Japo Oktoba 15 mwaka jana ilikuwa siku ya maumivu makali kwake na kunusurika kifo, tarehe hiyo hiyo mwaka huu ameungana na wanafunzi wenzake wa kidato cha nne, kusherehekea kumaliza masomo ya kidato cha nne
“Panya road azinduka akiwa mortuary”, ni kati ya vichwa vilivyobeba habari mbalimbali zilizomuhusu mwanafunzi huyo katika tukio lililotokea Mbagala, jijini Dar es Salaam ambako zaidi ya vijana 10 walitiwa mbaroni siku hiyo.
Isack anasema kupona kwake na kumaliza mitihani ya kidato cha nne ni kwa neema ya Mungu tu na si vinginevyo.
“Siamini kama leo hii namaliza shule, nilikata tamaa, kiukweli bila polisi kufika eneo la tukio siku ile na kuniokoa ningekufa,” anasema.
Ni kumbukumbu mbaya isiyofutika kichwani kwa Isack, hata hivyo ilishatokea.
“Kuna wakati nikikumbuka nashtuka, nimeathirika kisaikolojia, sipo sawa na zamani hata uwezo wangu darasani umepungua. Ninachoshukuru ni mzima tu,” anasema Isack.
Jana Jumatano, Isack alimalizia elimu yake ya sekondari kwa kufanya mtihani wa baolojia kwa vitendo.
Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto wakati huo alisema baada ya polisi kupigiwa simu na raia wema kuwa kuna vijana watatu wamefariki dunia, walikwenda eneo la tukio na kuwakuta wakiwa na hali mbaya.
Alisema mmoja wao anayeitwa Kelvin Nyambocha (14) alifariki dunia baada ya kupigwa na kuchomwa moto na wananchi baada ya kuwapora huku wakiwa na silaha za jadi.
Alieleza kuwa Isack alipigwa kiasi ambacho walijua amefariki dunia na ndipo alipopelekwa chumba cha kuhifadhia maiti na kufanyiwa taratibu zote, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo na kuwekewa namba tayari kwa kuingizwa kwenye jokofu.
“Wakati amewekwa chini kwa ajili ya kuingizwa kwenye jokofu, alizinduka kwa kupumua na kuonekana bado yupo hai, hali iliyosababisha kupelekwa Chumba cha Uangalizi Maalumu (ICU),” alisema Muroto.
Mwenyewe anasimulia kuwa siku ya tukio akiwa na wenzake waliamua kwenda kwenye tamasha la kuinua vipaji lililofanyika Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, baba yake anasema siku hiyo mwanaye alimuaga kwamba anaenda kuangalia mpira hivyo, hakuwa na wasiwasi.
Walifika salama kwenye tamasha hilo lakini lilipoisha wakiwa njiani kurejea nyumbani ndipo, purukushani ilipoanza.
Isack anasema kati yao wengine walikuwa na miaka kati ya 13 hadi 16.
“Mimi nilikuwa nyuma, ndio nikasikia kelele za wezi kumbe wale walio mbele walianza kuwapora watu vitu,” anasema.
Anasema ghafla alishangaa mwenzake mmoja amekamatwa na kuwekwa kwenye tairi kisha kuwashwa moto.
“Ilibidi nikimbie kujiokoa. Huku nikikimbizwa kwa kuitwa mwizi, nilifanikiwa kufika eneo la Sabasaba nikitokea Zakhem Mbagala,” anasimulia.
Anasema watu waliokuwa mbele yake walifanikiwa kumkamata na kuanza kumpiga kwa nguvu huku wengine wakitaka achomwe moto mara moja.
Isack anasema huku akipigwa, alisikia wananchi hao wakibishana kwani walikuwepo waliotaka achomwe moto hapohapo na wengine, wakitaka apelekwe walikokuwa wakipigwa wengine.
“Walianza kubishana, wengine wanasema nichomwe moto hapo hapo, wengine wanataka nirudishwe waliokokuwa wenzangu…kwa kweli maisha yangu yakawa mikononi mwa Mungu, nilijitahidi kujitetea bila msaada,” anasema mwanafunzi huyo.
Mwanafunzi huyo anasema wakati akiendelea kupigwa, ghafla walitokezea polisi ambao waliwatawanya watu na wakati huo bado alisikia kila kinachoendelea.
“Ghafla nilisikia kishindo kikubwa na kuanzia hapo nilikuja kujiona hospitali ya Temeke. Tangu hapo sijui kilichoendelea ndio nasikia nilipelekwa chumba cha kuhifadhia maiti,” anasema.
Baba mzazi wa Isack, Ernest Chalo anasema anakumbuka siku hiyo alikuwa anafuatilia mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, alipopigiwa simu na mtu asiyemfahamu akimpa taarifa kuwa mtoto wake amefariki dunia, hivyo anatakiwa kwenda chumba cha kuhifadhia maiti, ili amtambue mwanaye.
“Nilichanganyikiwa, sikujielewa yaani ilibidi nitoke mbio hadi Temeke, moja kwa moja nilielekea kwenye chumba cha kuhifadhia maiti nikaonyeshwa miili ya vijana waliokuwa wameuawa. Kwa sababu waliumizwa sana usoni sikuwatambua,”anasema.
Aliamua kuwakagua tumboni akiamini kwamba angemtambua mwanaye kwa upekee wa kitovu lakini hakufanikiwa, ndipo akatokea msamaria mwema akamwambia mtoto wake alizinduka.
“Kutokana na baridi kali ya chumba cha kuhifadhia maiti, mtoto wangu alipoingizwa mle ndani alipumua na hivyo akatolewa. Niliambiwa alivishwa nguo za mwenzake kwa sababu zake zilivuliwa,” amesema.
Anasema huenda kabla mwanaye hajapoteza fahamu aliitaja namba yake ya simu hivyo ikasaidia yeye apate taarifa.
Anasema alifanikiwa kumuona mwanaye akiwa hai japo alikuwa akivuja damu kwa kipigo huku hali yake ikiwa mbaya.
Taarifa za kifo cha Isack ziliwafikia walimu wake shuleni.
Makamu mkuu wa shule hiyo Amosi Tinde anasema taarifa hizo ziliwashtua na kuwashangaza kwa sababu siku za masomo, Isack alihudhuria vipindi vyote na hatukuwahi hata kuhisi kwamba ni ‘panya road’.
“Tulishangaa kuambiwa Isack ameuawa akiwa miongoni mwa vijana ‘panya road’ na tukapigiwa simu mwili wake upo chumba cha kuhifadhia maiti, kiukweli hakuwa mwanafunzi mtoro na ni kijana mwenye nidhamu tu, hizi habari zilitushtua sana.” anasema.
Mwalimu huyo anasema baada ya kupokea ujumbe huo, iliwalazimu waanze kuandaa taarifa za mwanafunzi huyo shuleni.
Hata hivyo, baadaye tena wakaambiwa hajafariki dunia, isipokuwa alizimia tu.
Isack anasema hofu yake kubwa ilikuwa ni kupoteza masomo yake kutokana na kuhusishwa na ‘panya road.’
Lakini walimu wanasema, waliamua kumsaidia ili awe mwanafunzi mzuri na hatimaye kumaliza mitihani yake ya kidato cha nne,
“Uzuri wake leo hii anamaliza kidato cha nne, tunamuombea Mungu afaulu na ikitokea vinginevyo, anaweza kusoma hata ufundi,” anasema Tende.
Mwalimu Tinde anasema hatua ya kumaliza mitihani yake ni ujasiri mkubwa kwani, mwanafunzi mwingine angeweza kuacha shule kwa woga au aibu.
Maisha yake baada ya tukio
Awali haikuwa rahisi kwa Isack kurejea shuleni na kuendelea na masomo.
Baba yake anasema baada ya matibabu na kesi kuisha, ilimlazimu ampeleke Tanga kwa ndugu zake ili akakae kidogo kurejesha fahamu zake vizuri kabla ya kuendelea na masomo.
Walimu wake pia waliamini kwamba hataweza tena kuendelea na masomo.
Mwalimu Tende anasema ilibidi walimshauri baba yake walau amuhamishie shule nyingine kwa sababu waliamini atakuwa ameathirika kisaikolojia.
“Lakini baadaye tukaona amerudi na anaweza kumudu masomo hivyo kazi kubwa ikawa kumsaidia kisaikolojia,”anasema.
Mwalimu wake wa darasa, Janeth Swai anasema moja ya jukumu kubwa lililokuwa mbele yake mwaka huu ni kumsaidia mwanafunzi huyo, sio tu kwamba aachane na tabia zilizomsababishia matatizo ya kupigwa, bali kuwekeza nguvu kwenye masomo yake.
“Nilikuwa naongea naye kila mara, nikamfanya rafiki yangu na akaanza kunisimulia vitu vingi. Kwa hiyo niliweza kumsaidia sana,” anasema.
Mwalimu Swai anasema Isack alikuwa mtulivu zaidi na akaanza kuwakwepa rafiki zake hasa wa mitaani.
Mwalimu mwingine, Joyce Madenge anasema isingekuwa makundi mabaya ya rafiki zake, mwanafunzi huyo asingekutwa na janga lililomkuta.
Anasema bado kuna kazi kubwa ya kumsaidia Isack kisaikolojia na kuhakikisha hajiungi tena na makundi ya aina hiyo baada ya kumaliza masomo yake.
Baba yake anasema ameshamuandalia sehemu ya kujifunza ufundi wa magari baada tu ya kumaliza kidato cha nne wakati akisubiri majibu.
Kuhusu kujihusisha na ‘panya road’
Anasema siku ya tukio hakuwa anajua kama wenzake hao wangefanya uhalifu huo na kwamba, alishtukia tu wameanza kupora kisha kuanza kupigwa.
“Kwa hiyo nilishtuka tu wenzangu mbele yangu wanaanza kupora mara kelele za wezi. Ndio tukaanza kukimbizwa na kupigwa,” anasema.
Hata hivyo anasema baada ya kupata ahueni, aliwapeleka polisi kwa mwenzake mmoja ambaye nyumbani kwao alikutwa na bendera ya kundi la ‘panya road’ wanaojiita ‘Taifa Jipya’ iliyochorwa picha za maghorofa, silaha za jadi na askari akikimbizwa.
“Ninachoshukuru nimekuwa kijana mzuri, sina tena marafiki na ninamaliza shule. Kweli sikuwa mwizi,”anasema.
Isack anatamani tukio hilo lisingetokea lakini limeshatokea.
“Naumia nikikumbuka na niwaombe vijana wenzangu waache tabia hizi mbaya zinawaumiza sana wazazi. Baba yangu aliumia na akaingia gharama kubwa kunitunza,”anasema.
Isack anatamani kuwa mwalimu wa sekondari.
“Napenda kuwa mwalimu mzuri kama Swai, napenda nije niwasaidie wenzangu hata hivyo masomo ninayoyapenda ya Kiswahili, Kingereza na History yananisukuma kuwa mwalimu zaidi kuliko kazi nyingine,” anasema.
Anasema mitihani si migumu sana na kwamba maswali mengi walikuwa wamefundishwa.
“Kama nitafeli ni kwa sababu ya tatizo lililonitokea, lakini naomba Mungu nifaulu,” anaema.
Mwalimu Tinde anasema jambo zuri ni kuwa amemaliza kidato cha nne.