Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Serikali imepiga marufuku halmashauri za wilaya na manispaa nchini, kuchukua ardhi ya wananchi bila kuwalipa fidia.
Amri hiyo imetolewa mjini hapa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi (pichani), wakati akijibu malalako ya wananchi kuhusu upatikanaji na umiliki wa ardhi.
Lukuvi, alisema halmashauri na manispaa nchini, zimekuwa zikichukua ardhi ya wananchi bila makubaliano na kuwalipa fidia kwa kisingizo cha upimaji viwanja au kutoa maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji.
Alisema kitendo hicho ni dhuluma kwa wananchi na kwamba kamwe hakikubaliki.
Awali baadhi ya wakazi hao, walimlalamikia Waziri Lukuvi wakidai kuwa wamekuwa wakiporwa ardhi na maofisa wa halmashauri na manispaa bila maelezo.
Walidai wanapofuatilia kwenye ofisi zao, wamekuwa wakijibiwa vibaya na wakati mwingine kulipwa fidia kidogo ambayo haitoshi kununua kiwanja na kuwa kero kubwa kwao na kukatisha tamaa.
Akizungumza huku akibubujikwa na machozi mbele ya Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Ismani, Zuhura Chavala, Mkazi wa Kijiji cha Migori, alidai maofisa ardhi wamekuwa wakiwadhulumu baada ya kuwaponya ardhi yao.
Zuhura alidai wanapofuatilia kwa lengo la kulipwa fidia, wamekuwa wakizungushwa hivyo kushindwa kujua hatma yao.
Wakati huo huo: Waziri huyo amewataka wakuu wa wilaya nchini kushiriki mikutano ya vijiji na kutoa ardhi kwa wawekezaji ili kuondoa malalamiko ya wananchi.
Alisema wakuu hao wanatakiwa kuwadhibiti baadhi ya viongozi wa vijiji ambao wamekuwa wakighushi mikutano hiyo na kuuza ardhi ya vijiji kwa wageni bila kupita kwenye mkutano mkuu wa kijiji.
No comments:
Post a Comment