Deni hilo, ambalo ni sawa na dola 190 bilioni za Kimarekani limetokana na hesabu zilizopigwa kwa kutumia taarifa iliyotolewa na kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza usafirishaji wa mchanga wa madini unaofanywa na kampuni hiyo kutoka migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi.
Taarifa iliyotolewa jana na kampuni hiyo imekataa kulipa deni hilo kwa maelezo kwamba haijapewa ripoti ya kamati zote mbili.
“Hatuyakubali makadirio haya. Kampuni itaangaalia haki na namna zote zilizopo kuhusu suala hili,” inasema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa Acacia, deni hilo limeelekezwa kwa kampuni zake tanzu ambazo ni Bulyanhulu Gold Mine (BGML) inayoendesha mgodi wa Bulyanhulu, na Pangea Minerals (PML) inayosimamia mgodi wa Buzwagi.
Taarifa hiyo iliyopokelewa jana kutoka TRA inadai kodi hiyo ni kuanzia mwaka 2000 mpaka 2017 kwa BMGL na kati ya mwaka 2007 hadi 2017 kwa PML. Katika deni hilo, kodi ambayo haikulipwa ni dola40 bilioni za Kimarekani (zaidi ya Sh88 trilioni) pamoja na dola 150 bilioni (zaidi ya Sh330 trilioni) ambazo ni faini na riba.
Bajeti ya mwaka 2017/18 ya Serikali ya Tanzania ni Sh31.7 trilioni na hivyo fedha hizo zinaweza kugharimia bajeti ya miaka 13 na miezi mitatu bila kutegemea misaada ya wahisani.
Endapo kila Mtanzania atapewa mgao kutoka kwenye fedha hizo, kati ya wananchi milioni 56 (kwa mujibu wa Benki ya Dunia) kila mmoja angepata zaidi ya Sh7.57 milioni. Fedha hizo pia ni zaidi ya mara nane ya deni la taifa ambalo ni takribani Sh51 trilioni ka sasa.
Mkurugenzi wa Elimu ya Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo.
“Kwa sasa siwezi kutoa maoni yoyote kwa sababu mawasiliano hufanyika kati yetu na mteja. Hata hivyo, sina waraka wowote ninaoweza kuutumia,” alisema Kayombo.
Sakata la Acacia lilianza wakati Rais John Magufuli alipozuia usafirishaji wa mchanga nje mwaka jana na baadaye Machi mwaka huu.
Makontena 277 yaliyokuwa bandarini kusubiri kupelekwa nje kwa ajili ya kuyeyushwa, yalizuiwa na baadaye Rais kuunda kamati kwa ajili ya kuchunguza kiwango cha madini kilichokuwa kwenye mchanga huo.
Siku chache baadaye, Rais aliunda kamati nyingine iliyopewa jukumu la kuangalia athari za kiuchumi ambazo nchi ilipata kutokana na kusafirisha mchanga huo nje.
Acacia inasafirisha mchanga huo nje kwa ajili ya kuuyeyusha kupata mabaki ya madini ya dhahabu na shaba ambayo yalishindikana katika hatua ya awali ya uchenjuaji ambayo hufanyika mgodini.
Acacia inadai kuwa kiwango cha dhahabu kilichomo kwenye mchanga huo ni takriban asilimia 0.3, lakini kamati iliyoundwa na Magufuli ilisema kuwa kiwango cha dhahabu ni mara kumi ya kile kilichotangazwa na wawekezaji hao kutoka Canada.
Matokeo hayo yalimfanya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, kumsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) pamoja na kamishna wa madini.
Pia aliagiza wafanyakazi wa TMAA kutoendelea kufanya kazi kwenye migodi hiyo hadi hapo utakapotolewa uamuzi mwingine.
Rais pia alimuagiza Waziri wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi kuunda jopo la wanasheria kwa ajili ya kuangalia mabadiliko ya sheria ya madini na kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko hayo.
Tayari mabadiliko hayo yameshapitishwa na Bunge, ambayo yanaipa mamlaka Serikali kufanya mazungumzo upya na kampuni za uwekezaji kwenye madini na pia kuongeza mrabaha kutoka asilimia nne hadi sita.
Kamati ya pili iliibuka na matokeo yaliyoonyesha kuwa Tanzania imepoteza zaidi ya Sh108 trilioni kwa kusafirisha mchanga huo kwa miaka 20.
Kamati hiyo pia ilidai kuwa Acacia haijasajiliwa nchini na haina leseni ya kufanya biashara nchini na hivyo shughuli zake ni kinyume cha sheria.
Kamati hiyo pia ilinyooshea vidole wanasiasa na watumishi wa umma walioshiriki kuingia mikataba na kampuni za uwekezaji kwenye madini na pia walioshughulikia mabadiliko ya sheria ya madini ambayo yalilenga kuipunja nchi.
Hata hivyo, Acacia imekataa kuzikubali ripoti za kamati zote mbili ikisema haikushirikishwa na kwamba kamati hizo hazikuwa huru.
Acacia imekuwa ikisisitiza kuwa uchunguzi huo haukufanywa na kamati huru na hivyo kutaka iundwe kamati huru kufanya uchunguzi huo.
Pia imekuwa ikijitetea kuwa imekuwa ikitoa taarifa sahihi kuhusu kiwango cha madini kilichomo kwenye mchanga huo kuwa ni sahihi na kwamba kama matokeo ya uchunguzi wa kamati ya kwanza yangekuwa sahihi, Tanzania ingekuwa mzalishaji mkubwa wa dhahabu duniani.
Kuhusu matokeo ya kamati ya pili, Acacia imesema pia inaipinga kwa kuwa ilifanya tathmini yake kwa kuzingatia matokeo ya kamati ya kwanza, ambayo haikubaliani nayo.
Pamoja na hayo, mwenyekiti mtendaji wa Barrick Gold, ambayo ni kampuni mama ya Acacia, Profesa John Thornton (pichani) alikuja nchini kwa ndege ya kukodi kutoka Canada kwa ajili ya kuzungumza na Rais Magufuli.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais aliwaambia waandishi wa habari kuwa Acacia imekubali kuwa ilifanya makosa na kwamba imeahidi kulipa fedha ambazo zitabainika kuwa hazikulipwa.
Alisema Serikali na kampuni hiyo zimekubaliana kuunda timu ya kufanya mazungumzo ya kutafuta muafaka wa suala hilo.
Hata hivyo, Acacia imesema haitashiriki kwenye mazungumzo hayo na badala yake Barrick ndiyo itahusika isipokuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa ni lazima yaridhiwe na kampuni hiyo.
Acacia pia imeshatoa notisi mahakamani kuonyesha nia yake ya kufungua kesi kupinga maamuzi hayo ya Serikali.