Kondoa. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa wiki moja kwa waajiri nchini kuwapa mikataba ya ajira vibarua wao.Profesa Mbarawa alitoa agizo hilo jana alipokuwa kwenye ziara ya kukagua ujenzi wa Barabara ya Dodoma-Arusha, katika vituo vya Chiko wilayani Chemba na Mela kilichopo Kondoa, Mkoa wa Dodoma.Profesa Mbarawa alisema, “Ninachokisema katika kituo hiki (Chiko) ndani ya saa 12, wafanyakazi wote wawe wameshapatiwa mkataba ili waweze kwenda na muda uliopangwa wa kumaliza mradi wa ujenzi wa barabara, hili ni agizo kwa nchi nzima ndani ya wiki moja.”Wafanyakazi wa kituo cha Chiko wapo kwenye mgomo wakishinikiza kupatiwa mkataba wa kazi.Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Faisaly Shaaban alisema uwapo wao katika eneo la kazi siyo shida lakini wanataka mkataba kwanza ndiyo wafanye kazi.Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiomba wapewe mkataba, lakini wameendelea kuzungushwa hadi leo.“Sisi tumeamua kufanya mgomo baridi, hatuna kelele ila kazi hazifanyiki hadi tupatiwe mkataba, ndiyo tutaingia kazini.“Mwaka 2014, iliwahi kutokea tukaahidiwa ndani ya wiki moja tutakuwa tumepatiwa mkataba lakini kilichotokea hakuna hadi leo, tunanyanyasika kufanya kazi tukiwa vibarua, hili halikubaliki,” alisema Shabani.Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Ramadhani Maneno alisema Serikali inafanya mambo kwa mikataba hivyo ni vyema watumishi wakafanya kazi kwa kufuata taratibu hiyo.“Barabara hizi zipo kwenye mkataba, hivyo ikifika wakati wa kukabidhi inabidi ikabidhiwe ikiwa imemalizika na siyo vinginevyo, hivyo kwa wafanyakazi wa hapa kila mmoja apewe mkataba wake kulingana na kazi anayoifanya,” alisema Maneno.Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Kanda ya Dodoma, Injinia Leonard Chimagu alisema ni kosa kumpa kazi mtu yeyote bila kumpatia mkataba kwanza.Aliutaka uongozi ufanye haraka kutoa mikataba kabla ya wafanyakazi kuendelea na kazi zao.“Nimeshangazwa na mgomo huu, maana kabla ya kuanza kazi tulitoa mafunzo elekezi kwa waajiri kuhusu kuwapa mikataba wafanyakazi.“Sasa leo mgomo unatokea kwa kosa ambalo tulilimaliza taratibu, ni vyema wakalimaliza haraka kabla ya tatizo jingine halijaibuka,” alisema Chimagu