeni ya siku ya kimataifa ya wanawake ina kauli mbiu isemayo ''Chochea kwa ajili ya maendeleo''
Takriban watu 500,000 wameandamana WashingtonHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Image captionTakriban watu 500,000 waliandamana Washington siku kama ya leo mwaka jana
Mwaka jana, mamilioni ya waandamanaji nchini Marekani na duniani kote wakipaza sauti kuhusu haki za wanawake baada ya ushindi wa Donald Trump kuwa Rais wa Marekani.
Mwaka 2018 maelfu ya watu wameingia mitaani tena katika miji mbalimbali ya Marekani,kumpinga Rais na kuwahamasisha wanawake kujiandikisha kupiga kura.