Ndivyo anavyosema Anselimi Nere (82) mkazi wa Kimara Stop Over ambaye wapangaji wake wamegoma kumlipa kodi ya nyumba ya mwezi Agosti wakihofia bomoabomoa.
Uwekaji wa X katika majengo yaliyo kando ya Barabara ya Morogoro kuanzia Kimara hadi Kiluvya ni mpango kuipanua unaofanywa na Serikali chini ya Wakala Barabara (Tanroads).
Nere ambaye nyumba yake bado haijawekewa alama ya X, amekuwa akiishi maisha ya hofu yeye na wapangaji wake tangu alipoona jengo la jirani yake Revy Kapinga likiwekewa alama ya X.
“Kila siku nimekuwa na kazi ya kuamka asubuhi na kukagua nyumba yangu, hata nikiwa nje nikiona vijana wamebeba mabegi mgongoni moyo wangu unashtuka paa! Nafikiri wanakuja,” alisema.
Nere ambaye anaishi peke yake huku akisumbuliwa na maradhi ya pumu, alisema wapangaji wake ambao ndiyo tegemeo lake wamegoma kabisa kulipa kodi.
“Niliwafuata wakaniambia ‘wewe mzee ina maana huoni kinachoendelea, tutakulipaje kodi wakati muda wowote nyumba yako inavunjwa’,” alisema akimnukuu mmoja wa wapangaji wake.
“Wamegoma, nina wapangaji wanne wananilipa Sh40,000 kwa mwezi nikiwaomba wananicheka inaumiza sana,” alisema.
Hali halisi ya mzee
Mwandishi wetu alifika nyumbani kwa mzee huyo ambaye amewahi kuwa mhasibu mkuu wa taasisi moja ya Serikali kuanzia mwaka 1967 hadi 1995 kwa sasa ni mstaafu.
Baada ya kujitambulisha kwake, mzee huyo alifurahi na kusema alitamani kuonana na waandishi wa gazeti la Mwananchi ambao wamekuwa wakiandika habari za bomoabomoa ili atoe dukuduku lake.
“Nimefurahi, yaani hapa nilikuwa najiuliza ni vipi nitawapata ili nitoe dukuduku langu ni kama Mungu amewaleta,” alisema na kuongeza: “Leo nitalala, nimekuwa na amani moyoni maana ni kama nilikuwa na sumu ikiniumiza sasa nimepata pa kuitolea,” alisema.
Nere alitumia nafasi hiyo kumwomba Rais John Magufuli awaonee huruma wananchi wake hasa wazee.
“Hata nikipata nafasi ya kuonana na Magufuli leo, nitamlilia awe na huruma hata kidogo na wazee, wanaoumia na hili zoezi wengi ni sisi wazee na wajane,” alisema.
“Wazee hawataki kukaripiwa tunahitaji maneno yenye faraja, kwa nini anakosa hata huruma, anapotufukuza hapa anataka twende wapi?” alihoji.
Mzee huyo pia alisema anaishi peke yake kwani waliachana na mkewe miaka mingi iliyopita.
Alisema nyumba yake ndiyo kila, kitu kwani alikuwa na shamba la ekari saba eneo la Kwembe na lenyewe lilichukuliwa na Serikali bila kulipwa fidia.
Wapangaji na majirani
Wapangaji kwenye nyumba ya mzee huyo walikiri kutolipa kodi ya nyumba wakihofia bomoabomoa.
“Tutalipaje kodi ya nyumba wakati muda wowote wanakuja kuweka X kama wameweka alama ya X kwa wananchi wengine ambao ni majirani wa babu unafikiri na yeye atapona?” alisema Hamida Ally.
Hamida alisema ni kweli mzee huyo anaishi maisha magumu na tangu operesheni ya bomoabomoa kuanza kwani amekuwa hana amani.
“Kuna siku aliamka asubuhi akakuta kuna hiki kibanda cha Mpesa kimeandikwa maneno mekundu mzee alihamaki kwa kweli mpaka alipokuja kujiridhisha kuwa siyo,” alisema Sabrina Hassan mpangaji mwingine wa mzee huyo.
“Si wote ambao wamegoma ni wachache, lakini wengine tumemlipa, ila kiukweli hata sisi tunalala mguu ndani mguu nje mtu unajiuliza ukilipa kodi leo kesho wakaja kuvunja utafanyaje? alisema.