Zanzibar. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalumu, Zanzibar, Haji Omar Kheir amesema Serikali ya itachukua maeneo yote ya ardhi yenye mgogoro au iliyouzwa kinyume na taratibu ili yawe ya kilimo.
Waziri Kheir ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Baraza la Mapinduzi iliyoundwa kushughulikia migogoro ya ardhi visiwani hapa alisema: “Maeneo yaliyotolewa kinyume na taratibu na kusababisha migogoro baina ya wanunuzi na wauzaji yatachukuliwa na kupewa wananchi ili wayatumie kwa shughuli za kiuchumi na kilimo.
“Haya maeneo mengine ya Serikali yalikuwa yanatumiwa na wananchi kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo lakini ghafla yameuzwa kinyume na taratibu.”
Kheir alisema jambo kubwa linalochangia kuibuka migogoro ya ardhi ni kuwapo baadhi ya viongozi wasio waaminifu katika kutekeleza majukumu yao kwa kuwa wanaendeleza hujuma za kuuza maeneo hayo kinyume cha sheria.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Dk Sira Ubwa Mamboya ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alitaja baadhi ya maeneo yanayoongoza kwa uuzwaji wa maeneo kinyume na taratibu ni Bwejuu, Paje, Michamvi, Marumbi, Kidimni na Kiboje.
Baadhi ya viongozi wa maeneo hayo, waliahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha kila eneo ambalo limeuzwa kinyume na taratibu za kisheria linarudi mikononi mwa Serikali.
No comments:
Post a Comment