Wiki nzima iliyopita kwenye vyombo vya habari na mitandao Zimbabwe na Zambia, kulikuwa na habari kwamba Rais wa Zimbabwe aliyejiuzulu, Robert Mugabe, alilia mbele ya picha ya mke wake wa kwanza, Sally Mugabe.
Maelezo ya habari hiyo ni kwamba Novemba 15, baada ya Mugabe kuwekwa kuzuizini na jeshi la nchi hiyo ndani ya makazi yake, alimwaga machozi kumkumbuka Sally na mtoto wao aliyeishi duniani miaka mitatu tu, Michael Nhamodzenyika.
Chanzo cha habari hiyo kilitajwa kuwa wanajeshi waliohifadhiwa majina ambao walimweka Mugabe kuzuizini, ikiwa ni mwanzo wa safari ya kumshinikiza aachie madaraka. Kwa mujibu wa wanajeshi hao, Mugabe alisema: “Sally angekuwapo pengine haya yasingetokea.”
Ni hapo pa kukumbuka na kuchambua maneno ya mwanasheria wa Kenya, Profesa Patrick Lumumba kuwa maisha ya Mugabe yana sehemu mbili, moja kama kiongozi makini, shupavu na mtu bora akiwa mume wa Sally, pili ni kiongozi wa hovyo na asiyevutia kabisa akiwa mume wa Grace.
Mwaka 2008, meneja wa zamani wa Shirika la Ndege la Zimbabwe, Kevin Nolan, alifanya mahojiano na gazeti la Daily Mail la Uingereza na kutoa picha ambazo alimpiga Mugabe mwaka 1961 kwenye Kanisa Katoliki la jijini Salisbury, sasa Harare, Zimbabwe, siku alipofunga ndoa na Sally.
Katika mahojiano hayo na Daily Mail, Nolan alisema kuwa alimfahamu Mugabe kama mtu bora, msomi, mwenye maono ya kulikomboa taifa lake bila kujali tofauti za rangi.
Alieleza: “Nadhani Sally alichangia ubora ambao nilimuona nao Mugabe. Baada ya mwanamke huyo kufa Mugabe alibadilika kabisa.” Unapochukua maneno ya Nolan, yale ya Profesa Lumumba na taarifa za wanajeshi kuwa Mugabe alimwaga machozi kumkumbuka Sally, unapata taswira jinsi ambavyo mwanamke huyo alikuwa bora, vilevile namna Grace alivyombadili Mugabe kutoka kiongozi wa mfano bora kuwa wa mfano usiofaa.
Sally alifahamika kama Sarah Francesca Hayfron. Alitambulika zaidi kama Sally Hayfron na baada ya kufunga ndoa na Mugabe, jina lililovuma ni Sally Mugabe. Ni raia wa Ghana aliyegeuka mama wa ukombozi Zimbabwe.
Sally na Mugabe walikutana katika Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Takoradi, Ghana, wakati huo ikiitwa Pwani ya Dhahabu (Gold Coast) ilipokuwa koloni la Uingereza.
Wote walikuwa walimu na hapo ndipo mapenzi yalichanua kati yao kisha kufuatiwa na ndoa ya Kikatoliki mwaka 1961.
Sally alizaliwa mwaka 1931, ikiwa ni miaka saba baada ya Mugabe aliyezaliwa Februari 21, 1924. Zipo taarifa zinabainisha kuwa walipokutana Mugabe hakuwa na mawazo ya siasa, ila Sally kutokana na mwamko wa kiukombozi uliokuwepo nchini kwake (Ghana), tayari alikuwa ameanza kuvutiwa na siasa.
Kwa vile Sally alikuwa akivutiwa na vuguvugu la mabadiliko lililokuwa limeshika kasi Ghana, alipojua Mugabe anatokea Zimbabwe, wakati huo ikiitwa Rhodesia ya Kusini, alimshawishi kuingia kwenye harakati ili aikomboe nchi yake.
Zipo ripoti nyingine zenye kueleza kuwa Mugabe alikuwa mkimya na mwenye aibu sana lakini nadhifu, kwamba Sally ndiye alianza kumpenda kwa sababu alimuona mwenye akili nyingi, zaidi alivutiwa na ufundishaji wake, hivyo kujisogeza kabla ya kuunganisha nyoyo na kusafiri pamoja kimapenzi.
Ni mapenzi hayo yaliyowafanya waingie pamoja kwenye harakati za ukombozi dhidi ya Waingereza. Mugabe akiongoza mapambano, Sally akawa mama wa harakati, akiwahudumia wapiganaji waliowalazimisha Waingereza kukabidhi uhuru kwa Wazimbabwe.
Ni kipindi hicho cha mapigano ya kudai uhuru ambayo huitwa Chimurenga ya Pili au Rhodesian Bush War, ndipo Sally alipewa hadhi ya kuitwa Amai (Mama), akiwa mama wa Chimurenga hadi Mama wa Taifa. Chimurenga ya Kwanza ilikuwa vita ya mwishoni mwa Karne ya 19.
Sally alikuwa kishawishi kizuri cha wanawake Zimbabwe kuamka na kudai uhuru. Mwaka 1963 Mugabe alikamatwa na Serikali ya Rhodesia, kipindi hicho mtoto wake, Michael Nhamodzenyika alikuwa mchanga. Mwaka 1964 alihukumiwa kifungo cha miezi 21 jela. Hata hivyo, miezi hiyo ilipokwisha Mugabe alipewa sharti la kutojihusisha na harakati za ukombozi ili aachiwe, alipogoma hakuachiwa. Mwaka 1966 akiwa gerezani alipata taarifa za mtoto wake kufariki dunia lakini hakuruhusiwa hata kwenda kumzika.
Sally alisimama imara nyakati za msiba wa mwanaye, mwaka 1970 alifiwa na baba yake mzazi, ikabidi aombe makazi Uingereza kabla ya mwaka 1975 kwenda Msumbiji kuungana na Mugabe baada ya kuwa ameachiwa na kuendeleza mipango ya kudai uhuru.
Kuanzia mwaka 1980, Zimbabwe ilipopata uhuru, alitambulika kama Mama wa Taifa, akiwa mke wa Waziri Mkuu na Mkuu wa Serikali (Mugabe) kisha mwaka 1987, Canaan Banana alipoondolewa nafasi ya Rais kisha Mugabe kuchukua vyeo vyote, Rais kama Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Mkuu wa Serikali, Sally alitambulika kama First Lady.
Sifa kuu ya Sally wakati huo hakuwahi kujiingiza kwenye siasa. Alishughulika zaidi na masuala ya kijamii na kutoa misaada. Siku zote alimpa mumewe nafasi ya kufanya kazi. Hakuwa na kashfa. Alikuwa mwanamke wa heshima na maarufu mno.
Sally alifariki dunia mwaka 1992 baada ya ini lake kushindwa kufanya kazi baada ya kuugua muda mrefu. Inaelezwa kuwa kipindi akiumwa ndipo Mugabe alianza mapenzi na binti mdogo wakati huo, Grace, ambaye wakati Mugabe na Sally wakifunga ndoa mwaka 1961, alikuwa hajazaliwa.
Balozi ambaye alipata nafasi ya kuwa waziri kwenye Serikali ya Mugabe, Christopher Mutsvangwa, alipata kumweleza mwandishi wa mtandao wa Khuluma Africa kuwa Zimbabwe iliharibiwa na Grace kwa sababu alihonga vyeo vya uwaziri kwa vijana wasio na uwezo.
Mutsvangwa alitumia maneno “first boyfriends” kutambulisha mawaziri ambao alidai wengi wao walipata upendeleo kwa sababu za kuwa na uhusiano usiofaa na Grace ambaye ndiye alikuwa akiendesha Serikali baada ya kumzidi nguvu Mugabe.
Ipo kashfa kubwa iliyotikisa Zimbabwe, kwamba Grace alipata kuwa na uhusiano na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Gideon Gono. Kashfa hiyo ilivuma zaidi mwaka 2010 kuwa wawili hao walidumu kwa zaidi ya miaka mitano na waliutumia ukaribu wao kufuja rasilimali za umma.
Mtandao wa Zambian Observer ulipata kutaja wanaume wawili, Peter Pamire ambaye alifariki dunia kwa ajali tata ya gari, vilevile James Makamba aliyetoroka nchi, kwamba ni wanaume waliopata kuwa na uhusiano kijamii na Grace, likaongeza kwamba dada wa Mugabe, Sabina ndiye alibaini vitendo vya wifi yake na Gono.
Mifano hiyo mitatu ni kuonyesha jinsi Grace alivyougharimu utu na heshima ya Mugabe, kwani kukosa nidhamu ya ndoa na kujionyesha kuwa ni mwenye msuli mbele ya mume wake, ilikuwa sababu watu kumdharau kiongozi huyo na kuamini kuwa nchi iliongozwa na mkewe.
Hata namna Grace alivyoingia kwenye maisha ya Mugabe ilikuwa kwa kashfa kubwa. Kwani mwaka 1996, Grace akiwa Katibu Muhtasi wa Mugabe, vilevile akiwa mke wa rubani wa ndege za kijeshi Zimbabwe, Stanley Goreraza, alibainika kuzaa watoto wawili na Mugabe ambao ni Bona Nyepudzayi na Robert Peter Jr.
Kwamba katika watoto watatu aliokuwa nao Grace wakati huo ni Russell (mtoto wa kwanza wa Grace) peke yake ndiye alibainika kuwa baba yake ni Goreraza. Baada ya hapo Grace alifungua kesi mahakamani, akaomba talaka kisha akaolewa rasmi na Mugabe.
Kimsingi ndoa na Grace ilimvunjia heshima Mugabe kwa kumuoa mwanamke ambaye ni dhahiri alilazimisha talaka kwa mumewe aolewe na Rais, zaidi alizaa naye watoto wawili akiwa mke wa mtu. Goreraza baada ya kumpa talaka Grace alikwenda kusoma China kisha akafanywa ofisa Ubalozi wa Zimbabwe nchini China.
Grace ambaye amezidiwa umri wa miaka 41 na Mugabe, alizaliwa Afrika Kusini na wazazi wahamiaji. Aliungana na mama yake nchini Zimbabwe, akaolewa na Goreraza kabla ya kupata kazi ya ukatibu muhtasi Ikulu, Harare.
Baada ya ndoa na Mugabe, alijiingiza kwenye biashara ya madini lakini alianguka kila siku, hata hivyo alitia fora kwa kuishi maisha ya anasa mpaka akapewa jina la Grace Gucci. Alijilimbikizia mali na kusababisha Mugabe achekwe maana alionekana hana ubavu kwa mkewe.
Hali ikawa mbaya Grace alipotokeza na kukanusha madai hayo kisha akamwambia Mnangagwa: “Naweza kuwa Makamu wa Rais mzuri kuliko wewe, nipishe kwenye hiyo nafasi.” Kauli hiyo ya Grace ilichochea moto na kusababisha Novemba 6, Mugabe amfukuze kazi Mnangagwa na kuanza mchakato wa kumteua Grace.
Kitendo hicho ndicho kilibeba maudhui kuwa Grace alikuwa njiani kurithi urais, hivyo kuibua taharuki, jeshi likaingilia kati na kuidhibiti Serikali, chama (Zanu-PF) kikamuondoa Mugabe kwenye uongozi na Bunge likaanza mchakato wa kumvua madaraka, mwisho Novemba 21, alijiuzulu baada ya kuongoza nchi miaka 37.