Dk John Magufuli akiwasalimia Wajumbe wa Mkutano Mkuu
katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma kabla ya kuanza kupiga kura juzi usiku.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Kwanza kabisa napenda kumpongeza sana Magufuli kwa hatua aliyofikia na kumtakia kila la heri. Naomba kukiri kwa uwazi kwamba katika uchaguzi unaohusisha vyama vya siasa ni lazima mshindi atapatikana na kwa Tanzania ni lazima mshindi huyo atoke kwenye chama cha siasa.
Tanzania ina vyama 22 vilivyosajiliwa na vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake ni lazima rais wa nchi atatoka katika chama kimojawapo, na kwa sababu CCM imeshapitisha mgombea wake na yeye ana fursa ya kushinda uchaguzi kama ambavyo fursa hiyo ilivyo kwenye vyama vingine. Natumia nafasi hii kufanya uchambuzi wa dhati juu ya taswira ya serikali ya Magufuli ikiwa atafanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Taswira ya namna hii pia nitaifanya kwa wagombea wengine wa vyama ambavyo vitaamua kuweka wagombea urais.
Katika kulifanya jukumu hili nitachambua masuala 10 ambayo nafikiri kwamba yanaweza kujenga utawala wa Magufuli, ikiwa atachaguliwa na Watanzania kuwa rais wa awamu ijayo.
Mambo matano kati ya hayo nayatazama kama taswira bora na mengine matano yanaweza kuwa taswira hasi. Katika uchambuzi wa leo nitaanza na mambo matano ambayo ni taswira bora.
Usimamizi bora
Taswira ya kwanza ambayo Magufuli anaweza kuirejesha bila wasiwasi ni usimamizi thabiti wa serikali na nidhamu ya utendaji ndani ya serikali. Naamini kuwa serikali ya Magufuli itakuwa ya kiusimamizi na yeye mwenyewe anaweza kulifanya jambo hilo bila kusita. Katika nyadhifa nyingi alizopitia hadi sasa ameijenga taswira hii kila alikopita na bado inambeba hata ikitokea anachaguliwa kuwa rais wa awamu ya tano.
Tukumbuke kuwa moja ya mambo ambayo yameanguka kabisa nchini hivi ni utendaji ndani ya serikali. Tunafahamu kuwa wafanyakazi ndani ya serikali ukiachilia mbali matatizo waliyonayo kwa maana ya vipato, hata mambo madogo ambayo wangeweza kuyasimamia ndani ya dakika au saa chache huchukua wiki kadhaa na hata miezi kadhaa. Utaratibu wa utoaji huduma umekwama sana na nadhani kama akiwa na uwezo huo atafanikiwa kutatua changamoto kubwa na ya siku nyingi. Ikiwa utendaji wa serikali unaimarika na huduma zinatolewa kwa wakati, tutaweza kujenga taifa linalokwenda mbele bila kujali chama gani kiko madarakani.
Msimamo imara
Taswira bora ya pili ya serikali ya Magufuli inaweza kuwa ni misimamo katika masuala ya msingi na kutoyumba sana. Magufuli muda wote ambao amekuwa kiongozi ameonyesha jambo hilo. Kila mara amekuwa na misimamo hata kama siyo sahihi. Kwa tafsiri nyingine hii huwa ni njia bora ya uongozi wa nchi japokuwa misimamo ya serikali au kiongozi mkuu wa serikali huwa haipaswi kuwa juu ya haki na matakwa ya wananchi.
Moja ya mambo ambayo serikali iliyopita ilikosa, ni pamoja na kukosa misimamo na kuwa na “double standard”. Mfano mdogo tu ni kwenye mchakato wa katiba mpya ambapo Rais anayeondoka alisimamia uanzishwaji bora wa mchakato huo, akaunga mkono katika hatua zote na rasimu zote, lakini akaja kuwageuka wajumbe wa tume hiyo na rasimu yao ya pili alipolihutubia Bunge Maalumu la Katiba. Naamini Magufuli si mtu wa kugeuka na kuna masuala mengi anaweza kuyasimamia kwa dhati na kila mmoja wetu akakubali kuwa, naam! Hapa kuna kiongozi anasimamia masuala haya.
Uwezo wa kusimamia miradi
Taswira ya tatu ya serikali inayoweza kuundwa na Magufuli ikiwa atachaguliwa kuwa rais ni uwezo wa kusimamia miradi ya maendeleo. Magufuli ni mtu wa namna hiyo na ametuonyesha katika sekta ya ujenzi na hasa katika eneo la barabara. Moja ya masuala ambayo nayaona kama mafanikio makubwa ya serikali ya Kikwete ni ujenzi wa barabara, ukiniuliza, nitakwambia jambo hili ndilo Kikwete anapaswa kujivunia atakaporudi nyumbani kwake pale ‘Msoga’. Lakini aliyeleta mapinduzi hayo kiusimamizi ni Magufuli.
Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa “ikitolewa tenda ya ujenzi wa barabara nchini Tanzania na India halafu nchi zote zikakabidhi tenda hizo kwa watoto wa marais wa nchi, kule India walau barabara ya ‘kudanganyishia’ itajengwa lakini hapa Tanzania unaweza usione hata kokoto” (tafsiri yangu). Dhana hiyo ina maana kwamba huku kwetu wizi na kujijazia manoti ndivyo vitu vinavyoshamiri na kwa tafsiri ya Mwalimu “ilipasa Magufuli awe anaongoza kwa kuchukua noti za barabara na kuzijaza tumboni kwake”, jambo ambalo limekuwa nadra kutokea na kama liliwahi kuwepo ndiyo tutajua sasa wakati watu wataanza kutoa taarifa zake kwa sababu anataka kwenda Ikulu. Kwa uwezo huu wa kiusimamizi namuona Magufuli akisimamia miradi ya serikali kwa ustadi mkubwa hata kama siyo “waziri wa miradi” katika serikali atakayoiunda.
Mawaziri imara
Taswira ya nne nayoiona katika serikali ya Magufuli ikitokea anashinda urais wa Tanzania ni uundaji wa Baraza la Mawaziri na nyadhifa za kiutendaji zilizojaa watu wenye uwezo kuliko marafiki. Serikali zetu kadhaa zilizopita ikiwamo hii inayoondoka zimekuwa na sifa ya kubeba marafiki kufa au kupona. Siyo siri kwa JK amelalamikiwa mno na mara kadhaa serikali yake ilionekana kama “imejaa washkaji” watu wanaolindana na kuoneana haya kwa heshima za urafiki kuliko kuangalia maslahi ya nchi.
Magufuli anaweza kuwa dawa ya serikali za ushkaji kwani tangu kwenye mchakato wa kupata wagombea ndani ya CCM hakuonekana kama “kitisho” na hakuwa na makundi nyuma yake, penyeza yake ya kimya kimya hadi anakuwa mgombea urais wa CCM imemsaidia kuanza kujenga marafiki wasio na masharti ya kutaka kubebwa naye. Marais wengi huunda mitandao na mitandao hiyo huwapa fedha mapema na huwasaidia kila jambo, wanapofika madarakani huwa na deni la kuilipa mitandao hiyo, malipo yenyewe ni miradi ya serikali, tenda mbalimbali na vyeo lukuki. Naamini Magufuli hatakuwa na tatizo hilo na itamsaidia kutengeneza serikali isiyo na “washkaji kibao.”
CCM yenye nguvu
Taswira ya tano inayoweza kujitokeza ni uwezekano wa kurejesha nguvu ya CCM ambayo inasambaratika, na naamini hili linaweza kujitokeza sana hasa kwenye kipindi cha kwanza cha uongozi wake. Siamini kama ataweza kurekebisha taswira ya CCM kwa miaka mitano mingine (ikiwa atapata vipindi vyote viwili) kwa sababu hatujaona utendaji halisi wa serikali ijayo, ikiwa CCM ndiyo itashinda. Wananchi wengi hawaiamini tena CCM na jambo hilo linaweza kuipeleka ikaangushwa katika uchaguzi wa mwaka huu, lakini ikitokea CCM inavuka kizingiti na inapona kuangushwa halafu Magufuli anakuwa rais, anaweza kujizatiti na akatumia miaka mitano kufanya mambo makubwa yatakayowafanya wananchi warudishe imani kwa chama hicho. Ila akifanya vibaya sana atazidi kuididimiza. Kwa mtazamo wangu wa msisitizo ni kwamba naona akifanikiwa kwenye eneo hili, japokuwa naweka msisitizo wa pili kuwa ni lazima tusubiri kujua ikiwa atashinda kipindi chake cha kwanza kitakuwaje kiuongozi.