Thursday, April 12

Lazima tulinde haki za wasanii. Hotuba yangu Bungeni #kazizawasanii #hakizawasanii na zitto kabwe

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Muswada huu ambao unabadilisha Sheria Mbalimbali za Biashara. Kumekuwa kuna malalamiko mengi sana kwamba nchi yetu iko nyuma sana katika kuweka mazingira mazuri ya watu kuweza kusajili Makampuni, kupata leseni na kufanya biashara. Nakumbuka kwamba kwa miaka mitatu sasa mfululizo nchi yetu imekuwa ikipata alama ambazo si nzuri katika ripoti ya Benki ya Dunia inayoangalia mazingira ya biashara (Doing Business Report) ambapo ripoti ya mwaka 2012 inayoonyesha kwamba tumeshuka zaidi kutoka nafasi ya 125 duniani katika nchi 180 na zilizofanyiwa kazi mpaka nafasi ya 127. Kwa hiyo naamini kabisa kwamba mabadiliko haya ambayo tunayafanya yataweza kusaidia kupunguza muda ambao mtu anaweza akasajili biashara au kusajili Kampuni na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuanzia pale ambapo mzungumzaji aliyepita alianza kuzungumza na suala ambalo napenda leo nichukue muda mrefu na wa kutosha kabisa ni suala la biashara ya sanaa. Biashara ya sanaa kwa sababu ni biashara ambayo imekuwa haiangaliwi nami niseme kabisa kwamba tulichokishuhudia jana heroic funeral ambayo alifanyiwa marehemu Kanumba inadhihirisha kabisa kwamba Watanzania ni wapenzi sana wa sanaa. Kwa hiyo ni jukumu letu sisi kama wawakilishi wa wananchi, kama watunga sheria, kama watunga sera kupata ujumbe kutokana na umati wa Watanzania wa mkoa wa Dar es Salaam na waliotoka mikoa ya jirani na waliotoka mikoa ya mbali ambao walienda kumzika na kumpunzisha ndugu Kanumba jana. Kwa hiyo ule ni ujumbe ambao tunaupata na leo tunapoandika sheria hii tuwe na kumbukumbu tuangalie wananchi waliojitokeza kwenye mazishi yale na kuweza kuona tuweke sheria maalum ambazo zitaweza kuwasaidia na kuwalinda wasanii wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya marekebisho kwenye merchandise marked act ambapo tunaangalia pamoja na mambo mengine copy right neighbouring right act, paterns act, trade and services marked acts na hizo zingine mbili ambazo kwa leo sitaweza kuzichangia. Nataka nichangie hasa copy right and neighbouring act. Katika hotuba yetu ya Kambi ya Upinzani Bungeni mwaka jana tulitoa mapendekezo maalum ya kuweza kuangalia namna ya kuweza kulinda kazi za wasanii waweze kufaidika na kazi zao tuzuie wizi wa kazi za wasanii ambao Watanzania wanashiriki kwa sababu tunapoenda kununua kazi ya msanii ambao una uhakika kazi hii sio original, una uhakika kazi hii ni ya kutengenezwa na wewe ukatoa fedha yako ukanunua maana yake ni kwamba unamwua msanii ambao ungepaswa kuweza kumsaidia. Sasa njia pekee ya kuweza kuzuia hali hiyo ni kuweka sheria jinsi ambavyo inavyopaswa kuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimegawa sekta hii katika maeneo matatu ambayo ni ya kawaida unayakuta sana katika sekta ya mafuta au madini. Kwamba kuna up stream, mid stream na down stream. Kwenye up stream ni pale ambapo msanii anatengeneza kazi yake, pale sioni shida kwa sababu msanii atakaa nyumbani kwake, atakaa wapi ataandaa kazi yake. Lakini kwenye mid stream kwenye studios ambapo wasanii wanaenda kurekodi na baada ya hapo kazi zao zinaenda kusambazwa hapa kuna shida kubwa sana na ni eneo ambalo ni lazima tuliwekee regulations. Lazima tuliwekee kazi maalum na ningependa katika hili eneo la part four bahati mbaya sheria niliyonayo ni ile ambayo ilichapishwa tarehe 29 Julai, 2011. Kwa hiyo mtaweza kuangalia, muangalie namna ambavyo tutaweka leo katika sheria jinsi ambavyo tutalinda mid stream part katikati hapa ya kazi ya msanii pale anapoenda kurekodi na kuhakikisha kwamba kinachozalishwa pale kinafahamika, msanii anakifahamu na lile pendekezo ambalo lilitolewa na Waziri wetu kivuli wa masuala ya Habari, Utamaduni na Michezo la stickers lianzie pale ili kuweza kujua ni kiwango gani ambacho kimezalishwa katika studio na kiwango gani ambacho kinaingia kwenye soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili eneo ambalo ningependa Mheshimiwa Waziri liongezwe pia katika part four hii ni down stream part kwenye retail kwamba kazi ambayo inauzwa ya msanii biashara ile ya rejareja ya msanii iwe ni kazi ile ambayo ilizalishwa, kwa hili eneo pia tuweze kuliona namna ambavyo tutakavyoweza kulitilia nguvu katika sheria hii. Kwa maana hiyo ni kwamba nilikuwa napendekeza kwamba yale maeneo ambayo yameachwa ya Sheria ya Hatimiliki cap. 218 yachukuliwe na kuingizwa ndani ya mabadiliko haya ambayo tunayafanya ili kuweza kuhakikisha kwamba kazi za wasanii zinalindwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili hivi sasa tumepata taarifa kwamba TRA wanaandaa regulations kwa ajili ya stickers. Lakini nimeongea na mmoja wa wasanii wa muda mrefu Ndugu John Kitime anasema tayari regulations zipo wanaita epigram zipo lakini bado hazijaanza kutekelezwa. Kwa hiyo nilikuwa nadhani kwamba Mheshimiwa Waziri kwa sababu yeye ndio Waziri wa Wizara ambayo yuko responsible kwa hili ukishirikiana na Waziri wa Fedha kuhakikisha kwamba zoezi hili la TRA la kuandaa regulations nyingine za stickers liunganishwe na regulations ambazo tayari zimeshatengenezwa na ziko tayari toka mwaka 2006 ili ndani ya mwaka wa fedha unaoanza tarehe 1 Julai, 2012 stickers ziwe tayari na kazi za wasanii ziweze kutambulika pale ambapo zinakuwa zimetengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili nadhani hili litamhusu sana Mheshimiwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwamba tayari kuna regulations kuhusiana na royalties ambazo broadcasters wanapokuwa wanacheza miziki hii zile regulations kwa ajili ya royalties hazijawa enforced na hasa haya Makampuni makubwa, televesheni kubwa, redio kubwa hazi-enforce hili. Kwa hiyo miziki na filamu na kadhalika za wasanii wetu zinapokuwa zinachezwa hawapati zile royalties ambazo zinatakiwa na kama tulivyosema kwamba hii ni biashara na ni biashara ambayo inaweza ikawafaidisha sana wasanii wetu. Nilikuwa naomba tu Waziri tena narejea kwamba natumia iliyokuwa published tarehe 29 Julai 2011 kwa mtu anaweza kuangalia namna ambavyo inakwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 36 Prohibition to deal in counterfeit goods. Nimeangalia hapa orodha ya offence ambazo mtu atafanya kutokana na counterfeit sioni moja kwa moja mtu ambaye atahusika na wizi wa kazi za sanaa. Kwa hiyo nilikuwa naomba ile “a” mpaka “i” tutafute mahali ambazo tutaweka tuta-include copy right issues katika counterfeit act ili kuweza kuhakikisha kwamba tunaposema counterfeit hatutakuwa na maana tu ya bidhaa kama maji, bidhaa zingine hapana, lakini pili kazi ya msanii iweze kuwa included katika jambo hilo. Kwa hiyo tu-include katika ile “a” mpaka “i” masuala ya piracy, book leading na kadhalika yawe ndani ya sheria. Lakini lingine ambalo nimeliona hapa ni adhabu, sasa sijui itakuwepo kwenye amendment maana yake amendments nimezipata sasa hivi sioni adhabu kwa mtu ambaye hatakutwa anafanya biashara ya kazi ambazo zimeibwa za wasanii, sioni katika kifungu hiki cha prohibition to deal in counterfeit.

Kwa hiyo nilikuwa napendekeza sio tu adhabu ya kawaida iwe ni adhabu kali, adhabu ambayo ita-discourage kabisa watu kuiba kazi za wasanii wetu na kuweza kuziuza. Kwa hiyo nilikuwa nashauri kwamba nimeona kuna maeneo kuna faini za shilingi milioni 20, kuna miaka mitano jela sasa sina uhakika maana yake leo nimeiona sasa hivi kama hizi zinahusiana na hii yaku-deal na counterfeit. Kwa sababu hii section yote ya counterfeit imetajwa offences lakini haitaji adhabu. Kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri na watu wa Idara ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iongeze kipengele cha adhabu mara baada ya zile offences na iseme kabisa kwamba mtu yoyote at a written level atakayekutwa anauza ama ni CD au ni DVD ambayo ni Pirated ambayo ni counterfeit adhabu yake isiwe chini ya shilingi milioni 50. Hiyo ita-discourage kabisa kabisa kazi ambazo zinafanywa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hivyo tu sio mtu tu atakayekutwa anauza lakini pia mtu yoyote atakayekutwa in possession kwa hiyo hata kama wewe umepita pale Ubungo vijana wamekuuzia lakini ni kazi ya wizi umekaa labda umempa lifti Polisi akaona akagundua kwamba hii ni kazi ulionunua ni ya wizi wewe ambao umekutwa in possession uadhibiwe ili kujenga mentality ya Watanzania kuacha kununua kazi ambazo ni za wizi dhidi ya wasanii wetu. Kwa hiyo haya ndiyo mapendekezo ambayo nilikuwa nayaomba tuyaweke kwa sababu kuna fedha nyingi sana kwenye sanaa.

Commitment ya Serikali kulinda wasanii wetu(hansard) by zittokabwe

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA:

Napenda kutoa kauli ya Serikali, kwamba kutokana vikao vyote hivyo ambavyo nimesema kumi na sita vya Mawaziri lakini leo tena tumekutana mara ya kumi na saba, tumeazimia kwamba hotuba ya bajeti ya mwezi wa sita Mheshimiwa Waziri wa Fedha atalizungumzia jambo hilo na utekelezaji wa mambo yote pamoja na utengenezaji wa sticker, na jinsi ambavyo TRA watafanya jambo hilo yatawekwa bayana na mara baada ya bajeti speech kuanzia tarehe 1 Julai, kutakuwa na mabadiliko kubwa katika kazi za wasanii wa nchi yetu ya Tanzania.

Kwa hiyo nataka niwashukuru Waheshimiwa Wabunge, nataka tu watambue kwamba Serikali inaliona hilo Serikali iko pamoja na wao na ndiyo maana tumekutana namna hiyo na kwa hakika katika hili tuko pamoja kabisa na mtaona utekelezaji wake.

KAMATI YA BUNGE ZIMA

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeleta mapendekezo, Jedwali la Marekebisho kipengele hicho cha 38. Wakati Mheshimiwa Waziri anafanya winding up alitoa commitment ya Serikali kuhusiana na mabadiliko makubwa ya eneo la copyrights kwa ajili ya kulinda kazi za wasanii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri arejee ile commitment kabla sijaweza ku-move hii amendment. Tafadhali. Airejee kwa faida ya Taifa na kwa faida ya Bunge.

MWENYEKITI:

Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Zitto pamoja na amendment aliyoleta, amezingatia sana kauli yako wakati unajibu hoja za Waheshimiwa Wabunge. Anaomba ile commitment ya Serikali ya kufanya marekebisho kwenye sheria ya copyright. Sasa hiyo commitment ya Serikali ndiyo itakayomsababisha yeye kuondoa jedwali lake la marekebisho ili sasa tuhoji kifungu hiki.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA:

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati ninafanya majumuisho nilisema kwamba mimi na Mheshimiwa Mkulo – Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Nchimbi tumekutana mara nyingi sana kwa ajili ya suala hilo la kuangalia haki za wasanii Watanzania kwamba hazipotei. Lakini vile vile tumeagiza mamlaka zilizoko chini ya Wizara zetu; COSOTA kwa Viwanda na Biashara, TRA kwa upande wa Wizara ya Fedha na BASATA kwa upande wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wakae. Wamefanya vikao mara tatu. Kutokana na yaliyokubaliwa katika vikao vyote vya Waheshimiwa Mawaziri na wajumbe wa zile Kamati, Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia commitment ya Serikali kwamba kwenye Bajeti ijayo, Serikali italeta mapendekezo makubwa ambayo yatakuwa yamezingatia maoni yote ambayo yametolewa na BASATA, COSOTA na TRA kuhusu namna bora ya kulinda haki za wasanii wa aina zote katika nchi yetu ya Tanzania.

MHE. KABWE Z. ZITTO:

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka hiyo commitment ili itakapofika siku ya bajeti tutumie Hansard hii kuhakikisha kwamba commitment hiyo imetekelezwa. Kwa maana hiyo nikwamba naondoa amendment yangu ambayo nimeileta.

MWENYEKITI:

Nakushukuru. Na nafikiri kwamba Serikali iko makini, inavyofanya commitment hapa inaelewa nini inachokifanya.