Maelfu ya Wapalestina wamebakia katika mahema katika mpaka wa Gaza Jumatatu (April 2), wakiendelea kuandamana wakidai haki ya kurejea kwa wakimbizi na vizazi vyao katika eneo ambalo leo ni Israel hata baada ya waandamanaji 16 kuuwawa na majeshi ya Israeli.
Idadi hiyo iliyokusanyika Jumatatu ilikuwa ndogo ukilinganisha na ile iliyoandamana mwisho wa wiki, ambapo ilionekana kuwepo uvunjifu wa amani uliopita kiasi katika ukingo wa Gaza tangia vita vya Israeli na Hamas vilipozuka mwaka 2014. Hamas ni jeshi la kundi la Kiislam ambalo linalishikilia eneo la pwani lililozingirwa.
Waandamanaji wengi Jumatatu wamekaa katika eneo salama mbali na mpakani, wakichukua tahadhari juu ya kuwepo majeshi ya Israeli ambao wameendelea kukalia eneo lenye kizuizi upande wa pili wa mpaka huo.
Jeshi la Israeli limesema kuwa baadhi ya wale waliorushiwa risasi Ijumaa, siku ya kwanza ya maandamano hayo, walikuwa wamewatupia risasi wanajeshi wa Israeli, wametuma matairi yaliyokuwa yanawaka moto kuelekea kwa wanajeshi hao na pia kutupa mawe na mabomu yakutengeneza wenyewe kwenda upande wa pili wa mpaka huo.
Hamas imesema watano kati ya wale waliouwawa walikuwa ni wanachama wa kitengo cha wapiganaji wake. Israel inasema wanane kati ya watu 15 waliouwawa walikuwa ni wa kikundi cha Hamas, na wengine wawili wa kikundi kingine.
Hata hivyo Hamas imekanusha kuwa wapiganaji wake hawakurusha risasi dhidi ya majeshi ya Israeli na wala hawakutumia waandamanaji kama ngome yao.
Siku ya Jumatatu, idadi ya Wapalestina waliouwawa ilifikia watu 16, baada ya madaktari wa Kipalestina kusema kuwa mtu mwenye miaka 29 alikufa kutokana na majeraha yaliyotokana na kurushiwa risasi siku ya Ijumaa.