Hakuna matumaini kwamba hali ya vuta nikuvute katika ulingo wa siasa hapa Kenya itafika tamati karibuni.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga na mshindani wake wake Rais Uhuru Kenyatta bado wanatunishiana msuli, kila mmoja akidhihirisha mzozo utaendelea.
Wanasiasa hao na wafuasi wa mirengo hii miwili pia wanaendelea na migogoro yao inayochochewa na ukabila, siasa mbaya na ukosefu wa njia mwafaka ya kusuluhisha mizozo ya kisiasa. Hali hii inaweza kusababisha kudorora kwa uchumi na miradi ya maendeleo.
Raila hangeweza kuhimili joto la kisiasa na akaamua kuzuru Zanzibar ambapo alifanya mikutano ya faragha na viongozi kutoka mataifa ya kanda ya Afrika Mashariki.
Raila bado yuko katika mchakato wa kujaribu kufanya mataifa mengine yaelewe mazingara ambayo yalimsukuma kutoshiriki uchaguzi wa marudio.
Mwanasiasa huyu anayeenziwa na wafuasi wake, alirejea nchini hivi majuzi kutoka ughaibuni alipofanya mikutano na viongozi kadhaa wa siasa kuhusu hali ya siasa nchini na hatua zinazofaa kuchukuliwa kurejesha hali ya kawaida. Haijulikani ikiwa ziara zake zitasaidia kutibu makovu ya siasa yanayotishia kupasua Kenya na kuleta maafa.
Kenya imeshikwa mateka na siasa duni za kumalizana na kufungia wengine nje wahisi baridi huku wengine wakiendelea “kula mapochopocho”. Ni kwa sababu hii ambayo baadhi ya viongozi wanapendekeza kuwe na nyadhifa zaidi kwenye upeo wa uongozi ili wale waliokosa kushinda kwenye uchaguzi, haswa wagombea wa urais, waweze kupata nafasi za kuongoza.
Kiini cha matatizo ya upinzani ni kura za hivi majuzi ambazo mrengo huu unaamini zilifanywa kinyume cha sheria. Lakini, Jubilee na wafuasi wake, hawataki kusikia hadithi hii kwa sababu wana uhakika uchaguzi ulikuwa haki na huru. Wanasema Raila hana budi kukubali uamuzi wa Mahakama ya Juu uliosema Uhuru alichaguliwa kulingana na sheria.
Ingawa Raila hakwenda mahakamani safari hii kupinga tena ushindi wa Uhuru, inaaminika na wengi kwamba waliofikisha kesi hizo mahakamani (Mwanasiasa Harun Mwau na mwanaharakati wa haki za kibinadamu Njonjo Mue) walikuwa wanawakilisha matakwa ya Nasa kortini.
Lakini Nasa imeapa kuwa haihusiki kwa njia yoyote na kesi hizo wakiongeza kwamba, matokeo ya kesi hizo hayawezi kuathiri mipango yao kuhusu hatua itakayochukua kuhakikisha “wanarejesha Kenya kwa demokrasia.”
Raila amekuwa akijikuta pabaya kila alipojaribu kukutana na wafuasi wake. Wiki jana alipokuwa anarejea kutoka ng’ambo, aliponea chupuchupu wakati gari lake lilipopigwa risasi mara kadhaa. Wanasiasa wa Nasa pamoja na wafuasi wao wanasisitiza kuwa, risasi hizo zilikuwa jaribio la kumuua kiongozi huyo.
Kwa bahati nzuri, gari la Raila haliwezi kupenywa na risasi. Nasa imetangaza kwamba inapanga kumwapisha Raila ikiwa Rais Uhuru ataapishwa Jumanne bila muafaka kuhusu hatma ya badaye ya nchi. Wabunge wa Nasa pia wamesema wataendelea kususia Bunge hadi suluhu ya kisiasa ipatikane.
Hata hivyo, wahenga wanasema, kelele za chura hazimzuii ng’ombe kunywa maji mtoni. Serikali ya Jubilee inaendelea na matayarisho ya kumwapisha Uhuru Novemba 28 jijini Nairobi. Waziri wa Mashauri, Fred Matiang’i ametangaza siku hiyo itakuwa mapumziko.
Nasa imesema siku hiyo wataandaa mkutano mkuu katika bustani ya Uhuru, Nairobi kuomboleza na waliofiwa kutokana na ghasia zilizotokea wakati polisi na wafuasi wa Raila walipokabiliana.
Viongozi wa upinzani wamesema hawawezi kumtambua Rais Uhuru na hiyo ndiyo sababu kuu ya wao wanapanga kumuapisha Raila kivyao eti kuongoza eneo fulani la Kenya ambalo upinzani umebuni.
Upinzani unasema Raila alishinda uchaguzi wa Agosti 8 uliobatilishwa na mahakama na ana haki ya kuapishwa. Unasema, Rais Uhuru ataongoza sehemu ya Kenya inayoitwa Central Republic of Kenya). Eneo hili la Wakikuyu na Kalenjin na Wenye asili ya Somalia. Kwa mawazo haya Je, Kenya yaelekea wapi? Siasa itatumaliza.
Hakuna siku Jubilee itaketi ikakubali kuona nchi ikigawanywa mara mbili ama tatu. Eneo la Pwani limekuwa likisema linataka kujitenga. Nawasihi wanasiasa wasiaje nchi itumbukie kwenye bahari ya utengano. Kenya ni moja na watu wake ni wamoja.
Viongozi waache ulafi na tamaa ya siasa na kujilimbikizia mali. Wakumbuke kwamba Kenya si yao. Rasilimali zinazopatikana katika nchi hii ni za kila Mkenya, bila kujali msingi wa kabila wala mrengo wa siasa. Kizungumkuti hiki italeta maafa zaidi kwa watu wasio na hatia. Bila shaka, polisi watakabiliana nao na baadhi yao watauawa.
Wiki tatu zilizopita, viongozi wa Nasa walizindua sare rasmi za mrengo wa wapiganiaji wa muungano huo. Sare hizo zina nembo ya ngumi kuashiria wameanza mapambano ya ukombozi wa tatu wa Kenya.
Nasa inasema Kenya inahitaji ukombozi ili Katiba izingatiwe na wale walionyanyaswa kwa miaka nenda miaka rudi, wapate kujisihi kama Wakenya.
Mwanasiasa Miguna Miguna amewaambia Wakenya wasichukulie siku hiyo ya kuapishwa kwa Uhuru kama ni siku muhimu.
“Siku hiyo ni siku ya kawaida. Mwanasiasa huyo mbishi ambaye pia amejitwika wadhifa wa jemedari wa National Resitance Movement (NRM) ya Nasa, anasema siku ya kuapishwa kwa Uhuru ni siku ya kawaida kama ile ambayo kidikteta wa Uganda, Idi Amin Dada aliapishwa.
Alifananisha siku hiyo kuu kwa Kenya kama ile siku aliyoapishwa aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
“Kuapishwa si kitu,” akasema. “Kuapishwa kwa viongozi kama Uhuru na Naibu wake William Ruto, hakuwezi kuwapa haki ya kuongoza Kenya,” akaongeza.
Matamshi ya Miguna ni mazito na yaliyojaa machungu lakini yanaungwa mkono na wafuasi na viongozi wengi wa Nasa. Hii inamaanisha kwamba, Rais Uhuru atakuwa na wakati mgumu wa kuongoza katika muhula huu wa pili na wa mwisho wa utawala wake ulioanza 2013.
Itakuwa vigumu kwa Rais kuongoza ikiwa sehemu nyingi za nchi zinalalamika huku zikitaka kujiondoa kutoka ramani ya Kenya.
Licha ya matamshi kama hayo na hisia zisizoambatana na sera za utawala wake, Rais Uhuru ambaye ni kama mzazi kwa Wakenya wote, anafaa kujinyenyekea na kutafuta njia mbadala za kuleta uponyaji kwa wananchi wote ili kila mmoja katika nchi hii ajihisi kama ni Mkenya.
Wananchi wanasema ikiwa kweli ulimwengu wote unaamini uchaguzi wa Oktoba 26 ulikuwa huru na haki, viongozi wa ulimwengu wangetuma risala zao bila kushurutishwa wala kuombwa.
Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kwa kutuma nyaraka kwa mataifa ya ughaibuni, Serikali ya Jubilee iliwashinikiza viongozi wa nchi hizo kutuma salamu hizo kinyume na mapenzi yao.
Ingawa Serikali imekana madai hayo, gazeti moja maarufu la kila siku lilichapisha mawasiliano kati ya Mohamed, balozi wa Kenya Uingereza na waziri wa Nchi za Kigeni wa Uingereza, Boris Johnson.
Johnson alijkuta pabaya baada ya kumpongeza Uhuru hata kabla ya nchi nyingine kufanya hivyo.
Hatua ya Johnson sasa imemweka pabaya Balozi wa Uingereza, Nicholas Hailey ambaye alikuwa anasubiri kuona mwelekeo wa siasa nchini kabla ya kutuma pongezi hizo.
Gazeti la Telegraph la Uingereza lilifichua kuwa, pongezi za Johnson zimeitenga Uingereza kutoka kwa mataifa mengine ya magharibi kwa sababu nchi hizo zimesita kupongeza Uhuru kwa pupa, zikisubiri kuona jinsi mambo yatakavyoendelea siku chache zijazo.
Hii si mara ya kwanza kwa Johnson kutuma risala bila kutafakari athari zake. Katikati ya mgogoro uliokumba ushindi wa Uhuru wa Agosti 8, Johnson alikuwa na haraka ya kumpongeza Uhuru. Ushindi huo ulifutilia mbali na mahakama na kuacha Uingereza na aibu kubwa.
Yote yanayoendelea nchini yanaonyesha Kenya ingali njia panda.
No comments:
Post a Comment