NA BASHIR YAKUB -
1.ZUIO LA MAHAKAMA NININI.
Ni amri inayotolewa na mahakama kumzuia mtu kutofanya jambo fulani kwa muda. Kampuni nayo ni mtu ambapo yaweza kuomba zuio au kuzuiwa. Aidha yeyote ana haki ya kuomba amri hii ikiwa anaona kuna jambo fulani linafanyika na ikiwa litaendelea kufanyika basi litaharibu au kupoteza kabisa kitu fulani.
Kwahiyo zuio ni amri inayobeba maagizo maalum kwa mtu au watu maalum kuwaamrisha kutoendelea na kitu fulani kama tulivyoona hapo juu.Sheria ya Mwenendo wa Madai, Sura ya 33 na Sheria nyingine mtambuka zimeongelea kuhusu zuio.
2. KATIKA MATUKIO GANI UNAWEZA KUOMBA ZUIO.
( a ) Kwa mfano, umeshindwa kulipa mkopo na tayari una taarifa kuwa benki au taasisi yoyote ya fedha inataka kwenda kuuza na unahisi kuna pahala hapaendi sawa katika mikataba yenu.
Basi unaomba zuio ili hiyo mali yako uliyoweka rehani isiuzwe mpaka hapo hilo eneo ambalo mmeshindwa kuelewana litakapopatiwa majibu.
( b ) Kwa mfano, umemuuzia mtu gari, pikipiki, au mashine yoyote. Mtu huyo hajalipa kiasi cha pesa iliyobaki kama mlivyokubaliana. Lakini anaendelea kutumia kifaa hicho. Unaweza kuomba kumzuia kuendelea kutumia mpaka atakapolipa kiasi kilichobaki ili asiendelee kuharibu au kuzeesha kifaa hicho.
( c ) Kwa mfano, we ni mpangaji katika nyumba ya kuishi au biashara. Mwenye nyumba,eneo anataka kukutoa kwenye pango hilo bila kufuata utaratibu au kwa kukiuka baadhi ya makubaliano kwenye mkataba wenu. Unaweza kuomba zuio asiendelee kukutoa.
Pia mazingira mengine yoyote ambayo unahisi kuna kitu, jambo linataka kuharibiwa au kuingiliwa, kuuzwa, kupotezwa,kufichwa kinyume na utaratibu unaweza kuomba zuio hilo.
3. SHARTI KUU .
Ili uweze kuomba zuio ni lazima pia kuwepo na shauri la msingi. Kwa maana utafungua shauri la msingi kulalamikia jambo fulani halafu utaomba zuio ndani ya shauri hilo. Kwa mfano unafungua shauri kulalamikia mwenye nyumba kusitisha mkataba wa pango bila kufuata utaratibu.
Hilo ni shauri kuu. Halafu ndani mwake unafungua shauri dogo la kuomba zuio ili asikuondoe katika nyumba mpaka kwanza shauri kuu la kukiuka utaratibu litatuliwe.
Kwahiyo ni sharti kuwapo shauri kuu ukilalamikia jambo fulani halafu ndani mwake ndio uombe zuio.
4. UMUHIMU WA ZUIO.
( a ) Linasaidia mali yako kutouzwa au kutoondolewa kwenye nyumba kama mgogoro unahusu nyumba.
( b ) Linalinda mali yako isiharibiwe ,isifichwe, isihamishwe,isiingiliwe kwa namna yoyote ile kama ipo katika mazingira hayo.
( c ) Linakupa nafasi ya kutafakari na kujipanga ikiwa upo katika presha ya kukimbizana na jambo ama mgogoro.
( d ) Linatoa mwanya wa mazungumzo kati ya mlalamkaji na mlalamikiwa.
5. WAPI UKAOMBE ZUIO.
Zuio linaombwa mahakamani. Na linaweza kuombwa mahakama yoyote katika shauri lolote. Linaweza kuombwa kwenye mashauri ya ndoa, mirathi, ardhi, biashara, mikataba, madai ya kawaida ya pesa au mali, makampuni n.k.
Na linaombwa katika mahakama zote yaani ya mwanzo, ya wilaya, ya hakimu mkazi mahakama kuu na ya rufaa pia. Lakini pia linaombwa kwenye mabaraza ya ardhi ya kata na wilaya.
6. KUKIUKA AMRI YA ZUIO.
Ikiwa utaomba zuio na kupata halafu aliyezuiwa akakiuka na kuendelea na kile alichozuiwa basi kosa linabadilika na kuwa la jinai. Inakuwa jinai ya kuingilia amri na shughuli za mahakama. Ni kosa ambalo aliyekiuka amri hiyo akithibitika ni kweli kakiuka basi atatakiwa kwenda jela miezi sita ama vinginevyo.
Kinachotakiwa kwako ni kuripoti tu kuwa amri iliyotolewa sasa haitekelezwi na yule aliyeamrishwa kutekeleza. Utaripoti mahakama hiyo hiyo iliyotoa zuio hilo.