Thursday, November 16

Spika Ndugai aigomea Serikali jina la shirika



Spika wa Bunge, Job Ndugai
Spika wa Bunge, Job Ndugai 
Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Alhamisi amegomea Serikali na kulazimika kuahirisha Bunge kwa muda wa saa moja ili warudi na kukubaliana kubadili jina la Shirika la Wakala wa Meli wa Taifa (NASAC)
Spika Ndugai alitoa agizo la kuahirisha Bunge baada ya mvutano wa Serikali na Kamati ya Bunge ya Miundombinu ambao walipendekeza kubadilishwa kwa jina hilo.
Mapema wakati Serikali ikijibu maoni ya wabunge kuhusu muswada huo, Spika alionyesha dhahiri kutokukubaliana na wazo la Serikali na badala yake akasimama katika mawazo ya kamati na wabunge wengine kuwa jina hilo halifai.
Mara baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kumaliza yake, Spika alihoji ni kwa nini asikubaliane na mapendekezo ya wabunge katika kubadili jina la muswada lakini mwanasheria huyo akatupia mpira kwa waziri kuwa angekwenda na majibu.
Hata hivyo, katika majumuisho ya michango ya wabunge, Waziri Profesa Makame Mbarawa alitoa sababu za kutobadilisha jina akisema halikuwa na maana yoyote na wala lililopendekezwa halikuwa na madhara kwani waliosema kuwa jina hilo ndilo lililofilisi hawakujua kuwa kulikuwa na usaliti.
“Mheshimiwa Spika, jina halina shida yoyote kwani hata lile la awali siyo kwamba lilipeleka madhara bali kilichotokea ni namna ambavyo baadhi ya watu waliokuwa ndani ya chombo hicho walikuwa ni wasaliti,” amesema Mbarawa
Baada ya hoja za waziri huyo Bunge lilikaa kama kamati na kuanza kuangalia vifungu hivyo ndipo Spika akampa nafasi mwenyekiti wa kamati hiyo Profesa Norman Sigala ambaye akasema Serikali ilikuwa imewadanganya.
“Nakushukuru mheshimiwa Spika, Serikali hapa ni kama imetudanganya maana kusema itaangalia huko mbeleni ni sawa na kutudanganya sisi, tulichokubaliana kwenye kamati sicho kilichowasilishwa bungeni,” amesema Profesa Sigala.
Spika alimpa nafasi Waziri ambaye aliendelea kuweka msimamo kuwa jina hilo liendelee kama lilivyowasilishwa na Serikali ili kama kutakuwa na marekebisho mbeleni Serikali itafanya hivyo.
Kauli ya waziri ilimuinua Spika ambaye amesema jina hilo linapeleka picha mbaya kwani haiwezekani Serikali kuunda chombo kipya kizuri lakini ikatumia jina ambalo lina maudhui mabovu.
“Hapa ndipo tunatunga sheria yenyewe, sasa kama mnaona kubadili jina kunaweza kuathiri kisheria niambie lakini kama hakuna, sioni kwa nini tuendelee kuvutana sana, naahirisha shughuli za Bunge kwa saa moja nendeni katika ukumbi wangu hapo mkutane na mjadiliane ili mkirudi hapa mniletee jina,” amesema Spika na kuahirisha Bunge
Wabunge walilipuka kwa makofi na makelele ya kumshangilia Spika huku wanasheria wakikutana kwa haraka ambapo Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi waliwaongoza wajumbe wa kamati na serikali haraka kuingia ukumbini kwa ajili ya kutafuta jina hilo.

No comments:

Post a Comment