Friday, August 11

‘Ka-ta’ yaingiza Sh41 bilioni


Dar es Salaam. Agizo la neno moja ambalo Rais John Magufuli aliligawa na kutoa mawili la (kata), akiagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwakatia huduma wadaiwa sugu, limeingiza Sh41 bilioni ndani ya miezi mitano.
Machi 6, wakati Rais Magufuli akiweka jiwe la msingi kwenye kituo kipya cha Tanesco mkoani Mtwara, alilitaka shirika hilo kuwakatia huduma wadaiwa sugu zikiwamo taasisi, mashirika ya umma na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) iliyokuwa inadaiwa Sh21 bilioni.
“Tanesco pasitokee taasisi au wizara, hata Ikulu isipolipa umeme we kata tu. Natumia maneno mawili ka-ta, hatuwezi kujiendesha kwa hasara wakati kuna watu wanakwepa kulipia gharama,” aliagiza Magufuli.
Kufuatia agizo hilo, Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa miongoni mwa wadaiwa sugu walianza kulipa.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda na Biashara (Tuico) tawi la Tanesco, Hassan Athuman alisema awali kiwango kilichokuwa kikidaiwa ni Sh275 bilioni.
Athuman alitoa mchanganuo wa malipo hayo kuwa ni Zeco imelipa Sh18 bilioni, taasisi za Serikali Sh18 bilioni na watu binafsi Sh5 bilioni.
“Wafanyakazi wa Tanesco tumeamua kumpongeza na kumuunga mkono Rais Magufuli kwa jitihada zake za kuhakikisha wadaiwa sugu wanalipa,” alisema Athuman.
Alifafanua kuwa wanamuahidi Rais Magufuli hawatamuangusha.
Katibu wa Tuico tawi la Tanesco, Mwandu Chandarua alisema licha ya madeni, wafanyakazi wamefurahishwa na Serikali kuahidi kutekeleza mradi wa umeme wa maji wa Stieglers Gorge wilayani Rufiji. Awali, Serikali ilisema mradi huo utakaotoa megawati 2,000 utajengwa kwa fedha za ndani.
“Tuna uhakika mradi huu na mingine inayotekelezwa, ikikamilika tutakuwa na umeme unaotutosha na mwingine tunaweza kuuza nje ya nchi,” alisema.
Kuhusu vishoka, Chandarua aliwataka wananchi kuhakikisha wanawasiliana na ofisi kama wanahitaji msaada, badala ya kutafuta watu mitaani.

No comments:

Post a Comment