Mshambuliaji wa Simba ya Dar es Salaam, Emmanuel Okwi amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Agosti wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/2018.
Okwi alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam jana (Jumatano) na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha wa viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa. Wachezaji wote hao timu zao zilishinda.
Walioshindana na Okwi katika hatua hiyo ya mwisho ni kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa ambaye alisaidia timu yake kupata pointi tatu kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo dhidi ya Stand United uliofanyika Uwanja wa Manungu, Turiani, ambapo alikuwa nyota wa mchezo huo. Mwingine aliyeshindana na Okwi ni Boniface Maganga wa Mbao FC.
Maganga alitoa mchango mkubwa katika ushindi wa ugenini wa bao 1-0, ambao timu yake iliupata dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba ikiwa ni pamoja na kufunga bao hilo.
Ushindi wa Okwi unatokana na kutoa mchango mkubwa katika mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 7-0, huku Okwi akifunga mabao manne.
Pia Okwi amekuwa mchezaji wa kwanza msimu huu kufunga hattrick (mabao matatu katika mchezo mmoja) katika Ligi Kuu ya Vodacom inayoshirikisha timu 16, ambapo hat trick hiyo alifunga ndani ya dakika 45 za kipindi cha kwanza.Mwezi huo ulikuwa na raundi moja tu iliyochezwa Agosti 26 na 27 mwaka huu ambapo kila timu ilicheza mechi moja.
Kutokana na kutwaa tuzo hiyo, Okwi ambaye pia ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) atazawadiwa kitita cha Sh. 1,000,000