Tuesday, July 25

Ruto awashutumu Nasa kwa kuchochea ghasia



Makamu wa Rais, William Ruto

Makamu wa Rais, William Ruto 
Nairobi, Kenya. Makamu wa Rais, William Ruto amewashutumu viongozi wa upinzani kwa kutoa madai ya uongo dhidi ya wanajeshi ili kuchochea wafuasi wao wazue fujo baada ya uchaguzi.
Ruto alidai jana Jumatatu kwamba muungano wa upinzani, Nasa, umetambua kuwa utashindwa uchaguzi ujao wa urais hivyo viongozi wake wanatafuta njia ya kupinga matokeo kwa kutumia ghasia baada ya uchaguzi.
“Inafahamika wazi kuwa upinzani umetambua utashindwa ndiyo maana unapanga kuanzisha ghasia kwa vile sasa mahakama imethibitisha uchaguzi utakuwa Agosti 8,” alisema.
Makamu wa Rais alisema hayo alipokuwa katika mikutano ya kampeni maeneo ya Kuresoi, Rongai, Likuyani na Amagoro katika Kaunti za Nakuru, Kakamega na Busia.
“Sasa wanatoa madai dhidi ya wanajeshi wetu na polisi kwa sababu njama yao ya awali ilifeli na wanataka kusababisha fujo siku ya uchaguzi,” akadai.
Viongozi wa Nasa wakiongozwa na mgombea urais Raila Odinga walidai wanajeshi wanatumiwa katika njama ya kuiba kura za urais.
Matamshi hayo ndiyo Ruto alisema ni ya uchochezi na yanatokana na kuwa upinzani hautaki pawepo usalama katika vituo vya kupigia kura.

No comments:

Post a Comment