Wednesday, October 11

Hospitali ya Aga Khan kupanuliwa


Dar es Salaam. Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Mtukufu Aga Khan amesema  wamedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kupanua hospitali.
Amesema Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam itapanuliwa na pia watajenga chuo kikuu kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki mkoani Arusha.
Mtukufu Aga Khan amesema hayo leo Jumatano Ikulu jijini Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na Rais John Magufuli.
Amesema upanuzi wa hospitali utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi 172, kuimarisha matibabu ya moyo na saratani.
Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema upanuzi wa hospitali pia utahusisha ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.
Kuhusu chuo kikuu, Mtukufu Aga Khan amesema jumuiya imedhamiria kujenga kikubwa ambacho kitafundisha viongozi si tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali Afrika nzima ili wawe chachu ya mabadiliko na maendeleo.
Rais John Magufuli katika taarifa hiyo amemshukuru Mtukufu Aga Khan kwa taasisi zake kutoa huduma za kijamii nchini Tanzania.
Ametoa wito kwa taasisi hizo kupunguza gharama za huduma ili wananchi wamudu na hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.
Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Aga Khan na amemuomba kiongozi huyo wa dini kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.
Kuhusu vyombo vya habari, Mtukufu Aga Khan amesema haamini kuwa ni kipaumbele kwa vyombo  hivyo kujikita katika masuala ya siasa.
Amesema anaamini kuwa vyombo vya habari vina wajibu mpana zaidi wa kujikita katika masuala ya maendeleo na hasa katika nchini zinazoendelea na kwamba, Aga Khan ipo katika mchakato wa kujikita katika wajibu huo kwa kuwa na waandishi wa habari na wachambuzi mahiri.
Soma: Rais Museveni amvika nishani ya heshima Aga Khan

No comments:

Post a Comment