Katika mkesha wa siku ya wanawake duniani, shirika moja la kutetea haki za binaadamu nchini Burundi limewaorodhesha wanawake zaidi ya 500 nchini humo waliohusishwa na biashara ya watu.
Shirika hilo limeitaka serikali ya Burundi kupambana na maovu hayo ya kuuzwa kinamama na wasichana kwa kusafirishwa katika nchi za kiarabu.
Kwenye Ripoti yake ya mwaka, Shirika la ONLCT la kutetea haki za binadamu na kupiga vita biashara ya watu, limesema wanawake zaidi ya 500 wameuzwa katika nchi za kiarabu ikiwa ni pamoja na Oman, Saudi Arabia, Kuwait na Lebanon.
Uchugunzi uliofanywa na shirika hilo unaonyesha kuwa wasimamizi wa mtandao huo wanapokea mapato yasiyopungua dola elfu moja kwa kila mwanamke au kwa kila msichana.
Wakili Prime Mbarubukeye ambaye ni mkuu wa shirika hilo la ONLCT, wanawake na wasichana 527 ndio wameuzwa katika biashara hiyo mwaka jana.
Amesema kuwa serikali ni lazima iunde Tume ya kitaifa ya kupiga vita biashara ya watu hususan wanawake.
Anasema changamoto nyingine ni rushwa wanayopokea baadhi ya maafisa wa Serikali ambao wanahusika katika biashara hiyo.
"Watu wa mitandao hiyo wana pesa nyingi kiasi kwamba kutoa hongo ni jambo la kawaida mno katika biashara ya watu."
No comments:
Post a Comment