Mchungaji Lusekelo asema kuwaza sasa ni utoto wa moyo, Sitta: urais unakuja wenyewe
Fidelis Butahe
MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo amesema mbio za urais za 2015 zitalipeleka taifa kubaya huku akisema wanaofanya harakati hizo kwa kasi hivi sasa ni sawa na watu wenye “utoto wa moyo.”Wakati mchungaji huyo akisema hayo, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema anachukizwa na tabia ya baadhi ya watu kuota urais kila siku na kuacha kuutumikia umma ambao umegubikwa na kero nyingi ikiwemo umasikini.
Kauli za Mchungaji Lusekelo na Sitta zinakuja kipindi ambacho baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakipigana vikumbo kuwania kumrithi Rais Jakaya Kikwete mwaka 2015, huku CCM kikiri kuwa mbio hizo zimekiongezea mpasuko.
Hivi karibuni sekretarieti ya CCM ilipeleka kwenye Halmashauri ya CCM (Nec), taarifa ya hali ya siasa ndani ya chama hicho ikieleza mambo matatu kuwa ndiyo yanayokisumbua. Hayo ni pamoja na mbio za urais 2015, mchakato wa kujivua gamba na kura za maoni za ubunge za mwaka jana.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika salamu zake za Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya, Mchungaji Lusekelo maarufu kama 'Mzee wa Upako' alisema umefika wakati kwa wanasiasa kutambua kuwa 2015 si mwisho wa dunia na kwamba kuna maisha baada ya mwaka huo.
“Ni heri ilivyokuwa miaka ya nyuma maana ili uwe mwanasiasa ulikuwa lazima usome… walikuwa wakisomea pale chuo cha Kigamboni, jambo hili hivi sasa halipo na kila mtu anataka kuwa mwanasiasa,” alisema Mchungaji Lusekelo.
Alisema siasa ni taaluma kama zilivyo nyingine na kitendo cha wanasiasa ambao kitaaluma si wanasiasa kulumbana katika jambo fulani wanaoumia si wao, bali ni Watanzania.
“Si vyema kwa viongozi wa kisiasa kulumbana kwani watakaoumia ni Watanzania na jambo hili lisipoangaliwa, hali inaweza kuwa mbaya zaidi mwaka 2015,” alisema.
Alisema kitendo cha viongozi mbalimbali wa Serikali kustaafu na kupewa kazi nyingine, ndicho chanzo cha kuwa na viongozi waliolewa uongozi.
“Huu ndiyo utoto wa moyo ninaousema, mtu anaacha uwaziri kisha anapelekwa kuwa kiongozi wa shirika au taasisi fulani ya Serikali, kila siku viongozi ni walewale na ndiyo mwanzo wa kuwa na viongozi walevi wa uongozi,” alisema.
Posho za wabunge
Akizungumzia posho za wabunge ambazo zimeongezwa kutoka Sh70,000 hadi 300,000, alisema tatizo si posho, bali ni mfumo mzima wa kulipana posho.
Licha ya kuitaka Serikali kutowatupa watumishi wake katika kuwalipa vizuri, Mchungaji Lusekelo alitoa angalizo kwamba kiwango kikubwa cha posho kitawafanya wasiokuwa wanasiasa nao kutaka kuwa wabunge.
“Tunaweza kuwa na bunge la watu fulani hivi waliofuata posho na si watendaji na wanasiasa makini,” alisema.
Katiba Mpya
Akizungumzia suala la mchakato wa Katiba Mpya ambao juzi Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji aliuponda kuwa ni mbovu na hautazaa katiba bora, Mchungaji Lusekelo alisema ili kufikia tamati ya uwepo kwa Katiba Mpya ni lazima Watanzania waaminiane.
“Muswada ndiyo huo umepitishwa, nadhani kinachotakiwa hivi sasa ni kuaminiana tu, Katiba Mpya ni jambo zuri na mwenye uwezo atoe maoni yake juu ya Katiba anayoitaka. Katiba iliyopo ni nzuri ila ina upungufu wake hasa katika kipengele cha madaraka makubwa aliyonayo Rais.”
Sitta: Urais unakuja wenyewe
Katika hotuba yake aliyotoa jimboni kwake Urambo Mashariki mwishoni mwa wiki, Sitta alisema urais ni jambo linalokuja lenyewe kwa watu waadilifu hivyo hakuna haja ya kuuota kila siku.
“Urais unakuja wenyewe kwa watu walio waadilifu. Nachukizwa na watu ambao wao kila siku wamekuwa na mawazo ya urais na kuacha mambo ya msingi ya kutumikia wananchi wa Tanzania,” alisema.
Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, alisema anachukizwa pia na kuhusishwa katika harakati za urais wa 2015 akisema ni mapema mno kufikiria jambo hilo sasa kwani bado kuna muda mwingi.
Alisema urais si suala la kukimbilia wala kulitafuta kwa nguvu na mbinu chafu akisema siku zote watu waadilifu wanafahamika na hakuna haja ya kutumia nguvu nyingi kutafuta madaraka hayo ya juu ya nchi.
“Haya mambo ya urais kila siku hayana maana. Kibaya zaidi watu wanahamisha mambo ya msingi na kuyapeleka katika fikra za ovyo. Hebu ufike wakati tuangalie matatizo ya wananchi kwanza tusifikirie vitu ambavyo havimsaidii mwananchi wala taifa,” alisema.