Thursday, July 16

UCHAGUZI CCM: Mambo matano ‘mabaya’ Magufuli akiwa rais

Dk John Magufuli akiwasalimia Wajumbe wa Mkutano Mkuu 
katika ukumbi mpya wa CCM mjini Dodoma kabla ya kuanza kupiga kura juzi usiku.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha Dk John Pombe Magufuli kuwa mgombea urais wa chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Tanzania ina vyama 22 vilivyosajiliwa na vinavyofanya kazi sasa, tutake tusitake ni lazima rais wa nchi atatoka katika chama kimojawapo, na kwa sababu CCM imeshapitisha mgombea wake na yeye ana fursa ya kushinda uchaguzi kama ambavyo fursa hiyo ilivyo kwenye vyama vingine. Natumia nafasi hii kufanya uchambuzi wa dhati juu ya taswira ya serikali ya Magufuli ikiwa atafanikiwa kushinda uchaguzi wa mwaka huu. Taswira ya namna hii pia nitaifanya kwa wagombea wengine wa vyama ambavyo vitaamua kuweka wagombea urais..
Uamuzi wa haraka
Moja ya taswira mbaya zinazoweza kujitokeza na kuikumba serikali ya Dk John Magufuli (ikiwa atashinda uchaguzi) ni maamuzi ya haraka na yasiyo na tija ya uhakika. Katika utendaji mzuri wa Magufuli serikalini, madoa makubwa aliyopata ni kwa nyakati kadhaa kusimamia mambo ambayo baadaye yalilalamikiwa sana. Niliwahi kutoa mfano namna ambavyo amewahi kulalamikiwa juu ya maamuzi yake ya kubomoa nyumba za wananchi bila kuwapa muda wa kutosha kuhama. Kibinadamu hayo ni matendo ya ukatili na yanatokana na ufanyaji maamuzi wa haraka katika jambo linalohitaji muda. Sijui kama Magufuli ataachana na tabia hiyo ya “haraka haraka” ili pia kuifanya serikali yake ijiendeshe kistratejia na kimipango kuliko haraka na nguvu. Ikiwa atasonga mbele na tabia hiyo na serikali yake ikaenda kwa kasi hiyo ya “pupa” kuna uwezekano kuwa kila mambo kumi atakayoyasimamia basi mawili hadi matatu yakawa yanafanywa bila kuwa na tija kwa taifa.
Kuyumba kichumi
Mtihani wa pili ambao unaweza kujenga taswira mbovu ya utawala au serikali itakayoundwa na Magufuli (ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania) ni usimamizi wa masuala ya kiuchumi. Eneo hili naliona kama muhimu sana kwa sababu kama nilivyoeleza hapo juu, Magufuli amekuwa waziri bora katika serikali inayomaliza muda wake na amekuwa akitumwa na kufanya kila jambo haraka kwa wakati na kwa maamuzi yenye misimamo. Sielewi uwanda wake katika masuala ya kiuchumi na misimamo yake kwenye eneo hilo, hapa sina maana kuwa Rais wetu lazima awe mchumi, la hasha! Benjamin Mkapa hakuwa mchumi lakini alikuwa na uwezo mpana wa kusimamia uchumi, Jakaya Kikwete ni mchumi lakini amefanya vibaya kwenye eneo hilo kuliko Mkapa. Magufuli amejionyesha mara zote kama mtendaji kuliko “mfikiriaji na mpanga mambo”. Uchumi wa nchi uliopo kama Tanzania unahitaji akili ya ziada kuweza kuufufua tena, nchi haina viwanda, inanunua kila kitu kutoka nje. JK anaiacha ikiwa hoi sana kwenye eneo hilo. Ikiwa Magufuli ataingia na mtindo wa kusimamia utendaji zaidi kuliko kufikiri na kubuni vyanzo vipya vya uchumi, serikali yake itabeba taswira ya kushindwa kusimamia uchumi.
Serikali ya mtu mmoja
Taswira nyingine ya tatu ambayo si salama na ambayo inaweza kujitokeza kwenye serikali itakayoundwa na Magufuli ni serikali ya “One Man Show” (serikali ya mtu mmoja). Watu waliozoea kuwa watendaji wa juu kama Magufuli huwa na kasumba ya kutaka kila jambo liende kama wanavyotaka kila wakati na wakiona haliendi huingilia haraka na kutaka walifanye wao wenyewe, hili ni jambo la kisaikolojia zaidi. Kilema cha serikali za namna hii huwa ni kumjenga mtu mmoja zaidi kuliko wengine si kwa makusudi, bali kwa sababu watendaji wake wanashindwa kwenda na uwezo wa rais wao. Madhara ya hali hii ni kujenga serikali inayokosa vionjo pale ambapo rais anapokuwa hayupo, kunakuwa na hofu ya dhahiri kuwa ni nani anaweza kusimamia masuala mbalimbali kama awezavyo rais na huyo mtu hayupo. Taswira hii itavunjwa tu iwapo mkuu wa nchi ataamua kuwaachia watendaji wafanye maamuzi magumu wao wenyewe, wajifunze kukosea na kukosolewa.
Haki za binadamu
Jambo la nne ambalo linaweza kuwa “taswira dhaifu ya serikali ya Magufuli” (ikiwa atashinda) ni uwezo wa kusimamia masuala ya haki za binadamu na haki za msingi za raia. Hili linaweza kuunganishwa na ile kanuni yake ya ‘kufanya maamuzi kwa mbio na haraka sana kila mara’. Maamuzi ya haraka na yasiyotoa mwanya wa kutosha wa kuzingatia masuala mengine muhimu ya haki za kiraia huwa hayana tija na huumiza dhana ya usimamizi wa haki hizo na yasipokomeshwa huwaumiza raia. Mmoja wa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM ambaye nimeongea naye na hakumpigia kura Magufuli katika mkutano mkuu huo amenieleza kuwa hakufanya hivyo kwa sababu nyumba yake ya urithi iliwahi kubomolewa bila kupewa muda wa kutosha kwa sababu ilikuwa karibu na barabara. Dhana ya usimamizi wa sheria lazima iendane na dhana ya kusimamia haki za raia, watu wa namna hii wanaweza kuwa wengi na ni kielelezo cha wazi kwamba Magufuli atawajibika kurekebisha sana taratibu za ufanyaji maamuzi katika serikali yake ili aweze kulinda haki za raia. Serikali yake inaweza kuepukana na taswira hii mbovu kwa kuchukua muda na kutafakari kwa kina juu ya mustakabali wa wananchi kila jambo fulani linapotokea
Mwenyekiti wa CCM
Taswira ya tano mbaya inayoweza kujitokeza katika uongozi “serikali” ya Magufuli ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ni uwezo wa kukiongoza Chama Cha Mapinduzi. Mtu yeyote hawezi kuwa na shaka na uwezo wa Magufuli katika utendaji wake muda wote serikalini, lakini kunaweza kuwa na shaka kubwa katika uwezo wa kukiongoza chama chake. Mahasimu wake kisiasa tayari wameanza kuwa na hofu na uwezo wa CCM miaka ya mbele chini ya Magufuli, namna ambavyo anaweza kupambana na changamoto za kuongoza chama chenye watu wengi wenye maslahi tofauti tofauti sana.
Ukweli uliopo ni kwamba muda wote ambao Magufuli amekuwa serikalini hakuwahi kuwa kiongozi mkubwa wa moja kwa moja ndani ya CCM. Jambo hili linatafsiriwa kama linaweza kumsababishia makosa ya kiutendaji kwa sababu ya “kutaka kujinasibisha kama yuko karibu na wanachama wa CCM” kumbe akawa anaingizwa kwenye makosa.
Mfano mzuri ni wakati anashukuru wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM na kabla hajataja jina la mgombea mwenza, mara kadhaa alisikika akisema “CCM kwanza, chama chetu kwanza….” Na kisha baadaye ndiyo anasema “Tanzania kwanza”. Wafuatiliaji wa mambo wanaweza kuanza kuhoji, gia hii ya Magufuli ndiyo kutaka kuwaonyesha wanachama kuwa yeye anaifahamu CCM vizuri sana? Kwa chama kikongwe kama CCM unatarajia kiongozi akitanguliza maslahi, kwanza aseme “Tanzania kwanza” chama baadaye. Kusimama hadharani na kusema “Chama Kwanza, Chama Chetu kwanza…” inaleta mtazamo kwamba anaweza kujikuta anafanya makosa ya kiutendaji katika serikali yake kwa lengo tu la kutaka “kuwaridhisha wana CCM”.  Ni bora Magufuli akajiamini, akajiona ni mwana CCM imara na asijione kama vile “kapewa hisani” kuwa mgombea wa chama hicho. Kujiamini kutamfanya akitazame na kukihukumu chama chake bila woga kila mara na pia aitazame nchi yake kama kipaumbele cha kwanza kabla ya chama, kama Rais wa nchi.
Hitimisho
Magufuli ni mtu mahiri ndani ya chungu kibovu. Ule ule mkakati wa kuiokoa CCM mwaka 2005 kwa “kumleta Jakaya” ndiyo unatumika mwaka 2015 tena, kwamba CCM inajitahidi na inajaribu kutaka kuendelea kuishi kwa kutumia mgongo wa kukubalika kwa mgombea wake, kwamba Watanzania wakaipigie kura kwa kumuamini zaidi Magufuli kuliko kutazama makosa ya kihistoria ya chama hicho tangu miaka 50 iliyopita. Kwa Watanzania waliokata tamaa na uongozi unaomaliza muda wake, aina ya watu kama Magufuli wanaweza kuwa kimbilio kubwa sana kwa maana ya upigaji kura, lakini hatujui baada ya kura hizo nini kitatokea, maana Magufuli anakwenda kuzungukwa na wana CCM, na watendaji lukuki serikalini ambao kwao “kuiba fedha za umma na kufanya utendaji mbovu ni amri ya kila siku”. Mambo haya yanaweza kuanza kuwa kikwazo kikubwa kwake hadi pale atakapoamua kuchukua hatua thabiti sana.Mimi binafsi napenda kumtakia kila la heri kiongozi huyu, katika safari aliyoianza.

No comments:

Post a Comment