Sunday, March 11

Tamko latolewa kulaani udhalilishaji wa wakunga

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania,
Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila 
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limelaani hatua zilizochukuliwa na baadhi ya viongozi kwa wauguzi.
Katika tamko la baraza hilo, limelaani tukio la Machi 7,2018 katika Hospitali ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara ambalo muuguzi Amina Nicodemus aliwekwa ndani kwa amri ya mkuu wa wilaya akituhumiwa kuuza nguo za watoto akiwa kazini.
Tukio lingine ni la Machi 8,2018 lililotokea katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambako muuguzi Hilda Ebunka alipigwa na diwani akiwa kazini.
Katika tamko lililotolewa leo Jumapili Machi 11,2018 na Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Lena Mfalila limeeleza vitendo hivyo ni udhalilishaji na ni kinyume cha miongozo ya kisheria inayosimamia ushughulikiaji wa tuhuma za uvunjifu wa nidhamu na sheria wakati wa kazi.
"Kumpiga mtumishi wakati akiwa kazini ni udhalilishaji na ni kinyume cha sheria. Nidhamu ya wauguzi na wakunga inasimamiwa na sheria inayotoa mamlaka ya kuchukua hatua za kinidhamu kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania," amesema Mfalila.
Viongozi wa kitaifa, wakiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tamisemi, Selemani Jafo; na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa nyakati tofauti wamekemea matukio hayo.
"Kwa tamko hili baraza linalaani vitendo vilivyofanywa na viongozi husika na linatoa pole kwa wauguzi waliopatwa na kadhia hii," amesema Mfalila.

Maandamano mtandaoni yamwibua Cheyo


Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo amesema mabaraza ya vyama vya siasa yakitumika kikamilifu yanaweza kuondoa malalamiko ya wananchi na viongozi wa upinzani.
Amesema hayo leo Machi 11,2018 akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu vuguvugu la maandamano yaliyopangwa kufanyika Aprili 26,2018 yanayoratibiwa kupitia mitandao ya kijamii.
Cheyo amesema maandamano hayo ni uchochezi na uvunjifu wa amani na kwamba, mambo yanayolalamikiwa yangeweza kutatuliwa kupitia mabaraza hayo.
"Tusitake kufika hatua ya kuandamana barabarani ili kudai haki, Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi. Tukifikia huko amani iliyopo Tanzania tutashindwa kuipata tena na wananchi watakosa nchi nyingine yenye amani ya kukimbilia," amesema.
Cheyo amesema kama tatizo ni fedha kwa ajili ya mabaraza hayo kukutana, Rais John Magufuli anapaswa kutoa fedha kuyawezesha kufanya vikao.
"Siungi mkono hoja za kudai kuwepo mikutano ya hadhara hata kama ni kwa ajili ya kuongeza wanachama kama wanavyodai wengine, naamini kwa sasa mitando ya kijamii ina nguvu kuliko kitu chochote nchini," amesema Cheyo.
Amesema kabla ya kudai haki ya kuandamana, zipo nyingine wananchi wapaswa kuzipa kipaumbele zikiwemo haki ya kuishi, kupata maji safi na salama, elimu na afya.
"Hatuwezi kufika mahali tuseme nchi hii imepotea na hakuna demokrasia kisa tumekosa haki ya kuandamana, haki ya kufanya mikutano ya hadhara. Kila mtu alishuhudia mikutano ya kampeni za uchaguzi wa ubunge wa marudio katika majimbo ya Kinondoni na Siha ilivyogeuka sehemu ya kutukanana," amesema Cheyo.
"Kama kitu mnachokidai kiliweza kusababisha watu kugombana na askari hadi mauaji yakatokea hicho kitu hakitusaidii kama nchi," amesema.
Cheyo amesema yanayodaiwa kwa nguvu hayana faida na manufaa ya kila siku kwa sababu watu wanahitaji kupata wakati wa kulima na kuvuna.
"Hiyo mikutano iliyoshupaliwa sasa na kuhitajika kwa nguvu zote si kweli kwamba kila siku watakuwa barabarani kuhutubia wananchi, fedha tutatafuta saa ngapi, tutalima saa ngapi, hivyo ni vyema tutambue kila kitu kinachofanyika kupitia mambo ya siasa kisiwe kisingizio cha kusema nchi haina amani, haina uhuru," amesema Cheyo.
Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuwa kiunganishi cha wananchi na viongozi wa vyama vya siasa na si kufanya kinyume cha hilo.

Hatua 10 zitakazokuwezesha kupandishwa cheo kazini


Uaminifu ni kitu kizuri na cha maana kinachowashinda wengi wetu. Wakati wowote unapopata nafasi ya kuongea na bosi wako, kuwa mkweli katika kila neno litokalo kinywani mwako, liwe dogo au kubwa, liwe kuhusu wewe mwenyewe au kuhusu mtu mwingine, kuwa mkweli hata katika yale yanayoonekana kukuathiri wewe, amua kuwa mkweli bila kujali mazingira. Kuwa mkweli katika yale unayoyatamani na katika maswala mazima ya maendeleo ya kazi yako, sio tu unazungumza kile unachofikiri bosi wako angetamani ukiseme. Staili za kuongea zaweza kutofautiana mtu na mtu lakini ujumbe ubaki kuwa wa kweli.
Penda mazingira masafi
Wakati wowote penda kuyaweka mazingira yako ya kazi safi, hatakama ofisi sio ya kuvutia sana lakini bado unaweza kuvipanga vitu katika meza yako au pale unapofanyia kazi vikawa vema na vyenye mpangilio mzuri. Wengine wamekuwa wakijidanganya kuwa kama wakipoteza muda wao kufanyia usafi eneo lao la kazi basi mabosi wao wataona kuwa hawana kazi za kutosha za kufanya, hii ni kinyume kwa maana hali yako ya ndani ya kiutendaji yaweza kuonekana pale tunapotazama mazingira ya wewe unapofanyia kazi.
Fanya kazi saa sahihi
Mara nyingi wengi wetu tumejidanganya kuwa kwa kufanya kazi masaa mengi sana, kutoka usiku makazini na kuwahi kufika mapema sana asubuhi ndio tunaandaa mazingira ya kupanda vyeo, bado kuwaza hivi ni kosa. Ukiendelea hivi kwa muda wanaokuzunguka pamoja na bosi wako wanapata ujumbe kuwa unahangaika sana na majukumu yako yanayoonekana kukushinda na hivyo itakuwia ngumu sana kukabidhi kazi katika wakati muafaka.
Jitahidi kufanya majukumu ya zaidi
Kama unadhani unahitaji kufanya majukumu ya zaidi ili upate changamoto za ziada basi inakubidi ukubali kujitolea kutoa msaada katika baadhi ya majukumu ya wengine pale inapobidi. Waweza kuzungumza na bosi wako kuhusu hili pia, jitahidi kuwa halisi zaidi katika matazamio yako na usiweke malengo yaliyo juu ya uwezo wako ka unajua hutoweza kuyatimiza.
Mara uchukuapo jukumu fulani ili kulifanya basi jitahidi kuonyesha kuwa unalifurahia na wala haulijutii, fanya kila ulilosema kuwa utalifanya, na kwa hivyo utaonyesha heshima kubwa na kujionyesha mtu unayeweza kutegemewa. Ni muhimu sana kuwa na tabia hizi kwa maendeleo binafsi.
Uliza maswali
Kukaa kimya tu huku umeinamisha kichwa chini pasipo kusema kitu hakutakusaidia chochote katika kupanda cheo, Usihofu kuuliza swali lolote na kama una kitu au wazo juu ya jinsi gani hali fulani inaweza kuboreshwa basi iseme kwa wahusika. Yawezekana ukajiona kama unayepitiliza mipaka yako ya kazi, na yamkini wengine wasikuelewe, lakini usihofu maana taratibu itawaonyesha kuwa unaipenda kazi na uko tayari katika kuboresha biashara au mafanikio ya ofisi kwa ujumla.
Fanya utafiti
Kama unakiu ya kupanda ngazi katika masuala ya kikazi na ajira basi lazima ufanye tafiti, kama kuna kazi maalumu unataka kuiomba hakikisha unajua kilakitu kuhusu kazi hiyo na uweze kuelezea jinsi gani ujuzi wako unaendana na ule unaohitajika katika kazi husika.
Onyesha mafanikio yako kwa undani iwezekanavyo lakini pasipo kujikweza au kujisifia, mfano; kama umefanikiwa kuvuka malengo ya mauzo yako kwa kipindi fulani, basi acha mabosi wako walijue hilo.
Jifunze kutengeneza nafasi mpya
Kama unafikiri kuna njia rahisi zaidi au za mafanikio zaidi katika utendaji wako wa kazi au kama unaona umuhimu wa kuwepo kwa nafasi nyingine ya kazi ni bora uzungumze na bosi wako. Kwa sababu wewe ndiyo uliyeona umuhimu wa nafasi hiyo na kulitolea wazo, kuna uwezekano mkubwa kwamba wewe ndiyo utakayeonekana kufaa kuchukua nafasi hiyo, hii inamaanisha kwamba utakuwa tayari kubeba majukumu mapya.
Ongeza ujuzi wako
Kama unaona kuna umuhimu wa kuongezea kidogo ujuzi ulionao basi tafuta kozi zinazoendana na kile unachotaka kukifanya, jitahidi kuhudhuria semina, warsha na makongamano mbalimbali ya mlengo wa kazi yako, penda kujua zaidi ya vile wenzako wanavyovijua. Waweza kuwauliza waajiri wako kama kuna fungu kwa ajili ya kujiendeleza ili ulifaidi, onyesha kuwa una kiu ya kujiongezea ujuzi kwa manufaa ya kampuni au ofisi, hii itawafurahisha wakuu wako na kupanua wigo wa kukufikiria kwa majukumu makubwa zaidi

‘Madiwani waliojiuzulu Chadema walitokana na mafuriko ya 2015’


Madiwani wa Chadema mkoani Arusha waliojiuzulu na kujiunga na CCM wamefikia 21 baada ya leo Machi 11,2018 Elirehema Nnko wa Kata ya Osunyai kujiuzulu akiunga mkono jitihada za Rais John Magufuli.
Nnko ambaye ni wa tano kujiuzuru katika Halmashauri ya Jiji la Arusha amesema amefikia uamuzi huo katika kumuunga mkono Rais kwa kuwa hakuna kazi anayofanya sasa katika kambi ya upinzani.
Amesema alipokuwa Chadema alikosa ushirikiano katika kutimiza majukumu yake kutoka kwa viongozi wa chama hicho.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia amekiri kupokea barua ya kujiuzulu Nnko na kwamba utaratibu wa kupeleka taarifa Tamisemi umeanza.
Amesema Nnko katika barua hiyo ameeleza hajashawishiwa kujiuzulu bali anaunga mkono utendaji kazi mzuri wa Rais Magufuli.
Katika Halmashauri ya Jiji la Arusha madiwani waliojizulu ni watano; Monduli (mmoja); Longido (watatu); Meru (sita); na Ngorongoro (sita).
Akizungumzia kujiuzulu kwa madiwani, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amesema hakutakiua chama hicho.
Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro amesema madiwani waliojiuzuru walitokana na mafuriko ya mwaka 2015 na walikuwa hawajui joto la kuwa kiongozi wa upinzani.
"Waache waondoke jiji tulikuwa madiwani 33 wa Chadema sasa wameondoka watano haitupi shida," amesema Lazaro.

Mita ya maji yaibua kizaazaa 21st Century

Mkurugenzi na meneja uzalishaji wa kiwanda cha nguo cha 21st Century wanashikiliwa polisi baada ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso kufanya ziara kiwandani hapo na kubaini mita ya maji hung'olewa usiku na kurejeshwa asubuhi.
Naibu waziri amefanya ziara kiwandani hapo leo Jumapili Machi 11,2018 akisema aligundua hilo baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
Aweso akiwa kiwandani hapo alikuta mita ikiwa imeng'olewa huku maji yakiendelea kutumika kiwandani.
Meneja uzalishaji, Clement Munisi amesema hakuwa na taarifa za kuchomolewa mita akimtaja mfanyakazi kiwandani hapo Samwel kuwa ndiye msimamizi wa kitengo cha huduma ya maji.
Alipopigiwa simu mfanyakazi huyo alisema yuko kanisani na hawezi kutoka.
Naibu waziri, Aweso amemwagiza mwanasheria wa mamlaka ya maji Morogoro (Moruwasa), Tumaini Kimaro kufanya utaratibu wa kisheria ili viongozi wa kiwanda hicho wafikishwe mahakamani.
Mkuu wa kitengo cha udhibiti upotevu wa maji cha Moruwasa, Bertam Minde alisema kiasi kilichoibwa kingesaidia maeneo mengine kupata huduma.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupunguziwa mzigo


Serikali imeifanyia mabadiliko ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuanzisha nyingine mbili mpya ikilenga kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi na kupunguza mzigo kwa Mwanasheria Mkuu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ofisi mpya zilizoanzishwa ni ya Taifa ya Mashitaka na ya Wakili Mkuu ambazo hazikuwepo awali.
Amesema hayo leo Jumapili Machi 11,2018 kupitia taarifa iliyotolewa na wizara akiwa katika kikao kilichowakutanisha watendaji wa wizara na taasisi zinazounda sekta ya sheria mjini Dodoma. Kikao hicho kilijadili na kuandaa makadirio ya bajeti ya wizara na taasisi zake.
Profesa Kabudi amesema kuundwa kwa ofisi hizo kutamfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kubaki na jukumu la msingi la kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria, kufanyia uhakiki mikataba ya kitaifa na kimataifa na kuratibu wanasheria wote walioko katika wizara, idara za Serikali na zinazojitegemea, wakala, mamlaka, mashirika ya umma na Serikali za Mitaa.
“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka sasa itajikita katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai katika Mahakama ikiwa na wanasheria wake, wakati Ofisi ya Wakili Mkuu kupitia wanasheria wake yenyewe itajikita katika uendeshaji wa mashtaka ya madai ya kitaifa na kimataifa, mikataba na utatuzi wa migogoro,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema watumishi wa umma ambao ni wanasheria wanapaswa kuwa tayari na kujipanga kutokana na mabadiliko hayo ambayo yatasababisha uhamisho kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kutekeleza kwa vitendo yale yote yanayotarajiwa kupatikana.
“Serikali imefikia uamuzi huo ili kufanikisha azma ya kuwaweka pamoja wanasheria wote na kuwaratibu ili kujua nani yuko wapi na anafanya nini,” amesema.
Amesema wakuu wa idara na vitengo vya sheria katika mashirika makubwa ya umma na ambayo Serikali imetoa mabilioni ya fedha zake ili kuyaendesha watakuwa chini ya mwanasheria mkuu na endapo hatakamilisha lengo la kuwepo ofisini hapo atapelekwa mtu mwingine atakayeweza kuisaidia Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi amesema watendaji wa ndani ya sekta ya sheria wanatakiwa kufanya kazi kama timu moja ili  kurejesha imani ya wananchi kwa wataalamu wa sekta hiyo.
“Niwaombe wanasheria wenzangu tuwe timu moja na tufanye kazi zetu kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha maendeleo ya kweli ya nchi yanafikiwa na ule mwelekeo tulioonekana kuupoteza awali kama sekta tuurejeshe kwa kuyachukulia maboresho haya ya miundo ya ofisi zetu kama chachu ya kuleta tija na ufanisi katika kazi zetu,” amesema Dk Kilangi.

Kubenea kudai Tume huru ya uchaguzi bungeni

Mbunge wa jimbo la Ubungo (Chadema), Saed
Mbunge wa jimbo la Ubungo (Chadema), Saed Kubenea akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Mbunge wa jimbo la Bukoba Mjini wa chama hicho, Wilfred Lwakatare. Picha na Ericky Boniphace 
Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea amesema amepeleka bungeni barua ya kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya kuwa na chombo huru cha kusimamia uchaguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Machi 11,2018 Kubenea amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) si chombo huru cha kusimamia uchaguzi.
Amesema barua hiyo aliiwasilisha Alhamisi Machi 8,2018 katika ofisi ya Katibu wa Bunge mjini Dodoma.
Kubenea amesema uchaguzi kusimamiwa na Tume isiyo huru inaweza kusababisha machafuko.
"Hatuwezi kuacha hali hii iendelee, vurugu zimekuwa zikitokea kwa sababu ya kuwa na Tume ya aina hii, tunataka chombo huru," amesema.
Amesema tangu nchi iingie katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 uchaguzi umekuwa ukifanyika kwa kusimamiwa na Tume isiyo huru.

Magufuli atoa neno ajira za wazawa


Rais John Magufuli amemwagiza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage kuhakikisha wamiliki wa viwanda vya ndani wanaajiri wazawa.
Ametoa agizo hilo leo Jumapili Machi 11,2018 akizindua kiwanda cha kufua vyuma cha Kahama Oil Mill mjini Kahama mkoani Shinyanga.
Rais amesema wananchi wazawa ndio waliompigia kura, hivyo wapewe kipaumbele cha ajira katika viwanda hivyo.
“Kama wewe ni waziri nimekuteua mimi, unaacha kuwaajiri wazawa walionipigia kura unaenda kuchukua watu wa nje hii hakubaliki,” amesema.
Rais Magufuli amesema, “Nitoe wito kwa mawaziri wangu na wakurugenzi, hakikisheni viwanda mnavyovianzisha nchini mnaajiri Watanzania, hawa ndio walionipigia kura.”
Amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatumia malighafi za ndani kutengeneza bidhaa badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
“Mwaka huu pamba nyingi imelimwa, Kahama Oil Mill pia mnatengeneza mafuta, hakuna haja ya kuagiza pamba kutoka nje wakati tuna pamba ya kutosha hapa,” amesema.
Kuhusu kiwanda cha chuma amesema malighafi inapatikana nchini, hivyo iwapo mkurugenzi wa Kahama Oil Mill anahitaji yupo tayari kumpa bure badala ya kuagiza nje.
Pia, amewataka Watanzania kununua bidhaa za ndani, huku akiwataka wamiliki wa viwanda kutengeneza zenye ubora ili kuhimili ushindani.

Mchungaji KKKT ataja mambo sita akisema yanaitafuna nchi

Mkuu wa pili wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Kilimanjaro Kati, Mchungaji, Fred Njama amesema kuna mambo sita nchini ambayo hayako sawa.
Alitaja mambo hayo kuwa ni pamoja na hali ya uchumi, ajira kwa vijana, ughali wa matibabu na tangazo la elimu bure.
Mchungaji Njama ambaye pia ni mchungaji kiongozi wa Usharika wa Karanga mjini Moshi, alitaja mambo mengine kuwa ni hali ya kisiasa nchini na kundi kubwa la wastaafu kutolipwa mafao yao. Alitoa kauli hiyo jana wakati akiwasilisha taarifa yake katika mkutano mkuu wa 21 wa usharika huo wa Karanga, uliohudhuriwa pia na Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Martin Shao.
Mkutano huo mbali na kuhudhuriwa na mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati, Mchungaji Kennedy Kisanga na wachungaji wa sharika jirani, ulihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka jumuiya 32.
Kauli ya Mchungaji Njama imekuja siku chache baada ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) kuitaka Serikali ifufue mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya uliokwama.
Naibu Katibu Mkuu wa TEC, Padri Daniel Dulle alisema majadiliano yanahitajika ili kudumisha amani, heshima na kujenga taifa linaloheshimiana.
Hali ya uchumi
Akizungumzia hali ya uchumi nchini, Mchungaji Njama alisema awamu ya tano ilipoanza, watu walikuwa na mategemeo makubwa kwamba uchumi utaimarika lakini mambo yamekuwa tofauti.
“Umaskini unaendelea kuongezeka kwa nguvu. Tumeshuhudia biashara nyingi zikifungwa, wakulima wamekata tamaa, gharama za uzalishaji zimekuwa kubwa sana,” alisema Mchungaji Njama na kuongeza:
“Serikali haitoi ruzuku ila wakati wa kuuza mazao yao, wakulima hawajui wauze wapi na kwa bei gani. Wafugaji wanazalisha kwa gharama kubwa. Vyakula vya mifugo na dawa ni ghali.”
Hali ya kisiasa
Katika hotuba yake hiyo, Mchungaji Njama alisema kuna dalili za kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari na siasa.
“Inavyoelekea uhuru umeanza kuminywa. Ulianza kwenye siasa, ukaja kwenye vyombo vya habari... Kwa mfano takwimu za uchumi au chochote hata kama kina ukweli lakini utawala hautaki kusikia ukizungumzia hadharani au kwenye daladala ni kosa la jinai. Matukio ya miili kuokotwa yamezidi,matumizi ya risasi yameanza kuzoeleka kama kitu cha kawaida. Watu kupigwa risasi kwa walio wanasiasa na wasio wanasiasa yanafanya watu waishi kwa hofu.”
Baadhi ya matukio ya watu kupigwa risasi, ni pamoja na lile la Septemba mwaka jana, la Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyeshambuliwa akiwa nje ya nyumba yake mjini Dodoma.
Kadhalika, tukio la hivi karibuni la mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini wakati wa maandamano.
“Hali hii ikiachwa, nchi itaingia kwenye umwagaji damu mkubwa,” alitahadharisha na kuungwa mkono na baadhi ya waumini.
Ukosefu ajira kwa vijana
Akizungumzia hali ya ajira nchini, Mchungaji Njama alisema miaka ya nyuma vijana walijua kwamba wakisoma watapata ajira, lakini leo imekuwa ni kinyume chake na karibu kila nyumba ina kilio.
“Karibu kila nyumba ina kijana aliyemaliza chuo kikuu au vyuo vya kati. Kundi la wasio na kazi limeongezeka maradufu na hii si dalili njema,” alisema.
Gharama za matibabu
Kwa upande wa matibabu, Mchungaji Njama alidai matibabu yamekuwa ghali akitolea mfano wa upasuaji wa kawaida kufikia Sh500,000 mbali na vipimo vya CT-Scan na MRI ambavyo ghamara yake pia kubwa.
“Watu wanashindwa kumudu gharama za matibabu. Bima za wasio na ajira za Serikali zinabagua matibabu na dawa. Wazee ambao wanapaswa kutibiwa bure imekuwa ni nadharia,” alidai.
Elimu bure
Mchungaji Njama alidai kuwa tangazo la elimu bure limeleta kushuka kwa elimu kuliko wakati wowote na kutolea mfano kuwa kati ya shule 100 zinazofanya vizuri, za Serikali ni chache.
“Ninashauri wajumbe wa mkutano mkuu tuwaelimishe wazazi wasicheze na maneno ya wanasiasa. Kuna msemo unaosema gharama ya ujinga ni kubwa kuliko gharama ya elimu,” alisema.
Katika hatua nyingine, Askofu mstaafu Dk Shao, alilitaka kanisa hilo lisikae kimya na lichukue hatua ya kuzuia mafundisho potofu ndani ya kanisa, yanayotolewa na baadhi ya wachungaji.
Dk Shao alisema upungufu wa mafundisho ya kidini ni mkubwa na kuwataka wachungaji wa sharika za kanisa hilo, kutoruhusu kualika wahubiri wanaotoa mafundisho potofu kwa waumini.

Mawasiliano yamewaponza RC Mnyeti na Dk Kigwangalla


Wachambuzi wa duru za kisiasa na kijamii nchini wamesema tatizo la mawasiliano ndiyo sababu ya wateule wawili wa Rais John Magufuli; Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla kuonyesha tofauti zao hadharani.
Machi 8, Mnyeti alitengua agizo la Waziri Kigwangalla aliyewapa miezi tisa wananchi wa Kijiji cha Kimotorok kuondoka katika maeneo wanayoishi wakidaiwa kuvamia eneo la Hifadhi ya Tarangire wilayani Simanjiro.
Akizungumza na wanakijiji hao, Mnyeti alisema hakuna atakayekwenda kuwafukuza na kama hilo lipo, yeye ndiye atawaambia wanafukuzwa au la, hivyo wawe na amani.
Mnyeti alitoa kauli hiyo baada ya kusimamishwa na wanakijiji hao alipopita kijijini hapo akielekea katika mkutano wa kuwapokea wanachama zaidi ya 3,000 wa CCM kutoka vyama vingine.
Alisema ofisi ya mkoa inajiandaa kutuma wataalamu kwenda kupima eneo hilo ili kutatua mgogoro.
Februari 25, Waziri Kigwangalla alitoa miezi hiyo kwa wanakijiji na vitongoji vya Massas na Loon’benek wawe wamehama kwa kuwa wamevamia eneo la Hifadhi ya Tarangire.
Katika agizo lake, Dk Kigwangalla alisema kabla ya kuondoka, Serikali itawalipa fidia na watatafutiwa maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kujengewa zahanati nje ya hifadhi kutokana na iliyokuwapo kuwa ndani.
Akizungumzia tofauti hizo zilizojitokeza baina ya viongozi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema tatizo hilo linachangiwa pia na upungufu wa kiuongozi.
Alisema pengine Waziri Kigwangalla alikosea katika mawasiliano lakini RC Mnyeti hakutakiwa kutumia vyombo vya habari katika kutengua kauli yake.
“Busara ya kiongozi inaelekeza kwamba RC alitakiwa awasiliane naye (Dk Kigwangalla) kiofisi, amweleze hatua zinazoendelea na sehemu gani aliyotakiwa kuzingatia kabla ya kutoa tamko lake.
“Halafu waziri pengine angetumia busara kurejea upya kauli yake kwa sababu wote wanatekeleza mipango ya Serikali,” alisema Dk Bisimba.
Profesa wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana alisema tofauti hiyo imechagizwa na ukosefu wa mawasiliano baina ya viongozi hao.
Profesa Bana alisema RC ni ‘rais wa mkoa’ hivyo kwa waziri yeyote anayehitaji kufanya uamuzi ni busara kufanya mazungumzo na RC husika kabla ya kutoa tamko.
“Haiwezekani waziri uingie mkoa fulani na kutoa maamuzi, lazima maelekezo ya waziri yawe yameshapata baraka kutoka kwa mkuu wa mkoa wa eneo husika. Ningeshauri wajenge tabia ya mashauriano ili kuepuka dosari kama hizo. Kwa utaratibu lazima upate ‘briefing’ (maelezo) ya hali halisi na mipango inayoendelea kuhusu jambo husika unalofuatilia,” alisema.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala bora UDSM, Dk Richard Mbunda alisema pamoja na tatizo la mawasiliano, viongozi hao walihitaji semina elekezi kabla ya kuanza kutumikia nafasi zao.
“Nafasi wanazotumikia kwa sasa ni kubwa, hawakuwahi kuzitumikia tangu waingie kwenye siasa, kwa hiyo inawezekana hawajui athari katika kauli wanazotoa. Semina ingesaidia kujua do’s and dont (mambo ya kufanya na kuacha), kujua direction (mwelekeo) ya rais mwenyewe anataka nini,” alisema.
Alisema kwa madaraka aliyonayo, waziri ana nguvu nchi nzima katika maeneo yanayohusu sekta yake na hufanya uamuzi kupitia vikao vya mawaziri hivyo haikuwa busara kwa mkuu wa mkoa kutengua kauli yake hadharani.
Alisema inatia shaka kwa viongozi kuonyesha wazi tofauti zao na kwamba athari zake itakuwa ni pamoja na kupunguza imani kwa viongozi wa Serikali.
Mkurugenzi wa shirika la Sikika, Irenei Kiria alisema mawasiliano ni tatizo ambalo limewahi kujitokeza si kwa viongozi hao tu, bali hata kwa Rais kutengua uamuzi uliopitishwa na waziri.
Rais Magufuli aliwahi kutengua tamko la Dk Harrison Mwakyembe wakati huo akiwa Waziri wa Katiba na Sheria, baada ya kupiga marufuku wananchi kufunga ndoa bila kuwa na cheti cha kuzaliwa.
“Kwa hiyo tatizo ni mawasiliano, rais ameshafanya hivyo, ni kawaida na inatokea kuwa na mawazo tofauti. Jambo la msingi ni mawasiliano,” alisema Kiria.

Supermarket zatii katazo la nyama kutoka Afrika Kusini


Idadi kubwa ya maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets) yametii agizo la Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania, (TFDA) la kuzuia uingizaji nyama kutokana Afrika Kusini.
Hatua hiyo imekuja baada ya soseji, zinazotengenezwa huko aina ya Polony kubainika kuwa na ugonjwa wa listeriosis uliosababisha vifo vya watu 180 nchini humo.
Soseji hizo, zinatengenezwa na kiwanda cha Tiger Brands Unit Enterprises na cha RCL Foods vya Afrika Kusini.
Katika taarifa yake Machi 7, TFDA ilisema usitishaji utaendelea hadi hapo itakapothibitishwa kuwa bidhaa hizo ni salama.
Baada ya taarifa hiyo, mwandishi wetu alitembelea maduka makubwa ya vyakula ya Shrijees lililopo Masaki, Mkuki House (Keko Darajani), Imalaseko (Posta) na Food Lovers la Oysterbay na kote huko bidhaa za nyama kutoka Afrika Kusini hazikuwapo.
Pia alibaini kuwa nyama za kusaga na soseji kutoka nje ya nchi zipo kwa kiasi kidogo na nyingi zinatoka Kenya.
Msemaji wa TFDA, Gaudencia Simwanza alisema bado wanaendelea na uchunguzi kubaini kama bado kuna maduka yanayouza soseji na nyama za kusaga kutoka nchini humo.
Hata hivyo alisema, “Sisi tulitaja kampuni yenye vyakula vyenye hilo tatizo, hivyo wananchi walizingatie hilo pia. Tunaendelea na kazi ya ukaguzi ndani na mipakani kuona kama bidhaa hizo bado zinaingizwa nchini, tutakachokibaini tutawafahamisha.”
Mmoja wa wateja aliyekutwa akinunua bidhaa katika duka la Food Lovers, Mwahija Haji alisema tangazo la uwepo wa nyama kutoka Afrika Kusini zenye bakteria limewaamsha na kuwa makini wanapokuwa madukani.
“Nasoma kabla sijanunua na kujiridhisha, hata ikiwa ya Afrika Kusini naangalia jina la kampuni ili nisinunue kutoka katika kampuni iliyotajwa” alisema Mwahija.
Alisema kuwa ili kuepuka usumbufu huo, ananunua zinazozalishwa hapa nchini ingawa alidai kuwa baadhi hazina ubora.
Mlipuko wa listeriosis ulianza Desemba mwaka jana na mpaka sasa umesababisha vifo vya watu 180 huko Afrika Kusini.
Akiuchambua ugonjwa wa listeriosis, Dk George Kanani wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza alisema ni aina ya bakteria ambao hupatikana kwenye maji, ubongo na kinyesi.
Alisema binadamu huambukizwa pale wanapotumia vyakula au maji yenye bakteria hao.
“Sababu kuu zinazosababisha listeriasis ni nyama na maziwa mabichi,” alisema.
Dk Kanani alisema bakteria hao ni hatari na huweza kusababisha kifo pale wanaposhambulia mfumo wa fahamu na wa damu.

Fanya hivi kujenga mahusiano bora na mfanyakazi wa nyumbani


Tunakubaliana kuwa wafanyakazi wa nyumbani ni mhimili mkubwa majumbani hasa kwa wengi wetu tulioajiriwa kwenye sekta ama za umma au binafsi – hata wale waliojiajiri. Ipo wazi kwamba tunatambua umuhimu wa wasaidizi hawa katika kutekeleza majukumu ya nyumbani pindi tunapoondoka kwenda kazini na hata tuwapo majumbani. Tatizo lipo kwenye mahusiano yetu na hawa wasaidizi wetu majumbani.
Uzoefu unaonyesha kuwa wafanyakazi wa nyumbani hawadumu katika ajira zao. Leo yupo, kesho hataki tena kazi, anataka kurudi kwao. Wengine hawatulii ndani ya nyumba kutwa kuzurura mtaa hadi mtaa huku kazi na huduma kwa watoto zikilegalega. Vitendo vya namna hii huwaweka waajiri wao katika hali ya taharuki pasi na hakika ya huduma zinazotolewa na wafanyakazi wa namna hii.
Tambua kama waajiri ni muhimu sana kutambua kuwa wafanyakazi wa nyumbani hutofautiana, kila mtu huvaa uhusika tofauti na sifa ambazo huathiri utendaji wao wa kazi. Kujenga mahusiano mazuri na mfanyakazi wa nyumbani kuna faida kubwa kwani kufanya hivyo ni kumuongezea ufanisi katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
Tafiti zinaonyesha kwamba kukosekana kwa mahusiano mazuri kati mwajiri na mfanyakazi ni chanzo cha wasiwasi na migogoro inayojitokeza makazini mwetu. Vivyo hivyo hata majumbani mwetu sisi kama waajiri tunahitaji kuhuisha mahusiano ili mazingira ya kazi yawe rafiki.
Mlipe mshahara mzuri. Mshahara mzuri ni kichocheo katika kufanya kazi kwa bidii na weledi. Hatuna budi kutambua kwamba wafanyakazi wa nyumbani hutegemea mishahara tunayowalipa kwa ajiri ya kujikimu. Aidha hutumia pesa hizo kwa kusaidia familia zao kwani wengi wao hutokea kwenye familia duni na zisizojiweza. Tatizo linakuja pale tunapowapangia kazi lukuki huku tukiwalipa mishahara isiyolingana na majukumu wanayoyatekeleza. hapa ndipo mgongano unapoibukia.
Mawasiliano mazuri. Lugha ya staha na busara itumike wakati wa kuzungumza na mfanyakazi wako wa nyumbani na hasa wakati wa kutoa maagizo. Ugomvi na kumkaripia siyo njia bora za kutumia wakati wa kuwasiliana naye kwani kutaleta uhasama kadiri siku zinavyozidi kwenda. Hakikisha unampa maelekezo sahihi ambayo hayataweza kumchanganya na endapo utakugundua kuwa anafanya kosa kwenye jambo fulani, basi msahihishe katika njia ambazo hazitaonyesha kumdharau.
Usimbague. Onyesha unauthamini mchango wake kwa kumfanya sehemu ya familia hasa unapopata wasaa wa kununua vijizawadi nyumbani usimsahau walau mara moja moja.
Upo ushahidi wa kutosha wazazi tunawanunulia watoto wetu nguo nzuri ilihali mfanyakazi wa nyumbani unamletea nguo kuukuu. Kwanini umbague? Mfanye ajue kuwa unamthamini kwani itasaidia katika kujenga uhusiano bora baina yake na hata kwa watoto wako pia.
Mheshimu. Hakikisha mfanyakazi wa nyumbani haonewi pasi sababu. Watoto, ndugu na jamaa zako wampe heshima inayostahili. Asitukanwe na mtoto wako na ukakaa kimya. Asisumbuliwe na wageni wako na ukaa kimya. Huyu anakaa na watoto wako ukiwa haupo hivyo ni vyema umpe heshima. Atakulipa heshima. Mlipe dharau na madhara yake yataonekana!
Haya ni baadhi tu ya mambo unayoweza kufanya kujenga mahusiano na mfanyakazi wako wa nyumbani. Hatusemi ukimpa haya basi uhakika wa kuhusiana naye vyema upo asilimia 100. Bado unaweza ukampa kila atakacho pamoja na heshima na ukorofi atakuonyesha. Hili lisikuulie moyo wa utu wema.

Hoja ya Bashe kuhusu ‘wasiojulikana’, demokrasia iungwe mkono, iboreshwe


Oktoba mwaka jana niliandika makala yenye kichwa “Bunge linaweza kumaliza utata wa wasiojulikana”. Nilijenga hoja kuhusu nafasi ya Bunge kikatiba, mamlaka yake na kuchukua mifano ya mabunge mengine duniani, nini hufanya yanapoibuka mazingira yenye kukosa majibu yaliyonyooka kutoka kwa Serikali.
Nilichambua zaidi jinsi Bunge la Marekani mwaka 1974, lilipomlazimisha Rais wa 37 wa nchi hiyo, Richard Nixon kujiuzulu, baada ya kufanya uchunguzi na kumbaini kuwa alitumia njia batili kushinda uchaguzi wa Rais uliofanyika Novemba 7, 1972 ambao alishinda na kuwa Rais wa Marekani kwa muhula wa pili.
Timu ya kampeni ya Nixon (chama cha Republican), ilivamia ofisi za kampeni za Democratic, zilizokuwepo kwenye jengo la Watergate, Washington DC, wakatega vifaa vya kunasa mazungumzo, vilevile waliiba nyaraka ambazo ziliwezesha Republican kujua mbinu zote za mgombea wa Democratic, George McGovern.
Watu waliokamatwa wakiingia ofisi za Democratic walibainika ni makomandoo wa Cuba waliokuwepo Marekani wakipikwa na kuwekwa tayari kwa ajili ya kumpindua aliyekuwa Rais wa Cuba, Fidel Castro. Baada ya idara ya upelelezi ya FBI kuwakamata makomandoo hao, mchezo uligeuzwa.
Makomandoo wa Cuba walisema walivamia ofisi za Democratic baada ya kupata taarifa kuwa McGovern alikuwa na mawasiliano ya ukaribu na Castro. Awali ikaonekana kweli Democratic walitenda jambo haramu kwa kuruhusu Castro kuingilia uchaguzi wa Marekani.
Hata hivyo, uchunguzi wa kibunge uliwezesha kubaini umafia wote ambao ulitekelezwa na Nixon, zikiwemo nyaraka za Democratic zilizoibwa, kukutwa Ikulu. Ikabidi Congress waanze mchakato wa kumpigia Nixon kura ya kutokuwa na imani naye, ndipo Nixon akajiuzulu.
Tafsiri ya mfano
Mfano huo wa namna ambavyo kashfa ya Watergate ilivyoshughulikiwa ni jawabu kwambe Bunge linapoamua kusimamia misingi huwezesha majibu magumu kupatikana. Kulikuwa na hila nyingi zilizofanywa ili kumlinda Nixon, zilizozuia vyombo vya kiuchunguzi kutimiza wajibu wake. Kwa Congress haikuwa rahisi kuizuia.
Mafanikio ya uchunguzi wa Bunge huambatana na nchi kuwa na wabunge wanaotambua hadhi ya mhimili wenyewe. Wabunge wenye kuelewa na kuheshimu kuwa Bunge ndicho chombo kinachoweza kuiweka nchi sawa, pale Serikali inapovurunda au kunapokuwa na matukio yenye kuwaweka watu roho juu.
Ukumbi wa Bunge kwa lugha nyingine huitwa August House (Nyumba Tukufu). Kwa maana ndilo jengo lenye kubeba hisia za wananchi kwa nchi yao, maana wabunge ni wawakilishi wa watu. Wabunge hutakiwa kuutendea haki uwepo wao bungeni kwa kuweka mbele maslahi na hisia za wapigakura wao.
Nyakati ambazo watu wanapotea na haijulikani wanapelekwa wapi. Wananchi wanakuwa na maswali mengi ambayo vyombo vya usalama nchini haviyajibu. Ni hapo sasa Bunge hutakiwa kuthibitisha utukufu wake kwa kuonyesha umahiri wa kuchimba jambo husika na kukata mzizi wa fitina.
Bunge kukaa kimya kipindi ambacho nchi inakuwa kwenye hali ya wasiwasi, watu wanakutwa wamekufa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi na Mto Ruvu, tena haliwi tukio la mara moja bali matukio yanafuatana. Wakati huohuo vyombo rasmi havitoi majawabu yenye kunyooka kuhusu hali hiyo. Hiyo ni aibu kubwa kwa Bunge.
Kwa bahati mbaya Bunge la 11 la Tanzania, limekuwa likivumilia sana aibu hiyo ya kukaa kimya kwenye nyakati ambazo nchi inakuwa imezingirwa na viulizo vingi kuhusu usalama wao. Lilikaa kimya hata wakati wa mfululizo wa mauaji Kibiti. Mpaka sasa Watanzania hawajui nini kilitokea na nini kinaendelea. Je, yale mambo yamekwisha au yamepoa kwa muda?
Bunge lina mamlaka ya kikatiba ya kuisimamia Serikali. Usimamizi huo ni kwa njia ya kuisikiliza au kuihoji. Kwamba kama idara za Serikali hazioni kuwa zinawiwa kujitokeza zenyewe kwenye kamati za Bunge na kueleza kinagaubaga masuala ambayo wananchi wanataka majibu, basi Bunge halina budi kuihoji Serikali, ama kupitia kwa wakuu wa idara, mawaziri na hata Waziri Mkuu.
Zipo nyakati mambo yanaweza kuwa moto kwenye nchi. Serikali inaweza kuziba masikio au ikawa inapuuza joto husika kama vile halipo. Bunge kwa sababu lenyewe ndiyo linawakilisha sauti, matarajio na hisia za watu, hupaswa kuibana Serikali ili ama itoe majibu au ifanyie kazi suala husika. Ikibidi, Bunge linachunguza na kuiwajibisha Serikali pale inapostahili.
Bunge linaweza kuiwajibisha Serikali si kwa sababu ya kutenda au kuhusika na vitendo husika, bali linaweza kuchukua dhima hiyo hata pale ambapo Serikali haikuchukua hatua stahiki au ilichelewa kutimiza wajibu wake.
Na tafsiri ya Bunge kutoichukulia hatua Serikali au kutoibana kwa matukio yaliyo wazi kabisa, maana yake haliwajibiki ipasavyo. Linakuwa Bunge lisilo na meno.
Hoja ya Bashe
Mwanzoni mwa Februari mwaka huu, wakati mwandishi wa habari wa kujitegemea, aliyekuwa akiripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda, alipokuwa na zaidi ya miezi miwili tangu alipotoweka, niliandika makala nikieleza aibu ya Bunge, kukutana na kuahirisha mkutano bila kupata fursa ya kujadili kupotea kwa Mtanzania huyo.
Nilisema kuwa aibu hiyo ya Bunge inamgusa moja kwa moja mbunge anayewakilisha jimbo la Azory, kwani vyombo vya habari vinaripoti, gazeti la Mwananchi lilikuwa linatoa kipaumbele kwa kukumbusha kila siku kuhusu idadi ya siku zinavyoongezeka tangu alipotoweka, lakini mbunge wa jimbo analotoka mwandishi huyo hajaguswa japo robo.
Kipindi ambacho Bunge linaonekana kubeba lawama kwa sababu ya wabunge kuonekana hawajali yanayoendelea au kutotimiza wajibu wao, ni hali ambayo inaweza kuwakatisha tamaa wananchi juu ya chombo chao cha uwakilishi. Wakati huo sasa anaibuka mbunge na kuweka kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ili Bunge lijadili yote.
Mbunge huyo wa CCM anataka Bunge liunde Kamati Teule ya kuchunguza mwenendo wa matukio yote. Anataka uchunguzi huru wa kibunge juu ya tukio la kushambuliwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Septemba 7, mwaka jana, vilevile kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Saanane Novemba 2016.
Mbunge huyo, Hussein Bashe (Nzega Mjini), ambaye mwaka jana alipata kulia bungeni, akitoa ushuhuda kwamba naye aliwahi kutekwa. Anataka uchunguzi wa kibunge mpaka kuhusu tukio la kifo cha Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif, Kinondoni, Daniel John, aliyeuawa wakati wa mchakato wa uchaguzi mdogo jimbo la Kinondoni, Februari mwaka huu.
Hoja ya Bashe inahusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, aliyepigwa risasi akiwa kwenye daladala, wakati polisi wakidhibiti maandamano ya Chadema.
Bashe anataka Bunge lichunguze kuhusu polisi kutumia risasi za moto katika tukio hilo. Kimsingi Bashe anataka uchunguzi dhidi ya matukio yote yenye kukiuka misingi ya haki za binadamu na kuminywa kwa demokrasia.
Hoja iboreshwe
Kuna la kujiuliza, je, Bashe anatania? Jawabu la swali hilo lipo Aprili mwaka jana. Bashe alisimama bungeni kuomba Bunge lijadili tukio la kutekwa kwa Saanane na mwanamuziki Ibrahim Mshana ‘Roma Mkatoliki’ na wenzake watatu ambao walikuwa wametekwa wakati huo kabla ya kuachiwa baada ya siku tatu.
Kulipokuwa na hali ya kupinga watu kujadili bungeni suala hilo la utekaji watu, Bashe alisema waliokuwa wakipinga ni kwa sababu hawajawahi kuonewa wala kunyanyaswa. Alijisema yeye kuwa amewahi kutekwa. Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alikataa mjadala huo.
Hivyo, hoja ya sasa ya Bashe unaweza kutafsiri kwamba ameamua kuirudisha bungeni kivingine. Kwa maana hiyo Bashe anastahili kuungwa mkono na kupongezwa kwa kuguswa na mwenendo mbaya wa matukio yenye kuvunja haki za binadamu na demokrasia. Muhimu aboreshe hoja yake kwa kuongeza ombi la Bunge kuchunguza matukio ya madiwani na wabunge kuhama vyama. Je, wanahama kwa utashi wao au kwa ushawishi wa fedha?

Kila nchi ina wajihi, siha na tabia zake...

Kila nchi utakayoitembelea...
Kila taifa, huwa na taswira yake.
Juzi rafiki yangu alirejea toka Misri. Shughuli zake ni vichekesho (“standup comedy”) sanaa iliyo juu sana Uzunguni. Ucheshi wa kibunifu hauudhi sana watawala.
Chukua mchekeshaji maarufu wa Afrika Kusini – Trevor Noah.
Husema mengi sana katika onesho la dakika kumi tu.
Aliwahi kuelezea namna Mama yake mzazi alivyopigwa risasi. Kiherehere cha kukimbilia hospitali, na mdogo wake asiyeelewa kunanini. Utacheka hapo hapo ukigundua mengi kuhusu ughali na dhiki ya matibabu leo Afrika. Usipokuwa nazo utafariki tu.
Sasa jambo la kwanza alilosema rafiki yangu mchekeshaji ni namna Wamisri walivyo poa.
Akaonesha picha alizowapiga ngamia. Wachekeshaji sio?
Hatuwawezi.
Niliwahi kuishi Canada miaka ya Tisini; na baridi kali kule kiasi ukitema mate hugeuka barafu kabla hayajagusa ardhi! Hapo hapo Wacanada wamejenga mazingira kuhimili baridi. Magari yana minyororo ya chuma katika magurudumu, nyumba zenye vipasha joto sakafuni na mazuliani, nk.
Safari ni mwalimu
Nilipowasili mara ya kwanza Ulaya miaka ya Themanini nilishangazwa na sura za watu wasiojua kucheka ...hadharani. Kila mtu mbio mbio; hasemi na mwenzake. Vyombo vya usafiri vikishasimama tu- kila mtu, kimbilia kukitoa.
Utamaduni wa kila mtu na lwake, kutosemeshana, mbio kasi za duma. Upande mwingine hawa hawa huwa marafiki wa kweli mkijuana. Huenda wasikusemeshe njiani, lakini ukiwa na shida, kama mnafahamiana, Utamshukuru Mungu.
Marekani ya Kusini ni kinyume cha Ulaya. Joto, jua, kelele za muziki kila mahali. Kama tulivyo Waafrika (kadamnasini) uzungumzaji mkali. Humjui hakujui katika basi, mtasalimiana, mtajuliana hali, mtachapa “mastore.”
Kuna wakati nilirudi Tanzania na wageni wangu. Ilikuwa mara ya kwanza kwa mmoja wao kuwemka mguu Afrika...
Nikaulizwa :
“Mbona Watanzania wana macho mekundu sana?”
Zamani nikiwa mdogo nakumbuka tuliona fahari mtu akiwa na macho mekundu.
“Jeuri yule...usimchezee!”
Utoto huo.
Ukosefu wa maji mwilini na baadhi ya vitamin ni kati ya sababu macho kubadilika rangi. Watanzania (na Waafrika kijumla) tunapenda sana vitu vya ladha. Vyakula vyenye chumvi na pilipili nyingi. Vinywaji vyenye sukari sukari (soda) ni mifano michache. Juzi hapa London nilikaribishwa mlo wa jioni na dada mmoja wa Kiafrika. Ile salad (tango, karote na nyanya) zilinakshiwa kwa chumvi.
“Mbona chumvi katika Salad?”
“Ladha, Bw Freddy.”
“Lakini chumvi si iko katika nyama na mchuzi ?”
“Si umeona utamu kaka.”
Hapo ndipo lilipo jehanam dogo la afya zetu. Watu weusi sasa hivi (dunia nzima) wanakabiliwa sana na tatizo la figo. Wanawake wanapata mawe sehemu hizo. Wanaume athari huenda hadi uumeni (haja ndogo, tezi kibofu, urijali nk).
Kazi kuu ya figo ni kusafisha damu na tumbo. Kupiga deki mwili. Unapolijaza tumbo na vitu vyenye ladha tupu, kila siku, kila mara, unahatarisha sana afya ya figo. Ongeza sasa kama hunywi maji...(wanywa tu wakati wa kula au soda). Au hufanyi mazoezi ya viungo. Tusishangae kuona maisha yetu mafupi. Kutokunywa pombe na kusema soda, chai au kahawa hakuna maana figo zetu zinapona. Tujifunze kujipenda na kupenda uasilia. Gharama za matibabu huwa juu kuliko zile za vyakula vya afya.