Sunday, March 11

Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupunguziwa mzigo


Serikali imeifanyia mabadiliko ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuanzisha nyingine mbili mpya ikilenga kuongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi na kupunguza mzigo kwa Mwanasheria Mkuu.
Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema ofisi mpya zilizoanzishwa ni ya Taifa ya Mashitaka na ya Wakili Mkuu ambazo hazikuwepo awali.
Amesema hayo leo Jumapili Machi 11,2018 kupitia taarifa iliyotolewa na wizara akiwa katika kikao kilichowakutanisha watendaji wa wizara na taasisi zinazounda sekta ya sheria mjini Dodoma. Kikao hicho kilijadili na kuandaa makadirio ya bajeti ya wizara na taasisi zake.
Profesa Kabudi amesema kuundwa kwa ofisi hizo kutamfanya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kubaki na jukumu la msingi la kuishauri Serikali katika masuala yote ya kisheria, kufanyia uhakiki mikataba ya kitaifa na kimataifa na kuratibu wanasheria wote walioko katika wizara, idara za Serikali na zinazojitegemea, wakala, mamlaka, mashirika ya umma na Serikali za Mitaa.
“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka sasa itajikita katika uendeshaji wa mashtaka ya jinai katika Mahakama ikiwa na wanasheria wake, wakati Ofisi ya Wakili Mkuu kupitia wanasheria wake yenyewe itajikita katika uendeshaji wa mashtaka ya madai ya kitaifa na kimataifa, mikataba na utatuzi wa migogoro,” amesema Profesa Kabudi.
Amesema watumishi wa umma ambao ni wanasheria wanapaswa kuwa tayari na kujipanga kutokana na mabadiliko hayo ambayo yatasababisha uhamisho kutoka sehemu moja kwenda nyingine ili kutekeleza kwa vitendo yale yote yanayotarajiwa kupatikana.
“Serikali imefikia uamuzi huo ili kufanikisha azma ya kuwaweka pamoja wanasheria wote na kuwaratibu ili kujua nani yuko wapi na anafanya nini,” amesema.
Amesema wakuu wa idara na vitengo vya sheria katika mashirika makubwa ya umma na ambayo Serikali imetoa mabilioni ya fedha zake ili kuyaendesha watakuwa chini ya mwanasheria mkuu na endapo hatakamilisha lengo la kuwepo ofisini hapo atapelekwa mtu mwingine atakayeweza kuisaidia Serikali.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi amesema watendaji wa ndani ya sekta ya sheria wanatakiwa kufanya kazi kama timu moja ili  kurejesha imani ya wananchi kwa wataalamu wa sekta hiyo.
“Niwaombe wanasheria wenzangu tuwe timu moja na tufanye kazi zetu kwa weledi na ufanisi mkubwa ili kuhakikisha maendeleo ya kweli ya nchi yanafikiwa na ule mwelekeo tulioonekana kuupoteza awali kama sekta tuurejeshe kwa kuyachukulia maboresho haya ya miundo ya ofisi zetu kama chachu ya kuleta tija na ufanisi katika kazi zetu,” amesema Dk Kilangi.

No comments:

Post a Comment